The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

BOT yawataka wamiliki wa hoteli kuingia kwenye mfumo rasmi wa biashara ya ubadilishaji fedha

Wamiliki wa hoteli visiwani Zanzibar wametakiwa kuendana na mabadiliko ya kanuni ya maduka ya kubadilishia fedha ya mwaka 2019, yanayozitaka hoteli kuingia kwenye mfumo rasmi wa biashara ya kubadilisha fedha kwa kuchukua leseni ya kuwa na huduma hiyo katika hoteli zao.

Wito huo umetolewa leo Machi 22, 2024, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, wakati alipokutana na wamiliki wa hoteli visiwani humo kwa ajili ya kuzungumza nao kuhusiana na mabadiliko hayo. 

Tutuba amesema kuwa hadi kufikia Julai 1, 2024, wamiliki wa hoteli wote watatakiwa wawe wameshajisajili kwenye mfumo huo wa kibiashara wa ubadilishaji fedha za kigeni, ili kuweza kutoa huduma hiyo kwa wageni wanaofika kwenye hoteli zao.

Serikali, kupitia marekebisho ya kanuni ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni ya mwaka 2019, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, imetoa nafasi kwa wamiliki wa hoteli za nyota tatu hadi nyota tano kutoa huduma za kubadilisha fedha, utaratibu ambao hauhitaji mtaji, ila kigezo kikubwa ni kumiliki hoteli yenye hadhi hizo.

Maombi na leseni za utafiti wa madini 2,648 kufutwa 

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini kufuta jumla ya maombi na leseni za utafiti 2,648 ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuomba na kuendeleza maeneo ya migodi kwa manufaa ya taifa na ukuaji wa sekta ya madini.

Hayo yameelezwa hayo leo Machi 22, 2024, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma. Ambapo, amebainisha kuchukua uamuzi huo kwa sababu kumekuwa na tabia ya baadhi ya wamiliki wa leseni kutozingatia utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Madini, sura namba 123. 

Miongoni mwa makosa ambayo Mavunde ameyataja kuwa yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ni wamiliki wengi wa leseni kutoanza au kutoendeleza maeneo na badala yake kuhodhi maeneo, kutolipa ada stahiki za leseni, kutowasilisha nyaraka muhimu kama mpango wa ushirikishwaji wa Watanzania kwenye shughuli za madini, mpango wa wajibu wa makampuni kwa jamii na nyaraka za taarifa za fedha kuonesha matumizi yaliyofanyika pamoja na vielelezo vya matumizi husika.

Nchini Tanzania, sekta ya madini ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wananchi. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/2023, migodi ilifanya manunuzi ya dola za Kimarekani bilioni 1.6, ambapo dola bilioni 1.4 zilihusisha kampuni za Kitanzania na hivyo kufanya zaidi ya asilimia 86 ya manunuzi yote ya migodi katika mwaka huo yawe yamefanywa na Watanzania.

CCM yawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuwaamini 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewashukuru Watanzania kwa kuendelea kukiamini na kukipa ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa nafasi ya udiwani uliofanyika Machi 20, 2024, nchi zima. 

Katika uchaguzi huo CCM ambayo imekuwa ikiunda Serikali tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, mwaka 1992 kimeshinda katika kata zote 23, ushindi ambao ni sawa na wastani wa asilimia 89. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Machi 22, 2024, na Katibu wa Idara ya Organaizesheni, Issa Haji, CCM imesema mafanikio hayo yametokana na umoja na mshikamano uliopo ndani ya chama, uteuzi wa wagombea bora pamoja na uadilifu katika kuwatumikia wananchi. 

Hata hivyo, itakumbukwa kuwa uchaguzi huo ulifanyika katika wakati ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilisusia kushiriki. Kwa upande wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, ambacho kilishiriki, kilidai kuwa kulikuwa na mazingira ya wizi wa kura yaliyopelekea wagombea wake kunyimwa ushindi.