The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rais Samia kutenga siku moja ya kukutana na wananchi kusikiliza kero

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda, ametangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti taifa wa chama hicho tawala, atatenga siku moja katika kila mwezi kwa ajili ya kukutana ana kwa nana kusikiliza kero za wananchi. 

Taarifa hiyo ameitoa leo Machi 5, 2024, wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi ndogo ya chama hicho, iliyopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam. 

Makonda ameeleza kuwa Rais Samia ataanza utaratibu huo ikiwa ni moja ya hatua ya kumuenzi Hayati Ali Hassan Mwinyi, ambaye pia anadaiwa kuwahi kuutumia utaratibu wa namna hiyo kipindi alipokuwa madarakani.

Mwinyi, ambaye alikuwa Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, alifariki Februari 29, 2024, wakati akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu katika hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es salaam. Mazishi yake yalifanyika huko visiwani Zanzibar siku ya Machi 2, 2024.

Mamlaka hiyo imedai kuwa upungufu huo unatokana na kufanyika kwa maboresho ya msingi katika mtambo huo

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam imetoa taarifa kwa wateja wake wanaohudumiwa na mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu chini kuwa kutakuwa na upungufu wa huduma ya maji kwa kipindi cha siku tatu kuanzia leo Machi 05, 2024  jioni hadi Alhamisi ya Machi 07, 2024. 

Baadhi ya  maeneo yaliyotajwa kuwa yatapata athari ni pamoja na Bagamoyo, Mapinga, Mabwepande, Bunju, Boko, Kunduchi, Mbweni, Salasala, Chuo kikuu ardhi, Mivumoni, Boko, Msasani, Oysterbay, Masaki, Kigogo, Mwananyamala, Chang’ombe, Kinondoni, Kurasini, Madale, Kawe, Goba, Buguruni, Vingunguti, Kiwalani, Airport, Ilala na katikati ya jiji. 

Kwa wakazi wa Dar es Salaam, jiji lenye watu wengi Tanzania, katika siku za hivi karibuni kumekuwa na vilio vingine vya changamoto za mgao wa umeme pamoja na kupanda kwa bei ya sukari mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa kiasi kikubwa.

Vijana wa mradi wa BBT wadai kutelekezwa na Serikali

Leo Machi 5, 2024, The Chanzo imechapisha habari kuhusu malalamiko ya vijana 268 wanaonufaika na Programu ya Kuwezesha Ushiriki wa Vijana Katika Kilimo Biashara (BBT-YIA), yanayohusisha kutelekezwa na Serikali. 

Vijana hao waliopo Chinangali mkoani Dodoma, wamemtupia lawama nyingi Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, kwa kile wanachodai kuwa amekuwa akiwatolea kauli zisizofaa kipindi wanapomtafuta kumueleza masaibu wanayoyapitia hivi sasa. 

Baadhi ya mambo ambayo wanayalalamikia ni pamoja na ahadi ya kupewa ekari tano kwa kila mmoja, lakini hivi sasa wanalazimika kulima shamba la ushirika linalokadiriwa kuwa na ekari zisizozidi 200. 

Jambo lingine ni sharti la kutakiwa kuuza mazao yatakayozalishwa kwa mnunuzi atakayekubalika kwa mujibu wa taratibu za Chama cha Ushirika wa Vijana BBT, suala ambalo wanadai halikuwepo hapo awali. 

The Chanzo ilimtafuta Bashe ili kufahamu juhudi za Serikali kutatua kero za vijana hao, lakini mpaka tunachapisha habari hiyo tulikuwa hatujafanikiwa kupata majibu kutoka kwake. 
Habari zaidi soma hapa