The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Benki Kuu Yazindua Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo (TIPS )

Katika juhudi za kuendeleza mifumo ya kielektroniki na kukuza ufanisi katika malipo, Benki Kuu ya Tanzania imezindua Mfumo wa Taifa wa Malipo ya Papo kwa Papo kwa kimombo Tanzania Instant Payments System – TIPS. 

Hatua hii inaonyesha dhamira ya serikali katika kuimarisha mazingira mazuri ya biashara na kupunguza gharama na muda katika malipo.  

TIPS, mfumo ambao umetengenezwa kwa viwango vya kimataifa, unawezesha wananchi kufanya miamala ya kifedha kwa haraka na kwa gharama nafuu zaidi na ulianza kutumika tangu mwaka 2023. 

Akizungumzia uzinduzi wa mfumo huo katika Mkutano wa 21 wa Taasisi za Fedha unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC),  Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, ameeleza kuwa mfumo huo unathibitisha jukumu la benki kuu katika kusimamia mifumo ya malipo na kudhibiti viashiria vya hatari.  

Ufunguzi wa mkutano huo umefanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ambaye ametoa wito kwa washiriki wa Mkutano huo kutafakari kwa kina changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni na hatua gani za muda mfupi na wa kati zinazopaswa kuchukuliwa zaidi ya zile zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania. 

Mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 wakamilika

Serikali imesema imekamilisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake ikiwataka wanahabari kuharakisha uundwaji wa taasisi za kusimamia sekta hiyo kwa mujibu wa Sheria.  

Haya yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alipofanya ziara katika Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) na kufafanua kuwa kuwa serikali imekamilisha mchakato na sasa ni wakati wa Wanahabari kushirikiana na Idara ya Habari (Maelezo) kukamilisha uundwaji wa taasisi hizo.

Sheria hiyo pamoja na mambo mengine imeanzisha Bodi ya Ithibati itakayokuwa na jukumu la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa. Pia inaanzisha Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari na Baraza Huru la Habari Tanzania. 

Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake zilianzishwa na mwaka 2016 ikiwa inalenga kudhibiti tasnia ya habari nchini Tanzania kwa kuweka viwango vya uandishi wa habari, usajili wa vyombo vya habari, na haki na wajibu wa waandishi wa habari. Itakumbukwa kuwa sheria hii na kanuni zake ilidaiwa kuwa baadhi ya vifungu vyake vinapunguza uhuru wa vyombo vya habari huku kanuni zingine zinachukuliwa kuwa ngumu sana kutekeleza.  

 Ado Shaibu Athibitishwa na wajumbe kuwa Katibu Mkuu ACT 

Wazalendo Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha ACT- Wazalendo, wamemthibitisha Ado Shaibu kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kwa miaka mingine mitano. Shaibu amethibitishwa leo Alhamisi, Machi 7, 2024 hii ikiwa ni awamu ya pili kwake kushika wadhifa huo. 

Chama hicho jana kimefanya uchaguzi mkuu wa kupata viongozi wapya, huku Dorothy Semu akitangazwa kuwa Kiongozi wa Chama (KC), akichukua nafasi iliyokuwa inashikiliwa na Zitto Kabwe. Wakati huohuo, Othman Masoud Othman alitangazwa mshindi wa nafasi ya uenyekiti wa baada ya kupata jumla ya  kura 539, sawa na asilimia 99.6 ya kura zote zilizopigwa. 

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara imechukuliwa na Isihaka Mchinjita aliyechaguliwa kwa kura 517 sawa na asilimia 96.1, huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar ikienda kwa Ismail Jussa aliyeshinda kwa kura 509 sawa na asilimia 99.6 ya kura zote zilizopigwa.