The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mtwara. Shahidi namba tisa wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Mussa Hamisi inayowakabili askari polisi saba, Fidelis Charles Bugoye amabye ni Mkemia Mwandamizi wa Serikali amewasilisha ripoti ya uchunguzi wa vinasaba vya mabaki ya mwili wa marehemu Mussa Hamis mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mtwara.

Bwana Bugoye ambaye pia meneja wa uchunguzi wa sayansi jinai na vinasaba kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ameiambia Mahakama kuwa mpangilio wa vinasaba vya mabaki ya mwili wa Mussa Hamis unalingana na ule unaotoka kwenye sampuli ya mate ya Hawa Bakari Ally ambaye ndiye mama wa Mussa Hamis.

Aidha kwa upande wa uchunguzi wa sampuli ya funza waliochukuliwa katika eneo lililochukuliwa mabaki ya mwili huo ulionyesha kwamba hapakuwa na sumu.

Matokeo ya sampuli ya funza yamebainishwa wakati wa maswali ya dodoso yaliyoulizwa na wakili kutoka upande wa utetezi Robert Dadaya anayemtetea mshtakiwa namba tano John Msuya ambaye ni daktari wa jeshi la polisi.

Itakumbukwa kwamba awali shahidi alisema kuwa mnamo tarehe 27 Januari, 2022 alipokea vielelezo kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya kusini Mtwara sambamba na barua kutoka ofisi ya upelelezi mkoa wa Mtwara iliyokuwa inaelekeza ufanyike uchunguzi juu ya kubaini kuwa mabaki hayo ni ya mwili wa binadamu, kulinganisha vinasaba kutoka kwenye mifupa nane ya mbavu, mifupa miwili ya mguu wa kulia na suruali na vinasaba vya sampuli vya kwenye sampuli ya mate ya Hawa Bakari Ally.

Barua hiyo vilevile iliekeza ufanyike uchunguzi kwenye sampuli ya funza ili kubaini kama kulikuwa na sumu. Baada ya uchunguzi huo shahidi aliandika ripoti na kukabidhi vielelezo hivyo mahamani na kuwa vielelezo vya ushahidi vya upande wa mashtaka.

Mabaki hayo ya mwili kwa sasa yapo chini ya Mahakama ambapo zinafanyika taratibu za kupata sehemu ya kuhifadhi mabaki hayo ambayo itakuwa inazingatia utu na usalama kwa kuwa kwa sasa mabaki hayo yanatambulika kama ni ya binadamu.

Kesi hiyo inatarajia kuendelea tena hapo kesho tarehe 30 Novemba,2023.