Zanzibar. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwepo kwa wanasheria wanawake Zanzibar ni msaada tosha wa upatikanaji wa haki kwa jamii inayokabiliwa na changamoto mbalimbali.
Ameyasema hayo wakati akifungua kongamano la siku 3 la maadhimisho ya miaka 20 ya Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA).
“Kuwasaidia wanawake na watoto kwenye kupata haki bila ya malipo ni suala ambalo linahitaji kujitoa kwa moyo na huku mkiwa hamtarajii malipo” amesema Hemed.
Katika kipindi kifupi cha Julai hadi Septemba Jumuiya hiyo imepokea mashauri 395 yanayohusu talaka, matunzo na madai ya mali kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria.
ZAFELA ilianzishwa mwaka 2003 kwa lengo la kuwasaidia wanawake kupata haki na kutoa msaada wa kisheria visiwani hapa.