The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zanzibar. Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA Zanzibar), Dkt. Mzuri Issa amesema bado kuna changamoto ya malezi katika jamii kuwaanda watoto wa kike ili kuja kushika nafasi za uongozi.

Dkt. Mzuri alikuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa kike yaliyoandaliwa na wadau wakiwemo ZAFELA, JUWAUZA na PEGAO hapo jana, amesema kuwa suala hili limedhihirika hata katika ngazi za chini za uongozi kwa wanafunzi wa kike wawapo shuleni.

”Utafiti tuliofanya umebaini kuwa wasichana wengi wanaogopa kushiriki nafasi za uongozi wakiwa shuleni, hali hii itaendelea hadi watakapokuwa wakubwa,” amesema Dkt Mzuri.

Tathmini ya utafiti uliofanyika na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na wadau hao unaonesha kuwa kuna muamko mdogo wa wanafunzi waliopo shuleni na vyuoni kwenye suala la kushika nafasi za uongozi. 

Akizungumza juu ya suala la malezi katika familia, Hawra Shamte, Mjumbe kutoka Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA) ameitaka jamii kuacha kuwaandaa watoto wa kike kuwa wasaidizi wa mambo pekee kwenye jamii na badala yake wawafunze pia wajibu wa kuwa viongozi.

“Familia ziache masuala ya kuwalea watoto wa kike kama wasaidizi wa kazi za nyumbani badala yake suala la uongozi pia lionekana kweye malezi,” amesema Hawra.

Tangu mwaka 2012 Umoja wa Mataifa ulitangaza maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani kila ifikapo  11 Oktoba, lakini kwa Zanzibar wadau hawa wameiadhimisha Oktoba 17, 2024 katika ukumbi wa Zura, Marisara, Mjini Magharib. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni Muwezeshe Mtoto Wa Kike, Apaze Sauti Yake.

Imeandaliwa na Najjat Omar