Dodoma. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema katika kipindi cha mwezi Septemba mwaka 2023 hadi kufikia sasa upungufu wa upatikanaji wa umeme umeweza kushuka kutoka Megawati 410 hadi kufikia Megawati 213 kwa sasa.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa TANESCO Mhandisi Gissima Nyamo-Haga amesema, takriban Megawati zaidi 197 zimeongezeka katika mfumo wa Gridi ya Taifa kutokana na juhudi mbalimbali za matengenezo ya mitambo.
“Hata hivyo, hali ya uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo vya maji bado haijakamilika, kutokana na mvua kuchelewa kunyesha katika mikoa ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji katika vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ya Mtera, Kidatu na Kihansi yaani mikoa ya Iringa, Mbeya, Tabora, Singida na Dodoma,” amesema.
Aidha, amesema Shirika linaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kukabiliana na upungufu wa umeme kwa kuendelea kufanyia matengenezo mitambo yake, kuongeza vyanzo vya kuzalisha umeme, kuongeza upatikanaji wa Gesi Asilia, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kusafirishia na kusambaza umeme.
“ Shirika linautaarifu umma kwamba hali ya upatikanaji wa umeme itaendelea kuimarika katika miezi ya usoni kutokana na kukamilisha matengenezo ya mitambo iliyokuwa na hitilafu.