The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba, amesema kwamba Serikali ya Israel imeijulisha Tanzania kuwa Mtanzania Joshua Mollel aliyekuwa akisoma nchini Israel kabla ya kupotea Oktoba 7, 2023 aliuawa mara tu baada ya kutekwa na kundi la Hamas.

“Tumejulishwa na Serikali ya Israel kwamba Joshua Mollel, kijana wa Kitanzania aliyekuwa anasoma nchini Israel,aliuawa mara tu baada ya kutekwa na kundi la Hamas mnamo tarehe 7 Oktoba 2023,” ameeleza Makamba katika ukurasa wake wa X.

Makamba amesema kuwa amewasiliana na baba mzazi wa Joshua mara baada ya kupokea ujumbe huo na kwa sasa Serikali inaendelea na mipango ya kumpeleka nchini Israel Mzee Mollel na mwanafamilia mwingine pamoja afisa wa Serikali kwa ajili ya kupata taarifa zaidi.

Kifo cha Joshua Mollel kinakuwa ni cha pili mara baada ya Mtanzania mwingine Clemence Mtenga aliyekwenda Israel kwa ajili ya masomo ya kilimo kuuawa na kundi hilo.

Mwili wa Mtenga ulifanikiwa kurudishwa Tanzania na ulikabidhiwa kwa familia yake na kuzikwa Novemba 28, 2023 huko mkoani Kilimanjaro.