Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mtwara imetoa msaada wa vifaa tiba wenye thamani ya zaidi milioni 5 kwa ajili ya kuimarisha huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya wilaya ya Mtwara ikiwa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya shukrani kwa mlipa kodi.
Akikabidhi vifaa hivyo Meneja wa TRA Mkoa wa Mtwara, Helirehema Kimambo amesema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kuwakumbuka walipa kodi waliopo hospitalina kukumbusha umuhimu wa kulipa kodi kwa kudai na kutoa risiti wakati wa kunua ama kuuza bidhaa.
Meneja huyo aliendelea kusema kuwa kwa sasa hali ya ukasayaji wa kodi kwa mkoa wa Mtwara imeendelea kuimarika ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Novemba 2023 TRA mkoani hapa imekusanya kiasi cha bilioni 45.08.
“Ukuaji wa mapato kwenye mkoa huu inatokana na elimu ambayo inatolewa kwa walipakodi na vilevile mwitikio wa walipa kodi kulipa kodi zao kwa hiari.” alieleza Kimambo.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi katika hospitali hiyo Nestory Masaganya, amesema vifaa hivyo vitaenda kuimarisha huduma ya mama na mtoto kwa kuwa kulikuwa kuna uhitaji mkubwa kwa sasa.