The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hata Dikteta Teodoro Obiang Hafanyi Vitimbi Kama Tanzania

Nimekuwa nikizifuatilia kwa ukaribu mkubwa chaguzi za nchi nyingi za Kiafrika tangu mfumo wa siasa za vyama vingi urejelewe Afrika. Mara mbili nilikuwa mmoja wa waangalizi rasmi katika chaguzi kuu za Equatorial Guinea kwa niaba ya taasisi iitwayo Taasisi ya Mikikati ya Kidemokrasia (au the Institute for Democratic Strategies) yenye makao yake makuu nchini Marekani.

subscribe to our newsletter!

Nimekuwa nikizifuatilia kwa ukaribu mkubwa chaguzi za nchi nyingi za Kiafrika tangu mfumo wa siasa za vyama vingi urejelewe Afrika.  Mara mbili nilikuwa mmoja wa waangalizi  rasmi katika chaguzi kuu za Equatorial Guinea kwa niaba ya taasisi iitwayo Taasisi ya Mikikati ya Kidemokrasia (au the Institute for Democratic Strategies) yenye makao yake makuu nchini Marekani.

Katika wiki hizi chache zilizopita nimekuwa nikizilinganisha chaguzi hizo na ule unaotazamiwa kufanywa Oktoba 28, 2020 nchini Tanzania.  Kumbukumbu zangu zinanambia kwamba chaguzi hizo ninazozikumbuka hazikuwa na vituko na vitimbi kama vya mwaka huu Tanzania.  Hata zile chaguzi za Equatorial Guinea, nchi ambayo imekuwa ikitawaliwa kimabavu kwa muda mrefu.

Tanzania na Equatorial Guinea zinafanana kwa jambo moja. Zote zina mfumo wa vyama vingi vya siasa lakini vyote vina vyama vyenye kutawala vyenye jeuri ya kujiona kwamba vyama vingine havina haki ya kutawala.  Vyama hivyo hujifanyia mambo utadhani kwamba vipo katika nchi zenye mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Equatorial Guinea ni nchi iliyopata umaarufu wa ghafla 2012, khasa kwa mashabiki wa mpira wa miguu, ilipokuwa mwenyeji bia wa kombe la soka la Africa Cup of Nations.  Kabla ya hapo waliokuwa wakiijua Equatorial Guinea wakiijua kwa mengine yenye kutisha ambayo bado yapo.  Kwanza, mbu wake wenye kuuma vibaya na kusababisha homa kali ya malaria. Pili, uchawi uliozagaa unaoithiri jamii nzima kuanzia Rais hadi raia wa chini.  Tatu, udikteta uliokubuhu ulioanza tangu zama za dikteta wa kifashisti Jenerali Francisco Franco alipokuwa akiitawala Hispania (1936-1975).

Equatorial Guinea ilikuwa koloni la Hispania tangu 1778 mpaka Oktoba 1968 ilipopata uhuru.  Rais wake wa kwanza alikuwa Francisco Macias Nguema aliyekuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanywa Septemba mwaka huo. Uchaguzi huo ni wa pekee nchini humo uliokuwa huru, wa haki na usiokuwa na mizengwe. Chaguzi zote zilizofanywa baadaye, pamoja na zile mbili nilizozishuhudia, zilikuwa na mapungufu mengi.

Macias Nguema alikuwa kama zimwi nchini mwake.  Kuna wasemao kwamba baba yake alimfunza uchawi na usihiri na aliutumia kujiendeleza kisiasa, hususan alipokuwa rais. Aliwaua watu kwa mkururo. Inasemekana kwamba nyumbani kwake kulikuwa na mafuvu chungu nzima ya vichwa vya watu aliowaua ili ayatumie kwa matambiko ya kichawi.

Pole pole Macias Nguema aliliangamiza taifa lake.  Alikuwa hasikii la mtu.  Akimuona kila mtu kuwa ama adui au anayeweza kuwa adui.  Aliupiga marufuku uandishi wa habari. Ilikuwa kosa la jinai kuwa mwandishi wa habari.  Adhabu yake ilikuwa kifo.  Wapinzani wa serikali wakikamatwa na kupelekwa kwenye kambi maalum ambako kazi ngumu za sulubu zikiwangoja. Wengine waliuliwa. Makasisi walitumbukizwa jela.

Mkesha wa Krismasi ya 1969 serikali ya Macias Nguema iliwaua kwa kuwapiga risasi watu 150 walioshtumiwa kula njama za kuipindua.  Miezi saba baadaye, Macias Nguema alivipiga marufuku vyama vyote vya siasa isipokuwa chake. Ulevi wa madaraka ulikwishampanda kichwani.

Mwaka 1972 alitangaza rasmi kwamba atakuwa rais wa maisha.  Haikuwa hivyo. Wanajeshi walimpindua 1979.  Aliyeyaongoza mapinduzi alikuwa mpwa wake mwenyewe, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo aliye rais hadi hii leo.  Teodoro Obiang ni Rais aliyetawala kwa muda mrefu duniani, miaka 41.  Anafuatiwa na jirani yake, Rais Paul Biya wa Cameroon aliye madarakani sasa kwa muda wa miaka 38.

Jarida la mambo ya biashara la Marekani Forbes lenye kukisia utajiri wa wenye vyao liliwahi kuandika kwamba Obiang ni miongoni mwa wakuu wa nchi wenye utajiri mkubwa laisa kiasi.  Gazeti hilo limeukisia utajiri wake kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 600 ($600m).  Hayo ni matunda ya mafuta yaliyogunduliwa nchini humo 1996.  Hamna shaka yoyote kwamba rais huyo hakuzichuma fedha hizo kwa njia ya halali.  Wizi ndio uliompatia utajiri huo.

Nilikutana na  Obiang safari yangu ya kwanza nilipokwenda nchini mwake.  Alitualika Ikulu, jijini Malabo, sote waangalizi wa uchaguzi na tukapata fursa ya kuzungumza naye na kumsaili kuhusu mchakato wa uchaguzi.

Juzi nilikuwa nikimkumbuka Obiang na madikteta wengine uchwara wa Kiafrika niliowahi kukutana nao.

Maswali kadhaa yalinipitikia kichwani. La msingi ni: nini kinachowaogopesha wakafika hadi ya kuwatesa wananchi wenzao wanaowatala? Kwa nini wanalazimika kutumia nguvu, vitisho, mateso, ghiliba na kila aina ya hila na vitimbi kuyang’ang’ania madaraka?

Tawala za kidikteta hutumia mikakati yenye kufanana ili ziselelee madarakani. Tumeyashuhudia hayo si Afrika tu bali hata katika nchi nyingine zisizo za Kiafrika.  Tawala hizo huanza kwa kutumia vitisho vya kila aina halafu huendelea kwa kuwatia hofu wananchi.  Baada ya hayo, au sambamba na hayo, wananchi huanza kufanyiwa uonevu mkubwa na haki zao za kimsingi hukandamizwa pamoja na heshima na utu wao.  Ishara za hayo ziko wazi Tanzania katika wakati ambapo uchaguzi mkuu unakaribia.

Miongoni mwa ishara hizo ni vitimbi vilivyofanywa na Tume ya Taifaya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) vya kuwaengua kwa sababu zisizo na mashiko wagombea wa ubunge au uwakilishi wa vyama viwili tu: Chadema na ACT-Wazalendo.

Ishara nyingine ni uonevu wa dhahiri aliofanyiwa mwanasheria na mwanaharakati huru Fatma Karume pamoja na jinsi wanavyopakwa tope waandishi wawili wa Kitanzania, Zuhra Yunus na Salim Kikeke, wanaofanya kazi katika shirika la utangazaji la BBC, London.  Hoja zilizotolewa dhidi ya wote watatu ni za kitoto, dhaifu na za kuchekesha.  Dhamira ya watawala ni kuwatisha wao na wengine wasiutumie uhuru wao wa kujieleza na kutoa rai zao.

Kuna tofauti baina ya dikteta aliyekubuhu na dikteta uchwara. Kwa kawaida, tabia ya dikteta uchwara ni kwamba huwa hajichukulii hatua yeye mwenyewe binafsi.  Juu ya kujidai kwake, dikteta uchwara huwa ni mtu aliyejaa woga.  Huwa hana ubavu wa kujifanyia mambo yeye mwenyewe.  Huzoea kutumia watu.  Aghalabu huwa na vibaraka vyake vya kumwitikia “hewala bwana” kwa kila anachotaka vimfanyie.

Watu hao huwa ndani ya chama cha dikteta, kwenye wizara na hata kwenye jeshi la polisi.  Katika miezi ya karibuni tumewasikia wakuu kadhaa wa Jeshi la Polisi la Tanzania wakitamka mambo kwa kibri kana kwamba wao ni makada wa chama kinachotawala.  Tena bila ya kuona haya.  Kujiamini kwao kunawafanya wayaone madhambi wanayoyafanya kuwa ni mambo ya kawaida.

Wanalolisahau ni funzo la mapambano: kwamba kila watawala wanapofanya ngumu kwa kuwakandamiza wananchi ndipo wananchi nao wanapozidi kuwa washupavu kupigania haki zao.  Hofu huwatoka. Hapo ndipo wasemapo “potelea mbali”.  Umma unaposimama pamoja, ukaanza kuimba nyimbo moja ndipo panapoanza kuchomoza ile iitwayo nguvu ya umma.

Ahmed Rajab ni mchambuzi na mwandishi wa habari wa siku nyingi anaweza kupatikana kupitia barua pepe yake aamahmedrajab@icloud.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @ahmedrajab. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. You may find such countries ruled by dictators are members of international organs including uno and it’s affiliated bodies. You ask yourself, what roles do those world bodies play to check dictatorship in accross many countries. Without the representation of opposition organizations in such world bodies dictatorship will never end in the world. Either, leaders of the advanced countries support dictators in return for business relationships through multileteral companies working in countries with dictatorships. It is an ordinary custom to hear voices from advanced countries appraising dictators because of oil and gold. African countries especially those run by dictators wouldn’t agree to introducing multipatism if it were not for the pressure from West, but the West is blind and dumb to leaders running multiparty elections with acute violation of its rules and traditions. The introduction of multi party democracy was internationally groomed and accepted but the running of multiparty elections are internal matter! This voice come from countries run by dictators in Africa especially and the West who forced African countries to accept it are ready to here such nonsense from dictators. I must conclude that dictators in our countries survive because of support from Western countries and China of course.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts