The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kauli Tata Za Viongozi Wetu Zinaijengea Tanzania Taswira Gani?

Jamii yetu imejikita kuangalia viongozi kama watoa dira, kiasi cha hata kusahau au kupuuza kwamba hao viongozi nao ni sehemu ya jamii.

subscribe to our newsletter!

Mwanahistoria Charles Siefert katika kijitabu chake cha mwaka 1938 The Negro’s or Ethiopian’s Contribution to Art anaandika kwamba, watu wasiotambua historia yao, asili na tamaduni zao ni kama mti bila mizizi. Ni wazi kwamba, kwa kawaida, mti usio na mizizi ni rahisi sana kudhoofika na kunyauka.

Tanzania kama nchi, tunapitia kipindi kigumu cha mabadiliko makubwa ya kijamii, kisiasa na kiteknolojia. Siasa za vyama vingi zinapamba moto, wakati huo huo teknolojia ya mawasiliano inaongeza kasi ya watu kupashana habari, hususan kwenye mitandao. Takwimu zinatofautiana, lakini karibu zote zinaonesha ukuaji wa matumizi ya mitandao hiyo.

Tuna changamoto kubwa katika kuhakikisha kwamba, kwanza tunakwenda na wakati tusipitwe na ulimwengu huu mpya. Lakini pia, kwenda huku na wakati kusitufanye tukose dira iliyowekwa na tamaduni zetu nzuri au kukosa nanga iliyowekwa na ustaarabu wa enzi wa kutuwezesha kuvuka ngwe hii kwa umoja wa kitaifa, amani na haki sawa kwa wote.

Napenda kurejea historia. Sitataka kwenda mbali sana. Jamii yetu, kwa kuilinganisha na, kwa mfano za magharibi,  ina muundo wa kuheshimu sana viongozi. Mpaka pengine naona kama kimakosa. Kikondoo.

Kuanzia viongozi wa kifamilia, wazazi, babu na bibi, wajomba, wakubwa wote, mpaka viongozi wa kijamii na kisiasa. Hawa ndio wahifadhi wa utamaduni na watoa muelekeo. Hawa ndio chachu ya kutufundisha. Na maneno yao hutuponya. Sio mara zote tumeheshimu wakubwa, lakini, huu ndio mpangilio wetu.

‘Mkubwa hakosei’

Kuwasema wakubwa kiutamaduni wetu ni nadra. Hii ndiyo maana ya msemo ‘mkubwa hakosei.’ Huu ni msemo ndumilakuwili. Kwa upande mmoja unatafsirika kwa kumkuza mkubwa, kwamba hakosei. Ukiona kakosea inaweza kuwa wewe ndiye umekosea kumuelewa. Atatungiwa hadithi ya ukweli au uongo, ilimuradi aonekane hajakosea. Akikosea, muundo mzima wa kijamii unaanguka. Kwa upande mwengine, msemo huu unabeza dhana hiyo, ila unakuonya kwamba, usishindane na mkubwa, hata kama amekosea, utaumia wewe. Ndiyo maana utasikia watu na akili zao wanasema: “Rais ana nia njema, ila washauri wake ndio wanampotosha.” Ni kama vile rais ni zuzu anayeweza kupelekwapelekwa tu na washauri wake bila kujitambua! Hata rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, aliyesifika kwa hulka ya kusikiliza washauri, alilikataa hili.

Jamii yetu imejikita kuangalia viongozi kama watoa dira, kiasi cha hata kusahau au kupuuza kwamba hao viongozi nao ni sehemu ya jamii. Napenda kuwamulika viongozi wetu, na kauli zao, kwa kutumia historia ya nchi yetu,  dira tulizoachiwa, na jinsi tunavyozienzi au kuzipuuza. Viongozi wetu si Wafalme wa nchi ya Thailand ambako kumsema vibaya kiongozi kidogo tu kunakupa kifungo kikubwa jela kwa mujibu wa sheria za huko. Huko nchini Thailand kwenyewe wananchi wake wanandamana kupinga upuuzi huu wa “mkubwa hakosei.” Imeandikwa katika Biblia — naitaja kama kitabu cha hekima — kwamba, wale waliopewa zaidi, watadaiwa zaidi (Luka 12:48). Wafaransa wanasema Noblesse Oblige. Waswahili wanasema ukubwa gunia la chawa. Viongozi wanatakiwa kuwajibishwa zaidi, kwa kuwa wamepewa dhamana kubwa zaidi. Si kukingiwa kifua zaidi wasisemwe.

Mwalimu Nyerere, rais wetu wa awamu ya kwanza, katika miaka ya mwanzo kabisa ya uhuru wa taifa letu, alijiona katika nafasi ya kutoa muongozo kwa viongozi wetu, hususan mabalozi wetu. Aliona kuna haja ya kuhimiza watumishi wa umma kujenga hoja, badala ya kuzozana. Aliandika kijitabu, kinaitwa “Argue, Dn’t Shout: An Official Guide On Foreign Policy By The President.” Akihimiza umuhimu wa kujenga hoja zaidi ya kupiga kelele. Viongozi wetu leo wanajenga hoja au wanapiga kelele? Wanajenga umoja wa kitaifa kwa kutumia nidhamu katika kujieleza au wanajionesha wamelewa madaraka? Nitatoa mifano michache, kuanzia na ya hapa karibuni tu.

Sumu ya ubaguzi wa rangi

Rais John Magufuli amesema atawasikiliza wanawake weupe zaidi kuliko weusi. Kauli hii inatoka kwa rais wa nchi ambayo, muasisi wake alipiga vita ubaguzi wa rangi kusini mwa Afrika. Mwalimu Nyerere ndiye aliyeanzisha mgomo wa kugomea bidhaa za Afrika ya Kusini ya kibaguzi, dunia ikamfuatisha. Kama sisi tunasahau, wanahistoria wa dunia bado wanakumbuka. Tumetokaje kuwa na rais aliyeongoza dunia kupinga ubaguzi wa rangi, mpaka kuwa na rais anayewagawa raia wake mwenyewe kwa ubaguzi wa rangi? Ukihoji utaambiwa: “Anatania tu”, au: “Ndivyo alivyo tu.” Anatania tu kwenye jambo nyeti kama hili mtu wa “Hapa Kazi Tu”?

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama, tarehe 21 Oktoba 2020 alikemea maneno ya ovyo ya Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump, kwa kueleza kwamba maneno ya rais yana uzito mkubwa sana, na wananchi hawatakiwi kusema rais ndivyo alivyo tu! Mizani hii inafaa kutumika kwa viongozi popote duniani.

Mwanamuiziki wa Jamaica, Buju Banton, katika miaka ya mwanzo ya tisini, ilimbidi awaombe radhi wanawake weusi wa Jamaica, kwa sababu aliimba wimbo “Love Me Browning” uliosheherekea mapenzi yake kwa wanawake wenye ngozi iliyoelekea weupe zaidi huko kwao. Wajamaica wakaja juu mpaka akaomba radhi na kuimba wimbo mwingine  “Love Black Woman” kuwapoza waliomkosoa. Sasa Tanzania kama nchi rais wetu anapopimwa kwa mizani iliyo chini ya mizani ya kumpima mwanamuziki wa Jamaica, jambo hilo linasema nini kuhusu uongozi wetu? Linasema nini kuhusu mizani inayotumiwa na jamii kuupima uongozi?

Makamu wa rais Samia Suluhu amewaambia wananchi kwamba “hata ukipiga kura kule kwingine, Chama cha Mapinduzi [CCM] kinakwenda kuunda serikali.” Kwa ufupi anajitapa wananchi wakiipigia kura CCM au wasipoipigia, itashinda tu. Hakuna mantiki inayoweza kuzuia kauli hii isiwe na ama tambo zinazoegemea wizi wa kura., ama kumfanya Makamu wa Rais awe mrithi wa mikoba ya utabiri ya Sheikh Yahya Hussein. Mwanasiasa makini anaomba kura kwa unyenyekevu, hizi tambo ni kukosa sifa za unyenyekevu kwa wananchi.

Vijana na mafunzo ya uongozi

Mara baada ya kifo cha Mzee Reginald Mengi, Katibu Mkuu wa CCM Bashiru Ally aliongea kuhusu umuhimu wa kuwalea vijana kushika uongozi. Bashiru Ally alikiri kwamba kazi hii haijafanywa. Akasema tunaanza kuvuna matunda ya kutowaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora, watiifu, wakweli,  wanyenyekevu, na wenye heshima. Bashiru Ally alitumia fursa hiyo kumuonya na kumuombea msamaha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, yumkinika kuhusiana na tazia yake mbaya iliyowachafua Watanzania wengi. Kitu ambacho hakusema Bashiru ni, kutowaandaa huku viongozi kumeanza lini? Utawala wa Nyerere? Ali Hassan Mwinyi? Benjamin Mkapa? Jakaya Kikwete? Au Magufuli? Matatizo ya Magufuli kutumia lugha yenye kuonekana kuwa na utata ni sehemu hii ya uongozi kukosa maandalizi? Je, mapungufu tunayoyaona mpaka kwa rais wa sasa katika maadili na kauli ni sehemu ya kutoandaa viongozi huku alikokusema Bashiru Ally? Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Polepole aliposema kwamba CCM viongozi wote wana magari aina ya V8, tambo hizo ambazo hazizingatii umasikini mkubwa wa Watanzania wengi, tambo hizo ni sehemu ya viongozi wa CCM kukosa maandalizi?

Awali nilipokuwa mdogo, nyumbani tulikuwa na televisheni. Tukiangalia Televisheni ya Zanzibar (TVZ). TVZ wakati inasitisha matangazo yake ya siku, TVZ, sasa Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), ilikuwa na kaulimbiu yake: Mapinduzi Daima. Nilipata tabu sana kuielewa kaulimbiu ile. Nikajiuliza, hawa watu wanataka kuuana kila siku katika mapinduzi?

Baadaye, nilipomsoma George Wilhelm Friedrich Hegel, nikaja kugundua kwamba, “Mapinduzi Daima” ni kaulimbiu iliyoendana na “Hegelian dialectics.” Kiufupi mambo yanatakiwa kufikiriwa upya na kupinduliwa kila wakati.

Hegel aliandika kwamba: “Serikali hazijawahi kujifunza chochote kutoka historia, au kujiendesha kutokana na kanuni zilizotoholewa kutoka historia.” Hili lina mjadala mkubwa wa kifalsafa. Lakini, kwa Tanzania, maneno haya ya Hegel, ukiondoa leseni ya ushairi kwenye “chochote”, inaonekana serikali yetu haijifunzi mengi kutoka historia. Vinginevyo tungewezaje kutoka kuwa nchi inayoheshimika na kuongoza dunia na kuwa nchi ya rais msema ovyo anayechekwa na wengine?

Sote tuna wajibu wa kukumbushana historia. Na zaidi, tuna wajibu wa kuzishurutisha serikali zitambue umuhimu wa historia katika kuchanja njia itakayotupeleka mbele katika muelekeo utakaotufaa. Ni wakati sasa wa kushurutisha viongozi wetu wawajibike kwa kila namna, kukataa ukondoo. Kuanzia kauli mpaka vitendo. Hususan kwa kutumia haki ya kikatiba ya kupiga kura.

Katundu Kassim ni mchambuzi wa masuala ya siasa na teknolojia nchini Tanzania. Anapatikana kwa barua pepe yake ambayo ni katundukassim1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi maoni ya The Chanzo Initiative. 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *