The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ally Saleh: Usiku wa Dk Mwinyi Utakuwa Mrefu Sana

Dk Mwinyi alisema anataka apate ushindi ambao hauna mabishano. Ukweli ni kwamba ushindi wake wa asilimia 76 una mabishano makubwa na utaendelea kuwa na mabishano.

subscribe to our newsletter!

Dk Hussein Ali Mwinyi ameshika uongozi wa Visiwa vya Zanzibar kwa miaka mitano. Ni muda wa kikatiba kwa nafasi hiyo. Ila naamini itakuwa miaka yake mitano mirefu kabisa katika umri wake. Najua ameshika vipindi kadhaa vya ubunge vya miaka mitano mitano. Ila muda huu utakuwa mrefu na kutamani  uishe. Lakini nina hakika pia itakwenda polepole sana, mpaka itamkirihi. Ni kama kusema usiku wake utakuwa mrefu sana.

Nasema itakwenda polepole kwa sababu naona kuna vitu vingi sana vitamkabili katika kipindi chake, vitamuelemea kupita vile vilivyowaelemea viongozi wengine wa Zanzibar ambao tunajua kwamba katika kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi, ushindi wao au uingiaji wao madarakani, umekuwa wa kuuliza, tuseme wa kubishaniwa.

Si kwa Dk Salmin Amour, si kwa Dk Amani Karume, si kwa Dk Ali Muhammed Shein na wala si kwa yeye Dk Mwinyi ushindi umekuwa wa kutizama mwezi, ushindi wa kusubiri taarifa ziso na uhakika kwa maneno mengine. Pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa chama kishika dola, lakini ushindi wake katika chaguzi za Zanzibar una masuali mengi. Upinzani Zanzibar kwa kweli umepunjwa chaguzi zote.

Ushindi usiokuwa na mabishano

Dk Mwinyi alipochaguliwa kuwa mbeba bendera wa CCM mwaka huu wa 2020 alisema anataka apate “ushindi ambao hauna mabishano.” Ukweli ni kwamba ushindi wake wa asilimia 76 una mabishano makubwa na utaendelea kuwa na mabishano. Yaani kwamba Maalim Seif Shariff Hamad, mgombea uraisi wa Zanzibar kupitia tiketi ya ACT-Wazalendo, amepata asilimia 19 hilo jambo litabishiwa sana.

Hiyo ni sawa pia kuwa tutaendelea kutoamini kuwa ushindi wa CCM wa majimbo 48 Unguja na Pemba, au wa majimbo 14 huko Pemba tunaubishania sana. Tukianza kwa hila za ushindi wa mezani wa pingamizi na kumalizia kwa  yaliotokea Oktoba 27 na 28, 2020. Kuwa Kura ya Mapema ilitumika kupata ushindi wa mapema nalo pia litaendelea kubishaniwa maisha yote ya siasa za Zanzibar.

Na hilo ndiyo la kwanza litakalofanya usiku wa Dk Mwinyi uwe mrefu maana sisi wapinzani, husuani sisi wa ACT-Wazalendo, kwa miaka yote mitano atayokuwa kitini tutakuwa tunaendelea kusema, akipenda asipende, kwamba ushindi wake umetokana na kupokwa sisi wapinzani. Hilo la usiku mrefu litaanzia hapo.

Maana sisi tutaendelea kuamini kuwa kila njia imefanywa kuibeba CCM katika uchaguzi wa mwaka huu. Hapatakuwa na yeyote wa kutunyamazisha kulisema hilo, kila tutakapolipatia fursa au kila tutapoona inafaa. Kwa hiyo usiku wa Dk Mwinyi utakuwa mrefu na itamlazimu ajifunze kuvumilia hili au kutustahamilia maana tutakuwa na uhuru wetu wa kikatiba.

Upinzani hauwezi kufa

Au asipoutaka au kuweza kuvumilia atataka kutumia nguvu au nafasi yake ya dola, na hilo pia litakwenda kupelekea usiku wake uzidi kuwa mrefu.  Au atataka kuchagua kutufunga midomo kwa kuzuia mikutano ya hadhara kwa kipindi cha miaka mitano. Kumbe tusiposema ghadhabu inazidi kuwa kubwa.

Usiku utakuwa mrefu maana anaweza Dk Mwinyi kuchagua kutunga sheria za kutunyamizisha kwa sababu chama chake kina wingi wa Wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi, lakini akichagua hilo basi pia usiku wake utakuwa mrefu maana hatutanyamaza.

Pengine pia inawezekana akashawishika kukubaliana na wenziwe ndani ya CCM kuwa upinzani kote Tanzania haufai kuendelea kuwepo, na kwa hivyo kutungwa sheria katika Bunge la Muungano kuwa vyama vya siasa vikatwe uhai wao. Hilo pia litakuwa na furaha ya muda, maana pia usingizi utakata na usiku utakuwa mrefu.

Hata hivyo, upinzani hauwezi kufa na zaidi huku Zanzibar ambako siasa imo ndani ya damu ya wananchi. Utakuwa mtihani mkubwa kwa CCM kujaribu kuamini kuwa kilichotokea 2020 ni kwa kuwa wamekubalika na kura walizopata ni za kukubalika kwao, na wakadhani wanaweza kubaki peke yao katika rubaa za siasa kote Bara na Zanzibar. Zanzibar upinzani ni jadi, na  bado utaendelea kuwa hivyo.

Usiku wa Dk Mwinyi utakuwa mrefu pia kama ataona mateso makubwa waliopitia wapinzani mwaka huu wa 2020 kwa sababu ya nia yao ya kuzuia walichohisi ni kuporwa uchaguzi uliokuwa na mwelekeo mkubwa wa kushinda. Hili hakuna la kuwageuza.

Watu 13 wanadaiwa kupoteza maisha. Watu kadhaa wamedaiwa kupigwa risasi. Watu kadhaa wamefanyiwa mateso kadhaa wa kadhaa. Akikaa peke yake katika usiku wake haya yatampitia Dk Mwinyi na hapana shaka usiku wake utakuwa mrefu.

Matumizi ya nguvu dhidi ya raia

Akiwa katika usiku wake Dk Mwinyi anaweza kuwaza sababu kadha wa kadha za kuhalalishwa matumizi ya nguvu dhidi ya raia, lakini kila atakapotafakari zaidi ndipo usiku wake utapokuwa mrefu zaidi, maana yaliyopita ni makubwa sana, sema basi tu na atawaza iwapo roho hizo au mateso hayo, yapite tu bila fidia?

Dk Mwinyi anaweza akaona picha ya Ismail Jussa, mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ACT-Wazalendo, alivyopigwa mikononi mwa polisi na kujeruhiwa bega na akiuguza mguu akiwa Nairobi, Kenya. Picha ya yule mama wa Garagara, Daraja Bovu, wa miaka 75 tena mgonjwa wa baridi, ambapo bomu la machozi lilorushwa ndani ya nyumba na chumba na kitanda chake na kujeruhiwa vibaya Au habari ya Nassor Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, aliyekamatwa na kushikiliwa pamoja na wanachama wengine wa chama hicho wapatao 15 kwa zaidi ya siku ishirini bila kufikishwa mahakamani, na baadaye kuachiwa kwa dhamana.

Atakuwa akifikiria miaka mitano ijayo kama anataka kurudi, hivi kweli haya yaliyofanyika mwaka huu yataweza kurudiwa tena? Au ACT-Wazalendo watasokotwa kama kilivyosokotwa Chama cha Wananchi-CUF na wakibaki watakuwa na nguvu zilizoiziba pumzi CCM mpaka wakaja na mbinu walizokuja nao, wakijua kuwa kwa njia hio ndio wamepona?

Upinzani Barazani, Serikalini

Pale 2015 mbinu ya CCM ilikuwa ni kubatilisha matokeo, 2020 ikawa ni kuchukua mchana kweupe na bila ya shaka mbinu za 2025 zitaanza kupangwa na usiku wake utakuwa mrefu hayo yakienda katika akili yake, maana atakuwa na mawazo kuwa atataka kugombea muhula wa pili, penye uhai na uzima.

Wala urefu wa usiku hautapungua kwa kuwa ACT-Wazalendo  wataingia kwenye Baraza la Wawakilishi au pia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tutaendelea kukosoa Serikali yake kwa maslahi ya umma, sio lazima ya kisiasa.

Hilo la kuingia Serikalini, ambalo ni la kikatiba, halitabadilisha urefu wa usiku wa Dk Mwinyi maana ACT-Wazalendo wakiwemo ndani ya Baraza la Wawakilishi na nje ya Baraza au ndani ya Serikali wataendelea kudai uchaguzi wa 2020 umeibiwa kutoka kwao na watakuwa wakiendelea kujipanga kwa 2025, maana bado wengi tunaamini kuondoka CCM ni suala la wakati tu.

Tuombe Dk Mwinyi apate usingizi wa amani na kama kutakuwa na malepelepe yawe ya afueni maana atakuwa na kazi ya kuiongoza Zanzibar katika muda huo pia.

Ally Saleh ni mwandishi wa habari wa zamani, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwanachama wa ACT-Wazalendo. Saleh pia alikuwa Mbunge wa Malindi kwenye Bunge la 11 kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi – CUF. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni allysaleh126@gmail.com.  Anapatikana Twitter pia kupitia @allysalehznz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts