The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ally Saleh: Nilichokisema Kura Ya Mapema Kimekuwa

Msingi wa sintofahamu ya kisiasa ya Zanzibar kwa sasa ni upigwaji wa Kura ya Mapema ambayo viongozi na wafuasi wa ACT-Wazalendo waliipinga wakihisi imewekwa kupora ushindi wao lakini mamlaka zikapuuza kilio hicho. 

subscribe to our newsletter!

Kuelekea Uchaguzi Mkuu Zanzibar, hususan karibu na Kura ya Mapema iliyokuwa imepangwa kufanyika Oktoba 27, 2020, siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 28 Oktoba, 2020, niliamua kumuandikia barua ya wazi Rais John Magufuli kutaka aingilie kati kura hiyo isifanyike, kwanza kwa sababu imegubikwa na utata mwingi lakini pili ni kukosa kwake mantiki.

Kura ya Mepema ilianzishwa mwaka 2018 kufuatia mabadiliko madogo kwenye Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuweka utaratibu kwamba wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wa kituo, askari polisi na watendaji wa Tume ya Uchaguzi wapige kura mapema, ambayo kwa Uchaguzi wa mwaka huu ilifanyika Octoba 27, ili wapate nafasi ya kusimamia zoezi la upigaji kura vizuri. Katika barua hiyo ya wazi, nilionya hatari ya kura hiyo kuwa chanzo cha fujo kwani tayari viongozi na wafuasi wa chama cha ACT-Wazalendo walishadhamiria kwamba watajaribu kuizuia wakihisi imewekwa kupora ushindi wao.

Kumbe nilisahau kuwa Rais Magufuli pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na hivyo ushindi wa chama chake Zanzibar ni wa muhimu na lazima. Hii inamaanisha kwamba yote niliyotahadharisha kwenye barua yangu hiyo ya wazi niliyoichapisha katika mtandao wa Facebook hayakufanyiwa kazi. Matokeo yake ni kwamba kile nilichohofia kutokea, kimetokea.

Madai ya watu kuuwawa, kujeruhiwa

Kwa taarifa zilizopo, zilizotolewa na Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, jumla ya wananchi wapatao 13 wanashukiwa kuuwawa kwa kupigwa risasi katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar. Jumla ya watu wengine wapatao 102 wanadaiwa kujerehiwa kwa kupigwa risasi, mabomu na vipigo na watu wanaosadikika kuwa ni wanajeshi. Wanachama wa ACT-Wazalendo wapatao 199 wadaiwa kukamatwa na kushikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar. Licha ya kwamba mamlaka visiwani Zanzibar zimekuwa zikikanusha uwepo wa matukio haya, picha na video zinazosambaa mitandaoni zinaonesha kwamba hali si shwari kama mamlaka zinataka kutuaminisha.

Ni maoni yangu kwamba matukio yote haya yanatokana na uwepo wa utaratibu mpya wa Kura ya Mapema na jitihada za wafuasi wa vyama vya upinzani, husasani ACT-Wazalendo, kutaka kuizuia. Kabla ya hata mchakato wa uchaguzi kuanza, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na mgombea uraisi wa Zanzibar kupitia chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad alisema kwamba kama kutakuwa na upigaji wa kura ya mapema basi na yeye atashiriki na kuwataka wafuasi wake wafanye hivyo. Kwa kauli hiyo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilimsimamisha Maalim Seif kufanya kampeni kwa siku tano, ikiita kauli hiyo ya kichochezi.

Kufuatia kauli hiyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar Awadh Juma Haji alionekana kwenye video akitishia watu wasioruhusiwa kushiriki katika kura hiyo kwamba watapigwa kama mbwa mwitu. Maalim Seif hakuweza kushiriki kwenye upigaji kura hiyo ya mapema kwani polisi mjini Zanzibar walimkamata wakati akiwa njiani akielekea kituoni. Na vivyo hivyo wafuasi wengi wa ACT-Wazalendo hawakuweza kufanya hivyo kama Mwenyekiti wao alivyowataka.

Kama nilivyoandika kwenye barua hiyo ya wazi kwamba pamoja na viongozi na wanachama wa ACT-Wazalendo wamehasishana kujitokeza kwenda kupiga kura hiyo ya mapema vyombo vya ulinzi na usalama visingeliruhusu hilo na ambacho kingetokea ni maafa.

Barua kwa Raisi Magufuli

Hii hapa barua ya wazi niliyomwandikia Raisi John Pombe Magufuli nikimtahadharishe juu ya hatari zinazoambatana na Kura ya Mapema. (Barua hii imehaririwa ili iweze kusomeka kwa urahisi).

Mheshimiwa Raisi, pole na kampeni ambayo najua kwamba imekuwa ngumu na ya ushindani mkubwa. Nimeamua kuandikia barua ya wazi kwako kwa sababu kadhaa ukiachana na ile ya kuwa sina njia nyengine ya kukufikia hasa kwa udharura kwa jambo ninalotaka kukufikishia. Sababu ya kwanza ni kutimiza wajibu wangu wa kikatiba kama mwananchi kusemea jambo ambalo lina maslahi na nchi. Pili ni ni kuweka rekodi kuwa tupo tuliopaza sauti juu ya jambo hili lakini pia kujaribu kushawishi kuchukuliwa hatua madhubuti juu ya jambo hili. Na jambo lenyeweni ni Kura ya Mapema.

Mheshimiwa Raisi, sitaki kuamini ukiwa ni Raisi wetu, Amiri Jeshi Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hujui kinachoendelea kwenye suala zima la Kura ya Mapema . Hata hivyo nimechagua kukupa shaka ya kutokujua, au benefit of doubt kama wasemavyo kwa Kiingereza.

Mheshimiwa Raisi, mimi na wenzangu wengi tunajua na tunakiri suala hili lipo kisheria. Hata hivyo, shaka yetu, au yangu, ni kwamba suala lenyewe limekosa uhalali na nguvu ya kisheria, au legitimacy and legality kwa kimombo, katika namna linavyotekelezwa. Napata mashaka kwamba utaratibu huu wa kura ya mapema umewekwa kukazia kauli ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk Bashiru Ali kwamba yoyote aliyepo madarakani atakuwa mjinga asipotumia dola lililopo mkononi mwake kubaki madarakani.

Mheshimiwa Raisi, yeyote yule aliyewaza huu mpango unaoendelea hivi sasa juu ya matumizi ya Kura ya Mapema hakuwaza kwa upana na kwa kina. Halikadhalika kwa wale watu wanaoshiriki kwenye kufanikisha utaratibu kuanzia mwanzo hadi leo. Kama ni mchezo wa chess basi ni kwamba walipanga mezani hatua zao zote mpaka kumteka Malkia, bila ya kutaka kujua kutakuwa na changamoto kadhaa pamoja na kuwa upande wa pili wana mbinu, fikra na mkakati yao.

Mheshimiwa Raisi, wapangaji wa mkakati wa Kura ya Mapema walichojua wao ni kuweka msingi wa kupata kura 7,000 za kutangulia kwa CCM dhidi ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kwa kura za Oktoba 27, 2020. Lakini ACT-Wazalendo wanajua kuwa kinachopangwa ni kura 14,000 kwa sababu wapiga kura hao 7,000 wa Oktoba 27 bila ya chembe ya shaka watapiga tena Oktoba 28, 2020.

Mheshimiwa Raisi, ACT-Wazalendo wanajua kuwa hiyo ndiyo njia pekee CCM wanaweza kulazimisha ushindi. Uchaguzi wowote ambao utahitaji wale wenye haki tu, yaani Wazanzibari, kupiga kura, uchaguzi wowote wa kura moja mtu mmoja, uchaguzi wowote wa kila kura kuhesabiwa bila kuchezea matokeo, CCM haina nafasi kabisa.

Mheshimiwa Rais, kwamba CCM  haina nafasi ya kushinda Zanzibar siyo la leo. Ndiyo maana kauli za “hatutoi nchi” au “tumeshinda kwa bunduki hatotoi kwa vikaratasi”  na kauli kama hizo zimekuwa zikitolewa zaidi ya mara moja na makada wa CCM Zanzibar kana kwamba chama chenye hati miliki ya Zanzibar ni CCM  pekee. Naelewa sana nikikuambia CCM haiwezi kushinda Zanzibar utakuwa unaumia, maana una wajibu wa kichama kukihakikishia chama chako ushindi kama mwenyikiti wake taifa. Ila nakupa tena benefit of doubt kuwa hujui kwamba ushindi unaousimamia umeingizwa wizi na magube, lakini ujue huo ndio ukweli.

Mheshimiwa Raisi likitokea la kutokezea kuhusiana na utaratibu huu wa Kura ya Mapema ni muhimu kukukumbusha kwamba vitendo hivyo ni lazima vitaambatana na uwajibikaji. Maana iwapo kama katika watu 7,000 watakaopiga kura kuna watu pengine nusu yao watatoka Tanzania Bara maana yake kama Mwenyekiti wa CCM umesimamia kuvunja Katiba ya Zanzibar ambapo mpiga kura ni lazima awe Mzanzibari.

Mheshimiwa Raisi, kwa hali nionavyo viongozi wetu wa ACT-Wazalendo wazi wazi wamehamasisha wanachama na wananchi wajitokeze kwenye Kura ya Mapema ya Oktoba 27, 2020. Siamini kama vyombo vyako havijakueleza hali halisi. Pia sitaki kuamini kuwa washauri wako wanakwambia kila kitu kiko sawa na kura hio itapigwa kama ilivyopangwa na bila athari wala madhara. Nakuomba usiwaamini.

Mheshimiwa Raisi, upinzani umeonewa sana, umedhulumiwa mara nyingi lakini unasema un’yan’ganyi wa mara hii hawatauvumilia. Maana yake kama Kura ya Mapema itapigwa kwa vyovyote vile na kura ya Octoba 28 itapigwa pia tusijidanganye kuwa matokeo yatakuwa na legality na legitimacy. Hii maana yake ni kwamba miaka mitano itakayofuata itakuwa ni miaka ya mizozo  kwa Zanzibar na kusema kweli hilo halina faida kwa mtu yoyote.

Mheshimiwa Raisi, ni maoni yangu kwamba chama cha ACT-Wazalendo hakitasusia Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini kutakuwa na faida gani katika hali hii tunayoelekea? Ndugu Raisi, Zanzibar iko pahala pabaya sana na una wajibu wa kuinusuru kuingia katika mgogoro. Binafsi sioni kama Kura ya Mapema ikiondoshwa kutakuwa na kasoro yoyote kwenye mchakato wa uchaguzi.

Mheshimiwa Raisi, njia yoyote ya kutumia nguvu kulazimisha Kura ya Mapema ipigwe  haina mantiki.  Hoja kwamba ni jambo la kisheria imevurugwa kwa kuingia na wapiga kura wasiotambuliwa na sheria. Kama kiongozi mkuu wa taifa hili, una uwezo wa kuinusuru Zanzibar na machafuko yasiyo na faida yoyote. Una saa 72 mikononi mwako [ya kuondosha Kura ya Mapema] na mimi nakuomba, nakusihi, uone namna unavyowea kurekebisha hali ya mambo.

Mheshimiwa Raisi, mimi na wewe hapa tuweke U-CCM wako na U-ACT-Wazalendo wangu pembeni kwa maslahi mapana ya Zanzibar maana uchaguzi utaisha na sisi tunaitaka Zanzibar yetu nzima  na wala si vipande vipande. Nitafurahi kama utapata wasaa wa kuisoma barua hii, na kama itakupendeza, ufanyie kazi ushauri huu kutoka kwa raia wako.

Ally Saleh ni mwandishi wa habari wa zamani, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwanachama wa ACT-Wazalendo. Saleh pia alikuwa Mbunge wa Malindi kwenye Bunge la 11 kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi – CUF. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni allysaleh126@gmail.com. Anapatikana Twitter pia kupitia @allysalehznz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ndugu yangu Ally Saleh, mwana fani mwenzangu wa tasnia ya habari na mwanasheria, nilisoma barua yako kwa JPM kabla ya uchaguzi na leo nimesoma tena maoni yako kwa kilichotokea Zanzibar kwenye uchaguzi huu.

    Kwanza pole sana na wewe kwa juhudi zako binafsi kuepusha shari, na poleni ndugu zetu Wazanzibari kwa kilichotokea, ikiwemo kuugharimikia uchaguzi mkuu wenu kwa machozi, jasho na damu, maadam this time ushahidi wa picha na video zipo, I hope this time mtafanya the right thing na sio kuishia kupiga tuu kelele kama uchaguzi wa 2015 ambapo niliuliza
    https://www.jamiiforums.com/threads/zanzibar-issue-kwanini-watu-wanapiga-kelele-tu-bila-kuchukua-hatua-zozote.974722/

    Kupitia matokeo ya NEC ya uchaguzi Mkuu wa 2015, yameonyesha mgombea wa CCM, Dr. John Pombe Joseph Magufuli, hakushinda Zanzibar, aliyeongoza kwa kura za Wanzanzibari kwenye uchaguzi wa rais wa JMT, ni mgombea wa upinzani, Edward Lowassa, na wapiga kura ni wale wale, then by proxy, kama uchaguzi wa Zanzibar usingefutwa, then CCM ingeshindwa na mshindi angekuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad
    https://www.jamiiforums.com/threads/imethibitishwa-pasi-na-shaka-kuwa-ni-kweli-kabisa-zanzibar-maalim-seif-na-cuf-ndio-walioshinda.1001701/

    Kutokana na matokeo hayo, then kuna possibility siku zote huwa anashinda lakini hapewi, jee mliwahi kufanya utafiti kwanini mtu wenu huwa anashinda lakini hapewi, ili kabla hamjaingia kwenye uchaguzi mwingine tena, mjiridhishe kuwa hizo sababu sasa hazipo, hivyo this time akishinda atapewa?.

    Mimi ni member wa mtandao maarufu wa Jamiiforums na japo nina chama, lakini naandika kama mchambuzi huru, hivyo kabla ya uchaguzi kule jf niliandika bandiko hili
    https://www.jamiiforums.com/threads/mwana-jf-be-the-first-to-know-kuwa-ccm-ndio-mshindi-wa-jumla-wa-uchaguzi-huu.1803177/

    Kwenye bandiko hilo, nilisema
    ” kama Mwana JF, be the first to know kuwa CCM ndio inakwenda kushinda uchaguzi mkuu huu kwa a landslide victory ya ushindi wa kishindo, kwa pande zote mbili za Muungano!.

    Ushindi huu ni kufuatia mimi mwana JF mwenzenu, Pasco Mayalla, nimesikia sauti ndani ya moyo wangu, yaani voices from within, kuwa katika uchaguzi huu, mshindi ni CCM!. Hii voices from within, is never wrong, maana ni sauti yake YEYE mwenyewe!

    Kwa upande wa Tanzania Bara, CCM itashinda kwa kishindo kwasababu ya track record ya Magufuli, itaibeba CCM na kushinda kwa kishindo.

    Kwa upande wa Zanzibar, kwa mujibu wa katiba, rais wa Zanzibar ni mjumbe wa cabinet ya JMT, Muundo wa serikali ya JMT, hatuna serikali ya mseto, ushindi ni by a simple majority, hata akishinda kwa kura moja, ni mshindi, and the winner takes it all. Hivyo mshindi wa Zanzibar lazima iwe ni CCM!”

    Nilimaliza andiko langu kwa maneno haya
    “Nawatakia maandalizi mema ya October 28, sio kwenda kuchagua, bali kwenda tuu kuthibisha kilichochaguliwa tayari kwa ajili tuu ya kukamilisha taratibu za mchakato wa kukamilisha uchaguzi, kama ni kuchagua, watu siku nyingi, wameisha chagua mioyoni mwao, tarehe 28 ni kukamilisha tuu taratibu”.

    Sasa kwa vile hayo yametokea na sio mapya, na uchaguzi umekwisha, uchaguzi mwingine ni 2025, na kwasababu hakuna kitu kingine chochote kinachoweza kufanyika sasa kubadili matokeo, nakushauri, washauri chama chako, hata kama mmedhulumiwa na hamjaridhika na matokeo, ili kuweza kuendelea na mapambano, tumieni kanuni ya ” If you can’t beat them,
    join them”, kanuni hii hutumika kwenye vita, ukiona unashindwa au anaelemewa, kuliko kuendelea ku fight and be wiped out, sometimes it’s wise to retreat kwenda kujijenga upya, or to surrender and join them. Hivyo natoa wito kwako na chama chako, yaliyopita sii ndwele, kubalini matokeo, join them na kutoa ushirikiano, pelekeni jina la Makamu wa Kwanza wa rais, na majina 2 ya mawaziri kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa, muijenge Zanzibar yenu.

    Kwa kuendelea kususa, you have everything to loose and nothing to gain, your will be wiped out completely and buried 6ft under!, hivyo there will be no one at all uchaguzi wa 2025, hivyo ni busara to join them for survival hadi 2025.

    By joining them, you’ll have everything to gain and nothing to loose, yaliyopita sii ndwele, gangeni yaliyopo na yajayo. The choice is yours.
    I wish you all the best.

    Your Media Comrade, and fellow Learned Brother
    Pasco.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *