The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mambo Kumi Muhimu Kuhusu Baraza Jipya La Mawaziri

subscribe to our newsletter!

Jioni ya Disemba 5, 2020, Katibu Mkuu Kiongozi aliujulisha umma wa Watanzania juu ya uteuzi  uliofanywa na Raisi John Magufuli katika kukamilisha safu yake ya Baraza la Mawaziri. Teuzi zilizofanywa jana zimefanya Baraza la Mawaziri kuwa na jumla ya mawaziri 23 na manaibu waziri 23. Ili kukuwezesha kuelewa safu hii ya mawaziri, The Chanzo tumekuandalia mambo kumi ya muhimu kuhusu baraza hili.

Jambo la kwanza ni kwamba kati ya mawaziri 23 walioteuliwa wanawake ni wanne, na kati ya manaibu waziri 23 walioteuliwa wanawake ni sita. Hii inafanya jumla ya wanawake kwenye baraza zima kuwa 10, sawa na asilimia 21 ya baraza lote. Katika baraza lililopita idadi ya mawaziri wanawake ilikua ni wanne kama ilivyo sasa.

Pili, mawaziri 17, sawa na asilimia 73, walikuwepo kwenye baraza lililopita, huku mawaziri wapya wanne wakiwa wametokea kwenye nafasi za Ukatibu Mkuu wa wizara katika baraza lililopita. Kwa upande mwingine, mawaziri wawili ni wapya kabisa hii ikijumuisha Mashimba Mashauri Ndaki atakayekuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Geoffrey Idelphonce Mwambe aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) atakayekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Tatu, jumla ya Manaibu Waziri 18, sawa na asilimia 78, wanaingia kwenye baraza kwa mara ya kwanza huku kati yao manaibu waziri 16, sawa na asilimia 69.5, wakiwa ni wabunge kwa mara ya kwanza Bungeni. Manaibu waziri watano walikuwa pia kwenye baraza lililopita.

Nne, kiwango cha elimu kwa Baraza la Mawaziri kinaanzia shahada mpaka uproffessa. Kuna jumla ya mawaziri wawili wenye shahada, mawaziri 13 wenye shahada ya uzamili  (Masters), mawaziri wanne wenye shahada ya uzamivu(PhD) na mawaziri wanne wenye ngazi ya elimu ya uprofesa.

Tano, kiwango cha elimu kwa upande wa  manaibu waziri kuna mawaziri nane wenye shahada ya uzamili(Masters), mawaziri 13 wenye shahada na na naibu waziri mmoja mwenye shahada ya uzamivu(PhD).

Sita, wastani wa umri wa mawaziri ni miaka 51, huku waziri Juma Aweso akiwa ndio waziri mdogo kabisa kuliko wote, akiwa na umri wa miaka 35, na Waziri George Mkuchika akiwa ndiyo waziri mkubwa zaidi kwa umri wa miaka 72.

Saba, wastani wa umri kwa Manaibu Waziri ni miaka 42, huku naibu Waziri Ummy Nderiananga akiwa ndio Naibu Waziri mdogo kabisa, akiwa na umri wa miaka 28. Katika baraza lote, Naibu Waziri Ummy Nderiananga ndio waziri mdogo zaidi kuliko wote.

Nane, manaibu waziri watano ni wanachama wa zamani wa chama cha upinzani cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokihama chama hicho na kukimbilia CCM katika kipindi cha 2015-2020. Huku waziri mmoja, Profesa Kitila Mkumbo akiwa ni mwanachama wa zamani wa ACT-Wazalendo.

Tisa, jumla ya mawaziri wanaotoka visiwani Zanzibar ni wawili, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Khamis Hamza Khamis na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mwanaidi Ali Khamis.

Kumi, wizara mpya imetambulishwa rasmi katika baraza hili ambayo ni Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itakayoongozwa na Dk Faustine Ndugulile. Wizara hii inategemewa kwenda kuondoa mkanganyiko uliokuwepo kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wizara ya Habari, hasa kwenye mambo kama Kamati ya Maudhui iliyokuwa chini ya TCRA lakini ikiwajibika kwa Waziri wa Habari.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts