Kwa Nini Watalii Wengi Wanaotembelea Tanzania Hawarudi Tena?

Tufungue madawati ya utalii kwenye balozi zetu na kila mwaka balozi husika ieleze imeleta watalii wangapi nchini
Thadei Ole Mushi30 December 202034 min

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Aloyce K. Nzuki amewachukua wahariri wa vyombo vya habari na kwenda nao Ngorongoro kujadili kwa nini watalii wakishakuja kutalii Tanzania hawarudi tena.

Kwa mujibu wa kinywa chake, Katibu Mkuu wa wizara hiyo alisema kwamba kati ya watalii wanaokuja kutalii Tanzania, asilimia 80 ni wageni wapya kabisa ambao hawakuwahi kufika Tanzania wakati asilimia 20 tu ndiyo huwa wanarudi kuja kutalii tena.

Dk Nzuki akawaachia swali hilo waandishi wajadili kwa nini hiyo asilimia 80 ya waliokwisha kutalii Tanzania hawarudi tena. Kwa sasa waandishi wetu wanasugua vichwa huko mbugani kutafuta ni kwa nini watalii wakishakuja Tanzania hawarudi tena.

Dk Nzuki anaamini kuwa waandishi wetu kama wakiandika vizuri nchi yetu basi watalii watakuja kwa wingi. Akinukuliwa na tovuti ya habari ya Michuzi Blog, Dk Nzuki alisema: “Wanahabari mnalo jukumu kubwa katika jamii hasa kwa kuandika habari za kujenga taswira chanya itakayosambaa duniani kote na kuvutia watalii kote duniani.”

Kabla sijaanza tafakuri yangu nilijiuliza hawa waandishi wetu wanasomwa nje ya nchi kweli? Maudhui wanayoandika yanavutia watu kusoma? Juzi juzi nilikuwa najisomea magazeti bora Afrika ambapo gazeti la Daily News la Tanzania lilijitokeza nafasi ya 50. Hii maana yake ni kwamba gazeti hilo halisomwi sana. Lakini tujaribu kumsaidia Katibu Mkuu baadhi ya majibu ambayo yanaweza kuharakisha kuchoma fedha za Serikali bure hapo Ngorongoro.

Mzizi wa fitna

Kuna sababu kadhaa zinazofanya wageni wanaotembelea Tanzania wasirudi tena. Moja ya sababu hizi ni gharama. Ukichukua nchi kumi Afrika zenye bei nafuu kwa utalii, Tanzania haitoonekana. Nimepitia mtandao wa Bigworld Small Pocket ambao unaoredhesha mataifa ambayo gharama za utalii ni ndogo kuliko nyingine. Nchi inayoongoza kwa kuwa na gharama ndogo ni Morroco. Mtandao huo unasema ukiwa Morroco mfukoni ukiwa na dola za kimarekani 30-40 (ambazo ni sawa na Sh69,570 hadi 92,762) unaweza kugharamia chakula, malazi, usafiri na viingilio vya sehemu mbambali zenye vivutio vya utalii.

Mtandao huo unataja nchi ya pili yenye gharama sawa na Morroco kuwa ni Tunisia na ya tatu ni Misri. Nikatamani kuangalia kwa Tanzania nikakuta kwa mtalii aliyejibana sana kwa siku anatumia Sh170,000, hapo hajakutana na waongoza watalii ambao wameshamsokota na kumuomba simu au chochote akiwa naye kwenye matembezi. Imekuwa ni kawaida kwa Tanzania mtu akishaitwa mtalii kumbambikia bei za ajabu ajabu kwenye mahitaji yake. Kwa mfano, chumba cha Sh40,000 atauziwa laki moja. Chakula Cha Sh5,000 atauziwa Sh15,000. Ukikutana na mtalii huko mtaani kawa mwekundu na anatembea kama kichaa kwa sababu ya mambo haya. Kwa nini arudi tena tena Tanzania? Katibu Mkuu wetu sioni sababu za kuendelea kujadiliana hapo Ngorongoro.

Sababu nyengine kwa nini wageni wetu wanaotembelea Tanzania huwa hawarudi tena inahusu utendaji kazi wa mabalozi wa Tanzania nje za nchi. Badala ya kuwaita waandishi wa habari, Katibu Mkuu Nzuki angeshugulika na mabalozi wetu kwenye maeneo mbalimbali duniani. Hawa wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuvutia watalii nchini kuliko waandishi wanaoandika habari za ajabu ajabu ambazo hazina tafiti. Waandishi wetu asilimia kubwa hawana uwezo tena wa kutafiti na kutengeneza ajenda. Badala yake wamebakia kuwa maripota wa matukio tu. Nafikiri tufungue madawati ya utalii kwenye balozi zetu na tuwape kazi na kila mwaka dawati hilo watajaza dokezo la wameweza kuleta watalii wangapi.

Sababu nyengine inahusiana na mipango na sera zetu kama taifa. Je, Tanzania tuna mpango wowote (kama vile nyaraka rasmi) inayoonyesha kwa miaka mitano ijayo ramani ya utalii inatuelekeza kwenda wapi? Hawa Morocco mwaka 2001 walianzisha mradi wa kukuza utalii uliopewa jina la ‘Plan Azur.’ Katika plan Morocco walilenga kujenga Resorts Hotel za kisasa kabisa lakini walizoziuza kwa bei nafuu sana. Mwaka 2010, Morocco ikaja na mpango mwengine uliopewa jina la ‘Vision 2020.’ Sisi tukaanzisha ya kwetu ya ‘Mpaka Kileleni’ iliyotaka kumuua Steve Nyerere kule Mlimani Kilimanjaro ambayo haina tofauti sana na hii ya waandishi wa habari kujadili utalii huko Ngorongoro!

Hoja nyengine za msingi

Maswali ya msingi yayobakia ni, pamoja na mengine: je, tuna mipango ya muda mrefu yenye kuakisi ushindani wa biashara hii ya utalii? Je, watalii waliokwisha kutalii hapa kwetu Tanzania tunawapa discount yoyote wakitaka kurudi? Je, tunawahudumiaje watalii wetu kuanzia wanapotua hadi wanaondoka? Je, wanaondoka wakiwa na furaha au wanaondoka wakiwa na maombi kibao ya kuombwa hela? Wahudumu wetu wanawahudumiaje huko mbugani na mahotelini? Mambo ni mengi ila tujiulize kwa haya je, kuna mtalii atakayetamani kurudi?

Mwaka 2019 Morocco walipata watalii Milioni 12.93, wakafuatiwa na Afrika Kusini iliyopata watalii milioni 10.23 na kwenye kumi bora Tanzania hatupo. Sisi tuliingiza watalii milioni 1.5. Kwa uwiano huo, itabidi tukae miaka kumi kupata watalii wa Morocco wa mwaka mmoja. Tuna kila aina ya kivutio. Tatizo letu linaanzia vichwani mwetu wenyewe kabla ya kufika Ulaya.

Kila la Kheri kwa waandishi wetu hapo Ngorongoro!

Thadei Ole Mushi ni mchambuzi wa siasa na masuala ya kijamii. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mushiole@gmail.com au kupitia ukurasa wake wa Facebook kama Thadei Ole Mushi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Waraka huu ulichapishwa kwa mara ya kwanza Facebook

Thadei Ole Mushi

3 comments

 • Charles Elias

  31 December 2020 at 11:06 AM

  Kabla hatujaangalia kuhusu sekta ya utalii, ni vema tukapata majibu, ni kwa nini kwenye migahawa ya njiani yanakosimama mabasi kwa ajili ya abiria kupata mlo bei za vyakula ziko juu mno?

  Tabia hii mbaya na ya hovyo imekuwa desturi na ndio maana hata kwenye maduka ya kawaida tu raia wa kigeni ana bei tofauti na mwenyeji. Sio hivyo tu, serikali imekuwa sehemu ya uhamasishaji wa mfumo huu, kiasi kwamba maumivu yanaanzia kwa raia wake kabla ya wageni. Kwa kifupi tunaongozwa na ujanja ujanja mwingi kuliko kanuni halisi za kiuchumi.

  Tutafakari

  Reply

 • Daniel Sempeho

  3 January 2021 at 7:00 PM

  Ulipotaja ongezeko la bei ukiwa unaonekana mtalii ni ishara tosha kuwa biashara ya utalii haina soko kama sio biashara imara. Angalia bei za vyakula. Tanzania ni miongoni mwa nchi zianzoongoza kwa uzalishaji wa nyama na maharage. Sasa angalia bei za hizo mazao hayo dukani na hotelini ukilinganisha na uwingi wake kwenye kipimo. Kwa mtalii akichagundua amelanguliwa ni wazi hatakubali kuwa pimbi tena.

  Reply

 • Alex Mtegeta

  12 January 2021 at 11:25 PM

  Tatizo moja kubwa ya watalii kutokurudi Tanzania, pamoja na yote yaliyosemwa, ni customer service. Wahudumu hawatilii maanani kazi wanayoifanya. Wanangoja tu mshahara mwisho wa mwezi, hawajua mshahara wao unategemea namna wanavyo wahudumia wateja. Yawezekana tatizo hili linahusu namna wanavyofundishwa kwenye vyuo.

  Nimekuwa mtalii nchi kadhaa duniani moja na Tanzania. Wahudumu wa sehemu mbalimbali (mbuga za wanyama, mahoteli, restaurants, madukani, nk), wakikuona wewe ni mgeni, wanakuomba hela bia hata aibu. Ni kwa vile tu, mimi ni wa asili ya Tanzania na nimpenzi wa Tanzania ndiyo maana hurudi tena. Ila nimeshindwa kuwashawishi watu wengine kwenda Tanzania (isipokuwa tukiwa wote).

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved