Nimefuatilia kwa makini mjadala wa vijana na wasomi katika mitandao ya kijamii juu ya Mapinduzi ya Zanzibar. Wengi wanauliza maswali na wengi wametoa uchambuzi wenye tafakuri nzito juu ya kwa nini Mapinduzi ya Zanzibar yanaonekana kuwa ni mali na ni utambulisho wa watu fulani na wengine hawana nasabu nayo. Wengine wanajiuliza ni nani hasa mwenye Mapinduzi kwa sababu wapo watu ambao wazazi wao walikuwa waasisi wa Mapinduzi na wao wenyewe pia ni waumini wa Mapinduzi lakini bado wanadhaniwa kuwa hawana nasabu nayo wala hawahusiki na Mapinduzi. Wengine wamekwenda mbali na kujiuliza hivi ni lini Zanzibar haya makundi ya wenye Mapinduzi na wanaoitwa si wenye Mapinduzi yataondoka. Kwa maoni yao uongozi wa sasa wa Zanzibar unayo fursa ya kipekee ya kuzika makundi hayo na kuwaunganisha Wazanzibari kama jamii iliyopita mapito mengi katika safari ya kujenga taifa lao mojawapo ikiwa ni Mapinduzi.
Jambo hili litakuwa rahisi kama tutakubali kuwa wakweli juu ya hali ilivyo na changamoto zake. Kwa sababu, kwa maoni yangu, tatizo kubwa la Mapinduzi ya Zanzibar kwa zama hizi ni kuwa wapo watu katika mamlaka na katika siasa ambao bila kujinasibisha na Mapinduzi watasita kuwa na maana (relevant) katika jamii. Boya lao la kuogelea ni Mapinduzi. Hawa ni wengi kidogo na zama zinawapita kwa nguvu.
Kundi la pili ambalo ni la rika la kati na vijana. Wengi wao mimi nawaita dhaifu (mediocre) ambao nao bila ya kujinasibisha na Mapinduzi nao watashindwa katika ushindani wa ajira, nyadhifa, siasa, ama kutajwa tu. Hawa watayeyuka haraka kuliko hata wa kundi la mwanzo. Kundi la tatu na ambalo ni dogo sana ni wale ambao kwa sababu ya uelewa wao wameaminishwa kuwa kila mwenye mawazo tofauti na chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) ni adui.
Malengo ya kujinufaisha kisiasa
Jambo la msingi ni kuwa wanaowalewesha watu dhana hii wanafanya kwa makusudi na kwa malengo ya kujinufaisha. Ukirudi katika dhana na itikadi ya Mapinduzi ya Zanzibar inabaki kuwa ni moja ya matokeo ya mikinzano ya kijamii sawa na Mapinduzi yoyote yale. Mapinduzi ya aina ya Zanzibar yametokea katika nchi nyingi na kwa sababu zinazofanana na zile za Zanzibar.
Mapinduzi ya nchi sita za Amerika Kusini yaliyoongozwa na Simón Bolívar, kiongozi wa kijeshi na kisiasa wa taifa la Amerika ya Kusini la Venezuela, ni miongoni mwa mfano mzuri. Hata Mapinduzi ya Uingereza yaliyoongozwa na Oliver Cromwell mwaka 1649 kwa kumuondoa mfalme na kuanzisha Jamhuri ni mfano mzuri.
Mapinduzi yoyote ni daraja tu na sio utambulisho (identity). Mapinduzi yanayofanywa kuwa ni utambulisho na kuwa mali ya mtu au kikundi cha watu hayadumu. Mfano mzuri ni Uingereza. Baada ya kufariki Oliver Cromwell mwaka 1658, mfalme alirudishwa mwaka 1660 na wakaendelea na mfumo wa kifalme hadi leo kwa sababu mapinduzi yalimilikiwa na watu wachache.
Na ni kwa sababu hizo ndiyo maana Simón Bolivar baada ya kupiga hatua ya mapinduzi aliasisi bunge la Venezuela na akatoa hotuba maarufu inayoitwa The Speech of Angostura Congress ya February 15, 1819. Hotuba hii imempa umaarufu kuliko hata hayo mapinduzi aliyofanya kwa sababu aliweka muongozo wa nini matarajio ya watu kwa mapinduzi.
Mapinduzi ya watu, siyo watawala
Pamoja na mambo mengine, Simón Bolivar alisema kwenye hotuba hiyo kwamba Wabunge wawape wananchi maendeleo, haki, utawala wa sheria na alisisitiza chaguzi huru na za haki na za vipindi. Mwanamapinduzi huyo alikataza kabisa utaratibu wa kutokua na ukomo wa madaraka (term limits) kwa sababu utazaa madikteta (despots) ambao hawatakuwa viongozi wa mapinduzi bali madhalimu ambao hatimaye watahitaji kupinduliwa.
Hivyo, Zanzibar napo Mapinduzi yanafanywa ni milki ya wachache. Mapinduzi yanafanywa ni utambulisho wa tabaka fulani na asiyenasibishwa nayo hana haki hata ya kuchagua seuze kuchaguliwa. Hana haki ya kiuchumi, hana haki ya kukosea. Ndiyo maana upepo wa sasa unaovuma chini ya Raisi wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi unawatisha, unawakosesha amani.
Na wana sababu ya kuwa na hofu. Wengi watasita kuwa na maana (relevant). Wengi watashindwa kuhimili ushindani katika nyanja nyingi. Lakini hofu kubwa zaidi ni kuwa upepo huu unavumishwa na mwana CCM wa aina ya Hussein Mwinyi; ni shida kumdhibiti, ni shida kumlaumu, ni shida kumpaka tope za uarabu, uhizbu, au upinzani. Walitamani hayo yangetokea mikononi mwa upinzani wakawa na sababu ya kuchafuliwa hali ya hewa. Kiroboto wa miaka ya 1980s akarudi wakapata pa kuanzia.
Iwe iwavyo, wingu hili la dhana ya Mapinduzi ya wachache linahitaji kusafika ili Zanzibar iweze kupaa. Ifike pale inapostahiki. Mapinduzi ni daraja, ni wakati lituvuushe litupeleke ng’ambo ya pili tuendelee na safari badala ya kubaki chini ya daraja tukijisifia usanifu na uhandisi wa daraja.