The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Utapiamlo Unavyoitesa Iringa, Mkoa Unaojitosheleza Kwa Chakula

Wazazi mkoani humo wanadaiwa kutumia muda mwingi shambani huku wakiwekeza muda mchache sana kwenye malezi na kuwapatia watoto wao lishe bora.

subscribe to our newsletter!

Ni saa saba mchana nafika kwenye nyumba ya Bi Juliana Kilasi mkazi wa Ilula, Mkoa wa Iringa, Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Hapa, napokelewa kwa ukarimu mkubwa na mwenyeji wangu Bi Juliana, mama mcheshi na mkarimu sana. Nyumbani kwake, Bi Juliana, 62,  anafuga kuku na mbuzi na kwenye shamba lake kuna mboga zilizostawi vyema kipindi hiki cha mvua. Sikuja hapa kujua hali ya mtoto, lakini baada ya mtoto aliyekuwa mgongoni mwa bibi yake kuamka nikapata shauku ya kuuliza umri wake na Bi Juliana kuniambia kwamba mjukuu wake huyo alikuwa na miaka mitatu na nusu.

“Mbona anaonekana kama ana mwaka mmoja?” nilihoji kwa kwa shauku kwani umri na muonekano wa mtoto havikuwa vinaendana. Bi Juliana akanieleza: “Mtoto anaumwa, nimeambiwa ni utapiamlo. Nipo nahangaika nae. Nimeshaelekezwa namna ya kumpa chakula. Nashangaa sana kwanini mtoto bado anaendelea kuumwa. Asubuhi huwa nampa chai na kiporo cha ugali au uji. Mchana ugali na maharage. Jioni pia hivyo hivyo lakini mtoto wangu alipata utapiamlo.”

Utafiti mdogo tu wa maisha ya Bi Juliana ulinibainishia kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa bibi huyo kumlisha mjukuu wake mlo kamili na akaondokana na tatizo la utapiamlo lakini kutokana na kazi nyingi za Bi Juliana pamoja na uelewa mdogo kuhusu masuala ya lishe ndio kunamfanya mjukuu wake kuugua. Kadi ya kliniki inaonyesha kwamba mtoto yupo kwenye alama nyekundu akiwa na uzito wa kilo nane, wakati anapaswa kuwa na kilo zaidi ya 15 kulingana na umri wake.

Moja ya kadi inayoonyesha maendeleo ya mtoto mwenye tatizo la utapiamlo

Bi Juliana anasema kazi nyingi za shambani zilikuwa zinamlazimisha aondoke nyumbani asubuhi na kurejea jioni, bila kujua milo halisi aliyopata mjukuu wake huyo. “Nisipolima atalima nani?” Bi Juliana, anayeishi na wajukuu zake watatu huku wanae wakiwa sehemu mbalimbali nje ya mkoa wa Iringa kutafuta maisha, anauliza huku akiendelea kuongea bila kusubiri majibu. “Hapa kuna wajukuu zangu wengine wawili hawakuwahi kupata tatizo hilo lakini huyu tu.” Anasema mwishoni mwa mwaka 2020, mjukuu wake aliumwa na akaamua kumpeleka hospitali ndipo alipogundua tatizo ni lishe.

Chakula kipo kingi na utapiamlo pia

Utapiamlo si tatizo linaloitesa familia ya Bi Juliana peke yake. Huo ni ugonjwa unaowaumiza watoto wengi mkoani Iringa licha ya mkoa huo kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara. Kwa mujibu wa Afisa Lishe wa Mkoa wa Iringa Neema Mtekwa, hali ya lishe kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano mkoani humo sio shwari. Mtekwa anasema takwimu za lishe za Mkoa wa Iringa zinaonyesha kuwa watoto wa miezi sita hadi 23 wanaopewa kiwango cha mlo kinachokubalika ni asilimia 12 tu. “Hii ni sawa na kusema kwamba asilimia 88 ya watoto wa umri huo kwenye mkoa wetu hawapewi kiwango cha mlo kinachokubalika,” anafafanua wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo. Mtekwa anaongeza kwamba asilimia 25 ya watoto wenye umri huo wanapewa mlo wenye mchanganyiko wa vyakula tofauti zikiwemo mboga za majani, matunda na vyakula vyenya jamii ya kunde. “Asilimia 77 ya watoto hawapewi mlo kulingana na umri unaotakiwa.”

Afisa Lishe wa Mkoa wa Iringa, Neema Mtekwa akiwa ofisini kwake wakati wa mahojiano maalum

Wataalamu wanataja uelewa mdogo kuhusu mlo kamili kwa watoto kuwa sababu zinazochangia tatizo la utapiamlo kuwa kubwa mkoani Iringa. Mtekwa, kwa mfano, ni moja kati ya wataalamu hawa akisema kwamba tatizo haliwezi kuwa chakula kwa sababu mkoa huo unazalisha chakula cha kutosha. Anafafanua: “Ikiwa watoto wanakula aina moja tu ya vyakula, yaani wanga kwa sana na maharage, kwa maana ya jamii ya mikunde tu, watapona hapo? Ulishaji unawaumiza sana watoto.” Kwa mujibu wa afisa huyo mwenye dhamana na lishe kwa mkoa wa Iringa mtoto anatakiwa kupata milo mitatu mikubwa na miwili midogo kwa siku. Milo hiyo inatakiwa kuwa na mchanganyiko wa vyakula vinavyoweza kulinda mwili, kujenga, kutia nguvu pamoja na joto. Kwa watoto wengi wa mkoa wa Iringa hicho hakipatikani.

Lakini kuna sababu nyengine inayochochea tatizo la utapiamlo kuwa kubwa mkoani iringa nalo ni wazazi kukosa muda wa kutosha kukaa na watoto wao kutokana na kazi za shamba kuwa nyingi na sababu nyengine. Mtekwa, ambaye ana uzoefu mkubwa sana kwenye suala la lishe mkoani humo, anasema: “Ulevi kupindukia, usafi duni wa chakula, uhifadhi na matumizi mabaya ya madini joto kama chumvi zinachangia sana watoto kudumaa.” Akitolea mfano uandaaji mbaya wa chakula, Mtekwa anasema kuna mtindo wa kuandaa unga na kuupa jina la ‘lishe’ wakati umewekwa aina moja tu ya chakula, yaani nafaka. “Unga unachanganywa mahindi, ngano na mchele wakati mwingine wanaweka maharage na karanga, wanatunza ndani mpaka unavunda halafu wazazi wanawalisha watoto. Hii ni kama sumu tu, ni hatari sana,” anasema.

Edwick Mapalala ni mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia na Mkurugenzi wa Shirika la Regional Psychosocial Support Initiative (REPSSI) anapigia msumari hoja ya Mtekwa kuhusu umuhimu wa kuwalisha watototo mlo kamili akisema ulaji mbaya wa chakula kwa watoto unaweza kuathiri ukuaji wao kwa kiasi kikubwa. Hapa Mapalala anafafanua wakati wa mahojiano maalumu na The Chanzo: “Hali hiyo sio nzuri wala sio ya kuichekea. Utapiamlo ni hatari kwa ukuaji wa mtoto. Ni rahisi kuja kupata taifa la watu wasio na uwezo mzuri wa kufikiria kama watoto hawatapewa lishe bora tangu tumboni mwa mama zao.”

Harakati za kubadilisha tabia

Hali hii imeifanya Serikali ya Mkoa wa Iringa kuandaa mikakati ya kubadilisha tabia za wananchi wa mkoa huo ili watoto waweze kupata lishe iliyo bora na kuwa na ustawi mzuri. Kwa mujibu wa Mtekwa, ambaye yuko mstari wa mbele kuhakikisha juhudi hizi zinazaa matunda, elimu ndio jambo la msingi la kwanza Serikali ya Mkoa wa Iringa ilianza kufanya ili kuondokana na tatizo hilo. Hii ilitokana na ukweli kwamba mkoa huo haukabiliwi na uhaba wa chakula bali tabia za wazazi na uelewa finyu kuhusiana na suala zima la lishe.

Moja kati ya watu waliofikiwa na uhamasishaji huu ni William Kalinga ambaye anakiri kupokea ushauri wa namna bora ya kuwapatia lishe watoto wake na tangu hapo ameanza kuzingatia maagizo ya wataalamu wa chakula ili kuimarisha afya zao. Kalinga anaieleza The Chanzo: “Kuku wakitaga mayai kumi, matano namuwekea mtoto na siku nikichinja, nampa kipaumbele sio kama zamani. Nampa matunda na mbogamboga kwa wingi, nashukuru kwa elimu waliyotupatia.”

Mtekwa anasema tayari Serikali ya Mkoa wa Iringa imeanzisha klabu za lishe shuleni ili watoto wapate nafasi ya kujadili jambo hilo ili wanaporejea nyumbani wawasaidie wazazi kuelewa umuhimu wa lishe bora lakini pia na wao wakikua wawe na uelewa. Mkakati mwingine uliowekwa kukabiliana na tatizo hilo ni kushirikiana na wadau kuhamaisha ulimaji wa bustani za mbogamboga, ufugaji wa kuku na mbuzi ili kuongeza upatikanaji wa vyakula vya aina zote.

Tumaini Msowoya ni mwandishi wa habari wa kujitegemea wa habari za watoto na kijamii aliyepo Iringa, Tanzania. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni msowoyatuma@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatile, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. Naomba kufahamu Hall halisi ya utoaji wa chakula mashuleni kama Sera ya elimu ya 2014 NA miongozo ya utekelezaji ynamba y5 NA 6 ya nwaka 2015 NA 2016

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts