The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hii Ndiyo Njia Bora Ya Kukabiliana Na Magonjwa Yasiyombukiza

Kuna haja ya kubadilisha mfumo mzima wa uzalishaji mali na usambazaji wake na siyo kuhubiri watu wale vizuri na kufanya mazoezi tu.

subscribe to our newsletter!

Wakati dunia ikishuhudia mapinduzi makubwa ya kiteknolojia na maendeleo ya usasa na hatua hiyo kuonekana kuwa ndio kielelezo cha ustaarabu, utamaduni mpya umejengeka wa watu kuwa tegemezi kwenye vyakula vya haraka (fast food) na vyakula vinavyo kaa muda mrefu kwenye maduka makubwa (shopping malls) bila kuoza. Hali hii, hata hivyo, inaenda sambamba na kushika kasi kwa magonjwa yasiyoambukiza yanayoendelea kutesa mamillioni ya watu duniani, wakiwemo Watanzania. Utandawazi umetengeneza utamaduni kwamba mtu mstaarabu ni anayekula baga na kuku wa kisasa. Kwamba mwanamke mzuri ni yule anayejichubua na hivyo kuwalazimisha wadada wengi kujichubua ili wapate rangi hiyo. Hii yote imepelekea kuibuka kwa maradhi mengi yanayowanyima raha raia na Serikali zao.

Historia inatuonesha kwamba magonjwa yasiyoambukiza yalitokana na ujio wa Mapinduzi ya Viwanda yaliyoenda sambamba na ukuaji wa ubepari wa kiviwanda. Hali hii ilibadili mwelekeo mzima wa jamii juu ya afya kwa ujumla, kuongezeka kwa uchafuzi wa hali ya hewa, na kuwalazimisha wafanyakazi kufanya kazi kwenye mazingira hatari yaliyopelekea baadhi yao kupata matatizo ya mapafu na saratani.

Mnamo karne ya 19 wakati dunia ikishuhudia kupungua kwa magonjwa yanayoambukiza, magonjwa yasiyoambukiza yakaanza kushika kasi. Mlipuko wa magonjwa haya ulipiku ule wa magonjwa yanayoambukiza na kusababisha vifo vingi kiasi ya kwamba katika kila vifo kumi vinavyotokea duniani kila mwaka saba ni vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukizwa kama vile saratani, kisukari na mengineyo mengi. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni 41 wanakufa kila mwaka kutokana na magojwa yasiyoambukiza sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani, katika idadi hiyo vifo vya watu milioni 15 wenye umri kati ya miaka 30 hadi 69 vinatokana na matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe kupindukia, vyakula visivyo na virutubisho na kutofanya mazoezi.

Mfumo wa uzalishaji wa jamii

Wakati wa kikao kilichoitishwa na WHO na kuwakutanisha wadau mbali mbali ili kuweka mikakati ya kukabiliana na janga la magonjwa yasiyoambukiza kilichofanyika Geneva, Uswizi, Machi 2018, Rais wa zamani wa Uruguay Tabare Vazguez alisema: “Tujiulize sisi wenyewe kama tunataka kulaumu kizazi kijacho kwa watu kufa wakiwa vijana na maisha ya watu kuwa ni ya kutokuwa na afya. Jibu ni hapana. Lazima tufanye jitihada za dhati kuweza kulinda afya za watu katika kuwalinda katika matumizi ya tumbaku, matumizi ya pombe, na kula vyakula visivyo na afya na unywaji wa vinywaji vyenye sukari.” Vazguez, aliyefariki kwa saratani mnamo Disemba 2020, alikuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya tasnia ya tumbaku na aliipa vita hiyo kipaumbele katika vipindi vyote viwili vya utawala wake kama kiongozi wa siasa za mrengo wa kushoto wa taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Mipango iliyowekwa na WHO na wadau wengine katika kukabiliana na janga la magonjwa yasiyoambukiza ni ya kupongezwa lakini bado haigusi kiini cha tatizo lenyewe. Mtazamo kwamba magonjwa haya yanatokana na tabia ya mtu binafsi katika maisha yake ya kila siku hautoi suluhu ya kutosha juu ya kuyazuia na kuyafuta kabisa katika uso wa dunia. Kusema kwamba magonjwa yasiyoambukiza ni zao la tabia ya mtu na kwamba yanaweza kumalizwa kwa watu kubadilisha mitindo ya maisha yao tu ni kulidogosha tatizo lenyewe. Hii inatokana na ukweli kwamba ukitaka kutizama mtu anaishi vipi kwenye jamii yoyote ile kwanza ni muhimu kutizama mfumo mzima wa jamii hiyo, hususani kwenye eneo la nani anazalisha nini na kinchozalishwa kinagawanywa vipi. Kwa maneno mengine, itakubidi uangalie mfumo wa uzalishaji na mahusiano yaliyopo katika mchakato mzima wa uzalishaji. Hatuwezi kulitenganisha tatizo la magonjwa yasiyoambukiza na mfumo wa uzalishaji ambao utengenezaji wa faida ndiyo msingi wa uzalishaji mali, yaani mfumo wa kibepari.

Ni maoni yangu kwamba utaratibu huu wa uzalishaji ndio umeleta vyakula visivyo na maana katika jamii zetu na kufanya watu wasiwe na mbadala wa vyakula hivyo. Ni mfumo wa kiuchumi wa kibepari unaotanguliza faida kuliko kitu chochote kingine ambao umebadili mwenendo mzima wa watu kutumia. Leo hii bidhaa ambazo hazina  vitamini ndizo zinapigiwa debe na kunadiwa kote ulimwenguni na ambazo zinatoa mchango mkubwa kwenye kukua kwa tatizo la magonjwa haya yasiyoambukiza. Hivi sasa ulimwenguni kote, kuna mpango wa kuondoa mbegu za kilimo za asili na kuleta mbegu za uhandisi geni (Genetic Modified Organism – GMOs) ambazo zinaleta athari kwenye afya zetu na kutusogeza zaidi kwenye magonjwa yasiyoambukiza.

Si suala la mtu binafsi, ni la kimfumo

Ni katika muktadha huu ambapo nafikiri kwamba kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza si suala la mtu binafsi bali ni la kimfumo. Ili kuweza kukabiliana na tatizo hili hatuna budi kukabiliana na mfumo wa uzalishaji wa kibepari ambao unatufanya tuwe watumwa wa chakula na kufanya vyakula vyenye afya kuuzwa kwa bei ghali zaidi kitu ambacho kinawafanya wananchi wengi wa kipato cha chini kukosa aina hiyo ya vyakula. Tafiti zinaonesha kwamba nchi za vipato vya kati na zinazoendelea magonjwa haya yanazidi kuongezeka. Hii inajumuisha Tanzania ambayo Waziri wake wa Afya Dorothy Gwajima alibainisha hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa Idara ya Magonjwa ya Saratani katika hospitali ya Benjamin Mkapa Mkoani Dodoma kwamba nchini kwa sasa kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani 50,000 na kwamba inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 wagonjwa wapya watafikia asilimia 50 ya wagonjwa waliopo sasa.

Nani asiye jua kwamba sigara zinaleta magojwa, na imeidhinishwa kisheria na wakati wafanyabiashara wanafaidika watu wengi wanaumia kwa kupata maradhi wasiyoweza kujitibu? Imethibitika kisayansi kabisa kwamba athari za uvutaji wa sigara hazimkuti mvutaji tu bali hata wasio vuta. Hivyo suala siyo mabadiliko ya tabia bali ni mabadiliko ya mfumo wa uzalishaji ambao faida ndio kitu cha kwanza na si maisha na uhai wa binadamu. Matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza pia ni ghali sana kwa mwananchi wa kawaida kumudu gharama zake. Na moja kati ya sababu kwa nini mwananchi hawezi kumudu gharama za matibabu ni kwamba mfumo wa uzalishaji mali wa kibepari umefanya afya nayo kuwa  bidhaa kama zilivyo bidhaa nyengine tu zinazoweza kuuzwa na kununuliwa madukani. Kwa mujibu wa WHO, kila mwaka watu zaidi ya millioni 100 wanatupwa kwenye dimbwi la umasikini kutokana na kugharamia matibabu, na kila mwaka watu milioni mbili hufa kwa kushindwa kulipia upasuaji wa kuwekewa kifaa kinachodhibiti mapigo ya moyo. Hii ni hatari kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku. Lakini swali la msingi ni: Upi ni mwelekeo wetu kama taifa katika kuhakikisha kwamba magonjwa haya tunayamaliza na matibabu yake yanakuwa rahisi na kupatikana kwa wananchi walio wengi?

Wakati umefika sasa kwa Serikali na wadau wengine kwenye vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kutafakari janga hili kipekee na tusitumie muda mwingi kuhubiri kwamba watu wabadili mitindo yao ya maisha binasfi ili kujikinga na maradhi haya. Wakati hakuna ubishi kwamba hatua hizi zinaweza kusaidia kwa kiwango fulani, ni muhimu pia kutafakari namna ya kubadilisha mfumo mzima wa uzalishaji mali na usambazaji wake ambao nimejaribu kuonesha hapo juu japo kwa uchache kuwa ndiyo kiini cha janga hili linalozidi kuongeza mzigo kwenye bajeti yetu ya taifa ambayo tayari ni finyu.

Lazima tufahamu kwamba fikra na tabia ni zao la jamii na binadamu anafuata mfumo huo wa jamii unaoongoza. Hii siyo kwa bahati mbaya, bali ni mpangilio wa jamii husika katika mfumo wake wa uchumi. Sasa ubepari katika kipindi hiki cha uliberali-mamboleo unaelekea kufanya magonjwa haya yazoeleke kwa sababu umeshindwa kuyaondoa kabisa. Kwa sababu mfumo wenyewe ndiyo unazalisha magonjwa haya, hatuna budi kufikiria mfumo mpya ambao unalenga hasa uhai na usalama wa binadamu, mfumo ambao hauhitaji watu wafe ili uweze kupata faida. Kwangu mimi, mfumo huo ni mfumo wa ujamaa.

Nassoro Kitunda ni Mhadhiri Msaidi katika Idara ya Sosholojia, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT) – Mtwara. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nassorokitunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Kitunda anajitahidi sana kwenye chambuzi zake. Nadhani watu kama hawa wanahitajika sana kwenye jamii hii ili kuamsha bongo lala hasa za watu walioko kwenye maamuzi. Wengi tunaamini ni tabia binafsi kitu ambacho so kweli kama Nassoro anavyodai. Haya ni matatizo ya kimfumo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts