Ngozi Ya Dk Ngozi Haitoshi Kuifanya WTO Kuwa Rafiki Wa Nchi Masikini Za Afrika

Dr. Ngozi atapaswa kurejesha imani za watu juu ya taasisi hiyo iliyohusika kwa njia moja au nyengine kukandamiza mataifa mengi ya Afrika kwa kusimamia sera zinazoyanufaisha mataifa tajiri.
Nassoro Kitunda10 March 20215 min

Kufuatia hatua ya Baraza Kuu la Shirika la Biashara Duniani (WTO) la kumtangaza Dk Ngozi Okonjo-Iweala kama Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo inayoshughulika na sheria za kimataifa za kibiashara, kumekuwa na mjadala mpana miongoni mwa wafuatiliaji wa masuala ya kidunia kuhusiana na umuhimu wa hatua hiyo iliyochukuliwa na Baraza Kuu la WTO. Kwa baadhi ya wachambuzi, uteuzi huu ni ishara ya mafanikio kwa Waafrika huku wengine, hususani wale wanaofanya harakati za masuala ya wanawake, wakiupongeza uteuzi huo kwa mchango unaoweza kutolewa na mwanamke katika kuendesha taasisi hiyo yenye kusimamia mambo nyeti ya kidunia. Ni uamuzi uliopokelewa kwa bashasha tele na hakuna shaka kwamba waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Nigeria na Naibu Katibu Mkuu wa Benki ya Dunia ana uzoefu wa kutosha wa kumuezesha kufanya kazi iliyokusudiwa.

Wakati watu wana kila sababu ya kufurahia kwa Mwafrika, tena mwanamke, kusimamia taasisi hiyo yenye historia ndefu na yenye mashaka na bara hilo, tunalazimika kubainisha kwamba kinachoongoza taasisi hiyo si jinsia wala rangi ya mtu bali sera za mfumo wa uchumi wa soko huria ambazo kwa namna moja au nyengine zinahusika na hali ya sasa ya kiuchumi ya mataifa mengi ya ulimwengu wa tatu, ikiwemo nchi nyingi za Afrika kama Tanzania. Historia imejaa mifano na tafiti zinazoonesha kwamba WTO — kama ilivyo kwa ndugu zake Benki ya Dunia (WB) na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) — haitendei haki na inaziumiza nchi za zinazoendelea. Mwaka 2011, jarida la Uingereza la The Guardian lilichapisha habari inayobainisha mifano 10 ya namna WTO imeziangusha nchi masikini kwenye maeneo kama makubaliano ya kibiashara, madawa, vifaa vya kilimo nakadhalika.

Ni zaidi ya rangi, jinsi ya mtu

Hii yote inamaanisha kwamba kuifanya WTO kuwa ya msaada kwa mataifa masikini ya dunia itachukua zaidi rangi au jinsia ya mtu anayeiongoza taasisi hiyo. Hatua ya kwanza ya kulifanikisha hilo ni kutambua kwamba sera za uchumi wa soko huria ambazo WTO inazisimamia na kuzitekeleza hazipo kwa ajili ya mataifa masikini na hivyo haraka iwezekanavyo kuanzishwa kwa mchakato wa sera hizo kubadilishwa. Moja kati ya shutuma nyingi zinazoelekezwa kwenye taasisi hiyo ni kwamba mataifa tajiri yamekuwa yakiitumia WTO kusimamia maslahi yao ya kibiashara kwa hasara ya nchi masikini kama vile kuunda mikataba ambayo inarahisisha wao kutuma mitaji yao mataifa maskini na kunyonya rasilimali zao huku yakiweka masharti magumu kwa nchi masikini kufanya hivyo hivyo. Mfano mzuri wa mikata hii ni kama Economic Partnership Agreement (EPA) kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao Tanzania imegoma kusaini, huku Rais wa awamu ya tatu hayati Benjamin Mkapa akiutaja mkataba huo kama aina nyengine ya ukoloni.

Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania, ni moja kati ya wakosoaji wakubwa wa taasisi kama WTO, akizishutumu kama taasisi zinazohimiza demokrasia katika ngazi ya kitaifa lakini ndani yao wenyewe “hakuna hata kisingizio cha demokrasia.” Mwalimu Nyerere, aliyekuwa mstari wa mbele katika vuguvugu la nchi zinazoendelea za kutaka mabadiliko ya msingi ndani ya taasisi hizi ili maslahi ya nchi za ulimwengu wa tatu yaweze kuzingatiwa, aliwahi kusema kwamba sera za soko huria zinazosimamiwa na mashirika kama WTO hazitoi fursa sawa za kibiashara baina ya nchi matajiri na maskini. Mwalimu alibainisha kwamba kuishindanisha Tanzania na nchi kama Marekani ni sawa na kuwashindanisha bondia wenye uzito tofauti na ukawaweka kwenye uwanja/ulingo mmoja, na ukasema huo ndio uwanja ulio sawa. Hii ndio hali ilivyo ndani ya WTO. Wanadai wanaweka kanuni zinazo wapa watu fursa sawa za kibiashara, lakini mfumo wanaousimamia haulengi kuleta huo usawa wa biashara. Hii ni kazi nzito aliyo nayo Dk Ngozi, kuona ni kwa namna gani ataweza kuleta usawa wa biashara baina ya wanachama ambao hawapo sawa kwenye mizania hiyo ya biashara.

Kwa mfano, Dk Ngozi ataweza vipi kusimamia bei elekezi ya korosho ya wananchi wa Mtwara, ambazo kwa sasa zinanuliwa kwa bei wanazopanga wakubwa huko Ulaya bila ya ushiriki wa wakulima wenyewe?. Bei ya korosho imekuwa ya kusuasua kila mwaka na wanaofaidika sio wakulima bali wafanyabiashara na makampuni makubwa ya kimataifa. Kwa hiyo suala sio kuongeza thamani ya korosho, thamani ipo. Suala ni nani anayeamua bei ya korosho. Hapo ndipo wakulima hawa pengine wanauliza umuhimu wa mkurugezi mpya wa shirika la biashara  atawezaje kulikabili hili suala.  Vivyo hivyo kwa wakulima wa kahawa, bidhaa ambayo inanunuliwa kwa bei ndogo kwa mkulima na kuuzwa kwa milioni ya pesa huko ughaibuni. Kulima tunalima sisi lakini bei wanapanga wengine. Aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo Dk. Mary Mwanjelwa, aliwahi kuwauliza bodi ya kahawa Tanzania swali hilo, kwa nini kahawa inakosa bei nzuri kwenye soko la ulimwengu wakati ina ubora? Bodi ilijibu kwamba kahawa haikuongezewa thamani, na hakuna mtu aliyebainisha kwamba hali hiyo inatokana na matatizo ya mfumo wa uchumi wa dunia ambapo bei haitokani na ubora wa bidhaa bali matakwa ya soko, yaani ugavi na usambazaji.

Mategemeo ya wakulima kwa Dk Ngozi

Mkulima wa Tanzania ananyonywa na soko la ndani na la nje. Matumaini ya wakulima wa Tanzania, na naamini kwa wakulima wengi wa nchi zinazoendelea, kwa Dk Ngozi ni kuona wanapata bei nzuri ya mazao yao kwenye soko la dunia. Na si kuachia soko huria ndio liamue bei ya mkulima kwenye pamba yake. Ingawa Serikali ya Tanzania imekuwa ikibainisha zaidi ya mara moja kwamba haitatoa bei elekezi ya pamba lakini si kuachia soko huria. Maana hii inamuathiri mkulima lakini pia taifa kwa kushuka kwa pesa za kingeni na uchangiaji kwenye pato ghafi la taifa. Kwa hiyo, Dk Ngozi anapaswa kutambua kwamba matatizo ya kibiashara duniani yanatokana na mfumo wa uchumi wa soko holela na ni lazima ahakikishe analenga kubomoa ufumo huo wa uchumi. Dk Ngozi hana budi kuvunja sera ambazo zinalenga kuendeleza unyonyaji kwa mataifa madogo duniani kwenye biashara, kama vile masuala ya vikwazo vya kibidhaa kwamba bidhaa hizi za Afrika hazina ubora wa kuuzwa huko ulaya. Ana nafasi ya kulipigania hili kama Mkurugenzi Mkuu wa WTO, kwa kuibua masuala haya na mengine ambayo mataifa tajiri kama G20 na G7 hayafurahii kuyasikia. Kwenye mikutano na mataifa haya, Dk Ngozi hana budi kuwaeleza umuhimu wa kusimamia utu katika biashara na sio kuendekeza unyonyaji na ukandamizaji.

Kimsingi, dunia ipo kwenye vita ya uchumi ya kitabaka kati ya mataifa matajiri na maskini, na tunashuhudia mapambano ya kibiashara yaliyopo kati ya Marekani na China. Kila nchi inaamua kufunga milango yake na kuhubiri masoko ya kizalendo na wanakimbilia Afrika kutanua mazingira yao ya biashara. Afrika inapaswa kufunga mkanda, na si kufurahi tu kuwa Dk Ngozi ataleta neema. Shirika hilo la biashara lina matatizo lukuki ya kimfumo likiwemo mikataba mibovu ya biashara ambayo imefanya wanachama kupoteza imani na shirika hilo na kusema kuwa limepitwa na wakati. Pia, kuna hoja kuwa shirika hilo limeshindwa kuleta suluhu ya migogoro ya kibiashara duniani, hivyo imepelekea kushindwa kuleta mabadiliko katika uchumi wa dunia. Ni kazi ya Dk Ngozi kurejesha imani za watu katika taasisi hiyo na ni imani yangu kwamba jinsia yake na rangi yake tu havitoshi kumuwezesha kuifanya kazi hiyo. Ni lazima ajitoe muhanga kwa faida ya watu wake, wanawake na Waafrika, ambao wanaendelea kushangilia uteuzi.

Nassoro Kitunda ni Mhadhiri Msaidi katika Idara ya Sosholojia ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) – Mtwara. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nassorokitunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.

Nassoro Kitunda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved