Machi 19, 2021, Tanzania iliandika historia mpya, ambapo aliyekuwa Makamu wa Rais wake, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa sita wa wa taifa hilo la Afrika Mashariki. Mama Samia, kama watu wengi wanavyopenda kumwita, ameshika nafasi hiyo kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021, katika Hospital ya Mzena jijini Dar es salaam kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya mfumo umeme wa moyo (Atrial Cardiac).
Mara nyingi kiongozi mpya yoyote anapoanza kutekeleza majukumu yake ni kawaida kwa watu kuwa na matumaini mapya na kiongozi huyo, na wengi hutamani kuona kiongozi mpya anapoanza majukumu yake basi yale mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake ayaendeleze na yale mapungufu yaliyobayana ayasahihishe ili zile changamoto zilizopo za kiuchumi, kisiasa, na kijamii ziweze kutatuliwa kwa manufaa ya mustakbali wa watu wa Tanzania. Katika adhima ya kuchochea tafakuri katika hilo, The Chanzo imejaribu kuangazia baadhi ya changamoto ambazo Rais Samia na Serikali anayoiongoza watakabiliana nazo katika kipindi chake cha uongozi.
Kwa kuanza na sekta ya uchumi, yapo mambo kadhaa ambayo Rais Samia atakabiliana nayo, mojawapo ikiwa ni madhara yatokanayo na kudorora kwa uchumi wa dunia kutokana na janga la ugonjwa unaosababishwa na Virusi Vya Korona (UVIKO-19). Kama ilivyobainishwa kwenye taarifa ya Benki ya Dunia kwamba licha ya Tanzania kuonesha ustahimilivu kwenye uchumi kipindi cha mwaka mmoja uliopita ukilinganisha na nchi nyingine za ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati, bado matumaini ya kurudi kwa uchumi wa dunia katika hali ya kawaida katika kipindi kifupi kijacho hayapo.
Sekta kubwa zinazoathirika na hali hiyo mbaya ya uchumi wa dunia ni pamoja na utalii ambao umeanguka kwa zaidi ya asilimia 77.7 kwa mujibu wa Benki ya Dunia pamoja na sekta ya uuzaji bidhaa nje ambayo imetetereka kupelekea kuongezeka kwa tatizo la ukosefu wa ajira na kuathiri jitihada za Serikali za kupambana na umaskini. Hivyo basi, Serikali inayoongozwa na Rais Samia itawajibika kuhakikisha ustahimilivu huu wa kiuchumi unadumishwa na kuboreshwa zaidi kufikia hatua itakayotoa ahueni ya kiuchumi kwa watu wengi zaidi.
Mazingira bora kwa wazalishaji wadogo
Serikali chini ya Rais Samia itakabiliwa na kuona namna bora ya kuweka mazingira bora kwa vijana, wajasiriamali na wazalishaji wadogo wadogo ili kuhakikisha sio tu wanaboresha maisha yao kwa kunufaika na shughuli zao, bali pia wanaendelea kutoa mchango mkubwa wa maendeleo na ukuaji wa uchumi wa taifa . Serikali iliyoongoza na hayati Rais Magufuli, kwa upande mmoja ilifanya jambo jema ilipochukua hatua kama kuwaruhusu mamilioni ya wamachinga kuendesha shughuli zao katika maeneo ya miji na majiji, kuruhusu wachimbaji wadogo wa madini kuendelea na shughuli zao kwenye maeneo yaliyokuwa yakihodhiwa na makampuni makubwa ya nje na kurudisha ardhi kwa baadhi ya maeneo machache kwa wakulima wadogo.
Pamoja na changamoto kadhaa zilizojitokeza, kwa ujumla hatua hizo zilitoa fursa kwa wananchi kujipatia kipato kupitia shughuli zao halali. Lakini kwa upande mwingine kuongezeka kwa vikwazo kadhaa kwenye mfumo na gharama za kodi na leseni imekuwa kikwazo kwa shughuli nyingi sana kwa wajasiriamali na wazalishaji wadogo, hususani vijana ambao wameamua kuchukua hatua binafsi za kujikwamua kiuchumi kutokana na wimbi la ukosefu wa ajira. Hii si tu sio inaumiza vijana, wajasiriamali na wazalishaji wadogo, pia inakwamisha jitihada za ubunifu na uvumbuzi zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ambao ungekuwa ni mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.
Changamoto nyingine ni ukweli kwamba Tanzania bado ina miradi mikubwa ya ujenzi ambayo haijakamilika kama vile Bwala la umeme la Nyerere, ujenzi wa reli ya kati kiwango cha Standard Gauge (SGR) na miradi mingine mingi ya mabarabara, viwanja vya ndege, madaraja, miundombinu ya huduma za afya nakadhalika. Miradi hii yote pamoja na kwamba baadhi yake ilizua mjadala kuhusu mzigo wa ugharamikiaji na manufaa yake kwa wananchi walio wengi, inahitaji kukamilishwa kwa sababu mingi tayari ilishaanza hivyo kwa namna yoyote ile Serikali ya Rais Samia italazimika kuikamilisha miradi hii ambayo utekelezaji wake ulianzishwa na mtangulizi wake. Kikubwa kinachopaswa kuangaliwa ni kuona ni kwa namna gani miradi hiyo inaweza kuendelea bila kuathiri miradi inayolenga ustawi wa wananchi wengi moja kwa moja.
Uwekezaji Kutoka Nje na Ndani
Moja ya malalamiko makubwa yaliyokua yakitolewa na wafanyabiashara wakubwa na wa kati Tanzania, ni pamoja na uwepo wa mazingira yasiyotabirika kwa uwekezaji. Hii ikijumuisha utendaji kazi wa kutumia nguvu kutoka taasisi za serikali zinazosimamia biashara, ukiritimba katika kupata vibali mbalimbali, pamoja na mabadiliko ya mara kwa mara ya sheria na taratibu za ufanyaji biashara nchini. Mfano, uwepo wa sheria za makosa mbalimbali zisizoruhusu dhamana kama sheria ya uhujumu uchumi, imewaweka wawekezaji wengi katika njia panda pale kunapotokea ukakasi au kutoelewana kati yao na serikali. Si mara ya moja au mbili katika kipindi cha miaka mitano kutokea watendaji wa makampuni mbalimbali kuwekwa mahabusu huku kesi zao zikijadiliwa, wengi waliishia kulipa mambilioni ya fedha. Serikali inaweza kuona njia hii kuwa ni rahisi katika kutatua migogoro ila kwa wafanyabiashara wengi ni kitendawili, waamue kuweka uhuru wao rehani na kusota mhabusu au kuulipia na kuendelea kufanya biashara, hii si namna endelevu ya kujenga biashara.
Pamoja na hayo kumekuwepo na malalamiko juu ya TRA kuleta makadirio makubwa kwa wafanyabiashara, na kisha kuchukua hela toka kwenye akaunti zao, kabla ya muafaka wa pande mbili kufikiwa au wakati mwingine kuishia kufunga kabisa biashara za watu. Jambo hili liliibuliwa Bungeni mwezi Februari na mbunge Nape Nauye, ambapo alielezea namna vikosi vya ukusaji kodi vilivyogeuka kuwa mwiba na kuangusha biashara nyingi. Raisi Samia atahitajika kuhakikisha mfumo wa ukusanyaji wa kodi unakuwa endelevu, mazingira ya biashara yanakuwa rafiki na yakuvutia kwa ustawi wa biashara na wafanyabaishara kwani ni kiungo muhimu kwa ustawi wa uchumi
Ripoti ya hali ya uchumi kutoka Benki Ya Dunia inaonyesha kuwa moja ya jambo lilosababisha ukuwaji endelevu wa uchumi wa takribani miongo miwili ilikuwa ni mafuriko ya uwekezaji toka nje. Hata hivyo ripoti inaonyesha ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita uwekezaji toka nje umepungua kwa kiasi kikubwa ikiwa chini ya wastani wa nchi zingine kusini mwa jangwa la Sahara. Raisi Samia atakuwa na jukumu la kuifanya Tanzania iwe tena kitovu cha uwekezaji wa mitaji mikubwa na ya kati kutoka nje.
Ujuzi na Elimu Ya Juu
Ikiwa imebakia miaka mitano kuelekea kukamilisha dira ya maendeleo 2025, dira iliyowekwa katika utendaji takribani miaka 30 iliyopita. Moja ya chachu kubwa inayotajwa katika kufikia malengo ya dira hii ni ujuzi wa nguvukazi, yaani ujuzi wa Watanzania katika sekta mbalimbali. Takwimu za kibiashara zinaonyesha mpaka sasa mfumo wetu wa mafunzo unatoa mameneja watatu kwa mtendaji (technician) mmoja, jambo ambalo linahitajika kubadilika na kutengeneza watendaji wengi zaidi.
Jambo lingine ambalo Serikali ya Rais Samia itakabiliana nalo ni mfumo wa ugharamikiaji wa elimu ya juu hapa nchini. Kupitia mfumo huu wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESLB) ilioanzishwa kwa sheria namba 9 ya mwaka 2004 na marekebisho yake ya mwaka 2007, 2014 na 2016, imepelekea mzigo wa deni kwa wananchi takribani laki tano ambao hutambulika kama wanufaika. Mfumo huu wa ugharamikiaji elimu ya juu unapaswa kuangaliwa upya sambamba na malengo la elimu ya juu yenyewe ili kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali watu wake bila ya kuwabebesha mzigo mkubwa wa madeni utakaoathiri hali za maisha ya wananchi hao.
Kujenga Umoja, Kuziba Ufa wa Mpasuko wa Kisiasa
Ni dhahiri kwamba hivi karibuni kumekuwa na mpasuko wa kisiasa hususani baina ya chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani. Hii ilimpelekea aliyewahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Tanzania awamu ya pili, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba hivi karibuni kuonya kwamba vyama vya siasa hivi sasa vinataka kuwagawa Watanzania, vimekuwa makabila mapya ambayo watu hujitambulisha nayo, kitu ambacho ni hatari kwa umoja wa taifa letu. Kauli hii ya Mzee Warioba ikichukuliwa kwa umakini na kuona haja ya kurekebisha ufa huu utakuwa ni uponyaji wa taifa letu ambao historia itamkumbuka Rais Samia Suluhu ambaye katika hotuba yake ya kwanza alionesha iko haja ya kuzika tofauti zilizojitokeza kwa ajili ya mustakabali mwema wa Tanzania. Ili mpasuko huu wa kisiasa uweze kumalizwa, unahitaji utayari wa makundi yote ya kisiasa, yaani wahusika wote wa vyama vya siasa nchini. Katika hili, wanasiasa wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuliponya taifa kuliko kusubiri wito wa viongozi wa makundi kama vile ya dini. Kihistoria, waasisi wa taifa la Tanzania walipoamua kujenga umoja wa kitaifa, walitumia siasa kutuunganisha, hawakutumia dini wala historia za makabila kuunganisha watu, vivyo hivyo viongozi wetu wa sasa wafanye hivyo.
Hivyo basi kisiasa rais Samia anakabiliwa na jukumu la kuimarisha umoja wa kitaifa. Kwa maana jukumu la kuwaleta watu pamoja kama taifa ni jukumu la kisiasa na yeye kama mwanasiasa mwenye madaraka ya juu kabisa katika nchi, yaani Urais, na anatarajia kukabidhiwa kijiti cha Unyekiti wa chama tawala CCM hivi karibuni, anao wajibu wa kutoa uongozi kwa makundi yote ya kisiasa na kijamii kushikamana kwa pamoja ili kuweza kudumisha uhuru, umoja na haki katika taifa la Tanzania. Hii ni muhimu ili wananchi wote wajione huru kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa lao, kutoa maoni pasipo bughudha na kutimiza wajibu mbalimbali kwa uhuru kama desturi na sio shuruti.
Sambamba na la umoja, Serikali ya Rais Samia itakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha maamuzi yoyote yale ya kisiasa nchini msukumo wake unatoka ndani hasa kwa kundi kubwa la wananchi ambalo ni wakulima na wafanyakazi. Sauti za kundi hili, yaani wakulima na wafanyakazi, kwa pamoja ni muhimu sana kusikilizwa na viongozi ili kuhakikisha maslahi yao yanapatikana kadiri iwezekanavyo. Pia, viongozi wa kisiasa wasiwabuguzi wafanyakazi na wakulima katika jitihada zao za kujiunga pamoja kupitia vyama, ushirika au jumuia zao zenye lengo la kupigania maslai yao.
Changamoto za UVIKO-19
Kijamii licha ya kuwepo changamoto mbalimbali katika sekta ya afya kwa ujumla, bado Serikali ya Rais Samia itakabiliana na changamoto ya UVIKO-19 kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya dunia ambayo inayokabiliwa na changmoto ya UVIKO-19. Janga hili sio tu limeendelea kugharimu maisha ya wanadamu pia kudhoofisha uchumi wa mataifa mbalimbali. Serikali chini ya Rais Samia inawajibika kuendelea kushiriki katika mapambano hayo dhidi ya janga hili.
Moja ya uamuzi uliowekwa kiporo na mtangulizi wake ni juu ya chanjo ya UVIKO-19, tamko la mwisho la Wizara ya Afya lilitolewa na Waziri Februari 2021 alisisitiza hakukua na mpango wowote wa kupokea chanjo ya UVIKO-19, hata hivyo Waziri alisema bado wanafanya tathmini ya chanjo hizo. Kwasasa zaidi ya mataifa 11 Afrika yameshapokea chanjo,huku kwa Afrika Mashariki Rwanda, Kenya na Congo DRC zikiwa za kwanza kupokea chanjo hizo. Je Raisi Samia ataendelea na msimamo wa mtangulizi wake uliosimamia zaidi kwenye kujifukiza na tiba za asili au kutakuwa na mabadiliko katika swala zima la UVIKO-19?
One Response
jamani Mbona uses usumbufu kwenye vibali vya mchanga umekua mkubwa