The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mfumo Wetu Wa Uchumi Na Dhana Ya Ukosefu Wa Ajira

Ukosefu wa ajira ni tatizo la kutegemea kwenye mfumo wa uchumi unaoweka mbele faida kuliko kitu kingine chochote kile.

subscribe to our newsletter!

Mijadala kuhusu tatizo la ajira nchini Tanzania imekuwa ikichukua sura nyingi sana. Hii inatokana na ukubwa wa tatizo lenyewe linaloendelea kuumiza vichwa vya watungaji sera na wadau wengine. Kwa mfano, kwa mujibu wa Taarifa ya ya Uchumi ya Mwaka 2018, kila mwaka wahitimu zaidi ya laki nane wanamaliza vyuo katika ngazi mbalimbali za elimu nchini Tanzania. Hata hivyo, uwezo wa kuajiriwa upo chini sana ya kiwango hicho.

Hali hii imepelekea baadhi ya wasomi na wachambuzi kuzilaumu taasisi za elimu kwa kusema kwamba zimeshindwa kuandaa wahitimu wao vizuri kulingana na “matakwa ya soko la ajira.” Lawama hizi zinaenda mbali zaidi kwa kutaka kupitiwa upya kwa mitaala ya elimu na kuifanya iendane na mahitaji ya soko la ajira. Hili limefanyika kwa kiasi fulani kwa kuja kwa Sera Mpya ya Elimu ya mwaka 2014 ambayo, pamoja na mambo mengine mengi, inalenga kuwasaidia wanafunzi kuwa na stadi maalumu zitakazo wasaidia katika maisha yao ya kawaida mara tu wanapo hitimu masomo yao.

Sambamba na hili, kuna wito wa kuwataka wahitimu kujiajiri na kuwa wajisiriamali, kwa madai kwamba nchi haina ajira za kutosha kwa ajili ya wahitimu wote. Hapa, lawama si kwa vyuo tena au wahitimu kwa kukosa sifa za kuajirika bali mfumo mzima wa kiuchumi ulioshindwa kuzalisha ajira za kutosha kwa ajili ya wahitimu wa kada mbali mbali nchini. Kwa ufupi, naona hoja ya ujasiriamali inalenga zaidi kumlaumu muhitimu binafsi kwa kushindwa “kufikiri nje ya boksi.” Hoja hii ya watu kujiajiri pia inapigiwa chapuo na wanasiasa wa vyama vyote vya kisiasa wakiwaeleza wahitimu kwamba wasikae na kubweteka kwa kusubiria kuajiriwa. Hapo ndipo tunaona masomo ya ujasiriamali yakifundishwa, sio vyuoni tu bali hata kwenye makundi ya watu kupitia taasisi mbali mbali au hata wanaoitwa wahamasishaji, au motivotional speakers, kama wanavyojulikana kwa kimombo.

Hoja za msingi zakwepwa

Nafikiri hoja hizi zinashindwa kubainisha chanzo hasa cha tatizo la ajira na nini kinapaswa kufanywa ili kutatua tatizo hilo. Nitafafanua. Tatizo la ajira ni tatizo la mfumo wa uchumi unaotawala dunia, yaani mfumo wa uchumi wa uzalishaji wa kibepari ambao kwa namna moja au nyengine unafaidika na kinachoitwa ukosefu wa jira. Hii ni kutokana na ukweli kwamba uwepo wa wimbi kubwa la watu wasiokuwa na ajira, hufanya wenye mitaji kuwa na uhuru wa kuwafanyisha kazi waajiriwa wao kwenye mazingira magumu ikiwemo kuwalipa mishahara duni bila kuwa na hofu ya kukosa nguvu kazi wakijua kwamba kuna kundi kubwa la watu wasio na ajira huko nje na wako tayari kujiunga na kampuni zao na kukubali malipo duni zaidi. Ubepari, mfumo wa uzalishaji mali unaosukumwa na malengo ya kujipatia faida zaidi, hauwezi kuwepo bila ya uwepo wa tatizo la ukosefu wa ajira.  Kwa hiyo, kuzungumzia tatizo la ajira ni kuzungumzia mapungufu ya mfumo wa kiuchumi wa kibepari ambao unataka kampuni iwe na wafanyakazi wachache kadiri inavyowezekana ili iweze kudumu kwenye mazingira ya ushindani na kuwahakikishia wamiliki wake faida. Kutatua tatizo la ajira ni kutafakari namna tunavyoweza kupangilia upya mfumo wetu wa kiuchumi na kijamii.

Kimsingi, tatizo la ajira pia lina uhusiano na uchumi wa kidunia. Tatizo la ajira limekithiri zaidi kwenye nchi masikini ukilinganisha na nchi tajiri, ingawa nchi hizo pia zimekumbwa na tatizo hilo. Lakini nchi tajiri zinanufaika na mfumo wa uchumi wa ulimwengu. Nchi tajiri zimeweka mirija ya kuchukua rasilimali za nchi masikini. Kwa hiyo, badala ya ajira kujengwa ndani, faida ya uwekezaji wa nchi tajiri kwa nchi masikini inakwenda kuwekezwa nje, yaani exploitation by repatriation kama inavyojulikana kwa kimombo.  Kwa hiyo, sera hizi za uwekezaji katika uchumi wa kidunia wa soko huria, mtaji una hama na faida inayojengwa haiwekezwi ndani ya nchi masikini bali inaenda nje ya nchi hizo kujenga ajira nje. Hili litapaswa likabiliwe ipasavyo ili juhudi za kutatua tatizo la ukosefu wa ajira nchini ziweze kufanikiwa.

Leo hii tunaona namna ujasiriamali unavyotukuzwa kama vile watu hawafanyi huo ujasiriamali, wakati ukipita mitaani utaona wamachinga, mama lishe na baba lishe na wafanyabiashara wengine wapo. Si jambo jipya watu kufanya hivyo kwani mwanadamu ana historia ndefu ya kutafuta majawabu ya maisha yake. Lakini leo watu wanapozungumza kuhusu ujasiriamali na kujiajiri kama vile hiki ni kitu kipya ambacho hakijawahi kutokea wala kufanyika katika dunia hii. Watu kujihusisha na ujasiriamali haiondoi umuhimu wa kuwa na uchumi imara unaoweza kuzalisha ajira za maana kwa wananchi wake.

Kwa hiyo tunaona kwamba suala si kuandaa watu waajirike kwenye soko, bali kuandaa wananchi ambao watakuwa sehemu ya uzalishaji wa nchi yao. Tunapaswa kufanya ajira iwe matokeo ya uzalishaji wa kijamii. Hii maana yake ni kwamba kadiri watu wanavyo shiriki kwenye uzalishaji wa nchi yao ndivyo ajira nazo huongezeka. Kumuandaa kijana ili aweze kuwa na bei nzuri kwenye “soko la ajira” ni kumfanya binadamu awe bidhaa kama zilizovyo bidhaa zingine inayoweza kuuzwa na kununuliwa. Moja ya athari ya dhana hii ni kwamba ajira inakuwa ni jambo la mtu binafsi na si la kijamii tena. Ni muhimu kujenga uchumi wa kitaifa ambao utazingatia suala la uzalishaji wa ajira kwa wananchi wake kwa kujenga viwanda vya ndani vingi, vitakavyotumia malighafi za ndani na zitakazochakatwa kwa kutumia teknolojia ya ndani.

Nassoro Kitunda ni mhadhiri msaidizi wa sosholojia, Mwenge Catholic University. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nassorokitunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Hii makala imeandikwa vyema sana, imejaribu kupanga propaganda za mwenye mitaji dhidi ya wafanyakazi, mfumo wa kinyonyaji dhidi ya nguvu ya kupinga unyonyaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *