The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Ukoloni wa Ndani’: Kwa Nini Watu Waishio Maisha ya Kiasili Wanaendelea Kuteseka Tanzania? 

Ujinga wa kutofahamu mienendo na hekima za wafugaji wa asili ndio chanzo kikuu cha mivutano na sera zinazoambatana na ubaguzi, vitu vinavyoshuhudiwa kwa sasa katika jamii za wafugaji Tanzania, ikiwemo Ngorongoro. 

subscribe to our newsletter!

Kufuatia tangazo la Machi 12, 2021, la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) juu ya amri yake ya kuwataka watu 45 wenyeji wa Ngorongoro kuondoka kwenye eneo hilo na kuwataka watu hao wavunje nyumba zao wenyewe pamoja na shule, zahanati, vituo vya polisi, makanisa na misikiti, kiongozi mmoja wa mila wa jamii ya Wamaasai, Mtevi Oleshando, alitoa maoni yake kama ifuatavyo:

“Tunashangaa mazingira haya ya sasa ambayo yanafanyika bila mazungumzo ya kukaa pamoja wakati tulikaa pamoja na wakoloni. Wakoloni walikaa na baba zetu, kwa nini leo sisi Watanzania tusikae na Watanzania wenzetu ambao ni wataalamu? Nchi yetu ni nchi ya amani, ni nchi ambayo binadamu tunatakiwa kuwa na upendo, ni nchi ya mshikamano. Lakini inaonekana kama sisi wafugaji tumebaguliwa na kuwekwa pembeni wakati sisi ni Watanzania halali kama Watanzania wengine walivyo.”

Tunafahamu kwamba usimamizi wa kikoloni ni aina ya mamlaka ambayo watu fulani wanalazimisha watu wengine kuwa chini ya utawala wao. Hata hivyo, kiasi cha nguvu walichotumia kilitegemeana na wakati na aina ya ubeberu (kwa mfano, ubeberu wa Wareno ulitofautiana na ubeberu wa Wajerumani na ule wa Wajerumani pia ulitofautiana na ule wa Waingereza). Ni dhahiri kwamba katika maoni yake hayo, mzee Mtevi Oleshando hakua na nia ya kusema kwamba wakati wa ukoloni hali ilikuwa nzuri sana. Alichomaanisha ni kwamba hata wakati wa ukoloni wao kama wafugaji waliweza kusikilizwa kwa kiasi fulani kuliko hali ilivyo leo!

Wakati wa ukoloni wa Waingereza, kulitengenezwa mfumo wa utawala usiokuwa wa moja kwa moja, au Indirect Rule kama unavyojulikana kwa kimombo. Mfumo huo hufafanuliwa kama njia ambayo Serikali ya kikoloni ya Uingereza iliitumia kwa ajili ya kuziendesha jamii za Kiafrika kupitia taasisi zao za kiasili, au taasisi za kimila. Lakini tusisahau kwamba, hata kama ule utawala wa nyuma ya pazia wa Indirect Rule ulitofautiana na sera ya Wajerumani, haikumaanisha kutokuwepo kwa maadili kutokana na mitizamo ya “viwango vya kistaarabu” vya watu “wa magharibi” yaani Wazungu.

Kwa maneno mengine, sera ya mamlaka ya Waingereza ilitathmini vipengele vya utamaduni wa makabila ya Afrika kama ni vizuri au ni vibaya kulingana na maadili yao wao Waingereza. Vilevile, tusisahau kwamba wakati wa ukoloni, piramidi la kijamii liligawanywa katika daraja tatu: Waingereza (au Wazungu/watu wa Ulaya) walikuwa kwenye daraja la juu na walipewa haki zote za kila aina; Wahindi waliwekwa kwenye ngazi iliyofuata na walipewa haki kadhaa; na Waafrika walikuwa chini kabisa ya piramidi na walinyimwa haki zote. Kwa hivyo mzee Oleshando alipouliza swali “Wakoloni walikaa na baba zetu, kwa nini leo sisi Watanzania tusikae na Watanzania wenzetu ambao ni wataalamu?” alikuwa anatafakari swali muhimu. Wafugaji wakisikilizwa hata na mamlaka za ukoloni, kwa nini leo Watanzania wenzao hawakai nao tena kwa ajili ya kuwasikiliza na kujaribu kuelewa matatizo ya maisha yao?

Uhifadhi Tanzania na kwengineko

Ni ukweli kwamba dhana ya fortress conservation (yaani, aina ya uhifadhi ambao hauruhusu watu kuishi ndani ya hifadhi za taifa) ilianzishwa kama mfumo wa uhifadhi kule Marekani ya Kaskazini na baada ya hapo imehamasisha utengenezaji wa hifadhi za mataifa mengine duniani kote.

Katika eneo la Tanganyika, hifadhi ya taifa ya kwanza ilikuwa Serengeti, ambayo ilikuwa ni matokeo ya ushawishi wa taasisi ya Uingereza iliyoitwa Society for the Preservation of the Fauna of the Empire (SPFE) iliyokuwa ikitetea utekelezaji wa hifadhi za taifa barani Afrika kwa lengo la kupata wanyama pori kwa ajili ya michezo yao ya uwindaji, au trophy hunting kwa kimombo. Lakini, kabla ya 1959, mwaka ambao Sheria ya Uhifadhi wa Eneo la Ngorongoro ilitangazwa na wenyeji wa Serengeti kuhamishiwa Ngorongoro, kulikuwa na uvumilivu fulani juu ya mwendelezo wa makaazi na shughuli za kibinaadamu pamoja na ufugaji ndani ya hifadhi ya kitaifa ya Serengeti (na ndani ya mapori ya akiba mbali mbali).

Wakati SPFE ilitaka kupiga marufuku makaazi ndani ya hifadhi, wasimamizi wakoloni waliokuwepo Tanganyika walikuwa dhidi ya mfumo wa fortress conservation kwa sababu walifahamu kwamba wenyeji wangeathiriwa sana, na migogoro ya ardhi ingeongezeka. Kwa hivyo, suala la kuwepo kwa binadamu katika hifadhi ya taifa likabaki katika utata kwenye sheria na halikuweza kutatuliwa mpaka toleo la National Parks Ordinance la mwaka 1959 lililokataza shughuli zote za kibinadamu, ingawaje katazo lenyewe lilihusu wakazi wanaohusika tu na si watalii ambao waliendelea kufanya shughuli zao kwenye eneo husika. Kwa ajili ya kulitatua tatizo hili, wakoloni walikaa na viongozi wa kimila na kukubaliana kwamba wenyeji wahamie sehemu za Ngorongoro na Loliondo. Makubaliano hayo yaliwaruhusu wafugaji kuishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na kuendelea na shughuli zao za ufugaji (hata bondeni) na kilimo cha kujikimu.

Baada ya Uhuru, kutokana na Arusha Manifesto, tamko lililotolewa na Julius Kambarage Nyerere wakati wa Arusha Conference, mkutano wa kimataifa juu ya uhifadhi wa mazingira uliofanyika miezi kadhaa kabla ya Uhuru, viongozi wa Tanganyika huru na baadaye Tanzania waliruhusu na kukuza utekelezaji wa mfumo wa fortress conservation kwa manufaa ya kiuchumi. Baada ya Uhuru, mfumo wa fortress conservation umeongezeka kwa nguvu na leo nchini Tanzania kuna jumla ya hifadhi za taifa zaidi ya 22 na mapori ya akiba au game reserves zaidi ya 38. Katika sehemu hizi za hifadhi makaazi na shughuli za binadamu haziruhusiwi. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba sehemu hizi zote zilikuwa makaazi na nyumbani kwa watu. Hata katika mapori tengefu, au game controlled areas, ambayo yanaingia kwenye ardhi za vijiji, wananchi wananyanyaswa kwa sababu ya safari za utalii za kuwinda wanyama pori.

Hata katika Eneo la Uhifadhi la Ngorongoro (NCA), Serikali pamoja na UNESCO na taasisi za kimataifa za uhifadhi zinalazimisha kuwekwa vikwazo vya kulima, kufuga, na kuishi bondeni, na kujenga nyumba zisizo za kimila. Na zaidi, siku hizi zimeanzisha tena utaratibu wa kuwaondoa wenyeji bila ya kukaa nao na kuwasikiliza maoni yao, kama tulivyoona mzee Oleshando akilalamika.  Ardhi walizopewa wafugaji kwa makubaliano ya zamani sasa ziko hatarini tena. Suala hapa linakuja, Je, ni kwa nini, baada ya Uhuru, wafugaji wamekuwa wanatengwa kutoka kwenye michakato ya kufanya maamuzi yanayowahusu wao wenyewe kiasi hiki huku haki zao zikiwa hazitambuliwi kabisa? Bila ya shaka sababu ni nyingi ila hapa ningependa kufafanua kidogo kuhusu dhana ya “ukoloni wa ndani” kulingana na kipengele cha ubaguzi.

Tatizo la Ngorongoro ni tatizo la ukoloni wa ndani

Kama mwanaanthropolojia Mbrazili, mimi nahusisha swali langu hapo juu na dhana ya “ukoloni wa ndani” iliyotumiwa kwa mara ya kwanza na wasomi wa Marekani ya Kusini wakiongelea jinsi Dola inavyokandamiza haki za makundi madogo, hasa za watu wa asili, au indigenous peoples. Matumizi ya aina hii ya madaraka yanaonekana kama yale ya utawala wa ubeberu wa kigeni lakini yanatumika na wenye mamlaka dhidi ya wananchi wenzao. Wale wanaopewa mamlaka ya taifa huru wanayatumia kama vile ni wakoloni wa aina fulani: wanachukua ardhi na maliasili za watu wa asili, na wanataka wananchi wa jamii hizi waachane na utamaduni wao na mfumo wao wa maisha.

Wakoloni hawa wa ndani wanayalazimisha maadili yao juu ya wenzao bila ya kufahamu vizuri wala kuheshimu mitazamo waliyonayo watu hao juu ya maisha, maarifa ya kiasili, au traditional knowledge, na changamoto wanazopata katika maisha yao ya kila siku. Ndiyo maana wanasosholojia na wanaanthropolojia kadhaa wanatumia hiyo dhana ya “ukoloni wa ndani” wanapoongelea kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na Dola. Kwa hivyo, ukoloni wa ndani ni matumizi ya nguvu yanayotumiwa na Dola dhidi ya makabila au makundi madogo ambayo yananyanyaswa, kutumiwa, na kubaguliwa. Licha ya kwamba michakato ya ujenzi wa mataifa ya Marekani ya Kusini na Afrika inatofautiana, ninaamini kwamba tunaweza kupata mifano kadhaa ya kutuwezesha kutumia dhana ya “ukoloni wa ndani” tunapoongelea kuhusu hali ya watu waishio maisha ya asili nchini Tanzania.

Kutokana na kukuwa kwa uwekezaji na utalii wa safari za wanyama pori, jamii zilizopo karibu au kwenye sehemu za hifadhi zipo hatarini. Jamii hizi hazipewi haki hata ya kusikilizwa kuhusu changamoto wanazozipata. Kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4, 1999, Rais wa Tanzania, akiamua, anaweza kubadilisha aina ya udhibiti wa ardhi kutoka ardhi ya kijiji kwenda ardhi ya jumla ama ardhi za uhifadhi. Hii maana yake ni kwamba hata kama wanakijiji wanazo hati za ardhi za vijiji, bado wanaweza kupoteza ardhi zao. Na hata kama sheria inathibitisha kwamba wao wananchi wana haki ya kusikilizwa, kutoa maoni, na kushiriki kwenye mchakato unaohusu ardhi zao, historia inatuonyesha kwamba utaratibu haufuatwi kama inavyotakiwa. Kama ilivyotokea kwa wafugaji wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), hakuna fursa inayotolewa kwa wahusika kukaa pamoja na mamlaka za Serikali na kusikilizwa maoni yao kwa ajili ya kutafuta njia muwafaka. Kama tangazo la hivi karibuni la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro lilivyotolewa, wanafamilia hujikuta tu ghafla wamepewa siku 30 kuhama kotoka katika ardhi zao.

Idhini ya kutengeneza

Wakati mwingine, “makubaliano” yanaonekana kama yapo vile, ila tukiangalia kwa karibu, tunagundua kwamba yanakuwa ni makubaliano yaliyotengenezwa na wenye nguvu (mamlaka), yaani yenye kuwaacha wananchi bila njia nyingine ya kutoka. Mwisho wa siku, masharti yanalazimishwa na wawekezaji wenyewe pamoja na Serikali. Wananchi wanatarajiwa wakubali tu. Wasomi kadhaa wanaita huu mchakato kama idhini iliyotengenezwa, au manufactured consent kwa kimombo. Kwa hivyo, kitendo cha kukaa pamoja bila ya kuwasikiliza watu wanaohusika kinaweza kuwa demokrasia ya mchezo wa kuigiza tu. Wananchi kama binadamu wanastahili kueleweka katika mahitaji yao na aina ya maendeleo wanayofikiria kuwa ni muhimu kwao kwa mukhtadha wa kosmolojia yao (yaani maana ya mfumo mzima wa maisha wanayoamini kutokana na itikadi na uhusiano kati yao na mazingira wanayoishi).

Tungeweza kusema kwamba kiini cha “ukoloni wa ndani” nchini Tanzania kinaonekana kwa kupitia dhana ya maendeleo. Na kwenye dhana ya maendeleo kama ilivyojengwa wakati wa Ujamaa, kilimo kinachukuliwa kama shughuli kuu na muhimu ya kiuchumi. Wale ambao wanaishi aina tofauti ya maisha, wanaongea lugha ambazo siyo Kiswahili (ama za kibantu) na wanaendelea kuvaa kimila wanabaguliwa. Tangu wakati wa Ujamaa, wafugaji na wawindaji wa asili wameonekana kama watu duni (Operesheni Dress up au Maasai Progress Plan ya mwishoni  mwa miaka ya 1960 ni mfano mmoja mzuri).

“Wamaasai wanaonekana kuwa muhimu kwenye matangazo ya Serikali ya kuwavutia watalii, ila hawakaribishwi kila mahali nchini.” – Aline Rabelo.

Wamaasai wanaonekana kuwa muhimu kwenye matangazo ya Serikali ya kuwavutia watalii tu, kama jinsi ya kuonyesha vipengele vya utajiri wa utamaduni wa Tanzania. Watalii wanavutiwa sana na Wamaasai na wafugaji wa asili wengine (na wawindaji wa asili vile vile). Ila hawakaribishwi kila mahali nchini. Licha ya kuwa ni muhimu sana kwa uchumi kupitia sekta ya utalii na vyakula, wakihama hama huwa hawafai tena. Wakihitaji sehemu za malisho wanaonekana ni wafugaji wenye kuleta shida, au troublemakers, tu. Si kila mtu asiye mfugaji anafahamu kwamba ufugaji wa asili unaleta maarifa yanayosaidia uhifadhi wa mazingira. Ujinga wa kutofahamu mienendo na hekima za wafugaji wa asili ndio chanzo kikuu cha mivutano na sera zinazoambatana na ubaguzi. Na kwa kweli mara nyingi wafugaji wanatizamwa na Watanzania wenzao kama vile ni wageni kutoka nje: Wakenya au mgeni mwenyeji, au an internal other kwa kimombo.

Lakini ukweli ni kwamba hakuna maendeleo ambayo yanaweza kudumishwa kwa mantiki hii. Maendeleo endelevu lazima yajumuishe makundi ya aina zote yawe makubwa au madogo – na hapa simaanishi kwamba hizi jamii ni za watu wachache tu; zaidi ninazungumza kuhusu dhana inayolingana na makundi madogo na wale ambao wametengwa katika mchakato wa ujenzi wa taifa. Hawa wanapaswa kusikilizwa na kueleweka katika nadharia na itikadi zao za maendeleo ili njia mpya zipate kuonekana. Kwa mantiki hii, kila mwenyeji ni lazima awe na haki yake ya kutambuliwa kama mwananchi halali na halisi na aweze kuhisi kuwa ni sehemu ya jamii hiyo ya kitaifa inayodhaniwa kuwa ni ya amani, upendo, na mshikamano.

Aline Rabelo ni mwanaanthropolojia na raia wa Brazil ambaye yupo mwaka wa mwisho wa masomo yake ya uzamivu (Ph.D) katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Rio de Janeiro (UFRJ) kilichopo nchini Brazil na Shule ya Masomo ya Juu ya Sayansi ya Jamii (EHESS) iliyopo nchini Ufaransa. Aline ameishi na kufanya utafiti nchini Tanzania kwa vipindi tofauti tofauti tangu mwaka 2012. Kwa maoni, anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni arabelo.anthropology@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

4 Responses

  1. Stop eviction of maasai society at ngorongoro conservation area authority

  2. Mimi ni Masai kutoka Simanjiro mkoani manyara,.Kwa kweli tunaonewa na kunyanyaswa, yaani hii inasikitisha sana kwamba Wamaasai wanaonekana kuwa muhimu tu kwenye matangazo ya kuifadisha serikali kwa kuwavutia watalii, lakini leo hii watanzania wameshindwa kutusikiliza? wanachukua ardhi na maliasili za watu wa asili, na wanataka wananchi wa jamii hizi tuachane na utamaduni wetu😓, naumia sana,

  3. Mi ni Edward ole phlilipo kwa kweli sisi wafugaji hasa wamasai tunatumika tu kama wanyama kwani sisi hata heshima yetu haipo tunafukuzwa tu kama wanyama wa porini serikali ikitaka eneo la wamasai utasikia inatakiwa mmhame kweli hata ustaarabu was kibinadamu hakuna, Kuna eneo la mkungunero simanjiro wamasai Kila wakati wanapigwa na watu was Park bila hata huruma , kiukweli The chanzo Initiative hayo yote ni ya kweli . Leo hii pamoja na ukoloni wa kizungu kuisha bado tu sisi wafugaji tu pale pale kwenye mnyororo was ukoloni hatuwezi toa maamuzi , tunaushi kwa hofu siku zote kwani serikali inatupeleka kama wanyama , INANIUMA SANA SANA

  4. MAUMIVU YALIYO WAPATA WAMASAI
    Wakati wamasai wa Loliondo wanaondolewa kule kwenye Ardhi yao kwa faida ya Mwarabu wamasai tuliumia Sana

    Wakati wamasai wa Ngorongoro wanapewa Notisi za kuondoka, wamasai tumeumia Sana

    Wakati wamasai wa Morogoro wananyang’anywa maeneo ya malisho kwa na Ardhi yao kupewa wakulima wakubwa,
    wamasai tuliendelea kuumia Sana
    Kweli sisi bado ni watanzania ?
    Jamii ya kimasai imewahi kuiona hii nchi haiwahusu kutokana na machungu walioyapitia kwenye Ardhi yao.mi naona kuwa sisi sio watanzania kulingana na matukio hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *