Kati ya Mei 3 na 4 mwaka huu wa 2021, kitendo cha kinyama kilitokea dhidi ya mtoto mwenye ualbino aliyekuwa na umri wa miaka kati ya mitano na sita aliyeokotwa akiwa amekatwa mikono yake yote na akiwa tayari amepoteza maisha. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Mei 17, 2021, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema kwamba LHRC kwa kushirikiana na wadau wake kutoka shirika la Tabora Vision Community (TAVICO) walipokea taarifa za kusikitisha kuhusu mauaji ya mtoto mwenye ualibino na mwenye jinsia ya kiume ambaye jina wala makazi yake hayakuweza kufahamika mara moja. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwili wa mtoto huyo uliokotwa na wanakijiji ukiwa umetelekezwa kwenye majani eneo lenye shamba karibu na dimbwi la maji katika kitongoji cha Usadala kilichopo katika kijiji cha Utemini, kata ya Ndono, wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.
“Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hili,” Henga aliendelea kusema kwenye taarifa yake hiyo, “mwili huo ulikutwa ukiwa umekatwa mikono yote miwili. Macho yote mawili yameng’olewa. Sikio moja la mkono wa kushoto limekatwa na sehemu zote za siri zikiwa zimeondolewa.” Taarifa za tukio hili zilitolewa kwenye Kituo cha Polisi Wilaya ya Uyui siku hiyo hiyo na viongozi wa kijiji majira ya saa sita au saa saba mchana ambapo maafisa wa jeshi hilo walifika kwenye eneo la tukio majira ya saa tisa mchana na kuukagua mwili wa marehemu ikiwa ni pamoja na kupiga picha mbalimbali.
Tukio hili ni la kwanza kuripotiwa tangu mwaka huu wa 2021 uanze. Ni habari mbaya na mpya kuanza kusikika tena masikioni mwa Watanzania, hususan jamii ya watu wenye ualbino nchini. Hofu, wasiwasi, na mashaka vimeanza kurejea tena baada ya kipindi cha takribani miaka kadhaa iliyopita. Tukio hili la kinyama ni la kukemewa na kupigwa vita na kila mmoja wetu kwa ustawi wa watu wenye ualbino nchini Tanzania.
Imani za kishirikinaÂ
Kwa mujibu wa jarida la shirika lisilo la kiserikali linalohusika na utetezi na ustawi wa watu wenye ualbino nchini Under The Same Sun la Septemba- Desemba, 2010, na la Julai- Septemba, 2018, matukio hayo ya ukatili, ukatwaji, au unyofolewaji viungo vya mwili, au ufukuliwaji makaburi na mauaji ya kinyama dhidi ya watu wenye ualbino yalianza kuripotiwa na vymbo vya habari katika kipindi cha miaka ya 2006 kwa kuhusishwa na imani za kishirikina. Juhudi mbalimbali zilianza kuchukuliwa kwa kushirikiana na Serikali ambazo ni pamoja na kuanzishwa kwa kambi za watu wenye ualbino. Baadhi ya kambi hizo ni pamoja na Kabannga (Kigoma), Buhangija (Shinynga), Mitindo (Mwanza), Pongwe (Tanga), Kitengule (Tabora) na Mugeza (Kagera).
Kwa mujibu wa Under The Same Sun, kisayansi, ualbino ni hali ya ukosefu wa rangi asili kwenye ngozi, macho, na nywele. Mtoto mwenye Ualbino huwa na ukosefu au upungufu wa rangi asili mwilini ambayo huathiri rangi ya ngozi, macho na nywele. Lazima baba na mama wawe na vinasaba vyenye ualbino. Lazima vinasaba vikutane wakati wa kutunga uja uzito. Kwa Tanzania na Afrika Mashariki mtu mmoja katika kila watu 1,400 ana ualbino.
Mbali na vitendo vya ukatili na mauaji, watu wenye ualbino tunazo changamoto mbalimbali. Changamoto hizo ni pamoja na saratani ya ngozi kwani jua linaharibu vibaya ngozi ya mtu mwenye ualbino. Watu wenye ualbino wengi hufariki katika umri wa miaka 40 kutokana na saratani. Matibabu stahiki hayapatikani kwa wakati. Changamoto nyengine ni uoni hafifu. Uoni hafifu unatofautiana kutoka mtu na mwingine. Imani potofu dhidi ya watu wenye ualbino pia ni changamoto nyengine, kwamba watu wenye ualbino ni mashetani, laana, chanzo cha utajiri, ni makosa ya mama, hawafi bali hupotea, vidonda mwilini ni maumbile yao, na hawana thamani yoyote. Dhana hizi potofu hazina ukweli wowote. Ni ukosefu wa elimu na uelewa juu ya watu wenye ualbino, jinsi wanavyopatikana, changamoto zao, na namna ya kuzitatua.
Serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine, inalo jukumu la kuendelea kutupia jicho juu ya usalama wa watu wenye ualbino katika jamii kwa kutoa elimu ya uelewa juu ya ualbino katika jamii. Jamii ikielewa, watu wenye ualbino wataishi kwa amani na utulivu. Serikali pia, kupitia wizara ya afya, iendelee kuboresha na kugharamia matibabu ya saratani ya ngozi na upatikanaji wa mafuta kinga kwa watu wenye ualbino. Serikali iendelee kusimamia sheria zake ili watu wenye ualbino wapate fursa za ajira. Hali hii itawasidia watu wenye ualbino na wenye sifa na vigezo kupata ajira na kujikwamua na utegemezi.
Serikali pia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iweke mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia kwa watu wenye ualbino ili wapate elimu bora itakayowawezesha kushindana katika soko la ajira kwa viwango na ujuzi stahiki kama wanafunzi wengine. Ni muhimu kwa jamii pia kusomesha watoto bila ubaguzi ndani ya familia. Watu wenye ualbino wanauwezo sawa na watoto wengine wasio na ualbino. Watu wenye ualbino ni binadamu kama walivyo binadamu wengine katika jamii na duniani kote. Kwa pamoja tuungane kupiga vita matendo yote maovu dhidi yao. Waishi kwa amani wakiwa hai na pia wanapofariki kusitokee ufukuliwaji wa makaburi walikoifadhiwa wakapumzike.
Tukisimama kwa pamoja, bubujiko la machozi ya watu wenye ualbino nchini Tanzania na kwengineko litakwisha.
Joram Bwire ni afisa programu anayehusika na masuala ya jinsia, wanawake, watoto na watu wenye ulemavu katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni jnyambaya@humanrights.or.tz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhrari wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.
2 responses
Jamii na serikali ina wajibu wa kutunza ustawi wa watu wenye ualbino.
Elimu inahitajika Kwa Watu Kuacha kuamini Imani Potofu na Imani Za Kishirikina dhidi ya Watu wenye Ualbino Na Kuamini Mungu🙏