Rais Samia Suluhu Hassan ameweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke Tanzania. Siku za hivi karibuni, Mama Samia alifikisha siku 100 za kwanza za uwepo wake madarakani tangu aapishwe kuchukua wadhifa huo Machi 19, 2021. Wadadisi kadhaa tayari wameshachambua siku 100 hizo kutoka katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kwenye masuala kama siasa na demokrasia, usawa wa kijinsia, uchumi na nyanja nyenginezo. Kwa upande wangu, ningependa kusema machache katika muktadha wa elimu ya nchi yetu. Msukumo mkubwa wa andiko hili ni ukweli kwamba elimu ni injini kubwa ya maendeleo ya mtu kwani katika ulimwengu wa sasa ili mtu aweze kuboresha maisha yake ni lazima awe na elimu.
Kuna hatua kadhaa ambazo Serikali ya Mama Samia imechukua mpaka sasa zinazoashiria kwamba kiongozi huyo mkuu wa nchi amedhamiria kutatua baadhi ya changamoto sugu zinazoukabili mfumo wetu wa elimu kama nchi. Moja kati ya hatua hizi ni uamuzi wa Serikali kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na mitaala ya ufundishaji. Wakati wa akilihutubia Bunge la 12 mnamo Aprili 12, 2021, Rais Samia alionesha nia ya kubadilisha na kuanzisha mchakato wa mapitio na uboreshwaji wa mitaala inayotumika kufundishia sasa ili iweze kukidhi haja, matakwa na hali ya sasa kuelekea elimu ujuzi itakayomwezesha mwanafunzi kuwa na maaarifa ujuzi.
Ni jambo la kufurahisha kuona kwamba Serikali, kupitia Wizara ya Elimu, imeanza kupokea maoni na mapendekezo yanayotolewa na wadau juu ya nini kifanyike ili kuboresha sheria na kanuni zinazounda Bodi ya Kitaaluma ya Walimu. Hatua hii ilifuatiwa na mkutano kati ya Wizara ya Elimu na wadau wa elimu uliofanyika Juni 26, 2021, jijini Dar es Salaam, ambapo maoni juu ya uboreshwaji wa sekta ya elimu ya Tanzania yalitolewa na Serikali kuahidi kuyafanyia kazi. Hatua hii ni muhimu sana ukizingatia kilio cha siku nyingi kutoka kwa wadua wa elimu nchini ambao zaidi ya mara moja wameitisha kuchukuliwa kwa hatua hiyo muhimu inayolenga kuifanya elimu inayotolewa nchini kuendana na mahitaji ya karne ya 21.
Ajira kwa walimu
Ndani ya siku hizi 100 za Rais Samia, Serikali pia imeweza kuongeza idadi ya walimu watakaofundisha shule za sekondari na msingi. Jumla ya ajira 6,946 kwa walimu zimetolewa, husasan wa masomo ya hisabati na sayansi kwenda kufundisha. Utoaji wa elimu bila ada na michango umepelekea kuongezeka kwa wanafunzi mashuleni huku kukiwa hakuna ongezeko la walimu hivyo kupelekea utoaji wa elimu kutokua bora.
Rais Samia pia ameweza kukarabati shule 17 kongwe nchini ili kuboresha mazingira ya kufundishia. Shule zilizokarabatiwa ni pamoja na Kilakala Sekondari, Shule ya Wasichana Tabora, Pugu, Korogwe, Sengerema na nyinginezo. Ndani ya siku zake 100 madarakani, Rais Samia amewezesha ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu mbalimbali katika shule hizo, ikiwemo kuboresha mifumo ya majitaka, madarasa, vyoo, mabweni, nyumba za walimu pamoja na ofisi.
Inafahamika kwamba ufundishaji hauwezi kufanikiwa kama hakuna vitabu vya kufundishia. Rais Samia anaonekana kulitambua jambo hili kutokana na hatua yake ya kuwezesha upatikanaji wa vitabu vya kufundishia hasa kwa shule za msingi. Kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, Serikali imewezesha kupatikana kwa vitabu vya kiada 4,443,386. Ni wazi kwamba ongezeko hili litapelekea wanafunzi kusoma kwa raha kwani imepunguza uwiano mkubwa uliokuwepo kati ya kitabu kimoja na mwanafunzi.
Kulipwa kwa madeni ya walimu
Kwa zaidi ya miaka mitano hivi sasa, mishahara ya wafanyakazi wa kada ya elimu haijawahi kupandishwa. Lakini ndani ya siku 100 za Rais Samia Serikali imeweza kulipa madeni ya walimu na kuwapandisha madaraja. Kwa mfano, Serikali imelipa malipo ya malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya Shilingi 74.12 bilioni kwa watumishi 36,126. Kati ya fedha hizo, Shilingi 32.669 bilioni zimelipwa kwa walimu 11,272.
Aidha, Rais Samia amewezesha kupunguza kodi (PAYE) katika mishahara kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane. Hii ni hatua muhimu kwani itaboresha maslahi ya walimu na kuongeza ari ya kufanya kazi. Kiuhalisia, walimu hali zao sio njema kwani ughali wa maisha unapanda kila uchwao huku kukiwa hakuna ongezeko la mishahara.
Eneo jengine ambalo Rais Samia ameweza kulifanyia kazi ndani ya siku zake 100 madarakani ni hili la kuongeza bajeti ya elimu kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ukilinganisha na mwaka wa fedha 2019/2020. Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anabainisha kwenye ripoti yake ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 2020 kuanzia 2013/2014 hadi 2019/2020, bajeti ya sekta ya elimu ilikua chini ya asilimia 15. Ongezeko la bajeti, ambapo kwa sasa ni juu ya asilimia 15, litaiwezesha Serikali kutekeleza mipango na malengo ya kutoa elimu bora inayokidhi mahitaji ya sasa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu na kuboresha vifaa vya kusoma na kufundishia.
Safari bado ndefu
Hata hivyo, pamoja na hatua hizi, bado sekta ya elimu ya umma nchini Tanzania inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zitahitaji utatuzi wa Serikali. Hii ni pamoja na changamoto ya uhaba wa fedha. Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, Wizara ya Elimu imepokea fedha sawa na asilimia 74 tu na kufanya kuwepo na upungufu sawa na asilimia 26. Upungufu huu bila shaka unahusika na uzoroteshaji wa utoaji wa huduma za elimu kwa kupelekea upungufu wa madawati na kukosekana kwa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Upangaji wa bajeti usiojitosheleza pia umepelekea Serikali kutumia fedha zilizopangwa kutoa na kuendeleza elimu kuingia katika matumizi mengine ya wizara. Kwa mfano, CAG alibainisha Machi 31, 2021, kwamba Wizara wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) haikupanga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za waafunzi wenye mahitaji maalumu.
Pia, wingi wa wanafunzi mashuleni, hali inayotokana na utolewaji wa elimu bila ada, unapelekea kuwa na uwiano finyu wa mwalimu na wanafunzi. Hali hii inaathiri ufanisi katika ubora wa elimu nchini. Kuongezeka kwa wanafunzi kunapelekea upungufu mkubwa wa walimu ambao ndio msingi mkubwa wa kufanikisha utoaji wa elimu hivyo kuathiri ujifunzaji na usomaji wa mwanafunzi kwani mwalimu atashindwa kumfikia mwanafunzi mmoja mmja.
Kukosekana kwa mipango ya kuwajengea uwezo walimu walio kazini nako kunapelekea baadhi yao kushindwa kumudu kazi zao vizuri kwa sababu ya kukosa mafunzo hayo. Hii huwafanya walimu washindwe kuwasaidia watoto kwa viwango tarajiwa na kutokana na baadhi ya walimu kukosa hisia za kazi na motisha kwenye ufundishaji, hawajitumi, kujiendeleza na wala kuwa wabunifu wa namna ya kuwasaidia watoto kujifunza.
Rais Samia ameonesha mwelekeo mzuri katika kutatua changamoto za sekta ya elimu nchini. Ni muhimu sana, hata hivyo, Serikali yake ijielekeza katika kukidhi mahitaji ya utoaji wa elimu bora inayokidhi mahitaji ya sasa. Inafahamika kwamba Ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii ni lazima elimu itolewayo iwe bora na yenye kumuwezesha mtu kuboresha maisha yake katika kufikiri, kubuni na kujitambua. Ili kukidhi haja hii ni lazima Serikali ikaongeza uwekezaji katika sekta ya elimu na kuifanya iweze kuendana na mahitaji ya sasa.
Muhanyi Nkoronko ni mdau na mtafiti wa masuala ya elimu na sera hasa katika elimu msingi. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe Muhanyinkoronko88@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @MuhanyiSenior. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.
2 responses
Hongera sana Kaka hakika nimependa sana kazi yako, MUNGU akuinue zaidi
Hongera sana kaka Mwenyezi Mungu azidi kukuongoza