Kuna baadhi ya viumbe ni vigumu kuwaainisha. Kati ya hao yuko popo. Popo anaruka kama ndege lakini ni mamalia. Kwa mujibu wa wataalamu, huyu ndiye mamalia pekee kwenye sayari yetu mwenye uwezo huo wa kupaa! Kuna nyangumi pia. Yeye huishi majini kama samaki lakini pia ni mamalia. Wawili hao wanabeba mimba, wanazaa na kunyonyesha, sifa zisizolandana na samaki na ndege. Mwanadamu asiyeeleweka msimamo wake anatajwa kuonesha tabia za upopo.
Upopo, undumilakuwili, na unafiki ni tabia isiyopendwa katika jamii nyingi na katika siasa tabia za upopo zina gharama kubwa. Aghlabu, hufikia hatua pande zote mbili kinzani ambazo mwanasiasa ananasibishwa nazo, humkataa na hatimaye hubaki anaelea hajulikani yuwapi! Chama cha ACT-Wazalendo kipo kwenye sintofahamu ya upopo. Ni chama cha upinzani lakini pia ni mshirika mdogo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya huko visiwani.
Huwezi kujadili chama cha ACT-Wazalendo bila kuiangalia Zanzibar na Tanzania Bara kila moja kiupekee. Mapambano ya ACT-Wazalendo (Zanzibar) yanaweza yasiwe sawa na yale ya ACT-Wazalendo (Tanzania Bara), ingawa pande hizi mbili zinahitajiana kupata uhalali na sura ya kitaifa ili kufikia malengo yao.
Chama hiki kipo kwenye hatua tofauti za ukuaji kila upande. Ingawa ACT-Wazalendo ilianza kupata nguvu zaidi Tanzania Bara, ni Zanzibar ndio imekuwa ngome yake kuu baada ya waliokuwa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), wakiongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, kuhamia ACT-Wazalendo. ACT-Wazalendo (Zanzibar) imerithi sehemu kubwa ya mtandao wa CUF na hivyo kukifanya kuwa chama kamili kinachoweza kushindana, na pengine hata kushinda, siku Tanzania itaweza kuendesha chaguzi huru na za haki.
Lakini hali ni tofauti Tanzania Bara ambako ACT-Wazalendo bado ni chama kichanga kisicho hata na ngome kuu, ukiacha kiasi ya ushawishi kwenye baadhi ya majimbo wanayotoka viongozi wake wakuu, akiwemo Kiongozi wa Chama Zitto Kabwe na Katibu Mkuu, Addo Shaibu. Lakini hata hao, kwao maoni yangu, huko kwao hawakubaliki kwa kiwango kikubwa kama Joseph Mbilinyi (Sugu) anavyokubalika Mbeya au Freeman Mbowe anavyokubalika Hai.
Ushawishi na nguvu ya CHADEMA
Ushawishi na nguvu kubwa ya CHADEMA ni mtihani mwingine kwa ACT-Wazalendo. Ukweli ni kwamba CHADEMA wamewaacha mbali sana ACT-Wazalendo kama tutarejea rekodi za chaguzi mbili zilizopita. Mnamo mwaka 2015, CHADEMA ilipata viti 35 (sawa na asilimia 13.26) vya kuchaguliwa ukilinganisha na kimoja cha ACT-Wazalendo, ambayo ni sawa na asilimia 0.38. Kwenye upande wa udiwani, tofauti ilikuwa ni asilimia 20.30 za CHADEMA kwa asilimia 0.81 za ACT-Wazalendo. CHADEMA pia ilipata nafasi 36 ya viti maalumu.
Mwaka 2020, licha ya kupata viti vinne kupitia Zanzibar, ambavyo ndio vingi zaidi vya ubunge kwa vyama vya upinzani, ACT-Wazalendo huku bara ilipigwa dafrau na kuondoka patupu, huku CHADEMA ikiambulia kiti kimoja na vingine 19 vya akinamama. ACT-Wazalendo haikufikisha hata asilimia tano ya kura zote za wabunge ambayo ingewawezesha kupata viti maalum.
Tafsiri ya takwimu hizi ni kuwa hata ongezeko la wanachama kutoka ACT-Wazalendo na nguvu mpya waliyoipata Zanzibar haikuwa na athari chanya kubwa huku Tanzania Bara kiasi cha kubadili nafasi yake ukilinganisha na vyama vingine. Ukijaribu kupima maoni na mitazamo ya watu, CHADEMA wameendelea kuaminika mbele ya Watanzania wengi kama chama kikuu cha upinzani kinachoweza kuwa mbadala wa chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM).
CHADEMA imeendelea kukua kwa kasi hadi katika maeneo ambayo hayakuwa ngome zao kiasili. Kwa kiasi fulani CHADEMA ilishaingia kusini mwaka 2015 na kushinda kiti kimoja cha ubunge. Isingekuwa vikwazo dhidi ya demokrasia katika awamu ya tano na wizi wa uchaguzi katika uchaguzi wa 2020, huenda CHADEMA ingepiga hatua zaidi kanda ya kusini ikifaidika na mgogoro na mmeguko ndani ya CUF.
CHADEMA imethibitisha uwezo wa kushinda mkoa wowote nchini, ukiacha Zanzibar ambako bado haijaweza kupenya vyema. Chama hicho kimekuwa chaguo la vijana wengi wasomi wanaotaka siasa za mabadiliko kiasi kwamba hata ilipoondokewa na viongozi wao mahiri, wengine waliziba nafasi kirahisi tu.
Udhaifu wa mkakati wa ACT-Wazalendo
Mtu anaweza kusema kwamba ACT-Wazalendo sio chama pekee kinachohangaika kukua, kuna vingine vina hali mbaya zaidi. Lakini chama hupimwa kwa rasilimali na fursa zake ambazo ingeweza kuzitumia na kupata matokeo makubwa. Huko Zanzibar, ACT-Wazalendo ina mtaji mkubwa wa watu wenye weledi mkubwa wa kisiasa. Huku Tanzania Bara nako, ACT-Wazalendo ina viongozi wasomi wenye maono na vipawa vya hali ya juu vya kujenga hoja, wakiwemo Zitto, Shaibu na wengineo.
Rasilimali ya watu wasomi wenye weledi waliyonayo ACT-Wazalendo imeweza kujitokeza kwenye nyaraka na machapisho kadhaa chama hicho imekuwa ikitoa. Vile vile, wengi kati ya waliopata kusoma ilani za vyama za mwaka 2020 wanaamini kuwa chama hiki kilikuwa na ilani bora kabisa kuliko vyama vyote. Hata idara yao ya mawasiliano ilijitahidi sana kusambaza vipeperushi vyenye taarifa za kuvutia mitandaoni.
Bahati mbaya ni kwamba mchango wa ilani na machapisho mengine ya kisera, kama yale ya uchambuzi wa ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hazina mchango mkubwa katika kukipa chama mvuto wa kisiasa, huenda labda kwa sababu Watanzania wengi si wasomaji. Siasa za Tanzania pia wala sio za tafakuri bali hisia zaidi. Kiitikadi, ACT-Wazalendo inajinasibisha na Ujamaa, kikidai kinataka kuhuisha Azimio la Arusha kupitia Azimio la Tabora, andiko tamu, lenye mvuto lakini, tena, lililoshindwa kuwashawishi makabwela.
Zitto na upopo wa ACT-Wazalendo
Wakati upopo wa ACT-Wazalendo (Zanzibar) unaweza kutokana na hatua ya chama hicho kujiunga na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa upande wa Tanzania Bara kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe anaweza kutajwa kama chanzo cha upopo wa chama chake katika upande huu wa Muungano.
Kuna madai kwamba Zitto amewekwa mfukoni na viongozi waandamizi wa CCM. Ukosoaji wake Serikali ya Rais Samia unaonekana una staha fulani, na wakati mwingine Zitto huonekana hata kumtetea zaidi. Wanaomfuatilia katika mitandao ya kijamii humtania kuwa anabembeleza uteuzi!
Namna Zitto anavyojihusisha na Serikali ya Samia ni wazi kwamba anakigharimu chama chake kwa kiasi kikubwa, hususani huku Tanzania Bara. Mbinu pekee inayoweza kukutambulisha wewe kama kiongozi imara wa upinzani nchini mwetu ni kuwa na uwezo wa kuiwajibisha Serikali kwa kuikosoa bila ya kupepesa macho.
Kitendo cha Zitto kujitokeza hadharani na kumsifu Rais Samia kila wakati anapofanya jambo linalomfurahisha lakini akakaa kimya pale Samia anapotoa kauli zinazoonekana kwenda kinyume na matakwa ya walio wengi, kama kauli ya kutaka Katiba Mpya na mikutano ya kisiasa isubiri, kinamuweka Zitto na chama chake katika hali mbaya sana kisiasa.
Unaweza kusema Zitto ana tatizo la taswira hasi mbele ya ‘wapambanaji’ kutokana na matendo yake hayo lakini pia kwa sababu ya historia yake. Tetesi nyingi zimesambaa dhidi yake hasa katika kipindi alipokuwa CHADEMA ambako alifukuzwa. Katika tetesi hizo, Zitto hutajwa kama mtu msaliti. Miongoni mwa tetesi nyingi ni zile zinazomtaja kama mtu wa karibu na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.
Wakati huu ambapo Kikwete anatajwa kuwa na ushawishi Ikulu ya Dodoma, shaka ya uaminifu wa Zitto inaongezeka. Tetesi hizi zina uzito na athari kisiasa kwa sababu siasa inaamuliwa na mitazamo bila kujali imejengwa kwenye misingi ya ukweli au uongo. Anavyotazamwa Zitto ndivyo kitakavyotazamwa pia chama chake kwa sababu yeye ni kiongozi mkuu wa chama hicho.
Kama kiongozi pia, Zitto ameshindwa kutoa muongozo kwa ACT-Wazalendo. Wakati CHADEMA wakiendesha programu mbalimbali za kujenga chama ikiwemo, kwa mfano, kampeni ya kugawa kadi mpya za kisasa za chama kwa wanachama wao, makongamano ya ndani na mikutano ya kukusanya fedha za kuendesha chama chao na mengineyo mengi, ACT-Wazalendo ipo ipo tu.
Ni ngumu kufahamu ni nini programu ya chama hicho kwa sasa. Hata kwenye mjadala wa Katiba Mpya uliopamba moto kwa sasa, ni ngumu sana kukiona chama hicho kikitoa mchango mkubwa katika kushinikiza takwa hilo. Unaweza kusema pengine wanajipanga, sijui. Lakini yote haya yanamuweka shakani zaidi Zitto Kabwe kama kiongozi wa chama.
Haja ya ACT-Wazalendo kujitafakari
Wasiwasi wangu ni kwamba kama ACT-Wazalendo watashindwa kukaa chini kama chama cha siasa cha upinzani na kutafakari mustabali wake chini ya Serikali ya Rais Samia, juu ya namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea kutokea nchini kwa sasa, chama hicho kitakuwa kipo hatarini kupoteza hata baadhi ya wanachama wake na viongozi wake waandamizi.
Wanachama na viongozi wa ACT-Wazalendo wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanakitoa chama chao kwenye hadhi ya upopo iliyonayo kwa sasa. Je, watahitaji kuchukua maamuzi magumu ya kumtoa Zitto, mwanasiasa msomi, mwenye akili nyingi, kama kiongozi wa chama? Hiki sirahisi kufanyika lakini nadhani ndiyo kitu muhimu kufanyika.
Katika siasa zetu za watu, haiba ya kiongozi wa chama kwa asilimia kubwa ndiyo huwa haiba ya chama husika. Si jambo jema lakini ndiyo uhalisia. Kwa kumtoa Zitto kama kiongozi wa chama, ACT-Wazalendo kitakuwa na nafasi ya kujitenga na makandokando yake yanayohusika na kukipa chama haiba mbaya.
Kuna suala la mbadala pia. Kama Zitto akiondolewa kama kiongozi wa chama, nani ndani ya ACT-Wazalendo anaweza kujaza nafasi yake kwa sasa? Haya yote ni masuala ambayo wanachama wa ACT-Wazalendo inabidi wayadadisi kwa kina. Kwa sasa, hata hivyo, ili Zitto aweze kukipa chama chake mafanikio kinachoyahitaji ni lazima ajitathmini yeye kama mtu binafsi na vipi matendo yake yanakiweka chama chake katika wakati mgumu.
Haya ni baadhi tu ya maswali magumu ambayo ACT-Wazalendo watapaswa kuyatafakari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.