Dar es Salaam. Banki ya Dunia (WB) imeonesha kusikitishwa kwake na ucheleweshwaji wa utolewaji wa takwimu kuhusu hali ya uchumi nchini na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), huku ikidai kwamba baadhi ya takwimu zitolewazo na ofisi hiyo ni “dhaifu.”
Taasisi hiyo ya kifedha ya kimataifa inayotoa mikopo na misaada kwa serikali ilibainisha hayo kwenye ripoti yake ya hali ya kiuchumi inayoangalia mwenendo mzima wa uchumi Tanzania kwa mwaka huu mpaka kufikia Juni 30, 2021 iliyozinduliwa mnamo Julai 29,2021.
“Ofisi ya Takwimu ilitoa takwimu za pato la taifa kwa robo ya pili na ya tatu ya mwaka 2020, Januari 25, 2021, lakini takwimu za robo ya nne ya mwaka 2020 hazijatolewa mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2021,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Ucheleweshwaji huu upo Tanzania tu kwani ripoti hiyo inabainisha kwamba nchi zote katika ukanda wa Afrika Mashariki zenye uwezo sawa wa kitakwimu na Tanzania zimeshatoa ripoti za robo ya kwanza ya mwaka 2021 na wameanza kupitia upya taarifa za mwaka 2020.
The Chanzo ilitaka kufahamu kutoka kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk Albina Chuwa ni kwa nini hali hii inatokea lakini jitahada za kumpata hazikuzaa matunda baada ya simu ya mkononi kuita bila kupokelewa.
Takwimu za pato la taifa hutolewa kwa vipindi vya miezi mitatu mitatu (robo za mwaka). NBS iliweka kwenye tovuti yake muhtasari wa takwimu (highlights) wa robo ya kwanza ya mwaka 2021 (Januari-Machi) mnamo Julai 2021. Tovuti ya NBS pia inaonesha muhtasari wa takwimu za robo ya nne ya mwaka ziliwekwa Machi 2021.
Katika ripoti yake ya Februari 2021, Benki ya Dunia ilieleza kwamba Tanzania ilikua nchi pekee kwa Afrika Mashariki ambapo ukusanyaji wa takwimu na utolewaji wa takwimu uliathiriwa vikali na janga la corona. Hii ni licha ya kwamba Tanzania ni nchi pekee ambayo iliendelea na shughuli zake kwa sehemu kubwa wakati janga la Uviko-19 lilipoingia.
Lakini mbali na ucheleweshwaji uliopo katika utolewaji wa takwimu, Benki ya Dunia pia inaonesha kusikitishwa na ubora wa takwimu zitolewazo na NBS, huku ikitaja vyanzo vya takwimu zinazotumiwa kwa uwekezaji, huduma, uzalishaji viwandani na ajira kuwa ni “dhaifu.”
“Utafiti wa biashara haukidhi viwango. Tofauti kubwa zinaonekana kati ya takwimu rasmi na zile zinazotoka kwenye makampuni yenyewe au takwimu za kodi ya ongezeko la thamani,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Benki ya Dunia imependekeza kuwa katika mapitio mapya ya sera ya pato la taifa iweke ulazima kuwa takwimu za kipindi kimoja zifanyiwe mapitio (revision) kabla ya takwimu zingine hazijaachiliwa.
Mapendekezo haya ni tofauti na utaratibu wa sasa ambapo mapitio ya takwimu yanafanyika baada ya takwimu za mwaka mzima kutoka.
Ripoti hiyo imeelezea kuwa Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha zimedhamiria kuendelea kutoa msaada wa kiufundi kwa Tanzania katika kuimarisha utoaji wa Takwimu