Dar es Salaam. Licha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kutangaza miongozo katika utumiaji wa usafiri wa umma ili kupambana na usambaaji wa ugonjwa hatari wa UVIKO-19, The Chanzo inafahamu kwamba utekelezaji wa maagizo hayo unafanyika kwa kiwango kidogo sana hali inayotia hofu kama lengo la kuwekwa kwake linaweza kufanikiwa.
Katika stendi nyingi za mabasi jijini Dar es Salaam ambazo The Chanzo ilizitembelea kuangalia utekelezwaji wa maagizo hayo ya Mkuu wa Mkoa ilibainika kwamba bado wananchi wengi hawavai barakoa, hakuna unawaji wa mikono kutumia maji tiririka na sabuni, wala upakiaji wa abiria kwenye vyombo vya usafiri wa umma haufanyiki kwa kuzingatia uwezo wa daladala husika kama maagizo yanavyotaka.
Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam ililazimika kutoa maagizo hayo baada ya ripoti kwamba hali ya usambaaji wa janga la UVIKO-19 kwenye jiji hilo kuu la biashara siyo ya kawaida. Misiba mingi imekuwa ikiripotiwa huku UVIKO-19 ukitajwa kama sababu. Wagonjwa wengi ambao ni waathirika wa virusi vya UVIKO-19 pia wapo mahospitalini wakipatiwa matibabu.
Baadhi ya miongozo ambayo Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imeweka kwa ajili ya kudhibiti usambaaji wa ugonjwa wa UVIKO-19 kwenye usafiri wa umma ni sharti la kuvaa barakoa kwa abiria wote wanaoingia kwenye vyombo vya usafiri wa umma kama vile daladala, vivuko na magari ya mwendokasi.
Dar es Salaam pia imepiga marufuku vyombo vya usafiri wa umma kujaza watu mpaka kupitiliza, na kuwataka wamiliki wa vyombo hivyo kuruhusu madereva na makondakta kupakia abiria kulingana na uwezo wa daladala husika, maarufu kama ‘level seat.’
Lakini utekelezaji wa maagizo yote haya unaonekana kuwa hafifu huku wananchi wakitaja sababu kadhaa kwa nini utekelazaji wa amri hizo na Mkuu wa Mkoa umekuwa wa kusuasua.
Matuga Maalim Matuga ni dereva wa daladala zinazofanya safari zake kati ya Posta na Makumbusho. Hapa anaieleza The Chanzo hali ya utekelezaji wa agizo la uvaaji wa barakoa katika daladala: “Hili agizo linatekelezwa kwa kiwango kidogo sana. Abiria wengi kusema kweli hawavai barakoa. Lakini sisi kama madereva na makondakta tunajitahidi kutoa elimu juu ya uvaaji wa barakoa. Tunajaribu wakati mwingine kuhakikisha kwamba abiria ambaye hajavaa barakoa hapandi gari ila muda mwengine inakuwa ngumu.”
Edwin Semkiwa, mkazi wa Ubungo na mtumiaji mkubwa wa usafiri wa umma, akitoa maoni yake kuhusu utekelezaji wa maagizo hayo, amesema: “Maagizo yanatekelezwa kwani muamko wa wananchi kuvaa barakoa umeongezeka kidogo kulinganisha na hapo awali. Lakini bado kunahitajika kuongeza nguvu ya uhamasishaji kwani bado wananchi hawajalichukulia suala la uvaaji wa barakoa kama jambo la msingi.”
Hata hivyo, Semkiwa ameonesha kusikitishwa na hali ya ukosefu wa maji safi na sabuni katika stendi nyingi jijini, kitu ambacho huwafanya watu wengi wasinawe mikono kabla ya kuingia kwenye daladala.
Baadhi ya abiria wameiambia The Chanzo kwamba kwa hali ilivyo sasa ni rahisi kwa maagizo hayo kupuuzwa kwani inaonekana kama vile ni hiari ya mtu kufuata au kutokufuata. Wamesema kwamba kama mamlaka zingefanya utekelezaji wa maagizo hayo kuwa ya lazima hali ingekuwa tofauti kwenye usafiri wa umma na juhudi za kupambana na UVIKO-19 pengine zingefanikiwa.
The Chanzo ilimtafuta Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla kufahamu kwamba kama ofisi yake ina mikakati yoyote ya kuhakikisha maagizo aliyoyatoa katika kukabiliana na janga la UVIKO-19 yanatekelezwa lakini juhudi za kumpata hazikufua dafu baada ya simu yake kuita bila kupokelewa mara kadhaa.
Suala la kuwepo kwa ulegevu ni jambo ambalo Makalla analifahamu. Akiongea na waandishi wa habari mapema mwezi huu, Mkuu wa Mkoa huyo alikiri kwamba tathimini iliyofanywa na timu kutoka ofisini kwake ilibaini kwamba kuna baadhi ya maeneo ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam masharti ya kupambana na UVIKO-19 hayatekelezwi ipasavyo.
Hata hivyo, Makalla hakubainisha hatua ambazo ofisi yake inapanga kuchukua ambazo zinalenga kubadilisha hali hiyo.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo aliyepo Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni haulelukelo@gmail.com. Kama una maoni kuhusiana na habari hii unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.