The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali Ina Mpango Gani Kutusaidia Kukabiliana na Makali ya UVIKO-19?

Viongozi wetu watushike mkono wasiache hili zimwi liitwalo UVIKO-19 litutafune bila ya kuwepo na msaada wowote.

subscribe to our newsletter!

Siku za hivi karibuni kumekuwa na vilio vingi mtaani kwetu, na kwa kiasi kikubwa vilio hivi vimekuwa vikitokana na uwepo wa idadi kubwa ya misiba inayotokea katika jamii zetu. Watanzania wengi pia wamekuwa wakigugumia sana na suala la ugumu wa maisha, hali inayotokana na kupanda kwa gharama ya maisha kufuatia ongezeko la bei kwenye bidhaa na huduma mbali mbali.

Ni wazi kwamba janga la UVIKO-19 linaloendelea kutesa mataifa mengi ulimwenguni, ikiwemo Tanzania, linahusika na vilio hivi. Ugonjwa huu hauathiri maisha ya watu kwa kuwafanya waumwe  na hata kufariki . UVIKO-19 unaathiri maisha ya watu kwa kudhoofisha uchumi wa nchi husika pia. Inaonekana Watanzania hawajanusirika na athari zote hizi. 

Huku mtaani, kuna viashiria kadhaa vinavyoonesha kwamba hali za maisha za watu walio wengi wa kipato cha chini ni za kusikitisha mno. Wakati upatikanaji wa pesa umekuwa mgumu, hiyo inayopatikana hupotea ndani ya sekunde chache kutokana na ughali wa bidhaa na huduma muhimu. 

Ngoja nikupe mfano. Lita moja ya mafuta ya kupikia ilikuwa inauzwa Sh2,000 hadi Sh2,500 hivi karibuni tu. Lakini kwa sasa kama huna Sh4,000 hadi Sh5,000 kwa lita hiyo hiyo, Mangi atakurudisha nyumbani.

Vita dhidi ya UVIKO -19

Ni ngumu kuacha kuipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua inazochukua kupambana na janga la UVIKO-19. Uamuzi wake wa kufuata mtazamo wa kisayansi katika kukabiliana na janga hili bila shaka utasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi ambao vinginevyo wangefariki kama Serikali ingeendelea kushikilia msimamo wake kwamba UVIKO-19 haipo Tanzania. 

Lakini kama wasemavyo Wahenga, “Kizuri hakikosi kasoro.” Juhudi hizi za Serikali za kukabiliana na UVIKO -19 zinawajibika kwa kiasi kikubwa kufanya hali za maisha ya Watanzania walio wengi kuwa ngumu. Nitatoa mfano mmoja wa namna juhudi hizi nzuri za kutulinda dhidi ya janga hili la kidunia zinavyochangia kufanya maisha ya baadhi yetu kuwa magumu. Nitatoa mfano wa eneo ambalo mimi nafanyia kazi na hivyo kuwa muathirika namba moja. Na hili linahusiana na agizo la kukataza mikusanyiko isiyo ya lazima kama vile matamasha.

Kama mdau wa masuala ya masoko, mimi na wenzangu tumekuwa tukishiriki katika kuandaa matamasha mengi ya muziki na burudani hali ambayo imekuwa ikitusaidia kujiinua kiuchumi. Lakini kwa sasa idadi ndogo ya matamasha yanayofanyika imekuwa ikitoa matokeo hasi kwa waandaaji.

Matamasha hayo yamekuwa yakifanyika lakini watu wamekuwa wakihudhuria kwa uchache, hali inayopelekea hata wateja/wadau wanaotegemea kutupa kazi za kuandaa matamasha kama hayo kusita na kusema watafanya kwa siku za usoni. Hii imeathiri sana juhudi zetu za kutupatia vipato kwani hizi ndiyo kazi tunazitegemea kuendesha maisha yetu. Ni wazi kwamba tukiamua kumsikiliza kila mmoja wetu atakuwa na ushuhuda wa kutoa wa namna juhudi zinazolenga kutulinda na majanga pia zinatuathiri kiuchumi.

Makali ya UVIKO-19

Sasa naomba nisije nikaeleweka vibaya nikaonekana kama vile nataka Serikali iachane na utaratibu wake wa sasa na kuurudia ule uliokuwepo zamani uliodai kwamba nchi hii ilishaushinda ugonjwa wa UVIKO-19. La hasha! Ninachomaanisha ni kwamba wakati Serikali inachukua juhudi za kuzuia maambukizi ya UVIKO-19, inapanga kuchukua hatua gani zaidi kuwasaidia wananchi kukabiliana na athari/madhara ya kiuchumi yanayosababishwa na juhudi hizi? 

Maana hili ni jambo la wazi kabisa kwa Serikali kuliona na haiwezi kujitia hamnazo kudhani kwamba haiwajibiki kuboresha ustawi wa wananchi wake. Unaposema kwamba daladala zipakie ‘level seat’ na wakati unajua hujapunguza bei ya petroli au diseli utakuwa unafahamu kwamba hiyo itaathiri vipato vya wamiliki wa daladala, madereva, na makondakta pia. 

Wajibu wa Serikali si kuwalinda wananchi wake wasipate maradhi tu bali pia kuhakikisha kwamba ustawi wa jumla wa wananchi hao unaimarika. Ni lazima Serikali isaidie wananchi wake kukabiliana na athari zitokanazo na UVIKO-19 na juhudi za kukabiliana na janga hilo. Hivi ndivyo Serikali nyengine ulimwenguni zinafanya. 

Majirani zetu hapo Kenya walitenga fungu maalumu la pesa kwa ajili ya jambo kama hili. Pesa hizo zilitumika moja kwa moja katika kusaidia kaya zote maskini zinazopambana na changamoto ya kukosa chakula. Kundi la wasanii, ambalo hujumuisha watu wengine wanaofanya kazi katika sekta ya burudani, nalo lilipatiwa fungu lake kwa ajili ya kupunguza makali ya ugonjwa huu. Hatua hii ilitokana na uamuzi wa Serikali ya Kenya kukataza matamasha ya aina yoyote nchini humo.

Nchini Rwanda na Uganda nako wananchi wa nchi siyo tu wamekuwa wakinufaika na mgao wa chakula bali pia wamekuwa wakinufaika na hatua nyengine mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali zao kukabiliana na athari za kiuchumi zitokanazo na janga la UVIKO-19. Nimetoa mifano ya nchi za Kenya, Uganda, na Rwanda ili iwe rahisi kwetu kuhusisha na hali yetu kama nchi lakini kusema kweli huu ndiyo utaratibu unaotumiwa na mataifa mengi duniani yenye uchumi wa chini, kati, na wa juu.   

Sasa hapa kwetu sijui Serikali ina mpango gani na sisi. Binafsi sifahamu mkakati wowote  uliowekwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kukabiliana na makali ya janga la UVIKO-19. Labda kama nyinyi wenzangu mnaufahamu mnijulishe. Kauli na matamko ninayoyasikia kutoka kwa viongozi ni yale tu ya kuwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na hayaendi zaidi ya hapo. Ni kama vile Serikali inaamini haihusiki na kuboresha hali za maisha za wananchi.

Hali ya uchumi

Pengine Serikali na watetezi wake wanaweza kudai kwamba haiwezi kutufanyia wananchi wake mambo haya, kwa sababu hali ya uchumi wa nchi mbaya. Watanukuu ripoti za Serikali zinazoonesha kwamba ukuaji wa pato la taifa umeshuka kutoka asilimia 7.0 mwaka 2019 hadi asimilia 4.8 ya mwaka 2020.

Watadai kwamba hali hii imetokana na uwepo wa mvua zilizozidi wastani hali iliyopelekea kusimama kwa shughuli nyingi za kiuchumi, pamoja na madhara yaliyosababishwa na uwepo wa janga la UVIKO-19, pamoja na sababu nyengine mbali mbali ikiwemo ufungwaji wa mipaka kusitishwa kwa safari za ndege. Naelewa yote haya.

Hata hivyo, zimekuwepo taarifa mbali nbali kuwa Serikali yetu imekuwa ikipokea misaada ya kifedha kutoka kwa mataifa wahisani na washirika wengine mbali mbali wa maendeleo ya Tanzania ili zisaidie katika kupambana na makali yatokanayo na UVIKO-19.

Mnamo Juni 2020, kwa mfano, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) uliidhinisha ruzuku ya jumla ya dola za kimarekani milioni 14.3 kwa Tanzania kwa ajili ya kuisadia kusawazisha tofauti kati ya fedha zinazoingia nchini na zile zinazotoka. 

Mnamo Novemba 2020, Umoja wa Ulaya (EU) ulibainisha utayari wake wa kuipatia Tanzania jumla ya Shilingi bilioni 70 kwa Serikali ya Tanzania ili iimarishe juhudi zake za kupambana na makali ya UVIKO-19. Wiki hii pia, shirika la Global Fund limeidhinisha msaada wa Dola Milioni 100 na kuipatia Sserikali ya Tanzania kukabiliana na Ugonjwa wa UVIKO-19.

Serikali inafanya nini na hizi fedha?

Sasa ni makali gani ya UVIKO-19 ambayo Serikali yetu inapambana nayo? Hayo mapambano yanaendeshwa kwa mtindo gani na walengwa ni wapi? Kwa nini Serikali imekubali kutuacha tupambane wenyewe licha ya kuongezeka kwa misaada ya kifedha inayotolewa na wahisani?

Sitaki niamini kwamba Serikali inafanya hivi ili kutukomoa lakini hali halisi huku mtaani inanifanya niwaze hivyo. 

Jaribu kufikiria kwamba katikati ya janga kama hili linaloendelea kuliza watu, huku Serikali ikishindwa kuchukua hatua yoyote ya kupunguza makali ya ugonjwa huu, bado viongozi wetu wanapata ujasiri wa kututwika mizigo mengine mizito ya tozo za miamala ya simu, kupandisha bei za mafuta ya petroli na dizeli pamoja na kututoza wapangaji kodi za majengo yasiyoyakwetu kila tununuapo umeme kupitia LUKU?

Nadhani Serikali yetu inaweza kufanya zaidi ya hapa. Sidhani kama ni suala la uwezo bali nia. Viongozi wetu wasisahau kwamba sisi kama wananchi hatujakubali uwepo wa Serikali ili iweze kukusanya kodi tu kutoka mifukoni mwetu tu. Hiyo siyo sababu ya kwa nini tunapanga foleni kuchagua viongozi mbali mbali kila msimu wa uchaguzi unapowadia. 

Tunapiga kura kwa kuamini kwamba tunaweka Serikali madarakani ambayo itapambana kuboresha ustawi wetu kama wananchi. Sasa ni muda sahihi wa viongozi wetu kulitambua hilo. Watushike mkono wasiache hili zimwi liitwalo UVIKO-19 litutafune peke yetu bila ya kuwepo kwa msaada wowote.

Jovine Johansen ni mchambuzi wa masuala ya data kutoka kampuni ya Cornerstone Solutions Limited. Kwa maoni unaweza kumpata kupitia jovin.johansen@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *