Dar es Salaam. Kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba kwamba fedha zitakazotokana na tozo ya miamala ya simu hazitachanganywa na fedha zingine inapingana na msimamo wa awali ambapo Serikali ilieleza kuwa hakuna umuhimu wa kuziwekea fedha hizo uangalizi maalum.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa, Agosti 20, 2021, wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alikuwa akitoa taarifa kuhusu kazi ambayo Serikali inaendelea nayo kuhusu tozo mpya za miamala ya simu na mafuta.
Wakati wa mkutano huo, Dk Nchemba aliujulisha umma wa Watanzania kuwa fedha za tozo zitawekwa katika uangalizi maalum, au ‘ringfenced,’ na hazitachanganywa na fedha zingine.
“Mheshimiwa Rais [Samia Suluhu Hassan] alielekeza fedha zozote hizi ambazo tunafanya kwa makubaliano na Watanzania zisichanganywe na za matumizi mengine,” Dk Mwigulu alisema. “Kwa maana hiyo, Sh100 iliyoongezeka kwenye mafuta kwa ajili ya TARURA haitachanganywa na kitu chochote hata iongezeke iwe nyingi kiasi gani inaenda kutengeneza barabara.”
Lakini The Chanzo inafahamu kwamba msimamo huu wa sasa ni tofauti na ule wa awali ambapo Serikali ilisema kwamba hakuna umuhimu wa kuziwekea uangalizi maalum fedha zitakazopatikana kwa tozo hizi mpya kwani zitakuwa zikienda moja kwa moja kwenye mifuko mbalimbali.
Hii ilikuwa ni Juni 22, 2021, wakati Dk Mwigulu akiongea ndani ya Bunge. Alisema: “Kwenye hili ambalo waheshimiwa Wabunge mmelisema kwa nguvu sana….mlisema sana, tuwahakikishie kwamba fedha hizi zitakuwa ‘ringfenced’. Na mimi niseme mbele yako Mheshimiwa Spika kwa sababu sekta hizi nyingi, hizi tunazozipelekea fedha, nyingi zina mfuko wala hatukuona sababu ya kuanzisha mfuko kwa sababu tumekitaja chanzo na tukataja zinapokwenda maana yake zinatoka kwenye chanzo zinakwenda moja kwa moja kwenye mfuko ule ambao upo.”
Waziri Mwigulu alitoa mifano ya mifuko ukiwemo wa maji na TARURA kama mifuko itakayotumika moja kwa moja kwa fedha hizi.
Hoja ya kuziekea uangalizi maalum fedha zinazopatikana kwenye tozo hizi inapata mashiko zaidi toka kwa wadau wanaosisitiza uwajibikaji. Msingi mkubwa ukiwa ni kuangalia wingi wa fedha zinazotegemewa, namna ya kukusanya na pia vipaumbele vilivyowekwa kuhusu fedha hizi.
Wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akili alitolea ufafanuzi kuhusu fedha zitakazopatikana kutoka Zanzibar, jambo ambalo liliulizwa na wadau mbalimbali.
“Kwa upande wetu Zanzibar, utaratibu unaendelea wa uhamishwaji wa hizi pesa tunategemea sana kwamba matumizi yetu yataelekezwa zaidi katika kustawisha jamii,” alisema Dk Akili.
Dk Mwigulu ameeleza kwamba toka tozo hizi zianze ndani ya mwezi mmoja, Serikali imeweza kukusanya Shilingi bilioni 48.4 ambazo tayari zimepelekwa katika shughuli za ujenzi wa madarasa na vituo vya afya.
Matarajio ya kibajeti katika fedha za miamala ilikua ni kukusanya Shilingi trilioni 1.25 kwa mwaka toka kwenye tozo hii mpya, hii ikimaanisha kama kiwango kilichokusanywa kwa mwezi mmoja kitabaki kilivyo serikali itaweza kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 581, ikiwa ni asilimia 46 ya lengo.
Waziri Mwigulu pia aligusia minong’ono iliyokuwepo kuhusu kushuka kwa shughuli za kutuma na kupokea fedha kwa simu na kusisitiza kuwa hakuna kushuka kwa miamala na kwamba mabadiliko katika miamala ni madogo.
Kwa upande wa tozo ya mafuta, Mwigulu ameelezea kuwa mpaka sasa Serikali imeweza kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 24 ambazo nazo zitaenda katika barabara hususani za vijijini ambazo hazipitiki.