Wakulima kutoka maeneo mbali mbali nchini Tanzania wamelalamikia ongezeko la bei ya mbolea nchini, wakisema kwamba ongezeko hilo “lisilo la kawaida” linahatarisha uzalishaji wa chakula nchini na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuingilia kati kwa kutafuta suluhu za muda mfupi na za muda mrefu kabla madhara hayajakuwa makubwa sana.
Wakiongea na The Chanzo kwa nyakati tofuati mwishoni wa juma lililopita, wakulima kutoka mikoa ya Iringa, Songwe, Ruvuma na Mbeya wamesema kwamba kwa sasa wanalazimika kununua mfuko mmoja wa kilogramu hamsini wa mbolea ya kukuzia kama UREA kwa shilingi 80,000 kutoka shilingi 50,000 waliokuwa wananunulia mwanzoni mwa mwaka 2021.
Kwa upande wa mbolea ya kupandia ya DAP iliyokuwa ikiuzwa kutoka shilingi 62,000, wakulima wanasema sasa wanapaswa kulipa takribani shilingi 90,000 ili kuweza kuipata. Mbolea nyingine ambazo pia zimepanda bei kwa mujibu wa wakulima hao ni pamoja na mbolea za kukuzia kama SA ambayo imepanda kutoka shilingi 38,000 hadi kufika shilingi 44,000; mbolea ya CAN kutoka shilingi 40,000 mpaka shilingi 55,000; na mbolea ya NPK kutoka shilingi 60,000 mpaka shilingi 90,000.
“Kuna kipindi hapa katikati mbolea iliadimika kidogo alafu baadae ikawa inapatikana. Lakini hivi karibuni mbolea imepanda sana bei,” Sayimba Darius, mkulima wa nyanya na mboga mboga kutoka Mgama, Iringa, anasema wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Tunaomba Serikali iangalie shida iko wapi ili bei ziendane na hali halisi.”
James Mbawala ni mkulima wa mahindi kutoka Palangu, Songea ambaye anasema kwamba suala la bei ya mbolea inapaswa lishughulikiwe mapema wakati huu wakulima wakijiandaa na msimu mpya wa kilimo wa 2021/22, vinginevyo itawakatisha tamaa wakulima.
“Kwanza bei ya mahindi sokoni imeshuka sana, tunauza mpaka shilingi 250 kwa kilo,” anasema Mbawala. “Sasa kwa bei hizi za mbolea, maana yake gharama ya kuhudumia heka moja ya mahindi msimu ujao itakuwa sawa sawa na mapato ya heka mbili tulizozalisha mwaka huu. Tutashindwa kulima.”
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) iliyotolewa Juni 2021, uzalishaji wa mazao ya chakula nchini Tanzania uliongezeka kwa asilimia 11.7 kutoka tani 16,293,637 mwaka 2019 mpaka tani 18,196,733 mwaka 2020.
Moja ya sababu inayotajwa kupelekea ongezeko hilo ni pamoja na matumizi ya teknolojia na pembejeo bora hususani matumizi ya mbolea za viwandani. Hii ina maana kwamba kama bei za mbolea zitabaki kuwa juu inaweza kupelekea kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo hususani chakula.
Mabadiliko ya bei katika soko la dunia
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dk Stephan Eliuth Ngailo ameiambia The Chanzo kwamba hali ya ongezeko la bei ya mbolea nchini imesababishwa na mabadiliko ya bei ya mbolea katika soko la dunia tangu mwezi Novemba 2020 hali ambayo imeathiri nchi nyingi ikiwemo Tanzania.
“Ukiangalia Juni 2020, tani moja ya mbolea ya kukuzia ya UREA hadi kufika Tanzania iligharimu jumla ya dola za kimarekani 270 (shilingi 626,130), lakini mwezi Novemba 2020 ikafika dola 310 (shilingi 718,890). Mwezi Machi mwaka huu [wa 2021] ikafika dola 420 (shilingi 973,980) na mpaka kufika mwezi Julai gharama imefika mpaka dola 506.5 (shilingi milioni 1. 1),” anasema Dk Ngailo.
Kwa upande wa mbolea ya kukuzia kama ya DAP ambayo mwezi Juni 2020 iligharimu dola za kimarekani 325, sawa na shilingi 753,675, kwa tani mpaka inapoingia nchini, Dk Ngailo amebainisha kwamba gharama hizo nazo ziliongezeka kufika dola 470 (shilingi milioni 1), Novemba 2020, dola 570 (shilingi milioni 1.3) mwezi Machi hadi kufika dola 617 (shilingi milioni 1.4) mwezi Julai 2021.
Dk Ngailo anasema pia kutokana na mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Korona (UVIKO-19) mwaka jana ulipelekea baadhi ya viwanda kwenye nchi wazalishaji wakubwa wa mbolea kupunguza uzalishaji. Anasema: “Kupungua kwa uzalishaji huko kumesababisha bei kupanda kutokana na kuwepo kwa uhitaji mkubwa ikilinganishwa na upatikanaji hususani kwa nchi watumiaji wakubwa wa mbolea kama vile Marekani, China, India na Brazili.”
Kwa msimu wa mwaka 2020/21 hadi kufika April 2021 uzalishaji wa mbolea kutokana na viwanda vya ndani ulifikia tani 32,239 huku tani 426,572 zikiagizwa toka nje. Mahitaji kwa msimu wa mwaka 2020/21 yalikuwa tani 718,051.
Hii ina maana kwamba hadi kufika April 2021 viwanda vya ndani vilizalisha takribani asilimia 5 ya mahitaji ya mbolea, hali inayoonesha kwamba Tanzania inatumia fedha za kigeni zaidi ya dola milioni 200, sawa na shilingi billioni 463.8, kwa mwaka kuagiza mbolea za viwandani kutoka nchi za nje.
Hatua za utatuzi
Kama hatua ya haraka za kukabiliana na changamoto hiyo, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda wakati akitembelea Ofisi ya Bodi ya Pamba jijini Mwanza mwanzoni mwa mwezi Julai, 2021, aliwataka wafanyabiashara wote wenye nia ya kuagiza mbolea nchini wafanye hivyo bila kupitia zabuni ya uagizaji wa mbolea wa pamoja ili kuongeza upatikanaji wa mbolea nchini kwa wingi na kwa bei shindani.
Lakini wakulima na wadau wengine wanabainisha kwamba hatua hii haiwezi kutatua changamoto inayosababishwa na mwenendo wa bei za mbolea katika soko la dunia. Wakulima wanasema kwamba Serikali haina budi kuwasaidia kwa kuchukua hatua ya dharura zitakazo wawezesha kupata ruzuku ili waweze kununua mbolea.
Wadau wa masuala ya kilimo pia wanapendekeza kwamba Serikali ihakikishe uzalishaji wa mbolea za viwandani nchini unaongezeka ili kuweza kujitosheleza na kuacha kutegemea uagizaji wa mbolea toka nje ya nchi.
One Response
Kiukweli hali ni mbaya sana, kwani kuna wengine tumeahirisha hata kulima baadhi ya mazao au kupunguza kias cha kulima kutokana na kutoweza kumudu gharama hizi… Serikali chukuen hatua za dharura kwakweli.