Kwa mujibu wa takwimu za mwenendo wa matukio ya kigaidi ulimwenguni, vitendo hivi kwa kiasi kikubwa hutokea katika nchi zenye Waislamu wengi. Hii maana yake ni kwamba waathirika wakubwa wa vitendo vya kigaidi ni Waislamu. Waislamu pia huathiriwa na matukio ya kigaidi kwa kunyanyapaliwa. Ukweli ni kwamba Waislamu wana nafasi kubwa ya kutiliwa shaka na kutuhumiwa kwa uhalifu huo kuliko watu wa dini nyingine yoyote ile.
Hali hii imewafanya Waislamu ulimwenguni kote kuwa na hofu mbili: hofu ya ugaidi wenyewe na hofu ya vita dhidi ya ugaidi inayoendeshwa na mataifa kadhaa ulimwenguni ikiwemo Tanzania. Fikiria mfano wa hivi karibuni wa masheikh 36 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) waliosota mahabusu kwa takribani miaka nane wakiwa ni wahanga wa vita dhidi ya ugaidi iliyoendeshwa na Rais Jakaya Kikwete. Kesi yao haikuwahi kusikilizwa na hivyo kuachiwa kienyeji kabisa.
Katika duru za kimataifa, tunasoma kuhusu makosa yafanywayo mara kwa mara na madege makubwa ya nchi za Kimagharibi wakati wa kampeni zao za ‘kupambana na magaidi’, ambapo badala ya kuua wahalifu majeshi ya nchi hizo huishia kuua raia wasio na hatia wakiwemo wakinamama, wazee, watoto, na walemavu. Haya yametokea nchini Aghanistan, Syria, Iraq na kwingineko ambako vita dhidi ya ugaidi imewahi kuendeshwa.
‘Msituzalie watoto kama Hamza’
Kwamba Waislamu wanakuwa wahanga wa vita dhidi ya ugaidi kwa kuwekwa kapu moja na watu wanaosadikika kujihusisha na matukio hayo si jambo linalokulazimu kwenda mbali sana kufahamu ukweli wake. Mnamo Agosti 28, 2021, siku chache baada ya tukio ambalo polisi wameliita la kigaidi lililomusisha kijana Hamza Mohammed kuuwa askari watatu na raia mmoja kabla ya yeye mwenyewe kuuwawa, Inspekta Generali wa Polisi Kamanda Simon Sirro aliwalaumu wazazi na ndugu wa Hamza kwa tukio hilo.
“Hiyo familia [ya Hamza] kwanza inajisikiaje?,” aliuliza Sirro akijibu swali kuhusu hatma ya mwili wa Hamza. “Hiyo familia ya Hamza, inajisikiaje? Fikiria ungekuwa baba yake na Hamza, mama yake na Hamza, mdogo wake ungejisikiaje? Kuzaa kwako umetuletea balaa Watanzania. Kwa hiyo, naomba Watanzania wengine wasituzalie watoto kama Hamza.”
Watu wengi, hata wale ambao siyo Waislamu, waliikosoa kauli ya Sirro, wakisema kwamba imekosa utu na kuwatupia lawama watu wasiohusika na uhalifu uliofanyika. Ni kama vile watu huchagua watoto wa kuwazaa! Ukweli ni kuwa hatuchagui. Tunachoweza kufanya kama wazazi ni kuwapa malezi bora iwezekanavyo na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu awaongoe. Lakini ijulikane kwamba hata ukimpa malezi bora, kuna nguvu nyingine za ushawishi ambazo mzazi huna udhibiti nazo.
Si kazi ya polisi kukagua mitaala
Katika kuongeza juhudi kwenye vita yake dhidi ya ugaidi, Sirro alitangaza mnapo Septemba 11, 2021, nia ya Jeshi la Polisi kushirikiana na Jeshi la Polisi la Rwanda kimafunzo na kiutalaamu katika kuhakikisha kwamba aina hiyo ya uhalifu inakoma. Moja kati ya mambo ambayo Sirro alisema amejifunza kutoka Rwanda na ambayo anafikiria kuyaanzisha hapa ni kukagua mafunzo yanayotolewa kwenye madrasa na Sunday School.
Kwanza, suala la ukaguzi wa mitaala si la Jeshi la Polisi. Tayari Tanzania ina vyombo kwa ajili ya kazi hiyo, ikiwemo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na mifumo yake hadi katika halmashauri.
Pili, ni kwamba huo utaalamu wa kuifanya hiyo kazi Jeshi la Polisi inautolea wapi? Ni hofu ya wengi kwamba jambo kama hilo likiruhusiwa kufanyika, Tanzania inaweza kugeuka kuwa taifa la kipolisi. Utaratibu huu ukitekelezwa, utakuwa ni mwendelezo wa mbinu zinazotumika kuwang’amua Waislamu wenye viashiria vya kigaidi hata kama muhusika hahusiki kwa namna yoyote na matukio hayo.
Na Jeshi la Polisi litatumia vigezo gani kusema kwamba mafunzo haya yanakubalika kufundishwa na haya hayakubaliki. Katika baadhi ya nchi walimu na wanafunzi wa madrasa wanazuia kufundisha/kujifunza somo la Tawhid, somo la msingi kabisa katika dini ya Kiislamu lihusikanalo na kumpwekesha Mwenyezi Mungu mmoja, ambao ndio msingi mkuu wa dini hiyo. Je, Sirro atafuata nyayo hizo? Inawezekana.
Mafunzo ya ukakamavu yanakuwaje haramu?
Nasema inawezekana kwa sababu hata kabla ya Jeshi la Polisi kuanzisha huo utaratibu linalotaka kuuanzisha tayari baadhi ya viongozi wa misikiti kadhaa nchini wamelalamikia hatua za vyombo vya ulinzi na usalama kupiga marufuku mafunzo ya ukakamavu ikiwemo sanaa za mapigano, wakidai huko ni kuandaa watu kwa ajili ya ugaidi.
Haya ndiyo manyanyapaa yanayohofiwa na Waislamu wengi ambayo hutokana na kinachoitwa juhudi za Serikali kupambana na ugaidi. Na manyanyapaa haya muda mwengine huenda mbali zaidi. Kwa mfano, kuna sifa za kimuonekano ambazo zinaweza kumuweka Muislamu matatani. Hizi ni pamoja na: kufuga ndevu, kuvaa kanzu fupi, kuvaa kofia ya kibandiko (nusu chungwa), kubeba bakora, kuwa na kipara, kubeba begi la mgongoni na kadhalika.
Kutumia vigezo hivi kung’amua wahalifu ni kosa kubwa la kimantiki kwani ingawa kuna wahalifu wachache wenye muonekano huo, kwa upande mwingine huo pia ni muonekano wa wengi kati ya mamilioni ya Waislamu safi.
Na inavyoonekana kadhia hii haitaishia hapo. Sirro anamaanisha nini anaposema kwamba Jeshi la Polisi linaratibu mpango wa kuwarekebisha vijana wadogo ambao wana dalili za kigaidi kupitia vituo maalum au rehabilitation centre kama vinavyojulikana kwa kimombo.
Wachina wanafanya haya kule kwenye jimbo la Xinjiang kwa Waislamu wa kabila la Wauyghur na matokeo yake si mazuri. Badala ya kupambana na ugaidi, Serikali ya China inakandamiza uhuru wa kuabudu kwa kuwazuia kutekeleza dini yao na kuwalazimsha kufanya waliyoharamshiwa ikiwemo kula nguruwe. Watu hao hawana hata uhuru wa kujiita kwa majina wanayoyapenda!
Vita dhidi ya ugaidi isizalishe chuki, visasi
Nihitimishe kwa kusema kwamba si busara kwa Serikali kuiga ya Rwanda, au ya nchi yoyote, kwenye vita yake dhidi ya ugaidi. Historia na muktadha wa siasa za Rwanda ni tofauti sana na sisi. Huenda hata magaidi wanaowalenga ni zaidi ya hao ambao Sirro anawafahamu.
Ugaidi si tishio la kimzaha mzaha na linapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote. Lakini ni muhimu sana kuhakikisha kwamba vita hii haibagui jamii fulani na kuijengea aina mpya ya manyanyaso na uonevu.
Ni vita ambayo inahitaji umoja na ushirikiano wa makundi mbali mbali ya kijamii yalipo katika nchi yetu. Vinginevyo, juhudi zetu za kutatua changamoto ya ugaidi inaweza kuzalisha changamoto nyengine za visasi na chuki. Sidhani kama hiyo ndiyo nia ya IGP Sirro.
Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.
5 responses
Makala nzuy Sana.
Nadhani wengi tutakubaliana kuwa Moja kati ya matatizo vya vyombo vyetu ni uwezo mdogo wa viongozi katika vyombo vyetu hivi.
Watu wasiomudu hata kuchafua lugha ya kuihutubu katika hadhara.
Je sirini husema na kupanga nini.
Great article!
Makala mazuri sana mwalimu, kwangu mimi mfumo bado unatreat uislamu kama uadui lakini wangeufanya utafiti wa kutosha watakuta huu ndio mfumo wa maisha ya mwanadamu uliokamilika zaidi kuliko kasoro zinazoripotiwa.
Uchambuzi mzuri kwa jambo zito lenye kutaka tafakuri
Good article. Natumai Kamanda atasoma na kuona concerns za Waislamu