Dar es Salaam. Wizara ya Fedha na Mipango imeweka wazi mpango wa Serikali wa kukabiliana na madhara ya uchumi na kijamii yaliyosababishwa na UVIKO-19 huku ikibainisha kwamba jumla ya shilingi trilioni 3.6 zitahitajika kugharamia mpango huo uliosainiwa mnamo August 2021.
Sehemu ya fedha hizi ni zile zilizotolewa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) hivi karibuni kwa Serikali ya Tanzania kusaidia juhudi zake za kupambana na madhara yatokanayo na janga la UVIKO-19 linaloendelea kutesa mataifa kadhaa ulimwenguni.
Kwa mujibu wa mpango huo wa Serikali ambao The Chanzo umeuona, Serikali inakusudia kutumia fedha hizo kukabiliana na madhara ya UVIKO-19 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Fedha hizo zitapelekwa kama nyongeza ya bajeti Bungeni baada ya tathmini ya nusu mwaka.
“Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022 imekwishapitishwa lakini haitoshi,” inasema sehemu ya mpango huo. “Hivyo, mpango wa kutafuta shilingi trilioni 3.6 za ziada umeandaliwa, ambapo kati ya hizo trilioni 1.3 zitatoka IMF.”
Madhara yanayotokana na UVIKO-19 ambayo Serikali imejipanga kukabiliana nayo ni pamoja na madhara katika sekta ya utalii ambapo kumekuwa na kupungua kwa watalii kwa asilimia 59 kwa mwaka 2020.
Kwa mujibu wa Serikali, kwa mwaka 2020, ni watalii 620,867 waliongia Tanzania ukilinganisha na watalii 1,527,230 kwa mwaka 2019. Halii hii imesababisha mapato kwenye sekta hii kushuka kutoka dola bilioni 2.6 kwa mwaka 2019 mpaka dola milioni 715 kwa mwaka 2020.
Hata utalii wa ndani uliporomoka kwa asilimia 37 kutoka watalii 902,569 kwa mwaka 2019 mpaka watalii 571,353 kwa mwaka 2020.
Kuporomoka kwa utalii kuliathiri pia sekta nyingine kama vile sanaa na burudani ambapo ukuaji wake ulizorota kwa silimia 4.4 (-4.4%) na pia sekta ya malazi na vyakula.
Eneo jengine lililoathiriwa ni elimu ambapo fedha nyingi zinaenda kwenye ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira salama na yanayozingatia umbali.
Mpango huo pia unaonyesha madhara ya UVIKO-19 kwenye uchumi wa Zanzibar ambapo kati ya mwaka 2017 na 2019, uchumi wa Zanzibar ulikuwa unakua kwa asilimia 7.3 lakini kwa sasa uchumi huo umeshuka mpaka ukuaji wa asilimia 1.3 kwa mwaka 2020.
Maeneo ambayo yatagharamiwa na mpango huo ni pamoja na afya ambapo itachukua shilingi bilioni 895 ya fedha zilizotengwa. Hii inajumuisha shilingi bilioni 436 kwa ajili ya kununua chanjo ya UVIKO-19 na usambazaji.
Sekta ya elimu inatarajiwa kutumia shilingi bilioni 196 ya fedha zilizotengwa. Sekta nyengine zitakazogharamiwa na mpango huo na kiwango cha fedha kitakachotumika ni kama ifuatavyo: utalii (shilingi bilioni 444), maji (shilingi bilioni 317), huduma za jamii (shilingi bilioni 82), uwezeshaji (shilingi bilioni 80), madeni ya wakandarasi (shilingi bilioni 533.9), ruzuku katika kilimo (shilingi bilioni 50), uwezeshaji wa biashara ndogo na za kati (shilingi bilioni 390) na Zanzibar (shilingi bilioni 497.4).