Dar es Salaam. Wakati akiongea katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia leo, Septemba 15, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan aliitaja Tanzania kama moja kati ya nchi zinazofuata misingi ya kidemokrasia duniani, akibainisha kwamba taifa hilo la Afrika Mashariki tayari limejipatia uhuru wake wa kisiasa na sasa linapambana kutafuta uhuru wa kiuchumi.
Siku ya Kimataifa ya Demokrasia husherekewa kila ifikapo Septemba 15 ya kila mwaka duniani kote ikiwa na lengo la kukuza na kuenzi misingi ya kidemokrasia ili kujenga na kudumisha amani na usalama ulimwenguni.
“Natambua kuna changamoto za demokrasia bado zipo nchini, na hii ni kwa sababu hakuna taifa duniani ambalo linaukamilifu katika masuala ya Demokrasia,” alisema Rais Samia katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam na kumkutanisha na wanawake wajasiriamali. “Demokrasia pamoja na ukweli kwamba ni lengo au shabaha lakini pia ni mchakato. Ni suala endelevu.”
Kama sehemu ya kuadhimisha siku hii, The Chanzo iliwauliza wakazi wa jiji la Dar es Salaam maoni yao juu ya hali ya kidemokrasia nchini na kama je, wanakubaliana na kauli ya Rais Samia kwamba Tanzania inaendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia. Baadhi ya wananchi hao wameitaka Serikali kufufua mchakato wa Katiba Mpya ili kuimarisha misingi ya kidemokrasia nchini.
“Tubadilishe kwanza Katiba, Katiba ikishabadilika haya mambo yote yatabadilika,” Vermund Kasala, mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam, anayejihusisha na biashara ndogo ndogo, ameiambia The Chanzo.
Kasala anasema kwamba “demokrasia Tanzania bado, bado sana,” akitolea mfano wa mfumo mzima wa uchaguzi ambao anauita “mbovu” kwani “Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi anateuliwa na Raisi, Mkurugenzi wa [Uchaguzi], makatibu wote, wakuu wa wilaya wote wanateuliwa na Rais. Kwa ufupi, mfumo wetu wa vyama vingi bado sana yaani tuseme mfumo wetu wa demokrasia bado upo chini sana kiukweli.”
“Masuala ya Katiba ndio muhimu,” anasema Nassor Iddi, mkazi wa Kariakoo Dar es Salaam. “Katiba ndio nchi. Katiba ndio mfumo wa sheria. [Katiba] ikibadilishwa tutakuwa na demokrasia na tutakuwa na tume huru ya uchaguzi. Mimi nadhani Katiba [ndiyo jambo la muhimu]. Unajua Katiba ndio kila kitu.”
Lameck Wagala, mkazi wa Tegeta, jijini Dar es Salaam, anasema kwamba hawezi kusema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia wakati vyama vya siasa vinazuiwa kufanya shughuli zao kwa kisingizio cha kuletea nchi maendeleo.
“Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu kabisa kwamba vyama vya siasa vina haki ya kufanya mikutano ya hadhara, kwa kuvizuia visifanye kazi zao tayari hapo tunaonesha kuna upungufu wa demokrasia,” anasema Wagala.