Dar es Salaam. Kuna changamoto nyingi sana zinazowakabili watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini Tanzania. Na jitihada nyingi zinachukuliwa kuhakikisha kwamba changamoto hizi, au watu hawa, wanaondokana na changamoto hizi. Lakini kwa kiasi fulani changamoto moja inaonekana ni kama vile haipiganiwi kama vile inavyohitajika. Na hii ni changamoto inayowakabili watu wanaoishi na VVU kuweza kupata wenza wa maisha kama mke, mume, au mpenzi.
Ni jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwaathiri watu wengi wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI hapa nchini Tanzania na pengine sehemu nyingine duniani. Bahati nzuri ni kwamba kuna jitihada zinafanyika kuhakikisha kwamba changamoto hiyo pia inatatuliwa. Na leo tumebahatika kufanya mazungumzo na mmoja kati ya Watanzania ambao ni waathirika wa maambukizi ya virusi vya VVU na ambaye anachukua jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba anasaidia wahanga wenzake wa ugonjwa huu kuweza kupata wenza wao wa maisha.
Ungana nasi kwenye podcast hii kuanzia mwanzo hadi mwisho kuweza kusikiliza simulizi ya Mtanzania huyu.
The Chanzo: Asante sana kwanza kwa kukubali kuongea na sisi, na nimeona kile ambacho unakifanya kwenye ukurasa wa Instagram. Kwa kuanzia tu labda ungeweza kutuambia tu kwa ufupi labda wewe ni nani? Labda kama majina yako? Na unaishi wapi? Na unafanya nini kwa sasa?
Aysha Hamis Msigwa: Mimi kwa majina kamili naitwa Aysha Hamis Msigwa, na ni mwenyeji wa Njombe, nakaa sehemu wanaita Makambako na ni muendeshaji wa ukurasa wa HIV positive dating [huko Instagram].
The Chanzo: Sawa sawa, na hii ni kazi ambayo unaifanya wenyewe wanasema full time [muda wote], yaani ndio kazi yako unayofanya, au kuna shughuli nyingine labda unajishughulisha nayo?
Aysha Hamis Msigwa: Hapana hii ni extra timing [muda wa ziada] ndo huwa nafanya hivi, full time job huwa nafanya kazi ya kuuza mafuta ya alizeti.
The Chanzo: Sawa sawa. Kwa hiyo, kimsingi ni kwamba, kwa sababu hapo umezungumza kwa Kingereza, kimsingi ni kwamba wewe kwa kutumia mtandao wa Instagram unaunganisha watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ambao wangependa kupata wenza wao wa maisha kati ya mwanamke na mwanaume, si ndio hivyo?
Aysha Hamis Msigwa: Huwa tunafanya hivyo, kwamba mwaka jana Agosti 30 ndio nilikuwa nimeanza hii page [ukurasa wa kijamii]. Kwa hiyo, wakati huo nimefikiria kwamba ukija ukiangalia mara nyingi maambukizi yanakuwa yanazidi kwa sababu tumekuwa tuna mahusiano [ambapo] watu positive [walioathirika] pamoja na negative [ambao hawajaathirika] ndo wanakuwa pamoja].
Na mara nyingi watu positive tumekuwa wasiri, kumwambia mtu kwamba mimi nipo positive inakuwa ngumu kidogo na unafikiria pia jamii itakuhukumu vipi. Kwa hiyo, hiyo ndio iliyonipelekea nikasema kwa nini tusiwe na jukwaa ambapo tutakutana positive kwa positive ambao kama wataelewana, mwisho wa siku tutategemea ndoa.
The Chanzo: Sawa sawa, na samahani kwa kuuliza, wewe pia ni moja kati ya watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI?
Aysha Hamis Msigwa: Ndiyo, mimi nimeathirika na nina miaka 20 sasa hivi [toka nigundulike nimeathirika].
The Chanzo: Mwaka wa 20 unaishi na VVU?
Aysha Hamis Msigwa: Ndiyo, nakunywa dawa takribani miaka kumi na nane sasa hivi.
The Chanzo: Na wewe una umri wa miaka mingapi?
Aysha Hamis Msigwa: Mimi nina miaka 31.
The Chanzo: Miaka 31?
Aysha Hamis Msigwa: Ndio.
The Chanzo: Sawa sawa. Na hapo mwanzo uligusia sababu ya kuja na hili wazo, labda ilitokana pengine na uzoefu wako wewe mwenyewe binafsi labda unaweza ukatuambia labda stori yako kwa ufupi kama hutojali?
Aysha Hamis Msigwa: Ni kwamba yaani ilitokea kwangu mimi, kwa sababu unajua kila kitu lazima kuna mwanzo wake. Mimi nimepata posa kama tatu alafu zote zikaghairishwa. Sasa nikawaza nikasema kama mimi nimekataliwa mara tatu na zote ukija ukiangalia sababu inayosababisha unakuta ni kwamba umeathirika. Sema tu mtu anashindwa kusema kwa sababu anagopa labda kukuumiza hisia zako.
Lakini unakuta anawasiliana na wewe siku mbili mwisho wa siku anaachana na wewe. Au yule anayefika nyumbani anapoelezwa tu kwamba huyu mtu ni muathirika wa HIV anaachana na mimi. Kwa hiyo nikasema, inakuwaje kama ninachopitia mimi wanapitia wenzangu pia? Kwa hiyo, ndio nikafikiria suala kama hilo, kwamba hebu ngoja nifungue ukurasa hapa Instagram hata kama itakuwa haina wafuasi, angalau basi hata mmoja wawili wataweza kunifuata.
The Chanzo: Sawa sawa, na mwitikio labda, kwa sababu umesema umeanza tangu Agosti mwaka jana wa 2020, labda mwitikio ukoje, labda ni kwamba unapata maombi ya watu ambao ni waathirika wanatafuta wachumba ambao pia wameathirika pia?
Aysha Hamis Msigwa: Ndio maombi yanakuwepo tena mengi sana lakini mengi ni ya wanawake. Wanawake wengi sana wanakuwa wa wazi kuhusu hadhi zao za kiafya. Wiki moja tu baada ya kuifungua page watu tayari walishaanza kunitafuta. Na unakuta katika walionitafuta, wanawake ni kama saba lakini wanaume wawili. Kwa hiyo, hapa ndio mtihani unapokuja. Kwamba una wanawake saba inbox lakini wanaume wawili, unafanyaje?
The Chanzo: Na unadhani hiyo inatokana na nini kwamba wanaofunguka, kwa kutumuia maneno ya watu wa mjini, ni wanawake zaidi kuliko wanaume, unadhani hiyo inaweza ikawa inasababishwa na kitu gani?
Aysha Hamis Msigwa: Suala ni ile mascuiline factor ya wanaume. [Mwanaume] ni ngumu kukubali kwamba amekosea. Yeye kukiri kwamba ameathirika ndio kabisa hawezi. Wanaume maumbile yenu yanapelekea mara nyingi vitu fulani mkaona kwamba ni vigumu sana kukubaliana navyo.
The Chanzo: Na pengine unafahamu labda watu ambao ni wanufaika na huduma unayoitoa na ambao walifanikiwa kufunga ndoa labda?
Aysha Hamis Msigwa: Kuna baadhi ya watu lakini labda nijaribu kusema kwamba, kama zilivyo dating sites [kurasa za kimahusiano] nyingine isiwe positive isiwe negative, dating sites nyingi zinakutana na changamoto ya [watu] kutokuwa wakweli. Na hiyo inaleta matatizo sio kwa mimi tu wa positive lakini kwa wote.
Kwa hiyo, unakuta kuna mwanaume hapo yupo na lengo la kweli kabisa la kuwa kwenye mahusiano na mtu aliyeathirika lakini unakuta mwanamke huku labda yeye tayari alikuwa na mahusiano mengine kabla hajakutana na page yangu. Kwa hiyo, unakuta hawa wawili ukisema uwakutanishe pamoja hamna kitu kitakacho kwenda kutokea kwa sababu wako katika mitazamo miwili tofauti.
Mwingine anawaza labda kupata mtu ambaye ataishi nae kwa sababu yeye ni positive mwingine anawaza sawa ngoja na mimi nipoteze muda kwa sababu mimi ni positive. Kwa hiyo, hilo linakuwa tatizo kubwa sana kwangu mimi.
The Chanzo: Hiyo unaidhibiti vipi? Yaani unahakikisha vipi kwamba huduma unayoitoa inakuwa ni yenye msaada kwa watu wenye uhitaji badala ya kutumika kama jukwaa la watu tu wanaotaka kujifurahisha labda, unadhibiti vipi hiyo?
Aysha Hamis Msigwa: Yaani huo ndio mtihani mkubwa nilionao, japo sasa hivi nimejaribu — japo sijafikia asilimia yoyote — ila nimejaribu kuwadibiti kwa picha zao labda na hata ile nakala ya cheti chao wanachochukulia dawa angalau nikiviomba vile vitu nawaambia jamani unavyoenda huko basi muwe na adabu ikiwa inatokea labda kama unajaribu kumtumia mwenzako basi mimi nina uwezo wa kufanya chochote na zile taarifa zako.
Japo niwe tu mkweli sio kweli kwamba unaweza kutangaza taarifa za mtu lakini angalau inasaidia kwamba huyu mtu ataenda atafahamiana vizuri labda miezi mitatu ama miezi minne halafu atarudi na jibu.
Lakini vilevile napenda sana mara nyingi kuwapa ushauri wanawake kabla sijamkutanisha na mtu, namwambia kabisa kwamba ndani ya huu ukurasa ambao tunakutana mtandaoni, simfahamu mtu ambaye nakukutanisha nae na ukiacha zile taarifa ananipa mimi simfahamu. Kwa hiyo, jitahidi sana unapokwenda kukutana nae uwe makini kwamba ujiheshimu wewe, mwili wako na mahusiano ya kimapenzi. Lakini ndio kama tunavyosema mitandaoni inakuwa mtihani kujua tabia ya mtu.
The Chanzo: Pale mwanzoni uligusia sababu ya kuchukua uamuzi huu na ukahusisha na stori ya maisha yako binafsi. Lakini nataka kukuuliza, kwa sababu kusema kweli watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI sasa hivi sio jambo geni sana wala si jambo la kutisha kama vile lilivyokuwa zamani na changamoto ambazo zinawakumba hawa watu zinazungumzwa kila siku. Lakini kwa tathmini yako unadhani suala hili la watu wenye kuishi na virusi vya maambukizi ya VVU kupata wenza wa maisha linazungumzwa kwa kiasi gani au unadhani ni jambo ambalo halipewi kipaumbele kwa kiasi fulani zinazungumzwa tu changamoto zingine? Unadhani jamii linalipa kipaumbele suala kwamba watu ambao wamegundulika wanaishi na virusi vya VVU wanahitaji kuwa na watu wa kuishi nao kama wapenzi, kama wake, kama waume?
Aysha Hamis Msigwa: Kwa kipaumbele mimi naona halipewi kipaumbele sana kwa sababu kuna maswala kama ubaguzi unaweza ukakuta ukianza kuliongelea kwamba aliyeathirika awe na mwenza aliyeathirika bila shaka watu ambao hawajaathirika watajisikia vibaya kwamba ina maana sisi hatuwezi kuwa na watu walioathirika?
Na ukija ukiangalia mimi kitu kingine ambacho kilinisukuma naweza nikasema hii page ukiangalia inaitwa HIV positive dating Tanzania lakini kuna kaka anaitwa Kaka Lawi yeye ana [ukurasa unaitwa] HIV positive living Tanzania, sawa? Huyu Kaka Lawi anajitahidi sana kutupatia elimu [na] kutuelekeza kila kitu kuhusu HIV lakini yeye anatoa elimu.
Ndio pale nikawaza tena, kwa mfano, wengi wanamfuata Kaka Lawi wanamwambia, ‘Kaka Lawi naomba tusaidie na sisi kupata wenza wetu.’ Kwa hiyo, Kaka Lawi nae anasema haya basi kama mnataka wenza na nyie rudini HIV positive dating kwa sababu na yeye [yaani mimi] ana watu kule. Kwa hiyo, kwa Instagram nzima katika pages ambazo nimefuatilia, watu ambao wamejitolea kwa positive kwa positive ni mimi na Dk Lawi.
Kwa hiyo, kwa mimi kwa upande wangu naona ni msisitizo wa watu walioathirika kupata wenza wa maisha ni mdogo sana. Kuna majukwaa ya watu wenye HIV kuhusu changamoto zingine lakini sio za mahusiano.
The Chanzo: Yaani maana yake ni kwamba kuna platforms au kuna majukwaa ambayo yanahusiana na kutatua changamoto za watu wanaoishi na VVU lakini si kuhusiana na masula ya …
Aysha Hamis Msigwa: Sio kuhusiana na mahusiano ya VVU kwa VVU. Hiyo ndo inakuwa changamoto. Na ndio maana nimesema hapa kwamba mara nyingi linakuwa suala la ubaguzi na watu wanaogopa. Kwa mfano, hata mimi mwenyewe inbox nafuatwa na watu wengi ambao ni negative wananiambia dada tafadhali kwa nini usiniunganishe mimi na mtu positive mimi ni negative?
Namwambia hapa itabidi kwanza nipate ridhaa ya mtu ambaye yuko positive kwa sababu mtu hadi amenifuata mimi inamaanisha anahitaji kuwa huru kunywa dawa zake, anahitaji kuwa huru kuongea chochote mbele ya mwenza wake kwa sababu wote watakuwa katika tatizo linalofanana. Lakini mtu ukishakuwa negative tena lazima awe na tahadhari na vitu atakavyofanya unaweza kukuta hata tendo la ndoa inabidi waende na condom. Sasa vitu kama hivyo wengi wanaonifuata mimi wanakuwa hawataki.
The Chanzo: Sasa wewe binafsi unanufaika vipi na hicho unachokifanya?
Aysha Hamis Msigwa: Binafsi mimi sasa hivi sina chochote ambacho ninachonufaika kwa sasa, kwa sababu si tozi chochote kile kabisa. Kwa mfano, kama kitu kingine ambacho nimejaribu kufanya niliona kwamba unaweza ukakuta umenitumia mimi ombi leo halafu hadi niende kukutafutia mtu inakuwa kidogo nachelewa au ndio yale niliyokwambia kwamba mimi nitaangalia zile sifa zako ulizoniambia kwamba, ‘Bwana mimi ni mwanaume wa miaka 31 nahitaji mwanamke wa miaka 26 hadi 31.’
Kwa hiyo, mimi nitaangalia zile mweusi labda ni mfupi. Lakini ukija ukiangalia labda nitakuunganisha sawa sawa na vitu ulivyoviomba lakini kumbe mwisho wa siku unakuta ile tabia ya yule mwanamke ni tofauti kutokana na vile ambavyo wewe uliniomba. Kwa hiyo, sasa hivi nikapata wazo, nikasema kwa nini nisifungue group la Whatsapp ambalo sasa wewe ukija ukiniomba nikuunganishe na mtu mimi nakuomba uende kwenye group.
Sasa kuingia kwenye hilo group napo inabidi tena nikuombe picha yako, jina lako pamoja na kile cheti unachochukulia dawa ili nihakiki kwamba kweli wewe ni positive. Basi ukishanitumia hivyo nakuingiza kwenye group, [ambako] kuna wanawake wengi [na] kuna wanaume wengi hapo baadae ndio watu ambapo tutaenda tutafahamiana unaweza ukamtumia ujumbe Jane, Jane akasema bhana mimi nipo tayari na mtu.
Na pale [kwenye group] tayari huwa tunatangaza kwamba fulani na fulani wakishaelewana wanakuja kutangaza mbele ya group, ‘Jamani mimi na fulani tupo kwenye mahusiano sasa hizi tuombe Mungu itatupeleka wapi’ na ikiwa hawajaelewana au kuna kitu chochote kimetokea basi wote wanakuja wanatangaza pale kwenye group kwamba, ‘Bhana mimi labda na Eric tulishindwa kuendana kwa hiyo na sasa hivi mimi na Eric tumeachana.’
The Chanzo: Labda ukiachana na kutengeneza hilo group la Whatsapp labda una mipango mingine mikubwa labda, kwa sababu tunafahamu kuna dating app kuna hizo Tinder na nyenginezo. Labda pengine unafikiria kutengeneza app ambayo itakuwa inawakutanisha HIV positives kwa ajili ya kuishi pamoja kama wenza labda?
Aysha Hamis Msigwa: Hiyo ni mipango ambayo ipo kwenye mipango ya muda mrefu. Lakini sasa hivi kuna kitu kingine ambacho ninafanya na nina waomba Watanzania kama wanaweza kunisaidia kufanya, na hata watu wangu hawa nilionao huwa nawaomba kwamba wakienda kwenye CTC [care and treatment center services – vituo vya uangalizi na matibabu kwa waathirika] zao wajaribu kuwashirikisha watu kwenye ukurasa wangu wa HIV positive dating.
Pia, kwa sababu kuna watu ambao wanahitaji lakini hawapo kwenye Instagram hawana Whatsapp tunawafikia vipi? Kwa hiyo, hawa watu nilionao huwa nawaomba jamani mkienda kuchukua dawa naombeni jitahidini kumpa muuguzi au mratibu mmoja pale mpe namba zangu mwambie huyu dada anafanya kitu moja, mbili, tatu. Baada ya hapo yeye kama kuna mtu atatokea, unajua kuna watu wengine wanaenda CTC kwamba bwana naomba nitafutie mwenza wangu. Watu kama wale wakishakutana na namba yangu basi tunakuwa tunawapata. Lakini suala la App ni la muhimu na tunaomba Mungu kabla mwaka hujaisha liwe kwenye mipango yetu.
The Chanzo: Na kwa mfano kama mtu anataka kukufuatilia kwenye mtandao wa Instagram unatumia jina gani?
Aysha Hamis Msigwa: Hapo inabidi aandike tu HIV positive dating Tanzania atakuta ina kabendera hivi.
The Chanzo: Hivi kwa nini uliamua kutumia Instagram badala ya Facebook kwa mfano au Twitter au upo huko pia?
Aysha Hamis Msigwa: Huko Instagram niliona sasa hivi kama ndio sehemu ambayo ina wafuasi wengi zaidi kuliko Facebook na kwingine kote, japo kuna ushauri pia nilipokea ambao walinishauri niwe kote kote Facebook, Twitter na kwengineko.
The Chanzo: Sawa sawa. Aysha mimi nakushukuru sana kwa muda wako na nikupongeze pia kwa hatua hii hapa na nadhani utaipeleka mbele zaidi ile iweze kuwanufaisha watu wengi zaidi.
Aysha Hamis Msigwa: Nashukuru, nashukuru pia kwa kunitafuta na niwaombe tu Watanzania wote kwa pamoja wawe huru, wawe wazi. HIV sio kitu ambacho kinaweza kikakuua leo wala kesho. Sasa hivi tuna dawa za kufubaza virusi, tuna kila kitu. Kwa hiyo, kila kitu kinakuwa vizuri na ushauri pia tunatoa ukija kwenye page yetu na kama hivyo wawe tu huru wala wasijali kila kitu kitakuwa sawa.
The Chanzo: Asante sana Aysha.
Aysha Hamis Msigwa: Haya nashukuru!
4 responses
Mie pia natafuta mwenza wa maisha Nina VVU
Sheila habari yako
Niko tayarikukuoa
Natamani kupata mchumba au mme