The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Pius Msekwa: Vyama Vingi Maana Yake Ni Ushindani

Kada huyo wa CCM anasema moja ya sababu ya kuingia kwenye vyama vingi ni kusikiliza maoni ya watu

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mnamo Disemba 9, 2021, Tanganyika inatimiza miaka 60 tangu ipate uhuru wake kutoka kwa Waingereza tarehe kama hiyo mwaka 1961. Tukiwa tunaelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, tunayofuraha ya kujumuika na Spika mstaafu na kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mzee Pius Msekwa.

Pamoja na mambo mengine, Mzee Msekwa alikuwepo wakati Tanganyika inajipatia uhuru wake na hivyo kumuwezesha kushuhudia mabadiliko mengi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo Tanganyika, na baada ya Muungano na Zanzibar mwaka 1964, Tanzania, imeyapitia katika kipindi hiki cha miaka 60.

Kitu cha kwanza ambacho The Chanzo ilitaka kufahamu kutoka kwa Mzee Msekwa ni tathimini yake ya safari hii ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, hususani katika eneo la maendeleo ya kisiasa ambayo Tanganyika, na baada ya muungano na Zanzibar bila shaka Tanzania, imeyafikia kama nchi. Endelea …

Pius Msekwa: Nashukuru sana kwa kunishirikisha. Ndiyo, ni bahati njema mimi nilikuwepo wakati wa uhuru unapatikana na nipo na ninaendelea kuwepo katika miaka yote sitini. Kwa hiyo, ninazo kumbukumbu nzuri naweza kuwasaidia Watanzania wenzangu kujua tulikotoka. Miaka sitini maana yake ni miongo sita, ni miongo sita ya uhai wa taifa jipya hili la baada ya uhuru.

Kwa hiyo, ninavyoiona mimi na nilivyoyaishi maisha na kuona matukio ya baada ya uhuru naweza nikasema bila kusita kwamba imekuwa safari yenye mafanikio makubwa, tena makubwa sana ijulikane [hivyo]. Na naomba ijulikane kwamba wakati tunapata uhuru nchi yetu ilikuwa katika hali mbaya sana kimaendeleo kwa kila hali, kijamii, kisiasa na hata kiuchumi. Ilikuwa hali ya chini sana.

Kwa hiyo, ilibidi kuanza upya. Kuanza tangu mwanzo na ndio ilikuwa kazi kubwa ya Mwalimu [Julius Kambarage] Nyerere, Rais wetu wa kwanza na Baba wa Taifa hili. Kazi yake alipoianza katika muongo wa kwanza ile miaka kumi ya kwanza ndio miaka aliyoitumia kuweka misingi imara, kujenga misingi imara ya maendeleo ya taifa jipya. Misingi itakayo tumika katika maendeleo ya taifa letu.

Kwa hiyo, kazi kabla ya kuweka misingi mipya ilibidi avunje vunje masalia ya ubaguzi yaliyoachwa na wakoloni. Maana utawala wa wakoloni ulikuwa msingi wake katika elimu [ni] ubaguzi. Katika kila nyanja ni ubaguzi hata katika starehe tu [kulikuwa na] vilabu vya Wazungu [ambapo] Mwafrika hakanyagi. Yaani mambo ilikuwa ni misingi ya ubaguzi. Kwa hiyo, kazi yake ya kwanza [Mwalimu Nyerere] ilikuwa ni kuvunja vunja mabaki ya misingi hiyo.

Kwa hiyo, akasimamia utungaji wa sheria ya kubadilisha sheria za kikoloni zilizikuwa zinatengeneza ubaguzi. Ndiyo kazi kubwa aliyoifanya mwanzoni kabisa katika hususani kuanzia mwaka wa [19]63 alipokamata kiti cha Rais wa Tanganyika na basi mambo yakaenda mbio mbio kwa maana ya kutunga sheria za kuondoa hiyo hali ya ubaguzi na kuweka hali ya kuweka misingi ya maendeleo mipya kwa ajili ya taifa jipya.

Na alifanikiwa sana. Alifanikiwa ndio maana nasema imekuwa safari ya mafanikio kwa sababu ya misingi iliyowekwa, misingi imara. Kwa hiyo, marais waliofuata baada ya hapo walikuwa wanaweka matofali; yalikuwa matofali tu juu ya misingi hiyo imara iliyokwisha kujengwa. Ndiyo maana tumeendelea mpaka sasa katika hali ya uhuru na amani kwa sababu misingi iliyojengwa ilikuwa imara na waliofuata wameendelea kuiheshimu na kuitekeleza. Kwako mtangazaji.

The Chanzo: Asante sana Mzee Msekwa, umefafanua vizuri tu na nilikuwa nataka kukuuliza, kwa sababu tunafahamu kusema kweli lengo la kupigania uhuru ilikuwa ni kuwawezesha wananchi wa Tanzania kuweza kujiamulia mambo yao wenyewe kama watu wa Tanzania waweze kujiamulia mambo yao wenyewe. Miaka sitini sasa tangu tupate uhuru, unatathimini vipi hilo, unadhani Watanzania wana nafasi gani katika kujiamulia mambo yao wao wenyewe kama watu huru?

Pius Msekwa: Tuangalie misingi iliyowekwa. Maana maamuzi yanafanywa na vyombo hamna mtu anajiamulia mwenyewe peke yake nyumbani kwake anaamua mambo. Mambo ya nchi yanaamuliwa na vyombo vilivyowekwa na chombo kikubwa cha kufanya maamuzi hayo ni Bunge; Bunge ambalo linawakilisha wananchi.

Kwa hiyo, Bunge lililowekwa na utaratibu ukatengenezwa kuwawezesha wananchi wenyewe wapige kura kuwachagua wawakilishi wao kwenda bungeni kufanya maamuzi kwa niaba yao. Haiwezekani wananchi wote wakaenda kufanya maamuzi. Haiwezekani. Kwa hiyo, maamuzi yanafanywa na wawakilishi.

Kwa hiyo, jambo la kwanza lililowekwa ni kuunda Bunge la nchi huru ya Tanganyika na kufanya maamuzi kwa niaba ya wananchi na Bunge hilo limeendelea kuwepo mpaka leo tunafikisha miaka sitini. Bunge linachaguliwa na wananchi na linafanya kazi nzuri ya kufanya maamuzi kwa niaba ya wananchi. Ni mafanikio mengine unaweza kuyaweka katika orodha ya mafanikio.

The Chanzo: Na wewe nafahamu ulikuwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kwenye hilo hilo eneo la watu kuwa na uwezo wa kujiamulia mambo yao wenyewe, unadhani ni kwa kiasi gani, kwa mfano, Bunge letu kwa sasa na muundo wake unatoa hiyo nafasi kwa wananchi kwa sababu ukiangalia ni ndani ya miaka mitano ndio mbunge anachaguliwa na unadhani, kwa mfano, kuna ushirikishwaji wa kutosha kati ya mbunge na wananchi wakati pengine mbunge akiwa bungeni katika mchakato wa kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na sauti kwenye uendeshaji wa nchi?

Pius Msekwa: Kwa sababu mimi narudi kwenye misingi iliyowekwa kuhakikisha kwamba wananchi wanawakilishwa vizuri ndio maana uchaguzi unafanywa kila miaka mitano. Kila Jimbo lina mwakilishi wake. Kama mwakilishi wao hakufanya kazi nzuri wanayopenda wananchi wanayo nafasi ya kumuondoa na kuchagua mwingine.

Naomba tuelewane vizuri kwamba namna ya kuwakilisha wananchi, namna ya wananchi kuridhika kwamba mwakilishi wao anafanya kazi nzuri ni kila miaka mitano na kama hakuridhika vizuri wanamuondoa wanamuweka mwingine. Na hiyo imekuwa ikitokea. Wewe ni shahidi watu wengi wanaonisikiliza pia ni mashahidi kwamba kila uchaguzi unapofanyika wabunge wengi hawarudi wanakuja wapya.

Hata katika Bunge la sasa nadhani asilimia 60 ni wabunge ni wapya. Unaona hiyo ndio fursa ya wananchi ya kuhakikisha kwamba wanayoyataka yanawakilishwa vizuri katika chombo hicho cha maamuzi. Umenipata? Kwako.

The Chanzo: Kabisa, nimekupata vizuri na unazungumiaje kwa mfano, kwenye muktadha huo huo kwa sababu tunazungumzia suala la uwezo wa wananchi kuweza kujiamulia mambo yao kupitia wawakilishi wao bila shaka.

Pius Msekwa: Ndio.

The Chanzo: Unazungumziaje suala la wabunge kupita bila kupingwa? Hivi karibuni tulimsikia Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi akawa anashauri kwamba wale wabunge wanaodaiwa kupita bila kupingwa wapigiwe kura za ‘Ndio’ au ‘Hapana.’ Bila shaka alikuwa anamaanisha hiyo hiyo kupanua hiyo fursa kwa wananchi katika kujiamulia mambo yao wenyewe. Mtazamo wako wewe ni upi?

Pius Msekwa: Hayo ni mawazo yake, hayo ni mawazo yake. Sasa, kwani misingi hiyo haikuwekwa na Nyerere? Misingi hiyo ipo katika dunia nzima kwamba nafasi inatolewa kwa wagombea kujitokeza, yaani utaratibu ni kwamba nafasi inatolewa na wananchi wagombee, wanajitokeza kugombea kupitia kwenye vyama vyao, sasa kama kuna vyama havileti, havisimamishi mgombea [unafanyaje]?

Basi ambaye amekuwa peke yake basi amepita bila kupingwa. Hiyo si tatizo hata kidogo. Wananchi wamewakilishwa bado kwamba wale wengine wote wameogopa kusimama basi akabaki huyu, dunia nzima ndivyo inavyofanya hakuna kura ya ‘Ndio’ wala ‘Hapana’ popote pale. Kuna nafasi ya kusimama [na kugombea]. Kama hukusimama basi maana yake hutaki basi.

Kwa hiyo, hakuna cha ‘Ndio’ au ‘Hapana.’ Usinipeleke kwenye mawazo ya mtu, hayo ni mawazo ya mtu. Hayo ni mawazo ya mtu sisi tuzungumzie misingi [ili] ieleweke kwanza.

The Chanzo: Ni sawa kabisa.

Pius Msekwa: Umenipata?

 

The Chanzo: Ni sawa kabisa.

 

Pius Msekwa: Baki kwenye misingi, baki kwenye misingi!

 

The Chanzo: Sawa sawa, na unadhani labda pengine hiyo ni afya kiasi gani, hilo suala la watu kwa mfano kupita bila kupingwa lina afya kiasi gani, Ukizingatia uhuru kama wa nchi na uhuru wa wananchi?

 

Pius Msekwa: Embu usiniulize maswali ya kitoto athari kiasi gani litaathiri namna gani? Ndio utaratibu uliopo dunia nzima. Sasa dunia nzima inaathirika kwa sababu watu wengine wameogopa kujitokeza kugombea? Wewe vipi?

 

The Chanzo: Unadhani haina athari yoyote?

 

Pius Msekwa: Sina ninachodhani ni misingi. Mimi nazungumzia misingi. Wewe unatafuta mawazo yako. Hiyo miaka sitini ya uhuru sio kwamba tusikilize mawazo ya mtu mmoja mmoja. Hamfiki [kwa] namna hiyo.

The Chanzo: Upo sahihi.

Pius Msekwa: Ehee basi. Umenipata sasa basi, umenipata?

The Chanzo: Nimekupata vizuri.

Pius Msekwa: Sheria ya mtu kupita bila kupingwa ilipitishwa na Bunge. Wawakilishi wa wananchi [waliopo ndani ya] Bunge ndio waliopotisha sheria hiyo. Sasa wewe kama kuna mtu ana mawazo yake basi amshawishi mbunge wake ayalete bungeni. [Huo utaratibu] hauwezi kubadilishwa na mtu mwingine wala na tume ya nani. Haiwezekani. Lazima sheria ibadilishwe na Bunge, umenipata?

The Chanzo: Kabisa nimekupata vizuri.

Pius Msekwa: Na yeye mwenye mawazo hayo anaye mbunge wake. Kwa hiyo, amridhishe mbunge wake alete wazo hilo bungeni aone kama litakubalika na wabunge [wengine]. Ndio misingi ya uongozi na utawala wa nchi yetu iliyowekwa na waasisi wa taifa letu.

The Chanzo: Pale mwanzoni kabisa uligusia kwamba katika kipindi hiki cha miaka sitini ya uhuru wa Tanzania kuna mambo mengi yamefanyika kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa, [na] kijamii. Na kusema kweli ni ukweli kabisa Tanzania ya leo ni tofauti na Tanzania ya mwaka 1961. Na moja kati ya jambo kubwa kusema kweli katika historia ya Tanzania kuwahi kutokea ni uamuzi wa Tanzania kama nchi kusema kweli kurudisha mfumo wa vyama vingi ile mwaka 1992 na hapo mwanzo uligusia kwamba wewe ulikuwepo tangu uhuru na bila shaka utakuwa ulishuhudia wakati mfumo huu unarejeshwa. Nataka kupata maoni yako, unadhani kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vya vingi Tanzania ulikuwa ni uamuzi sahihi?

Pius Msekwa: Kwa nini tuliweka uamuzi wa kuwa na chama kimoja? Hayo [ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi] ni matokeo. Ili kuelewa vizuri lazima turudi kwenye misingi. Kwa nini Mwalimu Nyerere katika miaka ya mwanzo aliweka utaratibu wa chama kimoja? Utaona kwamba kama misingi hiyo ilikuwa sahihi basi yakurudi kwenye vyama vingi nayo ilikuwa sahihi basi nisikilize vizuri.

The Chanzo: Naam!

Pius Msekwa: Kabla ya uhuru kulikuwa na chaguzi zilifanyika mara mbili 1957 [na] 1958 na mwaka 1960 ni chaguzi mbili tofauti zilifanyika. Na katika chaguzi hizo wagombea wa TANU, chama kilichopigania uhuru, wagombea wa TANU wengi, karibia wote, walikuwa wanapita bila kupingwa. Tunarudi kwenye swali la kupita bila kupingwa. [Basi] walikuwa wanapita bila kupingwa.

Kwa hiyo, wananchi wakawa hawana nafasi ya kupiga kura kuwachagua nani miongoni mwa wengi atawawakilisha wao. Katika uchaguzi wa mwanzo 1957/1958 ilitokea hivyo na pia uchaguzi wa pili wa mwaka 1960 ikatokea hivyo hivyo, yaani karibu wabunge wote wanapita bila kupingwa, [wabunge] wale wa TANU.

Sasa Nyerere akaona hiyo si nzuri kwa demokrasia [kwamba] watu wananyimwa haki ya kuinama kwenye karatasi na kusema miongoni mwa hawa namtaka huyu. Kwa nini walikuwa wanapita bila kupingwa? Wale [wagombea] wengine [kutoka vyama vingine mbali na TANU] hawana nafasi, watashindwa tu. Kwa hiyo, wanaogopa hata kujitokeza kwa jinsi TANU ilivyokuwa na nguvu.

Kila mtu anataka uhuru. TANU inataka uhuru, sasa wewe unampinga mgombea wa TANU hutaki uhuru, unaona? Basi ndio watu wakawa wanaona siwezi, siwezi, siwezi [kugombea dhidi ya mgombea wa TANU]. Ndio maana Nyerere akaona kama hali ndio hii basi bora tuweke chama kimoja ili watu waweze kugombea ndani ya chama kimoja waweze kugombea ili wananchi wapate nafasi ya kuchagua mmoja wapo.

Lengo zuri sana lakini hiyo hiyo yakuona kwamba kupita bila kupingwa ingawa ni mtu anajipima mwenyewe anaona hana basi anaogopa kugombea. Lakini bado haileti nafasi kwa wananchi kuchagua yule wanaye mtaka. Kwa hiyo, Nyerere akasema bora tuwe na chama kimoja ili wagombea wengi ndani ya chama kimoja hicho, maana yake huyu apate nafasi ya kupiga kura ndio ilikuwa sababu.

Na akasema kwa kuwa chama hiki kipo wazi kwa kila mtu anayetaka hakukuwa na masharti kwamba wewe huwezi kuwa mwanachama mpaka uwe wa namna gani. Mtanganyika yeyote alikuwa anaruhusiwa kwenye chama [na] alikuwa anaweza kugombea kwenye chama.

Kwa hiyo, ilikuwa ni kama chama cha wote. Hapakuwa na ufinyu wa ubaguzi wa namna yoyote kwamba huyu hukubaliki, wote, wote walikuwa wanakubalika. Kwa hali hiyo basi akasema basi ngoja tuweke Katiba itakayo ruhusu kila mwanachama aweze kugombea.

Ilipoonekana kwamba dunia, katika dunia watu wote na sio sisi tu peke yetu kulikuwa na nchi nyingi zenye chama kimoja karibu nchi nyingi za Afrika zote zilikuwa na chama kimoja kinachoongoza cha siasa. Lakini katika miaka hiyo ya mwanzoni, miaka ya tisini kuanzia themanini na tisa kuingia kwenye tisini, wimbi la dunia likabadilika likataka ushindani wa vyama vingi.

Ilianzia Urusi [ambapo] vyama vya kikomunisti vikapinduliwa, vikaanguka. Wimbi likaja mpaka huku Afrika watu wakawa wanadai vyama vingi na sisi basi ndio maana uamuzi ukafanywa kama hayo ndio matakwa ya sasa ya wananchi basi twende tuwasikilize, twende kwenye vyama vingi. Kwa hiyo, ilikuwa ni uamuzi sahihi unaotekeleza mahitaji ya wakati uliopo.

Yale kwenda kwenye chama kimoja tulikuwa tunatekeleza mahitaji ya wakati huo kwamba watu wanapita bila kupingwa wote, wote, wote haina maana ndio ilikuwa hali ya wakati ule. Hali ilipobadilika ukawa ni uamuzi unaoendana na wakati wa nafasi ya kushindana kwenye vyama vingi. Umenipata vizuri?

The Chanzo: Vizuri.

Pius Msekwa: Basi baki kwenye misingi angalia misingi ndio utaelewa vizuri zaidi.

The Chanzo: Upo sahihi. Na kwa mujibu wa ulivyoeleza ni kama vile shinikizo ni kama lilitoka nje, sivyo?

Pius Msekwa: Ndio nimekueleza kwamba ilianzia Urusi, kitu lazima kianzie mahali fulani. Lazima wazo lianzie mahali fulani na wengine ndio wanalidaka. Ndio nimesema hivyo mara ya kwanza na sababu yake ndio hiyo, kwamba hakuna wazo litakaloibuka dunia nzima kwa wakati mmoja. Lazima lianzie mahali halafu wengine wanaliona lakini hili linafaa.

The Chanzo: Na si kwamba labda, tunakumbuka tunafahamu kwamba kilichokuwepo ni chama tawala, si kwamba chama tawala …

Pius Msekwa: Nisikilize, na ndicho chama hicho kilichokubali wazo hilo.

The Chanzo: Ndio.

Pius Msekwa: Kwamba kulikuwa na shinikizo la kutoka nje? Hapana. Ni chama tawala chenyewe kilichokaa nikiwa mmoja wapo katika vikao hivyo, kikaona jamani katika hali hii tutaendelea kama tulivyo katika hali hii? Na Mzee [Ali Hassan] Mwinyi [Rais wa awamu ya pili] akaunda Tume ya Nyalali, mimi nikawa mjumbe wa wa tume hiyo tukawaulize wananchi [ambapo] asilimia 80 wakasema hapana, hatutaki kubadilika tuendelee kama tulivyo [na mfumo wa chama kimoja].

Tukaona kwamba hawa wako nyuma, hawaitazami dunia inavyokwenda wanaiangalia Tanzania peke yake hawaangalii dunia kwa ujumla. Na sisi tukapendekeza kwamba pamoja na kwamba asilimia 80 imekataa [tukasema huko] ni kwa kutokujua, kutokuelewa miaka 30 hawajaona vyama vingi wanavisikia tu kwamba kuna fujo, kuna ugomvi wakaogopa fear of the unknown kwa Kingereza, wakaogopa.

Sisi tukasema hapana. Sisi ambao tuna uelewa huo tunashauri chama hiki kikubali kukaribisha vyama vingine na chama kikakubali. Umenipata vizuri?

The Chanzo: Nakupata! Lakini si pengine kwa sababu mlikuwa hamna option nyingine?

Pius Msekwa: Ndio nasema, hatuna option nyingine kwa sababu kwa wakati huo hakuna nyingine. Kwani ungetaka ungepata wapi option nyingine? Dunia nzima inabadilika wewe utabaki na option utaganda hapo hapo ulipo utakuwa unaakili kweli? Bila shaka tulikuwa hatuna option nyingine kwa sababu dunia inabadilika na kama na nyie mnaakili mnabadilika pamoja na dunia. Umenipata?

The Chanzo: Kwa hiyo maana yake ni kwa sababu hakuna option nyingine kwa hiyo hata kama wananchi wanataka tubaki na mfumo wa chama kimoja, Chama Cha Mapinduzi kikasema hapana lazima twende mfumo wa vyama vingi?

Pius Msekwa: Ndio tukubaliane na mzunguko wa dunia, na hoja hiyo tulipoifikisha kwa Mwalimu Nyerere tukasema hali ndio hii sasa tufanyeje akasema wale [waliotaka tubaki na mfumo wa chama kimoja] ni kutokuelewa tu, wale asilimia ishirini waliobaki [ambao walitaka mfumo wa vyama vingi] lazima tuwasikilize kwa sababu ndio matakwa ya dunia sasa lazima muwasikilize wale ishirini msipo wasikiliza wataendelea kudai.

Halafu kutakuwa na vurugu ndani ya nchi mtaanza kutumia polisi kuwanyamazisha, mimi sitaki utawala wa polisi wacha watu watawaliwe kwa utulivu na amani kwa hiyo wakubalie wale watu [asilimia] ishirini na [Mwalimu Nyerere] akatuambia katika kikao hicho faida ya vyama vingi ni kushindana. Sasa kama asilimia 80 wanataka chama chao kishinde si watakipigia kura? Lakini si wakipigie kura ndio watashinda, waogopa nini?

Unaona mantiki hiyo? Na kweli katika uchaguzi uliofuata wabunge asilimia 80 ya wabunge wakawa ni wa CCM [kama] alivyokuwa ametabiri Nyerere kwamba kama mnataka chama chenu kiendelee kushinda si mkipigie kura katika ushindani huo? Kwa nini muwazuie wengine? Unaona?

The Chanzo: Naelewa.

Pius Msekwa: Basi ndiko tulikotoka huko.

The Chanzo: Tumetoka mbali kusema kweli.

Pius Msekwa: Tumetoka mbali!

The Chanzo: Na labda kusema kitu ambacho hukijui mimi [Khalifa Said, mwandishi] nimezaliwa 1992, kwa hiyo nina umri sawa sawa na mfumo wetu wa vyama vingi kama miaka 29 hivi. Labda pengine kwa kuangilia yale ambayo yametokea tangu mfumo huu wa vyama vingi urejeshwe bado unadhani kwamba tulifanya uamuzi sahihi kujiunga na mfumo wa vyama vingi, ukiangalia hii miaka ishirini na tisa yote tuliyopita?

Pius Msekwa: Hatujapata tatizo, wewe kwa kuwa bahati njema ulikuwepo wewe umeona tatizo gani? Maana yake narudia kwenye maana ya Mwalimu Nyerere vyama vingi maana yake ni ushindani, tumekuwa tukishindana kila baada ya miaka mitano tumekuwa tukishindana. Sasa tumepata tatizo gani? Hakuna tatizo.

Lengo limefikiwa, [namaanisha] lengo la kushindana. Tumekuwa tukishindana [ambapo] CCM inashindana na vyama vingine katika ngazi ya urais, katika ngazi ya ubunge, katika ngazi ya udiwani. Tumeshindana. Hilo ndio lilikuwa lengo. Hatujashindwa katika lengo hilo. Maana yake ushindani unakuwepo kila [baada ya] miaka mitano bila kukosa. Kila [baada ya] miaka mitano bila kukosa. Mwaka jana, 2020 ulikuwa ni mwaka wa tano tukafanya uchaguzi na tukashindana. Mwaka 2015 tukashindana na [Edward] Lowassa [aliyekuwa mgombea wa urais kupitia chama cha upinzani CHADEMA na kuungwa mkono na vyama vingine vya upinzani] akapata kura nyingi sana akakaribia kushinda unaona?

Kwa hiyo, naomba utazame malengo kama yamefanikiwa au yameshindwa kufanikiwa. Lengo ilikuwa ni kushindana kwa kuwa ushindani umekua, hatujazuia ushindani [nchini Tanzania]. Kuna nchi zinakaa miaka kumi hawajafanya uchaguzi wana matatizo yao. Sisi hatujakaa zaidi ya miaka mitano hatujafanya uchaguzi. Kila miaka mitano tangu uhuru, kila miaka mitano tunafanya uchaguzi. Ndio maana nikasema ni mafanikio. Kimekuwa ni kipindi cha mafanikio kwa miaka yote kwa malengo yaliyowekwa.

The Chanzo: Kabisa nakubaliana na wewe asilimia mia kusema kweli huwezi kulinganisha Tanzania na nchi nyingine, na ni mafanikio kusema kweli.

Pius Msekwa: Basi tuendelee.

The Chanzo: Lakini katika muktadha huo huo wa ushindani, na pale nyuma kidogo uligusia mantiki ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kwamba kama mnakipenda chama chenu washindane na wengine. Nataka kufahamu labda katika maisha yako ya kisiasa ulishawahi kufikiria kwamba inaweza ikatokezea siku chini ya mfumo huu wa vyama vingi na Tanzania hii ilivyo huru tangu tunapata uhuru, kuona kwamba Rais anasimama na kusema kwamba sasa tumemaliza uchaguzi na siasa inabidi zisimame sitaki kuona mikutano ya hadhara kwani sasa najenga uchumi au mikutano inazuia kutimiza kile nimewaahidi wananchi wakati wa kampeni. Ulishawahi kufikiria kitu kama hicho kinaweza kutokezea kwenye Tanzania huru ya vyama vingi.

Pius Msekwa: Rudi kwenye msingi. Misingi ndio ushindani. Sasa ushindani si wakati wa uchaguzi, baada ya uchaguzi mnashindana nini, kufanya mikutano kuna ushindani? Rudi kwenye misingi. Mimi nakurudisha kwenye misingi na malengo. Lengo la vyama vingi ni ushindani, ushindani ni wakati wa uchaguzi, mkisha shindana mkashinda wengine wakashinda wengine wakashindwa lengo limetimia sasa baada ya hapo mnashindana kwenye mikutano ya hadhara? Na wewe angalia, na wewe pima kwa akili zako baki kwenye lengo, [ambalo] ni ushindani, kushindana mmeshindana mmeshindwa sasa?

The Chanzo: Lakini sasa tunajijenga vipi kabla ya uchaguzi mkuu, yaani nashindana vipi na wewe bila kujiandaa?

Pius Msekwa: Mtapanga wenyewe namna ya kujiandaa si mnajiandaa kwa ushindani?

The Chanzo: Sasa tunajiandaa vipi wakati tunaambiwa tusifanye siasa?

Pius Msekwa: Sikiliza basi, naona na wewe akili yako haikukamilika, umeambiwa usifanye siasa kwani kufanya mikutano ya hadhara ndio siasa? Mikutano ya ndani ni siasa. Wewe jenga chama chako ongeza wanachama ili upate kura nyingi. Hiyo ni siasa. Mbona unaweza kuandikisha wanachama kwa kuwafuata nyumba hadi nyumba ukapata wanachama.

The Chanzo: Lakini inakuwa ngumu sana, inakuwa ni kama vile tumerudi zama zile ambazo ni za ukoloni?

Pius Msekwa: Sikiliza, sikiliza, sikiliza hayo ni mawazo yako mimi narudi kwenye [malengo], tujadili malengo na misingi imetekelezwa? Mimi nakwambia imetekelezwa ya ushindani imetekelezwa sasa kama wewe mawazo yako unafikiri mikutano ya hadhara ndio ushindani basi wewe endelea na mawazo yako potofu. Niulize maswali yanayohusu misingi.

The Chanzo: Si ndio hiyvo. Kwa mfano, kama tukirudi kwenye hilo eneo la misingi, tunafamu kwamba tulitunga Sheria ya Vyama vya Siasa tukatunga na Katiba ya 1977 na tulipokuja kurudisha mfumo wa vyama vingi tuliweka hizo haki za vyama vya siasa, [ikiwemo] haki za kufanya siasa. Hii si misingi, hudhani kuwa hii ni misingi ambayo …

Pius Msekwa: Sikiliza tuliweka haki ya kushindana sio ya kufanya siasa, wewe vipi? Tuliweka haki ya kushindana. Lengo la vyama vingi ni kushindana katika uchaguzi, [yaani] electrol competition ndio lengo, sio lingine. Na kama ni kushindana katika siasa mkishaingia bungeni mnashindana huko ndani ya Bunge kwa wananchi wameshamaliza kazi yao ya kuwachagua sasa nendeni mkashindane huko mlikopelekwa.

The Chanzo: Kwa mfano, kama chama chetu au chama cha watu fulani hakijapata mbunge?

Pius Msekwa: Basi mjipange muda mwengine mpate mbunge.

The Chanzo: Hapo ndipo linapokuja swali la kwamba wanajipanga vipi katika mazingira ambayo hawaruhusiwi kufanya siasa mpaka kipindi cha uchaguzi?

Pius Msekwa: Kwa kuandikisha wanachama kwani lazima kufanya siasa maana yake nini? Maana yake nini kufanya siasa? Andikisha wanachama ndio kazi, sio kufanya siasa.

The Chanzo: Sawa sawa.

Pius Msekwa: Kazi sio kufanya siasa. Kazi ni kuongeza wanachama ili waongeze idadi za kura zako. Haya nadhani nimekuelewesha hapo.

The Chanzo: Umenielewesha na nimeelewa vizuri tu.

Pius Msekwa: Basi tuendelee, tuendelee.

The Chanzo: Nataka [tubaki] kwenye hii hii miaka sitini ya uhuru. Hatuwezi kuzungumzia miaka sitini ya uhuru bila kuizungumzia Chama Cha Mapinduzi.

Pius Msekwa. Ndio, ni kweli.

The Chanzo: Au TANU kwa sababu kusema kweli ndio chama ambacho kilitupatia uhuru, tukakubali kukakataa. Sasa nilikuwa nataka kuuliza kuhusiana na tathmini yako ya jinsi Chama Cha Mapinduzi kilivyo, unajua, kubadilika au kuimarika au kama ni kudhohofika.

Pius Msekwa: Kilivyofanya kazi yake, usitamke kubadilika. Jinsi Chama Cha Mapinduzi kilivyofanya kazi yake.

The Chanzo: Ndio, namaanisha tangu tumepata uhuru mpaka leo unatathimini vipi kazi za chama chako cha mapinduzi?

Pius Msekwa: Na mimi nakwambia lazima kwanza ujue kazi yake. Kazi ya chama, wacha cha Mapinduzi, kazi ya chama chochote ni nini? Kazi ya chama tawala kinachokuwa madarakani ni nini? Sasa nakueleza kwamba kazi ya chama ni kutoa miongozo, inaitwa sera. [Kazi yake] ni kutengeneza sera ambazo zitaiongoza Serikali katika kuhudumia wananchi.

Sasa Chama Cha Mapinduzi tangu TANU kimekuwa kikitekeleza wajibu huo kwa ufanisi, tena kinatoa sera zake kwa maandishi. Kulikuwa na sera ya Azimio la Arusha kwa maandishi, kwamba tunataka uchumi wetu uendeshwe kwa namna hii, kwamba usimamiwe na dola usimamiwe na Serikali, ni sera na ikatekelezwa mpaka ilipofika mahali ukaonekana haifanikiwi ikabadilika.

Chama hicho hicho kikaweka sera nyingine ambayo kwamba sasa tunataka wananchi wenyewe waruhusiwe kumiliki uchumi kupitia makampuni ya umma, kupitia vyama vya ushirika, kupitia joint venture sera ile ikabadilika mwaka 1991.

Chama Cha Mapinduzi kikabadilisha sera, kikatoa miongozo na sheria zikabadilika zikawekwa fursa za kushirikisha watu binafsi, za kushirikisha mashirika binafsi katika kuukuza uchumi wa nchi. Kwa hiyo, yale mashirika yaliyokuwa yametaifishwa yakarejeshwa, [yaani] yakabinafsishwa [na] yakarejeshwa katika kuendeshwa na watu binafsi au makampuni binafsi tunaona.

Kazi ya chama kinachotawala chochote kile, chama chochote kinachotawala iwe Labour Party ya Uingereza iwe Conservative Party ni kutoa sera, yaani policy ambazo zitatekelezwa na Serikali. Sasa Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikitoa Ilani ya Uchaguzi, yaani sera zake zinaandikwa kwenye kitabu kinaitwa Ilani ya Uchaguzi, kama tukifanikiwa kuchaguliwa tutafanya hili na hili na hili na kweli Serikali inayoingia madarakani inafanya hayo hayo yaliyopendekezwa na chama.

Kwa maana hiyo, Chama cha Mapinduzi kimetekeleza kwa ukamilifu wajibu wake, na chama cha TANU kabla yake kilitekeleza wajibu wake wa kutoa miongozo na kusimamia Serikali itekeleze miongozo hiyo bila kupingwa [na Serikali].

The Chanzo: Nimekupata vizuri. Juzi juzi tu hapa nilikuwa naongea na Askofu Benson Bagonza ambaye ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Karagwe, ambapo pamoja na mambo mengine alisema, kwa maoni yake, kwamba chama cha CCM kimeacha kuwa chama tawala na sasa kinatawaliwa na dola, kwamba wakati …

Pius Msekwa: Usinipeleke-, sikiliza usinipeleke kwenye mawazo ya watu. Kila mtu ana haki ya kuwa na mawazo yake. Huyo ni mtu mmoja. Sasa mimi unataka nizungumzie mawazo ya mtu mmoja [inakuwa] sivyo. Mimi nazungumzia utendaji wa-, uliniuliza chama kimetekeleza wajibu wake, mimi nimekwambia ndio na nikakueleza wajibu ni nini. Sasa labda haelewi wajibu wa chama ni nini.

The Chanzo: Lakini …

Pius Msekwa: Usinipeleke kwenye mawazo ya mtu mmoja.

The Chanzo: Ni sawa, ni sawa

Pius Msekwa: Basi tuendelee. Achana na hiyo. Achana na kuniuliza mawazo ya mtu mmoja mmoja. Mimi siwezi ku comment kwenye mawazo ya mtu.

The Chanzo: Ni sawa, ni sawa.

Pius Msekwa: Mimi na comment juu ya miaka sitini ya uhuru.

The Chanzo: Kabisa kabisa, ni sawa. Na kwenye hii hii miaka sitini ya uhuru, unajibu vipi tuhuma dhidi ya chama chako kwamba kimekuwa chama dola, kwamba ni chama kinachotumia dola kuweza kubaki madarakani? Hizi tuhuma wewe, nafahamu kwamba ni kada wa Chama cha Mapinduzi, unajisikiaje unapo sikia chama chako kinatupiwa shutma kama hizi?

Pius Msekwa: Chama tawala maana yake ni chama kinachoongoza dola, yaani maana-, yaani watu hamuelewi maana ya maneno haya. Chama tawala maana yake ni chama kinachoongoza dola, ni chama dola kwani unataka iweje?

The Chanzo: Unadhani ni sahihi kwa chama- …

Pius Msekwa: Ndio mfumo wenyewe.

The Chanzo: Na unaounaje huo mfumo, unaona ndio mfumo mzuri, kwenye mfumo wa nchi ambayo inafuata misingi ya mfumo wa vyama vingi?

Pius Msekwa: Katika vyama vingi kitakuja chama kingine kiwe chama tawala kitafanya hayo hayo.

The Chanzo: Unadhani ni sahihi kwa chama tawala kutumia vyombo vya dola kubaki madarakani?

Pius Msekwa: Ni sahihi kwa kwa Chama cha Mapinduzi kutoa miongozo. Usinitoe kwenye mazungumzo.

The Chanzo: Sikutoi kwenye mazungumzo. Tunazungumzia kuhusiana na Chama cha Mapinduzi kwenye miaka sitini ya uhuru. Tunakifanyia tathimini.

Pius Msekwa: Sasa ndio nakufanyia tathimini kwa kukupa maana ya kazi za chama tawala na kama zime zitekeleza vizuri. Sasa kama wewe huoni, hayo ni mawazo yako, baki nayo.

The Chanzo: Hapana, mimi nataka kufahamu kwa sababu najua wewe ni kada wa Chama cha Mapinduzi na nilikuwa nina shauku- …

Pius Msekwa: Ndio nakueleza kwamba tumetekeleza vizuri, tumetekeleza yale ambayo yanatakiwa kufanywa na chama tawala. Yale ambayo yanatakiwa ni kutoa miongozo, tumetoa miongozo ya Azimio la Arusha. Tumetoa miongozo ya kuingia kwenye vyama vingi. Tumetoa miongozo [na] tumetekeleza vizuri. Sasa kama wewe una mawazo tofauti hiyo ni haki yako, kila mtu ana haki ya kuwa na mawazo yake usinishirikishe mimi kwenye mawazo binafsi.

The Chanzo: Hapana Mzee Msekwa mimi nilikuwa nataka kufahamu tu yaani- …

Pius Msekwa: Usitafute mawazo yangu binafsi. Mimi nazungumzia kazi za nchi. Zaidi ya hapo mimi sina mawazo.

The Chanzo: Kwa hiyo unakubaliana na madai kwamba Chama cha Mapinduzi ni chama dola kwa sababu ndio kipo madarakani?

Pius Msekwa: Hayo nakubaliana kwamba ndio mfumo wa dunia na kwamba chama kinachotawala ni chama dola. Ndio mfumo wa dunia.

The Chanzo: Na nilazima itumie vyombo vya dola kubaki madarakani?

Pius Msekwa: Hilo hulijui, hilo hulijui kwamba chama tawala-,wewe unapotoka, umepotoka kweli. [CCM] kinatumia wananchi kukipigia kura, hakitumii vyombo vya dola wewe vipi? Ni kura za wananchi sasa kama umeishiwa mimi nakata simu.

The Chanzo: Usikate simu Mzee Msekwa, usikate simu tunaendelea.

Pius Msekwa: Basi baki kwenye misingi ya mazungumzo sitaki ohoo maoni yangu binafsi. Maoni ya kwako binafsi mimi sitaki maoni binafsi. Tuzungumzie miaka sitini ya uhuru. Tumetekeleza malengo?

The Chanzo: Kabisa.

Pius Msekwa: Hiyo mimi nakwambia tumefanikiwa kutekeleza malengo.

The Chanzo: Mzee Msekwa, nataka nikuulize kitu kimoja. Kwenye hii hii miaka sitini ya uhuru tunatumia Katiba ambayo iliandikwa mwaka 1977, ndio ambayo ni katiba inayoongoza nchi yetu mpaka hivi sasa na kumekuwa na matamko, kauli kwa ajili ya kupatikana Katiba Mpya

Pius Msekwa: Sikiliza sikiliza usipoteze muda tuna Katiba ilianzishwa na Rais Jakaya Kikwete

The Chanzo: Mchakato ule- …

Pius Msekwa: Ni mchakato haujakamilika. Kwa hiyo wewe tambua hilo kwamba tuna Katiba Mpya ambayo inangoja kupigiwa kura ya maoni.

The Chanzo: Unadhani ni kitu gani kimekwamisha Serikali kupeleka [Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kwenye kura ya maoni?]

Pius Msekwa: Sijui, mimi sipo serikalini. Usitake sijui maoni yangu binafsi. Nakwambia huisikii, huisikii. Usitafute maoni yangu binafsi. Kila mtu ana maoni yake.

The Chanzo: Si maoni binafsi Mzee Msekwa kwa sababu tunajadili kuhusiana na masula ya uhuru, tunajadili uhuru.

Pius Msekwa: Wewe unaniuliza hiyo naonaje, maana yake mimi binafsi naonaje?

The Chanzo: Kabisa kabisa, yaani kwa mfano, kwa mfano Mzee Msekwa- …

Pius Msekwa: Bwana mimi nitakata simu kama umeishiwa.

The Chanzo: Usikate simu Mzee Msekwa, usikate simu.

Pius Msekwa: Sasa kwa nini unabishana?

The Chanzo: Sibishani, nafafanua tu kile ambacho nataka unisaidie kupata ufafanuzi.

Hello!

Hello!

[Mzee Pius Msekwa amekata simu].

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts