The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Simulizi ya Mama Aliyemshitaki Mwanae Kwa Kushindwa Kuwalea Wajukuu Zake

Serikali na Mahakama zabainisha madai ya bibi huyo dhidi ya mtoto wake hayana ukweli wowote.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Je, unaweza kumshitaki mtoto wako pale unaposhawishika kama ameshindwa kuwapatia wajukuu zako malezi wanayostahili? Hiki ndicho Bi Sabira Mohamed Ayoub amekifanya dhidi ya mtoto wake wa kiume wa kumzaa Fahim Mohamed baada ya mama huyo kutofurahishwa na kile anadai mtoto wake anawafanyia wajukuu zake, ikiwemo kuwapiga na kuwafanyia vitendo vingine vya unyanyasaji.

Mama huyo wa watoto wawili, wakike na wakiume, anayeishi Mnazi Mmoja, Nkurumah na Nyerere jijini hapa ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake katika nyakati tofauti kwamba aliamua kumchukulia hatua kijana wake huyo kwa kile alichodai kwamba tabia za mtoto wake huyo ni “katili” ambazo zimepelekea kushindwa kutoa malezi yanayostahili kwa watoto wake, ambao ni wajukuu wa Bi Sabira.

“Mtoto wangu nampenda sana, siyo kwamba simpendi,” Bi Sabira anasema wakati wa mahojiano na The Chanzo nyumbani kwake. “Lakini vitendo vyake ndiyo vinanikera. Na si mara ya kwanza kumpiga huyo mtoto [mjukuu wangu]. [Kuna siku] alikuwa anampiga na mwiko. [Siku zingine] anamchoma na moto [wa] sigara. Wake zake walikuwa wananiambia nimchukue mtoto [kutokana na alichokuwa anafanyiwa]. Ndiyo maana mimi nikatafute njia ya kumchukua huyu mtoto.”

The Chanzo imechukua jitihada kadhaa za kumpata Fahim, ikiwemo kumpigia simu mara kadhaa na kufika nyumbani kwake na sehemu zinazojulikana kama maskani zake, ili aweze kutoa mtazamo wake kuhusiana na shutuma hizi lakini bila mafanikio yoyote. The Chanzo itachapisha taarifa ya Fahim muda wowote atakapotupatia taarifa hiyo.

Juhudi za ‘kumuokoa’ mjukuu wake

Bi Sabira, mama mwenye umri wa miaka 57 anayejishughulisha na biashara, anasema alichukua hatua hiyo akiamini kwamba Tanzania ina vyombo na mamlaka zinazolinda ustawi wa watoto, akiamini kwamba kwa ushahidi alioukusanya, ikiwemo picha zinazoonesha vipigo dhidi ya mtoto na ushuhuda wa walimu wa mtoto kutoka madrasa na shule, ungemsaidia katika madai yake yaliyolenga kuhakikisha kijana wake anahukumiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kuanzia Ofisi ya Ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi mpaka wizara inayohusika na masuala ya watoto na Mahakama Bi Sabira amekuwa akipigania kesi hiyo tangu mwaka 2019, huku akizishutumu taasisi hizo kutokuwa na msaada wowote katika jitihada zake za “kumuokoa” mjukuu wake.

Akielezea tathmini yake ya msaada ambao ameupata kutoka kwa taasisi za umma, hususani Ofisi ya Ustawi wa Jamii, Bi Sabira anasema: “Kusema kweli, mimi sikupata msaada wowote kutoka [huko]. Kimsingi ni kwamba [Ustawi] walinigeuzia kibao kabisa. Badala ya kusimama na mimi, wao walisimama na mtoto wangu wakawa wanasimama na yeye.”

Kwa mujibu wa Bi Sabira, Moureen Mollo kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii ya Kata ya Mnazi Mmoja ndiye aliyekuwa anahusika na kesi. The Chanzo ilimtafuta Moureen zaidi ya mara moja kuweza kupata mtazamo wake iwapo kama shutuma hizi ni za kweli lakini alikataa kuzungumza lolote kuhusiana na kesi hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi uliofanywa na Idara ya Maendeleo ya Jamii ilibainika kwamba tuhuma za ukatili unaodaiwa kutendwa na Fahim dhidi ya mtoto wake “hazina ukweli.” Barua ya Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwenda kwa Bi Sabira iliyoandikwa Julai 18, 2021, na ambayo The Chanzo imeiona inasema:

“Kwa barua hii, nakujulisha kuwa Wizara imejiridhisha na uchunguzi uliofanywa na kufukia maamuzi kuwa mtoto atabaki kwa baba yake Mzazi Bwana Fahimu Mohamed pia Wizara kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii itafuatilia maendeleo ya malezi ya Mtoto huyo na mtoto aliyeko Kenya kwa Mama yake.”

Juhudi za uokoaji zagonga mwamba

Kesi yake ya jinai dhidi ya kijana wake aliyoifunga Mahakama ya Kinyerezi, ambapo alimshitaki kijana wake kumpiga mjukuu wake ilitolewa uamuzi Septemba 9, 2021, baada ya kwenda takribani mwaka mzima, ambapo Mahakama ilitoa uamuzi wa kumpendelea mtoto wa Bi Sabira, huku ikisema hakuna ushahidi kamili kwamba mtoto alipigwa.

“Mimi nilijisikia huzuni sana [kufuatia uamuzi huo],” Bi Sabira anasema huku akionesha namna ambavyo Mahakama haikutenda haki kwenye kesi hiyo. “Kwa sababu mimi ni mzazi wa huyu mtoto na siwezi kuzua uongo dhidi ya mtoto wangu mwenyewe. Nimemzaa kwa uchungu. Lakini vitendo vyake haviniridhishi. Najua tabia zote mbaya na za jinai za mtoto wangu lakini nilifanywa muongo.”

Bi Sabira anasema Mahakama ilitoa uamuzi huo licha ya kwamba kulikuwa na ushahidi wa daktari kwamba mtoto amepigwa. Pia, Afisa wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto, kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam kuja mahakamani na kuthibitisha kweli kwamba mtoto alikuwa na jeraha kwenye kichwa. Pia, ushahidi wa mtoto mwenyewe ulikuwepo kwamba alipigwa na baba yake na mkanda na akabamizwa na ukuta.

Hii ilikuwa ni kesi ya pili Bi Sabira kushindwa baada ya ile ya madai aliyoifungua huko nyuma katika Mahakama ya Watoto ya Kisutu aliyofungua mnamo Desemba 2020 akiiomba Mahakama impatie ruhusa ya kuwalea wajuku wake wawili anaodai kwamba walikuwa wakinyanyaswa na baba yao. Hii ilikuwa ni kabla ya kufungua kesi hiyo ya jinai katika Mahakama ya Kinyerezi.

Joel Kiiya ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utetezi wa watoto la C- Sema. Ingawaje anakiri kwamba ni mara chache kwa kesi kama za akina Bi Sabira kuripotiwa nchini Tanzania, ni jambo la kawaida bibi kumlea mjukuu wake. Akijibu swali iwapo kama Bi Sabira anayo nguvu ya kisheria ya kupigania hifadhi ya wajukuu zake, Kiiya anasema: 

“Ndio anaruhusiwa [kwani inaonekana kama mzazi] anamuathiri mtoto kulingana na mazingira hayo [ya unyanyasaji na ukatili]. Lakini kama kuna ukosefu wa matunzo ambao unaambatana na ukatili inakuwa ni mserereko kabisa [kwa Bi Sabira kushinda kesi] na [hivyo] kupata hifadhi ya mtoto. Katika mazingira hayo, [Bi Sabira] anapewa mtoto anamtunza mwenyewe na anakuwa wa kwake kabisa na baba anapewa tu nafasi ya kumuona.”  

Uhusiano na mtoto wake wavunjika

Kama ambavyo ungetarajia, uhusiano kati ya Bi Sabira na mtoto wake kwa sasa si ule uhusiano unaoweza kuutegemea kuuona baina ya mtoto na mama yake: Anafafanua: “Sasa [mimi na mwanangu tunaishi] kama mahasimu kwa sababu baada ya mimi kumshitaki yeye alivunja mawasiliano na mimi kabisa. Na alitamka kabisa kwamba mimi siyo mama yake.”

Kama kuna funzo lolote ambalo Bi Sabira amelipata kutoka kwenye harakati zake zote hizi za kupigania hifadhi ya wajukuu zake ni kwamba haki nchini Tanzania inapatikana kwa tabu sana.

Licha ya yote aliyopitia, ikiwemo kuvunjwa moyo na taasisi za umma na vyombo vya utoaji haki nchini, Bi Sabira hata hivyo hajakata tamaa na anaahidi kuendelea kumpambania mjuu wake, akiamini kwamba ipo siku haki itatendeka na mjukuu wake huyo “ataondoka kwenye mikono kandamizi ya baba yake.”

Anaiambia The Chanzo kuhusu hatua anazopanga kuzichukua: “Ninafikiria nikate rufaa dhidi ya huyu mtoto wangu kwenye kwenye hii kesi ya [jinai niliyoifungua Mahakama ya] Kinyerezi. Na pia nitaendelea kuiomba Serikali inisaidie kwani huyu mtoto mimi ni mama yake mzazi, na ninaelewa tabia zake, na ushahidi [wa vitendo anavyomfanyia mjukuu wangu] ninao. Vitendo anavyofanya si sawa.

“Ningependa kutoa wito kwa wahusika, hususan wadau wa watoto, wasipuuze maneno ya wazazi dhidi ya watoto wao kwa sababu mzazi ndiye anayejua tabia ya mwanae. Na pia, mzazi hawezi akafanya maovu dhidi ya mtoto wake mwenyewe. Kwa hiyo, [mamlaka] zichukulie kwa uzito maneno ya wazazi na wawatetee watoto ambao hawawezi kujitetea.

“Pia, ningependa kuwaambia wazazi wenzangu [ambao wanapigania ustawi wa wajukuu zao] kwamba wasirudi nyuma kuwatetea wajukuu zao. Kwa sababu, hawa vijana wa siku hizi wanajali maslahi yao, na wanajali maisha yao zaidi kuliko watoto. Hawa ni watoto, malaika wa Mungu, hawajui kuzungumza, wanategemea sisi tuwapiganie na tuwasimamie, kama mimi nilivyowasimamia hawa [wajukuu zangu] kutoka kwa baba huyu katili na mama ambaye aliwatelekeza.”     

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia lukelo@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusu habari hii unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *