Dar es Salaam. Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) iliyokabidhiwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba mnamo Septemba 29, 2021, inabainisha kutokufuata taratibu za manunuzi pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa baadhi ya taasisi za Serikali.
Wakati ripoti hiyo iliyojumuisha ukaguzi wa taasisi 86 za umma zinazofanya manunuzi mbalimbali na mikataba 8,838 yenye thamani ya Shilingi trilioni 9.16 inaonesha kwamba kwa ujumla hali ya kufuata taratibu za manunuzi katika taasisi zilizokaguliwa ni nzuri kwa wastani asilimia 75 ya vigezo, ingawa hali katika halmashauri chache na taasisi nyingine za umma ni isiyoridhisha.
Ripoti hiyo ambayo inaangazia kipindi cha Julai 2020 mpaka June 30, 2021, kwa mfano, inafichua ubadhirifu wa kufa mtu kwenye taasisi kama vile Wizara ya Kilimo na Mifugo, Wakala ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
PPRA wanabainisha kwenye ripoti yao hiyo yenye jumla ya kurasa 222 kwamba hali ya kufuata taratibu za manunuzi katika halmashauri kadhaa nchini ni yenye kusuasua, hali inayopelekea upotevu wa kodi za wananchi, rushwa, na ubadhirifu. Halamashauri zilizofanya vibaya zaidi katika kufuata taratibu za manunuzi ni pamoja na Kondoa TC, Mbogwe DC, Chato DC, Tanzania Livestock Research Institute na Biharamulo DC.
Upigaji wa Milioni 618 Wizara ya Kilimo
Katika ukaguzi wa mikataba yenye thamani ya Shilingi 9,278,473,500 katika mwaka 2018/2019 na 2019/2020, PPRA ilibaini kwamba mikataba mitatu ya kemikali za kilimo yenye thamani ya Shilingi 246,165,500 zilipokelewa zikiwa tayari zimekwisha muda wa matumizi. Wizara pia ilibainika kutoa hati ya ukaguzi na hati za kupokea bidhaa wakati ambao hakukua na timu ya wakaguzi au wapokeaji wa mizigo hiyo ya pembejeo.
PPRA pia ilibaini udanganyifu wa Shilingi 232,110,000 juu ya pembejeo zilizotoka katika maghala kwenda sehemu mbalimbali, ambapo ilionekana kiwango kilichofika sio kiwango kilichotoka kwenye maghala ya wizara. Pia, bidhaa zenye thamani ya Shilingi 349,800,000 zilitoka kwenye maduka ya wizara lakini hazikufika zilipokusudiwa. Hapo hapo ilionekana pembejeo zenye thamani ya Shilingi 36,690,000 zilipotea. Pembejeo hizi zilikua zimeripotiwa kuwepo katika ghala la Bodi ya Pamba Tanzania.
Lakini si hayo tu, PPRA katika ukaguzi maalumu wa mikataba pia iliweza kugundua kwamba jumla ya Shilingi 25,000,000 zililipwa kwa mtaalamu wa miamba katika miradi ya umwagiliaji ya Kigugu na Msolwa bila ya kufanya kazi yoyote, wala kutoa viambatanisho vyovyote vya kufanya kazi. Hapo hapo ilioonekana kulikua na nyongeza ya malipo kwa wakandarasi wa miradi hiyo ya umwagiliaji kwa takribani Shilingi 25,588,810 huku kukiwa hamna kazi yoyote ya ziada iliyofanyika.
Katika miradi ya ujenzi wa maghala ya Kigugu, Mbogo, Msolwa na Njage nako makando kando kadhaa yalikutwa. Kwanza, ilibainika kwamba mkandarasi alikabidhi kazi huku kukiwa na nyufa katika kuta, na hii ni baada ya muda wa kukamilisha kazi kuongezwa mara kadhaa bila sababu za msingi au kufuata taratibu. Lakini hapo hapo ripoti inaonesha kulikua na malipo ya ziada ya Shilingi 37,887,816 katika kazi hiyo. Fedha zilizolipwa kama ‘advansi’ kwa mkandarasi V. J. Ministry Ltd, jumla ya Shilingi 27,814,783 hazikuhesabiwa katika mkataba.
PPRA imependekeza Afisa Masuhuli wa Wizara ya Kilimo na Ufugaji kuhakikisha kwamba Shilingi 621,600,000 zinarudishwa serikalini na maofisa waliohusika na udanganyifu huu wanachukuliwa hatua za kinidhamu. Pia wamewasilisha taarifa hizo kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kutokana na ukweli kwamba taarifa hizi zina viashiria vikubwa vya rushwa.
Waliopewa tenda RITA siyo waliopitishwa na bodi
Katika ukaguzi wao wa mikataba yenye thamani ya takribani Shilingi 4,325,407,708 huko RITA, PPRA iligundua kwamba katika tenda moja ya bidhaa za ofisini ilionekana waliopewa tenda sio waliopitishwa na bodi.
Iligundulika pia kwamba bodi ya tenda ya RITA iliipa kampuni ya Times General Supplies tenda ya takribani Shilingi 933,479,400, kazi ya uchapishaji, bila kufuata utaratibu rasmi wa manunuzi.
Bidhaa za thamani ya Shilingi 293,226,900 pia zililipwa bila kuwa na mikataba halali, huku taratibu lukuki za manunuzi zikionekana kutokufuatwa.
PPRA inapendekeza kwenye ripoti yake hiyo kusukwa upya kwa timu ya manunuzi ya RITA, huku Afisa Masuhuli na watendaji wengine wakitakiwa kupigwa msasa.
Kampuni ya afisa wa SUA yavuna tenda ya mamilioni
Wakati sheria ya manunuzi na kanuni za manunuzi zinakataza muingiliano wa kimaslahi kwa timu inayohusika katika kupitia na kutoa tenda, huko SUA mambo yalikuwa tofauti.
Uchunguzi wa PPRA unabainisha kwamba kampuni moja yenye jina la Jamu Stationery and General Supply ilipewa tenda zenye thamani ya Shilingi 14,437,267.
Ilikuja kugundulika kwamba kampuni hii ilikua ni ya familia ya mmoja wa afisa SUA. Uchunguzi wa PPRA unaonesha sehemu kubwa ya makabrasha kuhusu tenda hii yalipotea, hivyo hayakuweza kukaguliwa na hata aliyekuwa anapokea bidhaa mbalimbali kutoka katika kampuni hii hakuwa mtu aliyethibitishwa na Afisa Masuhuli.
Katika hali nyingine ya kushangaza katika manunuzi ya chuo, kampuni ya Vigilante Security ililipwa Shilingi. 6,490,000 kwa kazi ya ulinzi ambayo haijawahi kufanyika. PPRA imeagiza fedha hizi zirejeshwe.
Upigaji katika uzoaji takataka Ilala
Katika ukaguzi wake wa tenda saba za uzoaji taka zenye thamani ya Shilingi 1,419,401,695 katika halmashauri ya Ilala, PPRA ilibaini kwamba baadhi ya wakandarasi, ikiwemo kampuni ya Mungia Engineering Group Ltd, iliondolewa katika mchakato wa tenda kwa vigezo ambavyo havikuwepo huku kampuni ya Gin Investment Ltd na Tirima Enterprises Ltd zikipewa ushindi wa tenda bila kuwa na vigezo husika.
Baadhi ya kampuni zilionekana zikilegezewa masharti wakati wa upitiaji wa tenda, ikiwemo Juhudi Cleaning and Gardening na kampuni ya Green Waste Pro Ltd.
Katika hali ya kushangaza zaidi, mikataba yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1 ilipitiwa na mwanasheria wa halmashauri badala ya Mwanasheria Mkuu kama inavyotakiwa kiutaratibu.
Baadhi ya wakandarasi walionekana kukusanya hela bila kuwasilisha kama mikataba inavyotaka, mfano kampuni za Tirima Investment Ltd and Kajenjere Trading Co. Ltd hawakufikisha jumla ya Shilingi 208,494,480 walizozikusanya.
Lakini pia hakukua na uthibitisho kuwa Shilingi 212,880,384 zilifikiswa katika halmashauri baada ya kukusanywa na kampuni za Sateki Trading Ltd na Kajenjere Trading Co. Ltd.
Mikataba ya ukusanyaji uchafu ilionekana haina kipengele chochote cha kumuwajibisha au kumpa adhabu mkandarasi pale anaposhindwa kupeleka makusanyo kwa halmashauri kama inavyotakiwa.
Masuala mengine yaliyotajwa kwenye ripoti hii inaytegemewa kufikishwa bungeni na Wizara ya Fedha na Mipango katika vikao vijavyo vya Bunge ni pamoja na Kamanda wa Polisi Singida kununua vifaa vya ujenzi na huduma zenye thamani ya Shilingi 825,258,000 bila kupata ridhaa ya bodi ya manunuzi.
Mkuu wa Wilaya Itigi aliyelipa Shilingi 27,819,207.20 kwa bidhaa ambazo hazikuwahi kukabidhiwa pia ametajwa.
Pia mkataba wa ujenzi wa ukuta wa soko la Mchikichini uliotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam unaonekana kuwa na viashiria vingi vya rushwa. Milioni 33 iliongezwa katika kuweka nakshi ya ukuta bila kupata idhini ya Afisa Masuhuli na bodi ya tenda. Mkandarasi aliendelea kufanya kazi bila kibali chochote na alilipwa Oktoba 2, 2020. Kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuweka nakshi ya gharama nafuu katika ukuta wa soko hilo.