Zanzibar. Utata umeibuka visiwani hapa kati ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kwenye Bustani za Forodhani na mamlaka za eneo hilo mashuhuri ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar juu ya suala zima la upatikanaji wa vitambulisho maalum ambavyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo kama sehemu ya kuwasaidia kuimarisha mitaji yao.
Wakati wafanyabiashara katika eneo la Bustani za Forodhani wakisema kwamba na wao ni wajasiriamali wadogo na hivyo wanastahili kunufaika na mpango huo wa Serikali, mamlaka za Bustani za Forodhani zinasema hilo siyo kweli, kwani bustani hizo hazipo chini ya Serikali bali zinaendeshwa kwa michango ya wafanyabiashara wenyewe.
Mnamo Septemba 23, 2021, Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi alizindua vitambulisho maalum kwa ajili ya wajasiriamali wa Zanzibar, akisema kwamba utaratibu huo unalengo kurasimisha shughuli za wajasiriamali hao, kuwatambua kisheria na kukuza mitaji yao.
Dk Mwinyi alikuwa akitimiza moja kati ya ahadi alizozitoa kwa Wazanzibari wakati akiomba ridhaa ya kuongoza sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Tayari utaratibu wa kuwagawia wajasiriamali vitambulisho maalum ulikuwa umeanza kutekelezwa kwa wajasiriamali waishio Tanzania Bara baada ya utaratibu huo kuanzishwa na Rais wa awamu ya tano Hayati John Magufuli ambaye mnamo Disemba 10, 2018, alitoa vitambulisho maalum 670,000 kwa wakuu wa mikoa yote ya Tanzania Bara kwa ajili ya kuwagawia wajasiriamali katika mikoa yao.
‘Wanataka tusipate vitambulisho’
“Nishakwenda mara mbili [kuomba kupatiwa kitambulisho] na nikapiga mpaka picha ila mpaka sasa sijapata taarifa yoyote kuhusu kulipia,” Hamad Msabaha Ally, mmoja kati ya wafanyabiashara katika Bustani za Forodhani ameiambia The Chanzo. “Kuna taarifa kwamba viongozi wa mamlaka [ya Bustani za Forodhani] wanazuia tusipate hivi vitambulisho. Lakini kufanya hivyo ni kwenda kinyume na kauli ya Rais [Mwinyi].”
Ally ni mmoja kati ya wajasiriamali 106 waliosajiliwa kufanya shughuli za biashara katika Bustani za Forodhani, kwa mujibu wa ofisi ya bustani hizo. Wajasiriamali hawa hulipa kodi za viwango tofauti kwa mamlaka husika kulingana na biashara wanazouza.
Kwa mfano, wauzaji wa pizza na vyakula vya pwani wanalipia Sh121,500 kwa mwezi. Wafanyabishara wa miwa ni shilingi Sh60,500 kwa mwezi, wakati wauza urojo ni Sh40,500, wanaotoa huduma za vyoo hulipa Sh450,000 kwa mwezi, wenye vibanda hulipa Shiling milioni moja wakati wale wenye vigari vya ice cream hulipa Sh30,000 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao ndani ya Bustani za Forodhani Hamis Ali, suala la ulipaji wa kodi ni changamoto kwao, akisema kwamba kodi wanayopaswa kulipa anazodai haziendani na ukubwa wa biashara zao.
Kodi haiendani na uhalisia
“Tunalipa kodi ila kodi yetu haiendani na uhalisia wa biashara hapa maana kuna changamoto nyingi ambazo Mamlaka ya Bustani za Forodhani walitakiwa kuzimaliza,” anasema Ali wakati wa mahojiano na The Chanzo mnamo Septemba 28, 2021.
“Kwa hiyo, suala la kulipia kwa mwaka ni jambo nilisikia nami nikawahimiza wenzangu na tulikwenda kwenye mamlaka husika ila mpaka sasa hakuna majibu na kuna mvutano kwenye hili maana sisi tuko tayari ila wahusika hawako tayari,” ameongeza Ali.
Suleiman Hamad Said ni mfanyabiashara wa juisi ya miwa katika eneo la Bustani za Forodhani.
Hapa anaeleza alichokutana nacho alipofuatilia kitambulisho cha wajasiriamali wadogo: “Nilipofika pale Ofisi za Halmshauri, nikaambiwa kuwa nyinyi wafanyabiashara wa Forodhani mna kesi maalum maana mtatakiwa kulipa shilingi laki moja badala ya Sh30,000.
“Niliona afadhali maana kwa mimi kwa mwezi nalipa Sh60,500 ambayo kwa mwaka ni sawa na Sh700,000. Lakini changamoto iloyopo ni kwamba mpaka sasa nimeshapiga picha mara mbili ila sijapata ujumbe wa kulipia na nilipokwenda mara ya mwisho wanasema picha yangu imeharibika.”
Bustani itakufa
Kwa mujibu wa Meneja wa Bustani za Forodhani Amir Hamza Amir, makusanyo ya mapato ya Forodhani kwa makadirio ni Sh8,900,000 mwezi huku matumizi yakiwa ni sawa na Sh7,800,000 kwa mwezi na hio ni kutokana gharama za uendeshaji kama ulipaaji wa umeme,maji ,taka na mishahara ya wafanyakazi wa Bustani ya Forodhani.
Akijibu suala la ipi hatma ya wafanyabiashara wa Bustani za Forodhani kuhusiana na madai ya kupatiwa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo, Amir anasema: “Hizi kodi ni tofauti maana Bustani inajiendesha kutoka kwenye kodi za wafanyabishara na gharama za uendeshaji zinatoka kwao.
“Kulipia Sh100,000 kwa mwaka ni jambo gumu. Labda ikiwa Serikali itaichukua Bustani na kuwa chini yake. Vinginevyo Bustani itakufa tu [kama wafanyabiashara watapewa vitambulisho vya ujasiriamali].”
Kwa mujibu wa Afisa Vitambulisho wa Manispaa ya Mjini Magharib Ikrima Jumanne, manispaa hiyo imeshatoa vitambulisho 78 vya wajasiriamali tangu mchakato wa utoaji uanze.
“Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni uelewa kwa wananchi juu ya vitambulisho hivi,” Jumanne anasema. “Wengine wanakuwa na mitaji mikubwa zaidi ya Sh5,000,000 lakini wanataka vitambulisho. Wanaostahili kupata vitambulisho hivi ni wajasiriamali wenyewe mitaji midogo chini ya Sh1,000,000.”
Najjat Omar ni mwandishi wa habari za kijamii kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najjatomar@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala haya, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.