Dar es Salaam. Tatizo kubwa la ukosefu wa ajira, hamu ya kutaka kutajirika kwa urahisi na haraka pamoja na tabia ya baadhi ya Watanzania kukataa kazi kwa makusudi na kutafuta ufumbuzi wa haraka wa kutatua matatizo yao zimetajwa kuwa ni baadhi ya sababu zinazowasukuma watu wengi kuingia kwenye biashara ya upatu haramu ambayo mara nyingi huwaacha na machozi.
Kulingana na tovuti ya masualaya kifedha ya Investopedia, biashara ya upatu ni uwekezaji haramu wa kitapeli wenye mfumo wa madaraja ambao hulipa wanachama wa juu zaidi katika muundo huo na pesa hutoka kwa wanachama wapya.
Wakati Serikali pamoja na wadau wengine wakiwemo wabunge, viongozi wa dini na hata wasanii wa vichekesho wakiwataka wananchi kuwa makini na mipango hiyo ya kitapeli huku wakionesha madhara ya kifedha na kisaikolojia yanayohusiana na biashara hiyo, idadi ya mipango hiyo ya kitapeli sio tu imekuwa ikiongezeka nchini Tanzania lakini pia suala la waendeshaji wake kupata wateja limekuwa likifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Licha ya kuwa biashara ya upatu inaendeshwa kinyume na sheria za Tanzania, pamoja na uwepo kwa kesi kadhaa katika mahakama za taifa hili la Afrika Mashariki ambapo utapeli unaohusiana na biashara ya upatu umekuwa ukifichuliwa huku wamiliki wa kampuni hizo wakiamriwa kulipa mabilioni ya fedha kama fidia kwa wateja wao wa zamani waliokuwa wahanga wa upatu haramu waliokuwa wakiendesha, tazama hapa, hapa na hapa.
Ndoto za kupata utajiri kwa haraka
“Kushamiri kwa biashara haramu ya upatu nchini Tanzania kunahusiana sana na ndoto za kutajirika kwa haraka ambazo baadhi ya Watanzania wanazo,” Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Nicodemus Mkama aliiambia The Chanzo wakati wa mahojiano nae hivi karibuni. “Watu wanapaswa kuwa waangalifu zaidi na matangazo ambayo yanawashawishi kushiriki katika mpango wowote wa uwekezaji unaoahidi faida kubwa ndani ya muda mfupi sana. Huo ni utapeli.”
CMSA ni mamlaka ya kiserikali iliyochini ya Wizara ya Fedha na Mipango inayosimamia biashara ya masoko na mitaji nchini Tanzania. Inadhibiti na kusimamia madalali, inashauri masuala ya uwekezaji, usimamizi wa hazina, pamoja na ulinzi wa dhamana. CMSA wamekuwa wakali sana katika kuonya watu dhidi ya kujiunga na biashara haramu ya upatu.
Lakini baadhi ya watu waliowahi kujiunga na mipango hiyo na kuishia kutapeliwa waliliiambia The Chanzo wakati wa mahojiano nao kwamba, ndoto za kupata utajiri kwa haraka na uvivu kama alivyozungumzia Mkama sio sababu pekee zinazowasukuma watu kujiunga kwenye mipango hiyo ya kitapeli.
Kwa mujibu wa watu hao, Watanzania wengi wanalazimika kujiunga na mipango hiyo ya kitapeli kutokana na kukata tamaa ya kufanya shughuli ambazo zingewaingizia kipato na kuwawezesha kuishi katika mazingira yenye changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi. Kwa maneno mengine, kujiunga na mipango hiyo ni njia ya kuishi.
“Mimi binafsi nilisukumwa kujiunga na biashara ya upatu kwa sababu sikuona kazi nyingine yoyote ya kufanya karibu nami hapa,” Martha Mwilongo, mfanyabiashara na mkazi wa Sinza Afrikasana jijini Dar es Salaam ambaye hapo zamani alijihusisha na biashara ya upatu haramu, aliiambia The Chanzo. “Hakuna kazi hapa. Watu huchukulia [biashara ya upatu] kama njia ya kujipatia kipato.”
Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake aliyoitoa jijini Mwanza ambapo alikutana na kuzungumza na baadhi ya vijana wa hapa nchini mnamo Juni 15, 2021, alieleza kuwa asilimia 11.4 ya vijana wa Tanzania walio katika umri wa kufanya kazi hawana ajira, hali inayowasukuma vijana wengi kujiingiza katika shughuli hatarishi, na wakati mwingine za kihalifu.
“[Biashara ya upatu] ni mipango ya kitapeli,” aliongeza Bi Mwilongo kwa msisitizo. “Watu wengi ninaowajua waliojiunga na mipango hiyo ni watu ambao hawakuwa na chaguo jingine la kujipatia kipato, ikiwa ni pamoja na mimi mwenyewe.”
Hawana taarifa sahihi
Lakini pia kuna wenye matumaini kuwa mtu atatumia fedha anazozipata kupitia biashara ya upatu haramu kuwekeza kwenye miradi mingine ya biashara kama ilivyokuwa kwa Rachel Nzengo, mkazi wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambaye aliwahi kuwekeza kwenye moja ya mipango hiyo ya upatu haramu jijini Dar es Salaam.
“Nilidhani ningeweza kupata pesa na kuwekeza mahali pengine,” Nzengo anasema, kabla ya kuishia kuzipoteza pesa hizo. “Naweza kusema sikuwa na taarifa sahihi kuhusu suala zima lakini kutokana na uzoefu, sitaki tena kusikia chochote kuhusu biashara za upatu. Na kama ikiwa nina mawasiliano na mtu kwenye simu yangu ambaye anashiriki kusambaza mambo kama hayo mimi naifuta mara moja namba hiyo bila hata ya kumtahadharisha.”
Lakini kwa mujibu wa watu wanaofanya biashara hizi, hatari za watu kutapeliwa zinakuzwa sana. Mmoja wa watu hao ni David Asiimwe, msemaji wa kampuni ya Alliance in Motion Global ya jijini Dar es Salaam inayojishughulisha na uuzaji wa bidhaa mbalimbali.
Asiimwe anasema utapeli, ambayo ndio changamoto kubwa kwenye biashara ya upatu, si matokeo ya moja kwa moja na biashara yenyewe bali tabia ya mtu binafsi. Anaieleza The Chanzo wakati wa mahojiano maalum: “Baadhi ya biashara zinaharibiwa tu na watu. Kwa mfano, suala la kuwadanganya wanachama wa [kampuni ya masoko ya mtandaoni]. Sio kampuni inayodanganya. Bali ni watu wake.”
Upatu haramu unaweza pia kuiangusha Serikali
Hata hivyo, Nicodemus Mkama, Afisa Mtendaji Mkuu kutoka CMSA, anasisitiza kuwa biashara ya upatu ni ya udanganyifu. Akitaja jinsi Tanzania kama nchi inavyoathiriwa na vitendo hivyo, Mkama anasema kuwa biashara ya upatu huruhusu watu kuhamisha fedha zinazohitajika kuwekeza katika shughuli za uzalishaji kwenda kwenye miradi ambayo haina tija yoyote ya kiuchumi.
“Wanaweza pia kusababisha uasi dhidi ya Serikali kwani watu wengi waliotapeliwa watakatishwa tamaa na majibu kutoka kwa viongozi wao ili kukabiliana na kile wanachoweza kufikiria kama ni dhuluma,” Mkama anasema. “Hivi ndivyo ilivyotokea [nchi ya kusini mwa Ulaya] Albania.”
Mnamo mwaka 1997, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka nchini Albania. Wanahistoria wengi wanaeleza kwamba vita hiyo ilisababishwa na anguko la biashara ya upatu haramu mara tu baada ya Albania kuingia katika uchumi wa soko huria. Serikali ilipinduliwa na zaidi ya watu 2,000 waliuawa.
“Watu wanapaswa kufanya utafiti au kushauriana na wataalam kuhusu biashara fulani ili kujua uhalali wake kabla ya kuchukua uamuzi wa kuwekeza [kwenye biashara hiyo],” anashauri Mkama. “Tunapaswa pia kukuza utamaduni wa kufanya kazi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji kama kilimo na biashara ili kujipatia kipato halali.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni lukelo@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.