The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wanawake Wanaolea Watoto Peke Yao Waelezea Uzoefu Wao

Ingawaje kuna changamoto nyingi za kulea watoto peke yao bila wenza wao, ikiwemo hali ngumu za maisha pamoja na mtazamo hasi wa kijamii dhidi yao, kila mama amedhamiria kuwapatia watoto wake malezi yaliyobora. 

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Ingawaje mpaka sasa hakuna utafiti mahususi uliofanywa kutambua idadi halisi ya wazazi wanaolea watoto wao peke yao nchini Tanzania, kwa maana ya mama kulea mtoto bila baba au baba kulea mtoto bila mama, zipo taarifa zisizo rasmi kwamba hali hiyo imeendelea kukua kwa kasi kwa siku za hivi karibuni katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Na ingawaje wapo wababa wanaowalea watoto wao wenyewe bila mama zao, mjadala kwa kiasi kikubwa umejikita kwenye jinsi ya kike, huku msemo wa single mother ukiendelea kupata umaarufu miongoni mwa misemo inayotumiwa kila siku na Watanzania kwenye mawasiliano yao ya kila siku.

Kulingana na mazungumzo ambayo The Chanzo imefanya na wanawake wanaolea watoto peke yao, ilibainika kwamba kuna sababu kadhaa zinazoweza kumpelekea mzazi aishie kulea mtoto wake peke yake bila ya baba/mama wa mtoto huyo. Hizi ni pamoja na sababu za kiasili kama kifo na zile za kibinadamu kama kuachana na uamuzi binafsi.

Hata hivyo, mjadala wa kijamii kuhusiana na single mothers nchini mara nyingi umekuwa wenye mwelekeo hasi, huku wanawake wanaoamua kulea watoto wao wenyewe bila ya usaidizi wa baba watoto zao wakionekana kama wanakengeuka kutoka kwenye viwango vinavyokubalika katika jamii zao.

Lakini ni upi uzoefu wa wanawake wanaolea watoto wao peke yao? Zipi ni simulizi zao za matumaini, mahangaiko, mapambano, furaha na huzuni? Kutaka kufahamu hili, The Chanzo imezungumza na single mothers watatu kuweza kufahamu haya na mengineyo. Tumelazimika kutumia majina ya kutunga kukidhi matakwa ya akina mama hawa waliotaka utambulisho wao kufichwa.

Mercy Jakob, 28

Mimi ni mama wa watoto watatu, wa kwanza akiwa na umri wa miaka nane, wa pili miaka mitano na wa tatu akiwa na miezi mitatu. Kitendo cha mimi kulea watoto peke yangu kilitokana na ajali ya gari iliyotokea mwaka huu wa 2021 na kuchukua uhai wa mume wangu. Haikua rahisi kwangu kukubali kuwa sasa ninatakiwa kulea watoto wangu bila ya kuwa na usaidizi kutoka kwa mume wangu.

Changamoto ya kwanza ninayokabiliana nayo kama single mother ni kwamba unakuwa hujaikubali hali hii. Inakuwa inaumiza. Na maanisha upweke. Changamoto ya pili, unajua, unakuwa umeshazoea kulea watoto na mwenzako. Kwa hiyo, ghafla tu inatokea unalea peke yako. Kulea watoto wewe kama wewe peke yako kwa kweli inakuwa ni ngumu.

Pamoja na ndugu wa mume kunisaidia baadhi ya mahitaji madogo madogo kwa ajili ya kuwalea watoto wangu, bado imekuwa ngumu sana kwangu kuikubali hali yangu. Huwa inaumiza sana. Watoto kwanza wanakuwa wapweke. Wanaathirika kisaikolojia maana wameshazoea kuwa na baba lakini kwa sasa wanakuwa na mzazi mmoja. Inaweza kupelekea wakati mwingine hata mtoto kuwa wa mtaani na hata kukosa huduma za kijamii.

Ninachokifanya ni kujaribu kufanya kile kilichopo ndani ya uwezo wangu. Ninatenga muda kuwa na watoto wangu kwa kuwajenga kisaikolojia  ili waweze kuzoea hali ya kuwa wenyewe bila ya kuwa na baba. Kikubwa kingine ninachojaribu kufanya hivi sasa ni kuhakikisha kuwa najishughulisha na kazi mbalimbali ili kuwapatia watoto wangu mahitaji ambayo yatasaidia kutojisikia wapweke.

Ninajishughulisha zaidi na kupambana ili kuhakikisha wanangu wanapata mahitaji yao ya msingi. Maana siwezi kusema kwamba nategemea kukaa nyumbani tu bila ya kujishughulisha. Lazima nifanye hivyo ili kuhakikisha watoto wangu wanapata mahitaji yote kama vile baba yao alivyokuwepo.

Atujalia Godfrey, 30 

Mimi ni mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka miwili na miezi 11. Kilichosababisha mimi kuishia kulea mtoto wangu peke yangu ni kutokuelewana na mzazi mwenzangu. Katika suala la malezi na makuzi kwa mtoto wangu, changamoto kubwa ninayoipata ni katika suala la matumizi kwani wakati mwingine inakuwa shida kwangu kumuhudumia mtoto ipasavyo.

Kwa sababu tunaishi mbalimbali na mzazi mwenzangu, mimi ndiye namuangalia mtoto muda mwingi. Kwa hiyo, unakuta unapohitaji matumizi inakuwa changamoto kidogo kutokana na tumeshatengana huko nyuma. Kwa hiyo, inakuwa changamoto kwanza kuanza kumbembeleza mtu fedha ya mtoto na nini. Wakati mwingine anahisi kama unaisingizia labda mtoto anaumwa, anahitaji nguo, anajitaji chochote. Mtu anaweza akahisi kama unasingizia, kwamba si kweli. Hiyo ndo changamoto kubwa ninayokutana nayo.

Kitu kigumu kwangu kama single mother ni namna ya  kumueleza mtoto sababu ya mimi kutengana na baba yake. Kwa hiyo, huwezi kumpa mtoto majibu ya moja kwa moja. Unakuwa unaugulia tu moyoni lakini ni vitu ambavyo tunavipata.

Inawezekana ikawa ni kweli  mtoto anayelelewa na mzazi mmoja huweza kupata athari wakati mwingine, hasa katika makuzi ya mtoto. Mtoto anajifunza kwa kuona. Kwa mfano, mtoto anaweza labda kwenye nyumba za majirani watoto wana baba zao, watoto wanapelekwa shule na baba zao, wanatoka na baba zao, wanaenda kanisani na baba zao. Kwa hiyo, lazima ile mtoto inamuathiri kwamba mimi mbona baba yangu hayuko? Maswali yanakuwa mengi. Kwa hiyo, yaani  inamuathiri mtoto kisaikolojia moja kwa moja kwamba kwa nini mimi baba yangu haonekani?

Kwa hiyo, kikubwa mimi ninachokifanya kwa sasa ni kumpatia mtoto wangu upendo ili asijione mpweke kwa kulelewa na mzazi mmoja. Kwa sababu, katika umri huu mdogo ambao watoto wanapitia wanahitaji sana upendo wa wazazi wote wawili. Lakini kama mmoja hayupo haina maana kwamba mtoto asipendwe kabisa kabisa. Najaribu kumtimizia mahitaji yake yote kwa wakati. Nikipata pesa nahakikisha anapata mahitaji yake yote muhimu.

Janeth Bosco, 29 

Mimi nilitofautiana na mzazi mwezangu na nimekuwa na jukumu kubwa la kumuhudumia mtoto wangu wa kike mwenye umri wa miaka miwili na miezi miwili. Sababu ya kutofautiana ni kwamba nilipopata ujauzito kuna watu walimfuata na kumuambia kuwa mimba siyo yake, kwamba atalea mtoto ambaye sio wa kwake.

Basi akawa hana mawasiliano na mimi. Ukipiga simu hapokei. Ukituma ujumbe hajibu. Lakini mwisho wa siku kuja kukaa mwenyewe, kama unavyojua sisi binadamu, akaanza kuona mbona kama mtoto anafanana na yeye, mbona kama ni damu yangu, ndo kujirudi na kujirudi kule ndo kusema kwamba ni kwa sababu nimeona mtoto anafanana na yeye lakini sio kuishi pamoja.

Changamoto ninazopitia kwenye malezi ya mtoto wangu ni kwamba kuna wakati najikuta sina pesa ya kumuhudumia mtoto. Kwa hiyo, najikuta nikiwaza endapo angekuwa na mzazi mwenzangu ingekuwa rahisi kukabiliana na hizo changamoto. Ukishaamka wewe ndio baba, wewe ndio mama. Changamoto kama hizi lazima zikusumbue.

Jamii mara nyingi huamini kuwa mtoto akilelewa na mzazi mmoja kuna vitu huvikosa au hata tabia huwa ni tofauti lakini mimi siamini hilo. Mimi nikupe mfano ambao ni hai. Mimi mwenyewe ninavyozungumza nimelelewa na mama mpaka nakua. 

Baba yangu mimi nilikuwa nikimuona ni mtu ambaye kaja leo kesho hayupo. Kwa hiyo, asilimia kubwa ya maisha yangu nimeishi na mama yangu na haikuwahi kuniathiri mimi. Nadhani ni msimamo wa mama mwenyewe. Mama ukisamama na ukajua mimi ni mama mtoto wangu hana upande wa pili unaweza kumlea mtoto vizuri.

Mimi najitahidi kuhakikisha kwamba mtoto wangu anapata upendo alioukosa kutoka kwa baba yake. Kwanza, kuna kitu huwa namtengenezea mwanangu. Unajua, mzazi akishakuwa mmoja yaani kuna baadhi ya vitu watoto wengine wenye baba na mama wanavipata. Kwa hiyo, mtoto mwenye mzazi mmoja anakuwa hapati. 

Kitu ninachokifanya nampatia mwanangu vile vitu ambavyo hata wale wenye wazazi wote wawili wanavipata. Kwa hiyo, huwa najitahidi kuhakikisha hilo nalifanya. Kwa hiyo, kama kuna kitu kinahitajika, najitahidi kumfanya kuwa sawa na wale ambao wana wazazi wawili.

Wataalam wanasemaje?

Unaweza kuona mpaka sasa aina ya maisha ambayo single mothers wanayaishi na changamoto ambazo wanazipitia kama walezi wakuu wa watoto wao. Lakini upi unaweza ukawa ni mtazamo wa kitaalamu kuhusiana na malezi ya mzazi mmoja kwa mtoto au watoto?

Mathias Njimba ni Afisa Ustawi Afya katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo makao makuu ya nchi Dodoma. Wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika hivi karibuni ofisini kwake, Njimba alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na u-single mother na malezi kwa mtoto:

“Mtoto aliyechini ya umri wa miaka 10, ukuaji wake unategemea sana mazingira kutoka kwa watu wanaomzunguka. Nikisema watu wanaomzunguka namanisha jamii ya karibu, jamii ya karibu inaanza na wazazi, yaani baba na mama. Hiyo ndiyo jamii ya karibu. Kwa hiyo, baba na mama hawa wanachukua nafasi kubwa sana katika malezi ya mtoto. 

Baba na mama wanahitajika kufanya nini? Kwanza, wanahitajika kumsaidia huyu mtoto kukua kiakili, kimwili, na kihisia. Lakini vile vile, kukua kijamii. Vitu hivi ni muhimu vinavyohitajika katika malezi na makuzi ya mtoto chini ya umri wa miaka 10. Kwa hiyo, zipo athari zinazoweza kujitokeza hasa katika malezi ya mzazi mmoja.

Ushauri wangu ni kwamba mzazi mmoja aliyebaki kulea mtoto ni lazima achukue nafasi ya pili katika malezi na makuzi ya mtoto. Pia, ni muhimu kwamba mzazi wa kike ama wa kiume anayelea mtoto peke yake anapaswa kuwa karibu na mtoto pamoja na kuhakikisha yale malezi yote muhimu anayapata katika makuzi yake. 

Hilo litamsaidia mtoto kukua kimaadili. Nazungumza hasa suala la maadili kwa sababu changamoto kubwa ya malezi ya upande mmoja mara nyingi sana huwa inaambatana sana na masuala ya maadili kwamba mtoto anatakiwa aishi vipi katika jamii, alelewe vipi. Kwa hiyo, hivyo vitu huwa vinaleta changamoto sana.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jackline@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *