Dar es Salaam. Katibu wa Shura ya Maimamu nchini Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda ameikosoa sera ya utaifishaji iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akisema kwamba sera hiyo ndiyo iliyofungua milango ya ukosefu wa uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma kwani iliwaaminisha kwamba Serikali inaweza kumiliki vitu hata vile visivyokuwa vya kwake.
Sheikh Ponda aliyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake Ilala, Dar es Salaam mnamo Novemba 19, 2021. Sheikh Ponda, ambaye amekuwa sauti muhimu katika kuchochea mabadiliko ya kijamii na kisiasa nchini Tanzania, alitoa kauli hiyo katika muktadha wa matatizo ambayo Tanzania inakabiliana nayo miaka takriban sitini baada ya kupata uhuru wake, akitaja ukosefu wa uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma kama moja ya matatizo hayo.
“Sisi tulivyoanza [kujenga nchi] tulianza na utaratibu au sera ya utaifishaji,” alisema Sheikh Ponda kwenye mahojiano haya ya takriban saa moja. “Yaani tulichukua mali [kwa] kutaifisha viwanda, tukataifisha mashamba, ardhi, tukataifisha biashara za watu. Na utaifishaji maana yake ni kuchukua kitu bila idhini ya mtu mwenyewe, hii utaifishaji ni lugha tu.Sasa, kwa namna moja au namna nyingine, hii ni kama aina fulani ya unyang’anyi, ni kama kuchukua na ni kinyume na uadilifu.”
Yafuatayo ni sehemu ya mazungumzo kati ya The Chanzo na Sheikh Ponda ambapo, pamoja na mambo mengine, anaelezea tathmini yake ya hatua ambazo Tanzania kama nchi imepiga miaka sitini baada ya uhuru na changamoto ambazo yeye anaona bado zinahitaji utatuzi kutoka kwa wale waliokabidhiwa dhamana ya uongozi wa nchi. Endelea …
The Chanzo: Watu tofauti wanaweza kukuelezea tofauti, lakini wewe mwenyewe unajielezea vipi, Sheikh Ponda Issa Ponda ni nani?
Sheikh Issa Ponda: Mimi ni kiongozi wa kijamii, kiongozi wa dini ya Kiislamu ambaye nafanya shughuli hizi za kutumikia umma kwa muda mrefu zaidi, kwamba ni mtu ambaye nafahamika.
The Chanzo: Unaonekana, kutokana na harakati zako, ni mtu unayeichukia sana dhuluma na ambaye hana hofu kuliweka hilo hadharani. Ni katika hatua gani ya maisha yako ulianza kupata mwamko huu wa umuhimu wa kupinga dhuluma na kupigania haki?
Sheikh Issa Ponda: Nafikiri jambo zuri huwa linafahamika tu, jambo zuri linaonekana kwamba hili ni zuri na jambo ambalo sio zuri linafahamika kwamba jambo hili sio zuri. Kwa msingi huo, mimi nilikuwa napenda kuona mambo mazuri yanafanyika lakini pia nilikuwa sipendi yale mambo ambayo sio mazuri. Kwa hiyo, huo ni utamaduni ambao nilikuwa nao tokea huko awali na ndio ambao nimekua nao mpaka sasa.
The Chanzo: Je, kuna sababu zozote zilizokufanya uwe mtu unayepinga sana dhuluma na kupigania haki pasipo kuwa na hofu?
Sheikh Issa Ponda: Kwa sababu kama nilivyosema kwamba sisi tunafikiria kwamba binadamu ni mtu ambaye anatakiwa aishi katika maisha yale ambayo ni aliyomkadiria Mwenyezi Mungu ambayo ni maisha mazuri, maisha ya furaha.
Sasa kinyume chake ikiwa kuna kikwazo ni jambo ambalo inatakiwa ifanyike jitihada ili kuondoa kile kikwazo. Kwa hiyo, ni kwa msingi huo maana yake ndio ambao ulionisukuma mpaka nikawa niko katika mazingira kama haya.
The Chanzo: Kuishi maisha ya kupinga dhuluma na kupigania haki si kitu rahisi. Ni gharama gani wewe binafsi umelazimika kulipa katika maisha yako ili uweze kuishi maisha ya aina hiyo?
Sheikh Issa Ponda: Katika kufanya kazi yoyote ile, iwe ni kazi ya biashara, iwe ni kazi ya kilimo, matarajio ni kwamba ile kazi iweze kuwa na matokeo mazuri. Lakini vyovyote itakavyokuwa, huwa kuna matatizo yanatokea, yaani kazi yoyote ile inakuwa ina matatizo. Kwa hiyo, matatizo yametokea kwenye vipindi vingi tu ambavyo tumekuwa tunafanya shughuli hizi na sisi tunachukulia kwamba ni sehemu ya utaratibu wenyewe kwa sababu huwezi ukafanikiwa bila ya kutokea kwa matatizo kwenye jambo lolote lile.
The Chanzo: Unaonekana kutokuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, hususani Jeshi la Polisi, unalitazama vipi suala hili katika harakati zako za kupinga dhuluma na kupigania haki?
Sheikh Issa Ponda: Nadhani hicho ulichokizungumza sio sahihi. Kwa sababu, kwa ujumla ni kwamba mamlaka iliyopo serikalini ni mamlaka ambazo tumeziweka sisi wenyewe wananchi na tunapaswa kuziheshimu. Yaani, kutenda vile ambavyo inatakiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa hiyo, hatuna mahusiano mabaya na vyombo hivi vya dola isipokuwa wakati fulani huwa kunaweza kuwa na tofauti ya mitazamo katika jambo. Inawezekana pengine nyinyi mkaona kwamba kufanya hivi ndivyo ambavyo sawasawa lakini pengine chombo cha dola kikaona kwamba hivi sio sawasawa.
Lakini hatimaye, kwa sababu kuna utaratibu, kuna mfumo wa sheria, huwa matokeo yake ni kwamba mnakwenda utaratibu ule wa kisheria na pale jambo huwa linafika linafahamika kwamba katika jambo hili sawasawa ni hivi, inawezekana hiyo sawasawa ni hivi ikawa pengine ni kwa chombo cha dola au sawasawa ni hivi ikawa ni kwa upande wako kama mtu.
Kwa hiyo, niseme kwamba sio kwamba kwa namna kama hiyo kutofautiana fikra kwamba ndio mnakuwa labda pengine mnauhusiano mbaya, sio uhusiano mbaya.
The Chanzo: Unaamini kwamba kuna wakati vyombo vya ulinzi na usalama huwa vinakuwa na hofu dhidi yako, kwamba kutokana na harakati zako za kupinga dhuluma na kupigania haki wewe ni mtu ambaye unastahiki kudhibitiwa?
Sheikh Issa Ponda: Kama nilivyosema, kwa maana kwamba kuna wakati mnaweza kuwa mnafanya jambo lakini pengine ikawa kwa chombo cha dola wakaona sio sawasawa. Sasa, ile haiitwi kwamba ni wasiwasi. Inaonekana kwamba ni wao katika kufanya zile kazi zinavyotakiwa kwamba pengine wameona jambo hili sio sawasawa. Wao wakaamua labda pengine kulifuatilia katika utaratibu ambao ni wa kisheria. Kwa hiyo, niseme hivyo maana yake.
The Chanzo: Tunafahamu kwamba wewe ni moja kati ya watu waliokuwa mstari wa mbele kupiga kampeni kwamba Masheikh wa Uamsho waachiwe huru, kitu ambacho Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilikifanya. Unaitathimini vipi Serikali ya awamu ya sita linapokuja suala zima la haki na utokomezwaji wa dhuluma kwa wananchi?
Sheikh Issa Ponda: Zile kesi zilikuwepo toka mda mrefu, toka mwaka 2013 mpaka leo, na tokea wakati huo tumekuwa tukifuatilia kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria. Kwa maana wale watu waliokuwepo gerezani tumewapa huduma za kisheria kwa maana ya kuweka wanasheria na mawakili wanaokwenda mahakamani kwenda kutetea zile kesi.
Sasa matokeo haya yaliyotokea juzi sisi tumechukulia kwamba ndio kilele, maana yake kilele cha kule tulikoanza yaani kumekuwa na mivutano ya kisheria na nin lakini mwisho jambo limefika mwisho.
Kwa hiyo, sisi tunatazama kama hili jambo wakati huu ndio limefika mwisho lakini katika mtiririko ambao tulianza nao tokea kule mwanzoni wakuja nao mpaka leo. Kwa ujumla, tunaangalia kama ni jambo ambalo limeamuliwa kwa mujibu wa zile taratibu ambazo zilizopo ambazo sisi tulianza kuzifuatilia tokea mwanzoni za kisheria.
The Chanzo: Unadhani baada ya Serikali ya awamu ya sita kuachiwa kwa wale Masheikh, je ni mwanzo mzuri wa kupinga dhuluma na wananchi kupata haki zao itakuwa ni mwendelezo?
Sheikh Issa Ponda: Kwenye suala la wale Masheikh sio kwamba walikuwa ni wao tu, kuna kesi ambazo zinawahusu Waislamu kwa ujumla na ni nyingi na ziko maeneo tofauti tofauti [ya nchi]. Ile kesi ya Masheikh ni kesi moja katika kesi nyingi zilizokuwa zipo hapa.
Kwa hiyo, hilo suala la kwamba ni mwanzo au mwisho wa dhuluma hatulizungumzii hivyo. Kwanza, sisi hatuzungumzii suala la dhuluma. Sisi tunazungumzia suala la kutendewa haki kwa mujibu wa sheria.
Sisi tunatazama kama vile kuna ukiukwaji wa haki katika suala hili kwa sababu mtazamo ni kwamba tulikuwa tunaamini kwamba watu wakishatuhumiwa wakipelekwa mahakamani basi shauri lizungumzwe lifike mahali mwisho.
Lakini kilichotokea ni kwamba watu wametuhumiwa halafu mashauri hayazungumzwi. Hilo ndio tunaliangalia kama ni kinyume maana yake na utaratibu ule ambao tunaona kama wa kisheria. Kwa hiyo, hilo suala la kwamba labda pengine ndio mwisho wa dhuluma au mwanzo wa dhuluma hatuwezi tukalizungumza kwa sababu kwanza hatuzungumzii dhuluma sisi tunazungumzia suala la hili jambo tayari lipo kwenye mkondo wa sheria.
Kwa hiyo, sheria itendeke katika jambo kama hili na tunaona kwamba hii ni sehemu ndogo maana yake kesi iliyotolewa ni kesi moja kati ya kesi chungu nzima zilizokuwepo pale. Kwa hiyo, matarajio yetu sisi ni kuona haki inaendelea kutendeka kwa maana ya mashauri mengine pia yasikilizwe ili yafike mwisho.
Kwa sababu, hata hilo suala la Masheikh ni kwamba lilikuwa limesikilizwa na ndio kitu tulichokuwa tunalalamikia sisi kwamba haya mashauri yaende mahakamani na yasikilizwe na suala la Masheikh lilianza kusikilizwa na ikawa hukumu zimetolewa kwenye baadhi ya mashauri mwishoni hapa ndio Serikali ikaamua kuliondoa.
Kwa hiyo, tulikuwa tunachosukuma sisi ni kwamba haya mashauri mengine pia yasikilizwe kwa sababu ni mashauri ambayo tayari yamechukua muda mrefu, ni zaidi ya miaka minane maana yake.
The Chanzo: Ukiangalia jinsi unavyoishi kwa sasa, ukijaribu kuyaangalia maisha unayoishi kwa sasa, unadhani hayo ndio maisha ambayo nafsi yako inakutuma uyaishi, au ni maisha tofauti?
Sheikh Issa Ponda: Mimi unajua maisha yanahusisha mambo mengi sana kwa ujumla. Hilo ni jambo moja tu. Kwa sababu, suala la kupigania haki maana yake ni kwamba wewe mwenyewe unakuwa unaitekeleza ile haki, yaani unawatendea watu haki na pale ambapo unahisi kwamba kuna mtu ambaye unahitaji kumsaidia basi mnauwezo wa kumsaidia unamsaidia.
Sasa hayo ni maisha ambayo mimi siwezi kuepukana nayo, ni maisha ambayo mimi nategemea kubakia nayo hivo hivo kwamba mimi mwenyewe kwanza kutenda haki, kuwatendea watu haki lakini kumsaidia yule mtu ambaye anatakiwa asaidiwe.
The Chanzo: Mnamo Disemba mwaka huu wa 2021, Tanganyika itaadhimisha miaka 60 ya uhuru tangu Mwingereza aondoke. Unadhani ni kwa kiwango gani Watanzania wako huru leo kuweza kujiamulia mambo yao wenyewe miaka 60 tangu tuondokane na ukoloni?
Sheikh Issa Ponda: Miaka sitini nafikiri ni miaka sitini ya uhuru kwa maana kwamba Tanzania ni taifa ambalo lipo huru kwa miaka sitini. Kwa kifupi, matarajio ni kwamba litakuwa taifa ambalo limepata maendeleo makubwa katika muda wa miaka sitini kwa sababu miaka sitini ya kujitawala wenyewe ni miaka mingi sana. Kwa hiyo, matarajio makubwa ni kwamba tuwe tumepata maendeleo makubwa.
The Chanzo: Unatathimini vipi suala la matarajio ya kuwa na maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka sitini ya kujitawala wenyewe?
Sheikh Issa Ponda: Nafikiri hilo tunaweza tukaliona katika mjadala wa kile ambacho unakusudia tukizungumze ndio tutakapoona.
The Chanzo: Sawa.
Sheikh Issa Ponda: Nadhani nimekuelewa swali lako kwamba hali ya kijamii ikoje kwenye miaka sitini baada ya uhuru?
The Chanzo: Ndio.
Sheikh Issa Ponda: Matarajio makubwa ya, kwanza, nitumie fursa hii kuwakumbuka wale waliotuongoza katika mapambano ya kupigania uhuru kina Machifu Songea. Hawa ni watu ambao wamepigania uhuru wa Tanganyika kwa vita, hasa tunaposikia vita vya Maji Maji. Vile vilikuwa ni vita vya kupigania uhuru. Lakini kina Mkwawa wote hawa na watu ambao walikuwa katika harakati za kupigania ukombozi wa Tanganyika. Lakini kwenye miaka hii ya 1920 kilikuja kizazi kingine, hiki ambacho ndio kipindi kimeanzishwa chama kile cha African Association, hicho kimewahusisha kina Kleist Sykes, kina Mufti Hassan Bin Amir, kina Sheikh [Suleiman] Takdir lakini tulipokwenda kwenye mabadiliko kidogo ya kisiasa ikatoka kwenye African Association ikawa Tanganyika African Association ndio kipindi ambacho pia wamehusika kina Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wengineo waliokuja mpaka tukaingia kwenye TANU na hatimaye tukapata uhuru.
Kwa hiyo, niitumie fursa hii kwamba kwa maana ya kuwapongeza hao watu. Ni watu ambao wametoa mchango mkubwa katika suala zima la uhuru. Tukija katika swali lako kwenye hali ya jamii yetu, yaani tulivyo baada ya kupata uhuru, leo tunakwenda kwenye miaka sitini, matarajio makubwa ya watu katika kupata uhuru kijamii maana yake ilikuwa ni kuhakikisha kwamba ile misingi yetu ya kizalendo inalindwa lakini vilevile tunapata maendeleo au tunaendeleza misingi yetu ambayo ni ya kizalendo.
Kwa kawaida, jamii yoyote ile huwa inakuwa na mambo makubwa, mambo ya msingi sana, ambayo yale mambo ndio yanayofanya jamii iweze kuwepo. Sasa moja katika mambo ambayo ni ya msingi sana katika jamii yetu sisi Watanzania ni suala zima la maadili au utamaduni. Kwa hiyo, katika zile harakati za kupigania uhuru ilikuwa ni kuhakikisha kwamba yale maadili yetu, utamaduni wetu unakuwa salama, tunaulinda ule utamaduni wetu. Lakini pia tunaendeleza maadili yetu.
Ilikuwa ni katika vitu ambavyo vilikuwa vinaangaliwa katika mambo ya msingi sana katika kuifanya ile jamii yetu ya Kitanzania iweze kuwepo na iweze kubakia kama vile ilivyo katika kipindi cha uhuru na iwe imepata maendeleo makubwa sana. Sasa, katika suala hili la maadili, yapo mambo ya kuzingatiwa, miongoni mwa mambo ya kuzingatiwa ni pamoja na ile utu, yaani ule ubinadamu. Sisi huko tulipokuwa huko nyuma tulikuwa tunaishi maisha ya kibinadamu, maisha yale ya kushirikiana, maisha ya kusaidiana, maisha ya kupendana, maisha ya kufanya kazi pamoja, maisha ya heshima, adabu na kuwajibika ipasavyo. Haya ni mambo ambayo tulikuwa nayo kabla ya uhuru.
Kwa hiyo, haya mambo tulikuwa tulitarajia kwamba katika kipindi cha uhuru haya mambo yalindwe, yawepo. Lakini vilevile yaweze kuendelezwa. Hii ndio jamii ambayo tulikuwa tunatarajia kwamba baada ya uhuru tuione iko hivyo. Sasa, tukiangalia tathimini haituoneshi kama tumefanikiwa kulinda yale maadili yetu au utamaduni wetu.
Maana yake, kama tulivyosema kwamba miongoni mwa utamaduni wetu ilikuwa ni ule utu na kupendana [na] kuheshimiana. Ukiangalia hilo jambo [kwa sasa] hulioni. Sasa hivi ukiangalia katika jamii ya Kitanzania mauaji makubwa yanaendelea. Tanzania sasa hivi maiti zinaokotwa kama tulivyoona. Watu wanauwawa, wanatupwa kwenye viroba, wanatupwa baharini, wanatupwa mtoni. Watu wanatekwa na madhara makubwa sana yanatokea.
Na hawa watu ambao mauaji haya yanaendelea Tanzania sio kwamba ni watu labda wametoka Kenya halafu ndio wakaja kufanya mauaji hapa Tanzania, isipokuwa ni mauaji ambayo yanatokea ndani ya nchi, ambayo bila shaka ni Watanzania na wale wanaouwawa pia wanakuwa ni Watanzania. Sasa, hii ya tafsiri ya au ile hali ambayo tulikuwa nayo kabla ya uhuru ya kuishi maisha ya kindugu na kupendana huoni katika hali ambayo tuliyonayo sasa hivi.
Lakini vilevile, suala la maadili, suala la maadili nalo ni jambo ambalo limeporomoka sana. Hakuna kabisa [maadili]. Ukienda kwenye jamii sasa hivi kwenye kila Kata utakuta kuna magodauni ya pombe na kila baada ya nyumba tatu kuna grocery ulevi maana yake, watu wamekuwa ni walevi kweli kweli maana yake. Lakini utamaduni ule wa mavazi. Watu sasa hivi wanatembea uchi kabisa vijana. Utakuta mwanamke anaweza kuvaa soksi tu, vazi la soksi lakini akatembea na akaenda mpaka kazini vilevile.
Lakini maadili yamekuwa ni ugonjwa sasa, yaani kuporomoka kwa maadili umekuwa ni ugonjwa ambao umefika mahala umeingia kwa viongozi sasa hata viongozi ambao wako serikalini ni watu ambao wameporomoka sana kimaadili. Watu wanafanya ufisadi katika nafasi walizonazo. Lakini, hata majukumu wanayatumia vibaya kwenye kuajiri. Unaweza ukakuta viongozi wanadai rushwa wakati mwingine wanadai mpaka rushwa ya ngono kwenye nafasi zile za uongozi wa juu. Kwa hiyo, mporomoko wa maadili umekuwa ni mkubwa na ni ugonjwa ambao sasa unamuathiri kila Mtanzania katika kiwango kile ambacho ni cha juu sana.
Lakini vilevile, katika suala lile la uadilifu ambalo ni katika mambo ya msingi tuliyokuwa nayo sisi Watanzania kabla kipindi cha ukoloni, umeporomoka sana uadilifu na hii imetokana na jinsi ambavyo tulivyoanza. Kwa sababu, sisi tulivyoanza tulianza na utaratibu au sera ya utaifishaji, yaani tulichukua mali kutaifisha viwanda, tukataifisha mashamba, ardhi, tukataifisha biashara za watu na utaifishaji maana yake ni kuchukua kitu bila idhini ya mtu mwenyewe, hii utaifishaji ni lugha tu.
Leo hii unapoona hapa Dar es Salaam kule mjini kule ile city center zile nyumba zinaonekana ni mali za Serikali, zile nyumba zina wenyewe, zimejengwa na wenyewe na wamezijenga kihalali na walikuwa wanazimiliki kihalali vilevile. Lakini kuna mashamba huko, mashamba ya mkonge yalikuwa yana wenyewe ambayo sasa hivi yamekaa kama ni mali ya Serikali. Kuna viwanda, vile vilikuwa vinawenyewe. Kwa hiyo, tumetaifisha tumevichukua na wale watu tulipochukua zile mali zao hawakupelekwa mahakamani kwa maana kwamba labda pengine ifahamike kwamba walikuwa hawazimiliki zile mali kihalali ni kwamba zimechukuliwa tu hivyo hivyo.
Sasa, kwa namna moja au namna nyingine, hii ni kama aina fulani ya unyang’anyi, ni kama kuchukua na ni kinyume na uadilifu. Hili jambo, kwa hiyo, ina maana kwamba tulifika mahali tunawafundisha watu kuweza kumiliki vitu ambayo hawakutolea jasho, si vyao maana yake na tunawafundisha watu kwamba inawezekana tukawa tuna mfumo wa uchumi wa namna kama hiyo. Hii ni katika namna ambayo tumefanya na yametuondoa katika ile hali ambayo tulikuwa nayo sisi kabla ya uhuru.
Kwa hiyo, kiujumla ni kwamba ukiangalia katika jamii yaani unaiona jamii hatukupiga hatua kwenye maendeleo, hatukuweza kulinda yale maadili yetu tuliyokuwa nayo kabla ya uhuru wala hatukuweza kuyaendeleza ambayo yalikuwa ni maadili mema yaani maadili ya utu, kupendana na heshima, kuthaminiana [na] uadilifu. Hayo hatukuweza kudumisha hiyo hali ndani ya uhuru. Kwa hiyo, miaka sitini sasa hivi unaona kuna matukio makubwa ambayo huko nyuma hayakufanyika, ukirejea huko nyuma tulivyokuwa tunaishi wakati wa ukoloni huwezi kupata mahali kwamba Watanzania walikuwa wanauana kwa kiwango ambacho tunaweza tukaokota maiti barabarani, labda pengine walikuwa wanaweza kuchukua mali za watu bila idhini ya wenyewe, wanaweza wakafika mahali ikawa hakuna heshima kwenye jamii, hakuna adabu tunaweza kuwa ni mahali ambapo tunashabikia ulevi, mambo ya kipuuzi kabisa.
Sasa hivi kila nyumba ukitembea baada ya nyumba tatu unakuta kuna grocery ya pombe watu wanaelewa, watu wamekuwa hovyo, watu wanatembea uchi, yaani jamii sio ile ya kiutu maana yake, ambayo ukiiangalia baada ya miaka sitini ya uhuru. Kwa hiyo, naweza kusema kwamba jamii yetu sio nzuri baada ya miaka hamsini tunakwenda miaka sitini ya uhuru.
The Chanzo: Tumeshaona kuna hayo maporomoko ya maadili, uadilifu na mambo mengine katika jamii zetu. Je, ni nini haswa sababu ya hayo maporomoko tunayoyashuhudia?
Sheikh Issa Ponda: Unajua miongoni mwa mambo ambayo kwanza tunakuwa na Serikali, Serikali huwa kazi yake ni kulinda mambo ya msingi katika jamii na kulinda kazi mbalimbali, miongoni mwa kazi ambazo zinafanywa na viongozi wa dini ni pamoja na kuwapigania watu, kuwafundisha watu umuhimu wa kuishi maisha yaliyokuwa mazuri maisha ya maadili.
Watu wanakuja katika majumba yetu ya ibada na tunawafundisha, miongoni mwa hao ni wale ambao wanakwenda kuingia serikalini na kuwa wafanyakazi serikalini. Lakini Serikali inawajibu wa kulinda hayo maadili. Kwa mfano, nichukulie suala dogo tu ambalo lilikuwa ni mfano bora. Mimi nimeshuhudia wakati wa awamu ya kwanza tulivyoanza anza kidogo tulikuwa kidogo tunazingatia yale mambo ya msingi. Nimeshuhudia wakati wa Serikali ya Mwalimu Nyerere askari mgambo wakipita barabarani wanakwenda wanakagua mavazi, wanakagua vitu mbalimbali lakini pia kwenye mamlaka tumefika mahali tukaunda vyombo vya ukaguzi, kuna vyombo ambavyo kwenye mambo ya habari kuna vyombo vya kupitia kuangalia filamu na vitu vingine vingi.
Lakini, hivi vyombo kwa bahati mbaya ni kwamba sasa hivi havifanyi kazi kwa maana hiyo ni kwamba ikiwa Serikali imeshindwa kusimamia haya mambo ni vigumu sana kwa viongozi wa dini kuyazuia. Viongozi wa dini watakuwa wanazungumza, wanazungumza lakini kama hakuna nguvu inayosimamia yale ambayo yanazungumzwa na viongozi wa dini vyovyote itakavyokuwa ile kazi ya viongozi wa dini itakuwa haina maana. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba sisi viongozi wa dini tunafanya ile kazi lakini tutakosa misaada ya muhimu sana ambayo ingeweza kusaidia kuyafanya yale mambo yaweze kuendelea. Na mfano mzuri nakupa kuwa ni huo tumepata kuona huko nyuma Serikali ikipita inakagua vitu vya msingi sana kama hivi vya kuzingatia maadili na kadhalika.
The Chanzo: Msaada muhimu ambao unauzungumzia hapa ni kutoka serikalini
Sheikh Issa Ponda: Ndio
The Chanzo: Hapo nyuma umenieleza kwamba viongozi wa Serikali ni moja kati ya watu ambao ninyi kama viongozi wa dini mnawafundisha, je, katika mafundisho yenu, hamuwafundishi na kuwaambia suala la kwamba wao ni watu ambao hawawapi huo msaada mnaouhitaji ili kutimiza malengo yenu?
Sheikh Issa Ponda: Sasa hiyo, kwa sababu unajua kuna taarifa, kuna maelezo, yale maelezo ambayo sisi tunawaeleza yanasikika sababu sisi tunahubiri kwenye vyombo vya wazi na wakiwepo kwenye nyumba zetu za ibada wanahubiriwa na wanasikia. Lakini sasa yale ambayo tunasema sisi kuna vyombo vya maamuzi ambavyo vile vyombo vya maamuzi vinasikia, vile vyombo vya maamuzi ndivyo ambavyo vilitakiwa sasa viyafanyie kazi yale katika kuyafanyia kazi wanakuwa hawaangalii kwamba huyu ni kiongozi au sio kiongozi wenyewe wanaangalia nani ambaye anakwenda kinyume na yale maadili wanayafanyia kazi. Kwa hiyo, viko vile vyombo vya maamuzi haviyafanyii kazi
Kwenye suala la kiuchumi [baada ya miaka sitini ya uhuru] niseme kwamba tunapozungumzia uchumi, yaani uchumi mzuri tafsiri yake kubwa huwa ni kufika mahali tukaona maisha mazuri kwa kila mwananchi. Na hiki ndio kipimo kizuri cha uchumi, kwamba uchumi wetu umekuwa au uko chini ni kuangalia ile hali ya maisha ya watu, upatikanaji wao wa rizki, huduma mbalimbali za kiafya, huduma za maji, huduma za umeme na mambo mengine yale muhimu, yale ndio kipimo.
Ukiacha mbali zile takwimu ambazo mara nyingi huwa zinatolewa na viongozi wa Serikali, labda uchumi umekuwa kwa asilimia fulani, yale ni mambo ya kiufundi, ya kiofisi, lakini kipimo ambacho kinaleta makundi yote kwa pamoja wakaweza kuona kwamba uchumi umekua au haukukua ni kuangalia ile hali ya maisha ya watu jinsi ilivyo. Sasa, huko mwanzoni tupokuwa tunapigania uhuru, tulipoingia kwenye uhuru, tulisema kwamba uchumi wetu unalenga kukabiliana na mambo matatu, yaani kukabiliana na kuondoa umaskini, kukabiliana na ujinga na kukabiliana na tatizo la maradhi. Haya ndio mambo matatu ambayo tulisema kwamba tunajenga uchumi ambao utakabiliana na hayo mambo matatu.
Sasa, tunaweza tukayaangalia mambo haya matatu. Ukiangalia mambo haya matatu kwa kweli hali ya maisha ya wananchi, maana yake ni duni sana, umaskini upo kwa kiwango cha juu sana hakuna mtu ambaye Tanzania sasa hivi unaweza kusema kwamba huyu anapata chakula cha kutosha, yaani anaweza kula milo mitatu. Waliopo ni wachache sana. Hali ya maisha ukiangalia ni duni sana. [Bei za] bidhaa zipo juu sana. Bidhaa za vyakula kwa kiwango ambacho watu hawamudu, kiasi ambacho mtu sana sana pengine anapata mlo wa siku moja.
Lakini huduma za afya zipo ghali na chache sana kiasi kwamba mtu wa kawaida, kwa sababu ya ule umaskini wake, hamudu. Sasa hivi mzazi tu akitaka kijifungua ni lazima awe na kati ya Sh500,000 mpaka Sh1,000,000 ndio anaweza kupata zile huduma za afya kule hospitali. Hali ya umaskini jinsi ilivyo tafsiri yake ni kwamba watu wanalazimika kupata huduma za kijifungua kwa kinamama kwa kienyeji kwa sababu hawamudu yale mazingira ya hospitali. Lakini, ukiangalia kwenye huduma za maji, huduma za maji ni duni sana na kwa asilimia karibuni kubwa ya watu wa Tanzania wanakunywa maji ya tope, maji yaliyochanganyika na tope na wataalamu wanatwambia kwamba karibuni asilimia kubwa ya magonjwa yanatokana na maji machafu.
Kwa hiyo, maradhi ni makubwa yanatokana na huduma za maji kukosekana maradhi pia yanazidi kuongezeka. Kwa hiyo, ukiangalia huduma zile ambazo tulizosema kwamba tutakabiliana nazo uchumi utakabiliana nazo ni kipimo kizuri licha ya kwamba zipo chini sana.
Elimu yetu pia, kama unavyoiona, si watu wote wanaweza kusoma na pia haipo katika kiwango ambacho ni kizuri zaidi. Lakini umaskini ndio hivyo tunaona upo duni sana lakini tukiangalia vilevile sera zetu katika masuala kama vile ya kilimo [na] biashara sio sera zile ambazo zinaweza kumsaidia mwananchi kuondokana na ule umaskini au kuingia kwenye utajiri. Tulianza na sera ambazo huko nyuma tunaangalia, kwa mfano, mkulima anafanya juhudi mwenyewe anakata msitu, anaweka mmea, anamwagilizia mmea, anapulizia dawa, anavuna lakini akishavuna Serikali inakwenda pale inamwambia kuanzia sasa hivi hizi bidhaa zako sisi ndio tutakao panga bei na ndio tutakao kutafutia soko na tutauza halafu baadae tutakupatia fedha wewe.
Hiyo hali tumekwenda nayo kwa muda mrefu na matokeo yake ni kwamba katika utaratibu huo matokeo yake mtu anakuwa maskini pamoja na kwamba amelima na amepata mavuno mazuri lakini mwisho wa yote anakuja kuwa maskini, na kilichomsababishia umaskini sio kwamba hakupata mavuno, mavuno alipata lakini kilichomsababishia umaskini ni pale ambapo Serikali imejitokeza kwenda pale katika ile kazi ambavyo ameifanya. Kwa hiyo, unaangalia sera yetu katika kilimo ni sera ambayo imesaidia sana kuleta umaskini na hii nafikiri imeonekana hata hivi karibuni kama unakumbuka nafikiri miaka miwili mitatu iliyopita imetokea kule Mtwara.
Watu wamelima korosho vizuri lakini matokeo yake korosho zikachukuliwa na zikawa mikononi mwa vyombo vya Serikali. Kwa hiyo, zile sera sio rafiki katika kumfanya mtu aweze kuondokana na umaskini. Lakini, tumeona hata katika biashara katikati hapa tumeona kuna wafanyabiashara wenye maduka ya fedha Serikali imechukua fedha zao na wamekuwa hali zao ni maskini mpaka leo hii. Lakini hata kwenye mambo ya kodi, watu wamekuwa wanatozwa kodi kubwa na karibuni mara tatu. Mtu anatozwa kodi halafu baadae anambiwa kwamba makadirio hayakufanyika sahihi, kwa hiyo kabla ya kukupa mzigo wako lazima ulipe kodi tena matokeo yake tunafilisika katika hiyo hali.
Yaani, umaskini ambao umejitokeza sana katika awamu ya tano umetokana na zile sera zetu katika mambo ya biashara na mambo ya kilimo vilevile. Kwa hiyo, lakini pia vilevile ukiangalia hata katika hizo sera katika utendaji au katika ile fursa au mamlaka za Serikali zenyewe namna zilivyokaa haziwezi kutueleza kwa sababu unakuja utawala wa awamu hii unaonesha kwamba itakuwa ni awamu ambayo inataka kukuza uchumi kupitia viwanda lakini ikija awamu nyingine inasema hapana uza viwanda bhana uza viwanda, ikija awamu nyingine inasema tunataka tena viwanda.
Kwa hiyo, sera sio zile ambazo zilizotuama ambazo zinaweza zikasukuma uchumi endelevu. Ukienda pale Shekilango, [Dar es Salaam] pale kulikuwa na kiwanda pale kinaitwa [Ubungo Farm Industries] UFI, kiwanda cha majembe na pembeni yake kulikuwa kiwanda cha Urafiki. Lakini hapa Gongolamboto [Dar es Salaam] kulikuwa kuna kiwanda cha Sungura Textile cha nguo. Sasa hivi ukienda ni ardhi tu, hakuna kitu. Ukienda kwenye vile viwanda vya UFI na Urafiki ukipita mule ndani mna magofu ya mashine, yaani hakuna [kitu] kabisa. Lakini kuna viwanda vingi pia vilivyokufa
Kwa hiyo, unakuta kuna hii sera tuliyonayo ambayo sio endelevu, haiwezi kuendeleza. Anakuja Rais huyu, utawala huo unasema kwamba tuwe na viwanda. Unakuja utawala mwingine unauza viwanda kwamba sio vizuri. Kwa hiyo, kiujumla ni kwamba utaangalia uchumi wetu sio uchumi ambao unaweza ukasimama sawasawa kwa maana ile ya sera zetu tukapata uchumi. Kwa hiyo, kiuchumi hatuna uchumi unaovutia ukilinganisha na matarajio yetu katika miaka sitini ambayo tuliyonayo.
Hali ya maisha ya wananchi inatafsiri uchumi tulionao. Kila mmoja anaiona hali ya maisha ya wananchi ni duni sana na watu wanaishi katika maisha ambayo ni ya dhiki sana. Ukienda Kariakoo sasa hivi biashara nyingi zimefungwa, yaani maduka yamefungwa watu wamepunguza hata ule ukubwa [wa biashara]. Mtu alikuwa na duka labda lina ukubwa wa fremu kama nne, amepunguza amebakia na fremu moja. Hii hali inaendelea nchi nzima. Uchumi sio mzuri kwa kweli.
The Chanzo: Hali ya kisiasa katika miaka sitini ya uhuru ipoje mpaka hivi sasa?
Sheikh Issa Ponda: Tulikuwa na mfumo wa vyama vingi huko nyuma wakati wa ukoloni, tulianza na vyama vingi halafu tukaingia kwenye chama kimoja baadae tukakatoka kwenye chama kimoja tukaingia kwenye vyama vingi. Mtazamo wetu wa kuhama kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja kwenda kwenye vyama vingi mambo mawili makubwa tulikuwa tunayatarajia la kwanza tulikuwa tunatarajia kuwa huru zaidi katika masuala ya kisiasa.
Huko mbele matarajio ni kwamba tutafikia au tufikie kwenye masuala ya kuunda Serikali iliyokuwa bora na kuwa matokeo yaliyokuwa bora. Lakini kimsingi tulikuwa na matarajio kwamba tuwe huru kwa maana ya kupata ridhaa ya mtu ya uongozi lakini tuwe huru kwa maana ya kuchagua mtu ambaye tunaamini kwamba huyu katika nafasi hii atatufaa, tuwe na huo uhuru wa namna hiyo na ule mchakato mzima ule wa kisiasa tuwe huru katika ule mchakato wa kisiasa.
Jambo la pili ilikuwa ni kwamba tunatarajia kwamba katika mabadiliko hayo ya kisiasa tuweze kumudu kutatua matatizo yetu sisi wenyewe. Maana yake huko nyuma tunaonesha kwamba wakati wa ukoloni tulikuwa tunabanwa, lakini tukiingia katika Serikali yetu wenyewe tutakuwa na uwezo wa kutatua matatizo yetu sisi wenyewe. Haya ni mambo ya msingi makubwa ambayo tulikuwa tunayatarajia tunapoingia kwenye uhuru wa kisiasa.
Lakini sasa ukifanya tathmini kwenye hili suala la uhuru kwa kweli unaona ni kama hakuna uhuru wa kisiasa. Yaani hivi karibuni mimi nilihudhuria kwenye kikao kimoja cha kama miaka miwili hivi mitatu nafikiri ambacho kilikuwa ni kikao kinachochadili mswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vingi vya siasa ilifanyika Dodoma katika ukumbi wa Pius Msekwa kwenye ukumbi wa Bunge. Niliingia kwenye kujadili kwa ujumla ile sheria imepita ni sheria ambayo ipo sasa hivi.
Ukiangalia ile sheria yaani ni kama vile hakuna vyama vingi na ni kama hakuna ule uhuru kabisa kwa sababu kwa ujumla, kwa kifupi, ile sheria ni kama ilikuwa inavichukua vyama vyote vya siasa inaviweka chini ya mtu mmoja ambaye ni Msajili wa Vyama, yeye ana mamlaka makubwa sana katika vyama vya siasa. Msajili wa vyama ana uwezo wa kutengua maamuzi yaliyofanywa na zile ngazi husika za chama ndani ya chama chenyewe. Kwa mfano, chama kimemteua kiongozi katika nafasi fulani, Msajili wa vyama anaweza akamuondoa yule mtu kwenye ile nafasi.
Na hivi vyama vinawawakilisha watu ambao kama ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA], kama ni ACT-Wazalendo, kama ni nani. Vinawawakilisha watu waliokuwa nyuma yao ambao ni mamilioni ya watu. Kwa hiyo, maamuzi yanayofanyika mle ni maamuzi ya hao watu walioko nyuma. Kwa hiyo, wanaweza wakafanya maamuzi katika ngazi fulani hawa watu kupitia hizo taratibu zao za kivyama lakini Msajili anaweza akayafuta hayo maamuzi. Kwa hiyo, dhana ya kwamba tunauhuru ni kwamba kwenye siasa hakuna.
Lakini tunashuhudia hivi sasa kwamba hata mtu akitaka kufikiri na zile fikra zake akitaka kuzieleza kwa mtu mwingine ni lazima aombe kibali, upate kibali cha kufikiri na kueleza fikra zako kwa mtu mwingine. Kiasi kwamba watu ambao wamefikia hatua wakaamua labda wakae kwenye kikao tena ndani ya ofisi zao, ama nyumba zao, ili wabadilishane fikra za mambo wanayoyatazama kisiasa na kuyawekea mkakati, basi vyombo vya dola vinakwenda kuwakamata. Vinawakamata na vikawazuia na vikawafungulia mashtaka kwamba wanafanya kosa.
Kwa hiyo, ukiangalia hii dhana kwamba kuna huo uhuru wa kisiasa ni kitu ambacho unakishuhudia kwa jicho lako na akili kwamba hili jambo halipo katika uhalisia ule wenyewe. Lakini hata watu wakitaka kutoka nje kufanya mkutano ili watu wawasikilize, mseme vile ambavyo mnaamini na mshawishi, hawaruhusiwi. Maana yake, watu kufanya mkutano ule wa pamoja au kuonesha zile hisia zenu na haya tunayoyazungumza ni mambo ukiyaangalia kwenye Katiba yameruhusiwa, sheria ya nchi imeruhusu lakini ukija katika ule uhalisia wenyewe ni mambo ambayo unakuta hayaruhusiwi, yaani mtu haruhusiwi.
Kwa hiyo, suala la kwamba tuko huru katika siasa hilo ni jambo ambalo kwa Tanzania pengine unaweza kusema bora hata wakati wa ukoloni kulikoni ambapo ilivyo sasa. Kama imefika leo hii katika kipindi ambacho tunasema sasa ndio tupo huru, miaka sitini sasa tunaingia, lakini wewe ukifikiri lazima upate kibali na ukitaka kuitoa ile fikra yako kwa mtu mwingine lazima upewe kibali. Sasa kuna ukoloni kuliko huo? Nadhani huo ni ukoloni mbaya zaidi ukilinganisha na ule ukoloni amao waliokuwa wanatufanyia wazungu.
Lakini hiyo ni hali ambayo tuliyonayo sasa hivi hapa Tanzania ambayo tunaishuhudia na tunaiona kwa macho yetu sisi wenyewe. Kwa hiyo, uhuru katika siasa ni kitu ambacho tulikitarajia sana ndio mabadiliko ya kisiasa tulikuwa tunayataka kutokea, kwamba twende kwenye hatua kama hiyo maana yake, tufike mahali tuweze kuwa huru katika mambo yale ambayo ni ya msingi sana.
Lakini nukta ya pili ni kwamba tulikuwa tunatarajia sana katika siasa tuweze kuwa na uwezo wa kutatua matatizo yetu sisi wenyewe. Lakini ukiliangalia hili jambo hatuna uwezo wa kutatua matatizo yetu sisi wenyewe mpaka sasa hivi na hili unaweza ukaliona kwenye matokeo ya wakati wa uchaguzi. Ukiangalia wakati wa uchaguzi, hatuwezi kutatua matatizo yetu kiasi kwamba baada ya uchaguzi huwa yanatokea maafa makubwa. Watu wanakufa. Watu wanapigwa. Watu wanaumia.
Yaani tuna mifumo, tuna sheria, lakini hatuwezi hata kutumia zile sheria. Hatuwezi kutumia sisi wenyewe kutatua yale matatizo yetu sisi wenyewe kiasi kwamba tunafika mahali mpaka tunauana. Ni kitu ambacho tulikuwa tunatarajia kwamba tunakwenda kwenye uhuru maana yake tufike mahali tuwe tuna uwezo sisi wenyewe wa kutatua yale matatizo yetu. Maana yake sio kwamba ifike mahali sasa labda pengine vyombo vya kimataifa au watu kutoka nje ndio waje kutusaidia kutatua matatizo yetu wenyewe. Kwa hiyo, hali ipo hivo
Lakini, hata ukienda kwenye masuala ya uchumi, hatuna uwezo wa kutatua matatizo yetu wenyewe. Bajeti yetu sisi pengine nusu inalazimika tupewe hela kutoka nje ndio tuje tuingize pale kwenye bajeti. Kwa miaka sitini maana yake hatuwezi kutatua matatizo yetu wenyewe. Na hata maji ya kunywa hatuwezi wenyewe hapa tunawataalamu mpaka wanakuja wataalamu kutufundisha jinsi ya kupanda miti ambayo ipo kwenye msitu wetu sisi wenyewe.
Yaani, watu wanatoka Japan wanakuja hapa kutufundisha sisi kupanda mti. Hata vijiti vile vya kuchokonoa meno vinatoka China. Maana yake hatumudu kwenye miaka sitini ni watu ambao tupo tu hatukuweza kutatua matatizo yetu wenyewe. Kwa hiyo, kwenye masuala haya ya kisiasa tulitaraji sana tuwe huru ni jambo la msingi sana ambalo linatuwezesha kuweza kufika mahali tukaweza kuunda Serikali ambayo ingekuwa madhubuti na Serikali iliyokuwa makini ambayo ingetusaidia sana katika kupata maendeleo.
Kwa hiyo, kutokua huru katika siasa ni jambo ambalo naamini liko namba moja, limetunyima fursa ya kuwa na Serikali makini katika jamuhuri yetu. Katika hili la kutokushindwa kutatua matatizo yetu wenyewe linaingia mpaka suala la Katiba, ni jambo ambalo tumekubaliana sisi wenyewe kwamba tuboreshe Katiba, kwamba tuiandike upya Katiba na ni utaratibu mzuri sana kwa sababu siku zote unapoona maendeleo wanayopata wenzetu maendeleo wanayapata kwa sababu ya kupitia ile mifumo yao mbalimbali, mifumo yao ya kiuchumi, mifumo ya kisiasa, mifumo ya kisheria na kadhalika.
Wanaipitia kila siku halafu wanaiboresha ndio maendeleo hata ukienda kwenye biashara, kwenye uzalishaji leo hii ukiangalia ile Toyota Land Cruiser iliyopo sasa hivi ukiangalia na ile Toyota Land Cruiser ya kwanza kabisa ni mbingu na ardhi, ni vitu viwili tofauti. Iliyopo sasa hivi ni bora sana ni kwa sababu ya hiyo kupitia maana yake zile kazi unazipitia.
Kwa hiyo, tunapozungumza Katiba Mpya maana yake ni kwamba tunapitia ile kanuni zetu, sheria zetu ili tuziboreshe na tulikubaliana hili jambo. Tulikubaliana na hatimaye tukatunga sheria ambayo ilikuwa na misingi miwili mikubwa. Msingi wa kwanza ni kutambua kwamba tumekubaliana suala la kupitia Katiba na kuandika Katiba nyingine.
Msingi wa pili ni kwamba tumekubaliana imewekwa hatua a utekelezaji wa namna ya kuleta yale mabadiliko ya Katiba, sheria ipo. Sasa katika hali kama hiyo halafu watu mnagombana, yaani watu mmefika mahali kwamba mnagombana yaani mnatofautiana kwamba inawezekana, haiwezekani, yaani mna makubaliano ya kisheria ya kwamba tumekubaliana hili jambo halafu vile vile tumekubaliana utaratibu wa namna ya kuliendea halafu mmefika mahali kwamba kuna ugomvi, yaani mnagombana hatutaki, tunataka, hatutaki, tunataka.
Kwa hiyo, nikirudi katika nukta kwamba tulitarajia sana katika kipindi cha uhuru tuwe na uwezo wa kutatua maatatizo yetu wenyewe lakini viashiria vingi vinaonesha kwamba hatuna uwezo wa kutatua matatizo yetu wenyewe. Kwa hiyo, siasa iliyopo tumefeli kwa kweli katika miaka sitini. Hatujapiga hatua ya maendeleo katika siasa.
The Chanzo: Katika miaka sitini ya uhuru je, hali ya uhuru wa Watanzania katika kujieleza na kujiamulia mambo yao wenyewe ipoje mpaka hivi sasa?
Sheikh Issa Ponda: Hilo kwanza ni nukta muhimu sana, yaani ule uhuru wa mtu mwenyewe. Kwanza, katika uhuru wa mtu mwenyewe nirudie pale pale kwenye siasa sasa hivi wewe huwezi ukaamua nikagombee nafasi fulani ya uongozi kama vile ubunge halafu ukapata hiyo fursa, yaani mfumo umewekwa pale unakuzuia. Sasa huo ni uhuru ambao umenyimwa si ndio? Tulitaraji mimi niwe huru, niwe huru kwa maana ya kugombea lakini pia niwe huru kwa maana ya nina weza nikamchagua mtu ninayemtaka
Sasa, kilichofanyika ni kwamba ule uhuru wangu mimi umewekwa ndani ya chama, kwamba wewe ukitaka kuwa huru, ukitaka uchukue nafasi ya upate nafasi ya uongozi, basi lazima uwe kwenye chama, yaani ina maana kwamba ule uhuru wa mtu binafsi haupo na hilo ni kosa kubwa sana kwa sababu mimi nahitaji kuwa huru kama Mtanzania ni lazima niwe huru maadamu tu ninakidhi vile vigezo au nafuata zile kanuni ambazo zilizokuwepo pale. Kwa hiyo hili lipo.
Lakini tukija kwenye uhuru wa kujieleza, hili linakwenda zaidi kwenye mambo ya vyombo vya habari lakini na ile mikutano ya umma, ile inazuiliwa kwa maana kwamba hawaruhusiwi kusimama ukaalika watu halafu wakafika pale na ukazungumza nao. Lakini pia, naona vyombo vya habari kuna masheria yamepita na yamelalamikiwa sana kwenye vile vyombo vya habari, kwa kiwango ambacho waandishi wa habari wakati mwingine wanachuja hata ile habari ukizungumza wanasema ukiandika hii habari hii itakuletea matatizo makubwa sana kwa mujibu wa zile taratibu na malalamiko ni makubwa sana.
Sasa hili jambo sio zuri. Ilitakiwa watu wawe huru ilimradi kwamba ule uhuru hauvurugi haki za mtu mwingine. Kwa mfano, mimi kusimama nikaomba ridhaa ya kugombea ubunge sichukui haki ya mtu wala hapa sijaingilia uhuru wa mtu mwingine, mimi mwenyewe nimejiona kwamba ninafaa na watakao jaji ni wale wapiga kura, wao watasema kwamba Sheikh Ponda hatumpi hiyo nafasi ya ubunge, wale ndio wanatakiwa sasa wale pia wananyimwa ule uhuru.
[Watu] wananyimwa ule uhuru wa kumchagua mtu kwa sababu tu hayuko kwenye chama lakini kama angeruhusiwa mimi nisimame ina maana wale watu wangeweza kunichagua na wangekuwa huru kumchagua mtu ambaye sio lazima awe kwenye CHADEMA, sio lazima awe [Chama cha Wananchi] CUF, sio lazima awe [anatoka Chama cha Mapinduzi] CCM, lakini mtu wanamjua kwenye jamii kwamba huyu ni mtu muhimu, ni mtu mweledi, ni mtu ambaye tukimpa dhamana anaweza akasimamia mambo yetu kwa sifa alizonazo.
Sasa haya yote haya yanapungua, yanazuiliwa haya yote haya kwa sababu tu huyu mtu hayupo kwenye chama. Hii ni kitu ambacho hakiwezekani na ninakumbuka wakati wa mchakato wa kuanzishwa vyama vingi katika tume nafikiri ni tume ya Jaji Nyalali alipendekeza Katiba nafikiri ilikuwa ni Katiba alipendekeza suala la mgombea binafsi. Kwamba ni mtu ambaye aruhusiwe mapendekezo yalikuwepo na namna hiyo lakini nafikiri yaliwekwa pembeni kwa namna moja. Kwa hiyo, nafikiri niseme hivyo katika uhuru wa mtu binafsi ni katika mambo ambayo hayapo hapa kwetu.
The Chanzo: Mpaka sasa tumezungumza mambo mnne yaani kijamii, kiuchumi, kisiasa na uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe kama Watanzania tangu kupata uhuru, na katika hayo yote umebainisha kwamba hatujafanikiwa, tumefeli. Je, unadhani tatizo lipo wapi?
Sheikh Issa Ponda: Sisi tunaweza kusema kwamba hatujaweza kufanikiwa kupata nafasi nzuri ya kuweka uongozi mzuri. Unajua, kwa mfano, suala la Katiba. Suala la Katiba ni suala la msingi sana kwa sababu suala la Katiba ni kwamba linaweka vigezo, vinaweza kulinda mambo ya msingi kama haki ya wananchi katika kufanya maamuzi. Katiba ikiwa nzuri, madhubuti inaweza kuwasaidia watu au kuwafanya watu waweze kufika mahali wapate yale mambo ya msingi kama vile uongozi bora.
Katiba zetu haziko hivyo. Unajua Katiba ambayo tuliyoipata ya kwanza kabisa sisi Tanzania haikutokana na ridhaa ya wananchi. Ilikuwa ni mchakato ambao uliwahusisha wanasiasa wachache pamoja na wakoloni wenyewe ndio tukapata Katiba ambayo tulikuwanayo na hiyo ndio ambayo tumedumu nayo tukiwa tunaitia viraka mpaka kufikia Katiba hii ya mwaka 1977 ni Katiba ile ile.
Kwa hiyo, sio Katiba nzuri ambayo imeweka misingi mizuri inayomwezesha mwananchi kuweza kuwa na fursa ya kuweza kuunda mamlaka zile ambazo zitakuwa zinatokana na ule uelewa wao na weledi wao. Katiba yetu sio nzuri. Kwa mfano, moja wapo katika mambo ambayo yamekuwa yanalalamikiwa ni suala zima la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Tume iliyopo [sasa] ni ile ambayo imetiririka kutoka kule kwa watawala ambao ndio hao walioingia madarakani kwa mfumo ule wa Katiba ile ambayo ilipatikana kutokana na wao pamoja na kushirikiana na wakoloni, wakaingia madarakani ambao kibinadamu wamefika mahala wameweza kuonja ile ladha ya utawala na wakaendelea kujenga mifumo ambayo inawafanya wenyewe waendelee kubakia madarakani kwa muda mrefu sana.
Na hii wamekuwa wanatamka wazi kabisa. Nakumbuka kwenye uchaguzi wa mwaka ule wa 2010, ambapo ulikuwa ni uchaguzi uliomuingiza Rais Jakaya Mrisho Kikwete madarakani kwa awamu ya mwisho. Rais aliyekuweko madarakani analazimika kufanya kampeni ya chama chake, alitamka Rais Mkapa alisema, “Hakuna mahali popote pale duniani chama ambacho kimeshika dola halafu kikose kuitumia dola kuhakikisha kinabaki madarakani.”
Haya maneno aliyasema Rais Benjamin Mkapa na nafikiria pia yamesemwa na viongozi wengine. Sasa kimsingi hawa wameweza kubakia pale kwa sababu ya ile Katiba iliyokuwepo na kwa sababu ya Katiba, mfumo ule wa Katiba uliokuwepo pale umeweza kuwanyima wananchi fursa ya kuweza kufanya mabadiliko makubwa. Leo hii, unazungumzia Tume ya Uchaguzi iliyopo ambayo kimazingira yake yote inateuliwa na mmoja katika wagombea ambaye anagombea na yeye katika uchaguzi.
Huyo ndio anayetengeneza kile chombo cha maamuzi, yaani kama vile mnataka kucheza mpira sasa mmoja katika zile timu mbili sasa timu moja ndio inamteua refa, inamteua mshika kibendera, inatunga sheria. Sasa haiwezekani mkapata ushindi na ndio mfumo ambao tulionao. Kwa hiyo, unaweza ukasema sababu za msingi ni kwamba wananchi wamenyimwa uwezo wa kuweza kuchagua mamlaka zile ambazo zinazotakiwa, naamini kwamba wananchi wangepata fursa nzuri tungeweza kupata Serikali iliyokuwa bora na iliyokuwa makini ambayo tunaweza kusema ingetuletea maendeleo makubwa sana ukilinganisha na hali iliyopo sasa hivi.
Nchi yetu haina sababu ya kuwa hapa tulipo, yaani nchi yetu sisi ni nchi katika nchi ambazo ni zenye neema kubwa sana. Tuna ardhi nzuri. Tuna madini ya kutosha. Tuna rasilimali nyingi sana hapa nchini Tanzania. Lakini ukiangalia nchi yetu ipo duni sana, ni nchi ambayo ni maskini kupita kiasi, raia wake ni watu ambao ni maskini kupita kiasi. Kazi yetu sasa hivi ni kupandisha kodi tu. Tunambana mtu ambaye hana kitu kabisa kwa sababu watu tulionao sio watu wabunifu ambao wanaweza wakatumia rasilimali zilizopo kuinua hali ya uchumi wa nchi na hali ya maisha ya watu sio wabunifu.
Tulianza na ile sera ambayo nimeizungumza kule ya utaifishaji. Haikuwa sera nzuri maana yake ni sera ambayo ilikuwa inawafundisha watendaji wetu yaani kupata vitu vilivyokuwa tayari, maana yake yaani sio kubuni, yaani wao walitakiwa wabuni kile kiwanda wanachotaifisha, walitakiwa watu wawe wabunifu, na wao wabuni kama alivyoweza kubuni yule aliyejenga kile kiwanda.
Lakini matokeo yake sisi tukachukua kile kiwanda chenyewe maana yake unamfundisha mtumishi au mtendaji wa Serikali kwamba hivi ndivyo ambavyo tunaweza tukajenga uchumi wetu kwa kupata kitu halisi kilichopo pale. Kwa hiyo, watu wetu ule ubunifu wa kuumba umeuawa kabisa kwa watu wetu. Wanashindwa kutumia ile hali halisi ya neema ambazo Mwenyezi Mungu ameziweka kwenye Tanzania hii tukapanda kiuchumi. Leo hii unaangalia dona Sh2,000, yaani dona maana yake ni chakula cha mkoa mmoja tu unaozalisha mahindi, lakini leo hii mwananchi wa Tanzania anauziwa dona, ugali wa dona, Sh2,000.
Ni ghali sana maana yake, na hakuna sababu zozote za msingi. Sisi tunaagiza chakula kutoka nje. Ukitoka tu hapo, ukiingia barabarani, ukiingia tu Pugu hapo, unakuta msitu mkubwa na ni wakijani, yaani maana yake ardhi ni nzuri kabisa. Ukienda hapo kuna bonde sijui liko pale bonde la mto Ruvu maji yanakaa mwaka mzima pale yanayoletwa na mvua pale mnaweza mkazalisha pale chakula cha kula nchi nzima. Lakini mpaka aje Mjapani ndio aje kutufundisha pale, aje atusimamamie pale.
Sasa tunaweza kusema kimsingi kwamba hatuna watu wazuri ambao wanaweza wakatuongoza katika taifa letu. Hiyo ni kasoro kubwa na hii si kwa maana nyingine sio kwamba hatujapata fursa ya kupangana vizuri sisi wenyewe na tunabanwa na hii mifumo ambayo ilikuwepo. Kwa hiyo, suala la Katiba Mpya iliyokuwa bora ni kitu cha msingi sana kwa sababu Katiba Mpya tafsiri yake ni kwamba tumepitia tumerekebisha, tumesahahisha ile Katiba iliyokuwepo na huo ndio mfumo unoleta maendeleo popote pale duniani, ni ule mfumo wa kupitia kazi zenu za kiuchumi, kazi zenu za kisiasa, kazi zenu za kijamii mnazipitia mnaboresha. Wenzetu wanafanya hivyo kila siku, kila siku. Sasa unapozuia maana yake ni kwamba unazuia mabadiliko ya mambo ambayo ni ya msingi sana.
The Chanzo: Baada ya kuonekana kufeli katika kila nyanja je, kitu gani kifanyike ili iwe ndio njia ya kurekebisha makosa tuliyoyafanya na hatimaye kama taifa tuweze kufanikiwa kwa miaka mingine mingi huko mbele?
Sheikh Issa Ponda: Mimi nafikiri, unajua huko nyuma kidogo mpaka tulipoingia kwenye kukubaliana kwamba tuwe na Katiba Mpya kulikuwa kuna jitihada fulani ambazo zilifanyika. Miongoni mwa hizo jitihada ilikuwa ni kusema, watu walikuwa wanapaza sauti, wanasema, wakati mwingine wanataka hata kutumia ile mifumo ya kisheria lakini katika hatua fulani, kwa mfano, tupite tutembee barabarani kwa maana ya kuonesha zile hisia. Kuna kipindi watu walikuwa wanaomba kibali ili waingie barabarani kwa maana ya kufanya maandamano ya amani ili kuweza kuonesha zile hisia lakini kulikuwa kuna vitu, kuna midahalo inaendelea kufanyika na kadhalika, tulikuwa tunafanya vitu hivyo.
Sasa tunachotakiwa sasa hivi ni kuongeza nguvu ya kupaza sauti ya kusema na kuna baadhi ya vitu vingine vikifika mahali kuweza kuvisusia. Kwa mfano, kuna kipindi fulani sisi tuliweza kushauri, tukasema kwamba hata kuchagua tunaweza tukasusia, mkasema kwamba vyama vyote na wananchi wote wa Tanzania sisi hatushiriki uchaguzi, hatushiriki uchaguzi kwa sababu tuna mambo ambayo kimsingi tunayataka kama wananchi. Sasa kwa sababu wananchi mkisema kwa sauti moja, yule anayepinga nani sasa, kwa sababu nyie mmesema kama Watanzania sasa yule atakaye kuwa anapinga ni nani?
Kwa hiyo, hatusemi kwamba tuingie kwenye vurugu lakini tunasema ipo namna kama tukifika mahali tukatoa sauti na tukaonesha kwamba tupo makini mpaka ikafika ulimwengu unashuhudia kwamba kuna tabaka tu la watu fulani ndio linagoma, linapinga basi hiyo hali itokee kwamba kuna tabaka la watawala linapingana na wananchi wake tunaweza tukafika hapo. Kwa hiyo, sisi cha kufanya kwamba ni lazima kama viongozi tuwashawishi na tufike mahali tusipokubali mambo madogo mnaweza mkakubali kuingia kwenye uchaguzi ambao unaepukika kabisa, yaani kwamba pale mbele mnaenda kuporwa, kunyang’anywa kwa sababu misingi yote ya kufanyiwa ile dhuluma ipo pale.
Tunaweza kufika mahali tukasema hapana, sisi basi, bora hilo jambo lisifanyike kama nchi yetu itakuwa ni ya kifalme basi iendelee, kama tunataka tutangaze kwamba nchi yetu sisi kama ilivyokuwa ya Kamuzu Banda basi tangazeni kwamba nchi hii ni ya kifalme na wataendelea watawala kuwaridhisha wale wa familia zao na watoto wao basi endeleeni na hiyo lakini kama ni nchi ya kidemokrasia, ni nchi ambayo ni yetu sote mnapaswa kutusikiliza sisi wananchi tunasema nini.
Kwa hiyo, mnaweza mkafika mahali mkagoma baadhi ya mambo kwa dhana kwamba yale mambo ya msingi yapatikane. Kwa hiyo, niseme kwamba sisi wananchi tunaweza tukatengeneza mazingira fulani yakusukuma wale ambao wamekaa kwenye maamuzi wakatusikiliza na tukakubaliana na hili tulifanya kwenye mchakato wa Katiba Mpya na ukapatikana. Kwa hiyo, na hii tunaweza tukafanya na ikawezekana pia kwenye mambo mengine.
Mpaka hapo nadhani tumepitia mambo yote muhimu tumepitia hali ya kijamii, tumepitia hali ya kiuchumi, tumezungumza hali ya kisiasa lakini pia tumejaribu kuangalia uhuru wa kuongea. La mwisho kwenye hili ni wito labda kwenye vyombo vyetu vya hawa watawala wetu kwamba ni muhimu sana kuwa na utamaduni wa mazungumzo, kuwa na utamaduni wa mazungumzo na kwa sababu hii nchi ni yetu sote, hii nchi ni ya Watanzania wote na wale walioko madarakani ni kwa sababu zile nafasi haiwezekani tukakaa wote kwenye zile nafasi isipokuwa wanakaa wachache ili wasimamie. Kwa hiyo, wao wanatakiwa wajue hivyo.
Lakini nchi ni yetu sote na sote tuna uwezo wa kuweza kuchangia katika nafasi mbalimbali za kisiasa tuna uwezo wa kuchangia kwa hilo lifahamike. Sasa, kwa dhana hiyo ni kwamba tuwe na utamaduni wa kukaa pamoja na kuzungumza. Wale walioko kwenye mamlaka waone umuhimu wa kukaa na watu wengine wakazungumza na tukaheshimu yale mazungumzo kwa sababu kuna tatizo hilo kwamba wakati fulani tunaweza tukakaa lakini watu wasiheshimu yale mazungumzo.
Huko nyuma kumekuwa na vikao vimefanyika lakini watu hawakuheshimu yale mazungumzo. Kwa hiyo, tujenge utamaduni. Huo ndio wito wangu, tujenge utamaduni wa watu walioko madarakani kuwa tayari kukaa na Watanzania wengine walioko nje ya Serikali kujadili masuala muhimu yanayohusu taifa kwa ujumla na vile vile kuheshimu yale majadiliano yatakayokuwa yamejadiliwa katika vikao kama hivyo. Huo ndio wito ambao ningependa kumalizia katika suala hili la miaka sitini ya uhuru tunatazamaje katika maeneo hayo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na mengineyo.
The Chanzo: Umezungumza Kiswahili sanifu sana katika mazungumzo yetu je, unadhani Serikali inaipatia lugha ya Kiswahili hadhi na nafasi kamili katika kuliunganisha taifa na kutatua matatizo yetu?
Sheikh Issa Ponda: Swali zuri, swali zuri sana. Kwanza nikwambie kuhusu lugha ya kiswahili. Lugha ya Kiswahili ni katika lugha kubwa duniani, nafikiri bara la Afrika itakuwa ni lugha kama ya pili ama ya kwanza kitu kama hivyo ambayo inabeba watu wengi sana na lugha ina vitu vingi sana ndani yake na sisi Watanzania ni lugha yetu na tulipaswa kuiheshimu na kuilinda, lakini katika uhalisia ukifanya uchunguzi ile lugha ya Kiswahili hatuiheshimu, hatuiheshimu na wala hatuilindi na hatuiendelezi.
Tunaweza kusema kwa namna moja au nyingine tumeshindwa kuilinda. Unajua lugha, yaani inatakiwa ilindwe, ndio maana ukienda, kwa mfano, katika nchi za wenzetu huwezi kumkuta mtu anachezea lugha halafu akaachiwa, yaani ni lazima atashughulikiwa akichezea lugha. Sisi kwa bahati mbaya zaidi kama kuna aina fulani ya hujuma juu ya lugha ya Kiswahili kwanza kabisa Kiswahili kimefanywa kama ni lugha ambayo haina kabila wala ardhi, hakuna lugha yoyote duniani ambayo haina kabila wala haina ardhi, hapana.
Ukisema kipare, yaani kuna kabila la Wapare na ipo ardhi utaoneshwa kabisa kwamba hii ndio ardhi ya Wapare. Ukisema Kihaya kuna kabila la Wahaya na unaoneshwa na watu kwamba hii Kagera ndio ardhi ya Wahaya. Ukisema Kikurya utaambiwa kuna kabila la Wakurya. Kila lugha ina kabila. Tanzania imefanywa kwamba lugha ya Kiswahili haina kabila na haina ardhi. Imefanywa ni lugha ya watu wote. Hiyo ni hatua ya kwanza ya kuiondolea ulinzi ile lugha.
Kwa hiyo, hatua ya pili imeundiwa bodi, yaani kuna bodi au mabaraza ya Kiswahili ambao wale sasa wanakuwa ndio wamiliki wa lugha ile. Sasa yale mabaraza ama bodi ndani yake kuna makabila mchanganyiko kuna Wamanyema, mimi ni Mmanyema, kuna Wahaya, kuna Wandengereko. Yaani hawa ndio wamiliki wa ile lugha ya Kiswahili, jambo ambalo sio kweli. Hakuna lugha ya namna hiyo. Kila lugha inakuwa ina wenyewe. Sasa huo ni msingi wa kwanza wa kuiharibu ile lugha. Sasa matokeo yake ile lugha imekosa ulinzi. Imekuwa ni lugha ambayo sasa watu wa nje wanaweza wakaiingilia ile lugha wakaipiga vita.
Mimi nimefanya uchunguzi kidogo kwenye eneo la Kiswahili. Sasa hivi kuna mambo mengi sana ya lugha za kigeni yanaingizwa kwenye Kiswahili na kufanywa Kiswahili hasa Kiingereza. Yaani, kuna maneno ya Kiingereza yanachukuliwa yanaingizwa kwenye Kiswahili halafu kinaitwa Kiswahili. Kwa hiyo, Kiswahili sasa hivi ukiingia kwenye kamusi ya Kiswahili utakuta kuna maneno kibao ya Kiingereza kama hii hapa computer basi inatamkwa kompyuta basi inakuwa ni ya lugha ya Kiswahili. Camera inatamkwa kamera halafu inakuwa ni lugha ya Kiswahili kitu ambacho sio sahihi. Inasemwa hivyo kwa sababu eti ni teknolojia iliyokuja katika kipindi ambacho Kiswahili kilikuwa hakina hilo neno lakini kuna mfumo wake kumbe mfumo wa teknolojia mpya katika lugha huwa ni wa kufananisha, yaani kuangalia kitu chenye matumizi sawa na kile kitu kilichokuja huko nyuma kitu cha matumizi kama yale ni kipi halafu ile teknolojia mpya inapewa jina la kile kitu ambacho huko nyuma kilikuwa kina jina kama hilo.
Kwa hiyo, naweza kusema kwamba lugha ya kiswahili kwa namna moja au nyingine kwa sababu sio jambo ambalo tulipanga kulizungumza ina aina fulani ya kuhujumiwa. Sasa wale wanaomiliki ile lugha yaani hawawezi kuwa wadhibiti wazuri. Yaani mimi kama nitamiliki lugha ya Kihaya mimi ni Mmanyema siwezi mimi kukifanya kile Kihaya kikawa ni lugha nzuri inayozungumzwa vizuri, inayosimamiwa vizuri, siwezi hata kama napenda lakini mimi ni Mmanyema, ile lugha ni Kihaya misingi yetu ni tofauti, sasa Kiswahili kimeundiwa bodi, bodi ina Wandengereko, ina Wakurya ina wanani? Halafu eti hao ndio wanashughulikia lugha ya Kiswahili na wanauwezo wa kubadilisha neno na kuingiza neno.
Sasa ukirudi nimesema kwamba ni kama inafanyiwa hujuma fulani. Tukirudi huko nyuma hapa katikati kuna mjadala mkubwa sana uliotokea wa wasomi kwamba lugha ya kufundishia iwe lugha gani? Wale ambao walikuwa wanasema lugha ya Kiswahili iwe lugha ya kufundishia walikuwa wapo sahihi kwa sababu unapomfundisha mtu kwa lugha yake anaelewa vizuri zaidi na kinachokusudiwa katika kufundisha ni ile elimu yenyewe, yale maarifa ndio yanakusudiwa na maarifa unaweza ukayapata katika lugha yoyote ile.
Wajapani hawajui Kiingereza lakini ni madaktari. Kuna Mchina hajui Kiingereza lakini ni daktari. Yale maarifa na lugha ni vitu viwili tofauti. Ule ujuzi na lugha ni vitu viwili tofauti kabisa. Kwa hiyo, tukirudi kwenye ile hoja kwamba inwezekana pengine watu wetu walioko kwenye uongozi wanatatizo hilo kwa sababu ya lugha na inawezekana ikawa na ukweli kwa sababu kwenye lugha yao wenyewe kuna matatizo makubwa sana na hatupo tayari kuingia kwenye majadiliano au kuiboresha hili jambo katika namna ambayo ni nzuri.
Kwa hiyo, Kiswahili ni lugha muhimu. Ni lugha ambayo inatakiwa ifanyiwe mchakato mkubwa na wanafunzi wanatakiwa wafundishwe halafu lugha nyingine kama Kiingereza iwe ni somo kama yalivyo masomo mengine. Lakini lugha ya kufundishia mtu anafundishwa kwa Kiswahili ataelewa vizuri lile somo lenyewe, atakuwa mtaalamu mzuri na Kiingereza anajua kwa sababu si amesoma kama somo, Kifaransa anakijua vile vile. Kwa hiyo, ile dawa ikija sijui ampicillin ataijua kwa sababu anajua lugha ikija sijui micro nini ataijua. Kwa hiyo, kuna huo ukoloni ambao umetubana. Ndio hayo mambo tunasema tu hatujawa na uhuru, yaani bado tuna tatizo kwenye uhuru. Hatujawa huru sawa sawa.
The Chanzo: Ungependa kuona Tanzania ya aina gani katika kipindi cha uhai wako, nini ungependa kuona kinatokea ambacho kitafanya moyo wako uwe na furaha?
Sheikh Issa Ponda: Kwa kweli swali zuri sana. Mimi ningependa kuona Tanzania ya watu ambao wanaishi kama ndugu, wanaishi kwa furaha halafu maisha yao pia ni maisha mazuri na hii kwa sababu ndivyo Mwenyezi Mungu alivyotaka kulingana na jinsi ukiangalia Tanzania jinsi ilivyo kwa sababu ni kati ya nchi zilizo na neema kubwa kabisa ni Tanzania. Yaani tuna uwezo kila mmoja kupata mahitaji yake hapa bila ugomvi, yaani nchi ilivyokaa, neema zilizopo Tanzania Mwenyezi Mungu alivyoineemesha Tanzania ni nchi ambayo ina neema zote.
Neema nyingine kubwa zaidi ni lugha tunazungumza lugha moja sisi, [lugha] ya Kiswahili. Lakini tabia ya Watanzania ambayo nimeizungumza kule mwanzo kwenye utamaduni, tabia ya Watanzania ni tabia ya kushirikiana na kupendana mpaka tunapata uhuru hakuna mapigano, hakuna mapigano kwamba kabila fulani na kabila fulani linapigana Tanzania hakuna. Yaani, tupo vizuri maana yake tunaishi kwa amani na nchi yetu pia ilikuwa imeshakuwa na misingi mizuri sana ya maendeleo kwa sababu nchi yetu imepata maendeleo miaka mingi sana.
Kuna miji kama Kilwa ni nchi. Kilwa ilikuwa na fedha walikuwa na fedha na walikuwa na maendeleo makubwa kwa sababu walikuwa wanamajumba ya maghorofa, ndio yale magofu unayoyaona yamebakia pale ni katika nchi ambayo ilikuwa ni nchi kabisa na walikuwa na biashara kubwa sana kati yao na Afrika Kusini, biashara ya dhahabu na walikuwa maji ya bomba wanafanya biashara kati ya Kilwa na Mashariki ya Kati na ukisoma katika historia mji wa Kilwa, Kilwa Kisiwani, ulikuwa mzuri kuliko London, yaani umeanza kuwa mzuri Kilwa kulikoni London.
Wamekuja huku kina Vasco da Gama wameshangaa kukuta maendeleo yaliyopo huku, wakashangaa kuona imekuwaje huku kuna maendeleo makubwa kiasi hiki kama kule tulikotoka? Kwa hiyo, mimi ningependa kuiona Tanzania ambayo ina misingi ile, Tanzania ambayo watu wanaishi kwa furaha, kwa amani.
Watu wanaweza kupata riziki zao vizuri, maisha yanakwenda vizuri na ni kitu kinachowezekana kabisa, ni suala la kuweka misingi mizuri ya uongozi na utawala, tunaweza kufika kuwa Tanzania ya amani kulikoni hii Tanzania ambayo tupo nayo sasa hivi unatembea unamashaka barabarani, mara umetekwa na anayekuteka Mtanzania mwenzako hujui anakutekea nini, na akishakuteka hasemi kwa nini amekuteka, anaweza akakuteka halafu akakaa na wewe tu na pengine akaendelea kukutesa, yaani ukimuuliza hicho kitendo taifa linafaidika na hicho kitendo kwa namna gani yaani hakuna maelezo, kwamba taifa kama taifa linafaidika na hicho kitendo kwa namna gani.
Kwa hiyo, ningependa kuona Tanzania nzuri ya watu tunaishi kwa amani [na] kwa furaha, kwa mapenzi, kwa ushirikiano. Hiyo ni Tanzania ambayo mimi nilikuwa naitegemea sana.