The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Namna Serikali Inavyoweza Kutumia Leseni za Kidigitali Kuwezesha Biashara za Mtandaoni

Leseni za kidigitali zinaweza kutolewa kwa kutumia kimbulisho cha NIDA na namba za simu rasmi za mteja husika. Inawezekana kabisa mfanyabiashara huyu mdogo akapata leseni na mtu akitaka kuthibitisha uhalali wake anaweza kwenda kwenye kanzidata maalum ya kuthibitisha leseni ya mfanyabiashara husika

subscribe to our newsletter!

Mara nyingi wafanyabiashara wakisikia leseni wanawaza maumivu, kukamuliwa, udhibiti na urasimu na Serikali ikisema leseni inawaza makusanyo, kukimbizana na wafanyabiashara. Kabla hujashituka, hii makala haihusu maumivu kwa wafanyabiashara na kwa Serikali, makala hii haihusiani na kutisha au kukimbizana na wafanyabiashara, ni makala kuhusu yajayo. Tuendelee!

Miaka ya nyuma kabla ya kuibuka kwa mitandao ya kijamii, iliwalazimu wafanyabiashara wengi wadogo kuzunguka nyumba kwa nyumba au mtaa kwa mtaa kutafuta soko la biashara zao. Hali hii imebadilika zama hizi hasa baada ya umaarufu wa mitandao ya kijamii kama Instagram, Twitter na WhatsApp.

Kuna biashara nyingi katika mtandao, ukienda Instagram unaweza pata wafanyabiashara wa kila kitu kuanzia mavazi, urembo, vyakula, mpaka wa huduma kama upambaji, ufundi, udalali au ujenzi. Kurasa za mitandao zimegeuka fedha.

Kupitia mitandao ya kijamii, watu wengi wameweza kutumia kufanya majaribio ya biashara zao; kufeli na kuanguka. Wako wengi waliofuzu na kuweza kuingia kwenye hatua nyingine kuwa na ofisi, maduka mazuri yenye kuvutia na hata kutoa ajira kwa watu wengi, yote yalianzia mtandaoni.

Chukulia mfano Mudi Mabiriani aliyeanzia kwenye kurasa za mitandaoni mpaka kuajiri watu na hata kudhamini mambo kadhaa. Au DalaliMwanamke ambaye amejenga jina mpaka kuwa na ofisi kupitia kufanya kazi ya real estate mtandaoni. Wako wengine wanaojenga chapa za kipeekee, mfano lavish_home_of_style na mtindo wake wa kuuza mavazi kupitia ‘catwalk’ maridadi. Au Chaurembo Food aliyeanza kujaribu biashara yake kwa pages za mitandao ya kijamii tu kabla hajafungua mgahawa wake.

Kuna mifano mingi ya namna watu walivyojenga biashara kwa kurasa tu za mitandao. Lakini wengi wanaoanza inabidi kukabiliana na vikwazwo mbalimbali, kikwazo cha kwanza ni kuaminika, wateja wengi katika kujiridhisha kitu cha kwanza anauliza ofisi yako iko wapi? Kama huna majibu, wakisikia ni mtandaoni tu, mashaka yanakuwa makubwa na wengine hata kubadili mawazo. Changamoto ya pili ni kuibuka kwa wimbi kubwa la matapeli wanaodanganya na kuwaibia wateja.

Kwa sasa moja ya jambo ambalo linafanya biashara kuaminika ni kuwa na leseni. Hii ni kwa sababu hatua za kupata leseni ni lazima mamlaka zijithibitishie kuwa una eneo maalum la kibiashara, na hufanya hivi kupitia Serikali za mtaa, pamoja na wewe kutakiwa kuorodhesha sehemu biashara ilipo.

Huu ni utaratibu mzuri, ila ni utaratibu unaoendelea kupitwa na wakati. Ni muhimu Serikali ikaanza kufikiria thamani ya biashara za mtandaoni hazijalishi mtaa au kuwa na majengo makubwa na dunia nzima inahamia huko. Tunaelekea kwenye nyakati ambapo kutakuwa na biashara kubwa ambazo hazina jengo, ofisi wala hata kiti kimoja, zipo mtandaoni tu na labda makazi ya kuishi ndo yakageuka kuwa ofisi, remote working.

Kuna umuhimu wa Serikali kuwaza namna ya kutatua tatizo wanalokumbana nalo wafanyabiashara wa mtandaoni, hasa katika kutengeneza uaminifu na mteja hasa kwa kuleta leseni za kidigitali. Kwa sasa hili jambo hakuna, na wala sheria hazitambui. Kwa nini ni muhimu? Kwanza, Serikali inajitengenezea mazingira ya kwenda na mabadiliko ya dunia. Lakini pili Serikali itajitengenezea miundombinu ya kupata mapato zaidi.

Leseni za kidigitali zinawezekana hasa ukizingatia kwa sasa utambuzi wa kidigitali nchini umefikia kwenye hatua kubwa, kuna vitambulisho vya NIDA na kuna namba za simu ambazo hazihamishiki, kampuni ya simu na NIDA wote lazima wamtambue na kumuona muhusika kabla ya kumpa kitambulisho au laini ya simu, huku alama muhimu za vidole zikichukuliwa. 

Leseni za kidigitali zinaweza kutolewa kwa kutumia kimbulisho cha NIDA na namba za simu rasmi za mteja husika. Inawezekana kabisa mfanyabiashara huyu mdogo akapata leseni na mtu akitaka kuthibitisha uhalali wake anaweza kwenda kwenye kanzidata maalum ya kuthibitisha leseni ya mfanyabiashara husika na kanzidata hiyo ikaonyesha mpaka kurasa rasmi za mtandaoni ambazo mfanyabiashara huyu anatumia.

Katika mazingira haya ukimwezesha mfanyabiashara mdogo na ukarahisisha hatua zote ni lazima atalipa kodi, tena bila shuruti. Maana kulipa kodi, hasa inayoendana na kipato chake inamwongezea thamani katika biashara yake. Hatua nyingine ni kuhakikisha kulipa kodi kwa mfanyabiashara huyu kuna kuwa rahisi na hata kupata hiyo leseni ya kidigitali kunakuwa rahisi pia. Sehemu kubwa ya kodi inapotea sio kwa sababu watu hawataki kulipa, ila kwa sababu utaratibu wa kulipa kodi ni mgumu na korofi.

Muhimu zaidi ni kufanya leseni za kidigitali kama sehemu ya kuongeza thamani ya mfanyabiashara mdogo, sio msumari wa kuzuia biashara mtandaoni. 

Wahafidhina wengi katika mifumo, wanaweza kuona leseni za kidigitali kama porojo au ndoto, ila  muda unavyoyoyoma ndivyo inavyozidi kuwa muhimu kwa Serikali kujifunza na  kuyaona mabadiliko yanayokuja na kujiandaa nayo.

Tony Alfred K ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tonyalfredk@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Naam kazi nzuri ambayo umetuelekeza ni kweli Kuna wakati mtu anafikiria sana kuhusu kujisajili kwaajili ya kuongeza ujasiri na WiGo wa biashara lakin vijana wengi hawapendi kufatiliwa na serikali pengine kama hili lingeweza kuchochewa na watu wengi waandishi wa habari, wachambuzi wa maswala ya siasa na uchumi na kuweza kufikia meza usika ingependaza sanaaa Kwan nchi ingeonekana kupiga hatua kwenye zama izi za kidigitali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *