The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Timu ya watu 19 TRA iliiletea serikali bilioni 108 za kodi, kwa nini serikali isiwekeze zaidi hapo?

Timu ya watu 19 kutoka Kitengo cha Kufuatilia Kodi za Kimataifa ndani ya TRA iliiletea Serikali Shilingi bilioni 108 za kodi baada ya kufanya ukaguzi kwenye makampuni 60 ya kimataifa.

subscribe to our newsletter!

Moja kati  ya mambo yaliyoibuliwa na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyotoka Machi 2021 ni namna timu ya watu 19 ilivyoweza kufanya Serikali ikapata mapato yake ya Shilingi bilioni 108, mapato ambayo tayari Serikali ilikuwa ikiyapoteza.

Timu hii ni ile ya Kitengo cha Kufuatilia Kodi za Kimataifa (ITU), ikiwa na jumla ya watendaji 19 ambapo kulikua na wachumi sita, wataalamu wa mahesabu na kodi 10 na wanasheria watatu.

Moja kati ya kazi kubwa ambayo timu hii inatakiwa kufuatilia ni ukaguzi wa makampuni ya kimataifa, hasa katika kuzitambua mbinu mbalimbali zinazotumiwa katika ukwepaji wa kodi kimataifa. Moja ya mbinu inayotumiwa na makampuni makubwa ulimwenguni katika kujipunguzia mzigo wa kodi ni kupitia uhamishaji faida na gharama au transfer pricing kama inavyojulikana kwa kimombo.

Ngoja nikupe mfano ili uelewe transfer pricing inavyofanya kazi.

Chukulia kampuni A ina ofisi Tanzania inayoitwa A Tanzania LTD na pia ina ofisi Canada inayoitwa A Canada Corporation. A Tanzania LTD inaamua kununua vitu kwa A Canada Corporation, ila badala ya kuuziwa kwa bei ya soko inauziwa mara nne ya bei ya soko. Gharama hizi za kununua ndani kwa ndani ya A zitarekodiwa na mwisho wa siku A Tanzania hatalipa kodi, sababu hajapata faida au atalipa kodi kidogo sababu ya gharama kuwa kubwa. Ukweli wa mambo hiki ni kiini macho cha biashara na anayepoteza ni Serikali kwa kukosa kodi stahiki.

Turudi kwenye timu hii ya watu 19. Pamoja na udogo wa timu, watu hawa waliweza kufanya ukaguzi kwa makampuni 60 ya kimataifa huku wakiwa wamemaliza ukaguzi  kwa makampuni 23 ndani ya kipindi cha mwaka 2016 na mwaka 2020. Kutokana na udogo wa timu hii hawakuweza kufikia makampuni 444 ambayo yalitakiwa kukaguliwa.

Makampuni haya 60 yaliyokaguliwa kati ya mwaka 2016 mpaka 2020 yalikua ni makampuni yenye ujumla wa mapato ya shilingi trilioni 4.23. Baada ya ukaguzi ilionekana kwenye haya makampuni jumla ya Shilingi bilioni 108.6 zilitakiwa kulipwa serikalini, na makampuni yakaridhia kulipa huku kodi ya Shilingi bilioni 44 zikiwa bado katika majadiliano, baada ya makampuni kuweka pingamizi.

Shilingi bilioni 108, ni sawa na asilimia 36 ya bajeti ya Wizara ya Kilimo. Shilingi bilioni 108 ni zaidi ya fedha zilizopangwa kuboresha miundombinu katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili , Hositali za Rufaa na za Kanda. Unaweza kuona kwamba hizi ni fedha nyingi sana.

Pamoja na kazi hii kubwa, bado kitengo hiki kinafanya kazi chini ya kiwango kwa sababu mbalimbali. Sababu ya kwanza ni kutokuwa na nguvu kazi. Sababu ya pili ni ufinyu wa bajeti. Na sababu ya tatu kukosekana kwa nyezo na kujengewa uwezo wa timu hii. Lakini pia bado Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haijawa na sera madhubuti na mfumo bora juu ya ufuatiliaji wa transfer pricing.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, kunahitajika wafanyakazi 49 zaidi ili kukifanya kitengo hiki kuweza kujimudu. Inawezekana katika nafasi za kazi zaidi ya 600 zilizotangazwa na TRA hivi karibuni suala hili likawa limetatuliwa kwani toka mwaka 2016 Serikali ilizuia TRA kuajiri wafanyakazi wapya.

Lakini pia ilionekana sehemu kubwa ya nyezo, hasa software zinazohusika na ukaguzi wa transfer pricing, hazikuwepo TRA. Nyezo hizi zilikosekana hasa kwa sekta ambazo zinatambulika zaidi kwa transfer pricing ikiwemo ujenzi, uziduaji (madini, gesi) na viwanda.

Kutokana na jitihada za Serikali kuvutia uwekezaji hasa katika viwanda, madini na gesi, kuna umuhimu mkubwa wa Serikali kukiimarisha hiki kitengo cha kodi za kimataifa (ITU), hasa katika kuhakikisha Serikali inapata kodi inayostahili na rasilimali za Watanzania zinawanufaisha.

Ni muhimu wakaguzi na watendaji kutoka Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati kuwa na ukaribu na kujenga utendaji wa pamoja na kitengo hiki, ili kuhakikisha hakuna shilingi ambayo inapotea na fedha hizi ziweze kutumika katika miradi mbalimbali.

Tony Alfred K ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tonyalfredk@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *