The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ufisadi Kama wa TPA Utakomeshwa na Mikataba ya Manunuzi Serikalini Kuwekwa Wazi

Mamlaka ya Bandari na Kampuni ya Huduma za Meli wamekuwa wakiingia kwenye mikataba ya kipigaji na isiyokuwa na tija kwa taifa

subscribe to our newsletter!

Moja ya sura ambayo tumeizoea kuiona kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan ni ile ya ukarimu, upole na yenye kuonyesha kujali. Pamoja na mamlaka makubwa aliyonayo, tumekuwa tukishuhudia hata anapotoa maelezo, amekua akitumia lugha yenye kuonyesha unyenyekevu, ‘naomba mkayafanyie kazi’ moja ya kauli amekua akiitumia sana.

Mara chache Rais Samia ametuonyesha sura yake ya ukali, ingawa hatoi maneno makali au mazito, ila kwa lugha ya mtaani naweza kusema ukikutana na siku Rais Samia kakasirika ‘panawaka moto.’

Leo, Disemba 4, 2021, ilikua ni moja ya siku ambayo Rais Samia kaonyesha sura yake ya ukali, siku nyingine ambayo naikumbuka kwa haraka haraka ni September 13, 2021, akielezea kwa nini ameamua kubadili Baraza la Mawaziri.

Ufisadi mamlaka ya bandari 

Kitu kilichomkasirisha Rais Samia leo ni namna Mamlaka ya Bandari na Kampuni ya Huduma za Meli wamekuwa wakiingia kwenye mikataba ya kipigaji na isiyokuwa na tija kwa taifa. Kwa mfano, kazungumzia jinsi utengenezaji wa baadhi ya vifaa bandarini umekuwa ukitumiwa kama chaka la wapigaji.

Akizungumzia hilo Rais Samia anabainisha: “Lakini jingine lililojitokeza huko nyuma ni ukarabati wa tags zile zinazovuta na kuongoza meli. Ni kweli zina uchakavu zimetaka kukarabatiwa lakini jinsi zilivyokuwa zinataka kukarabatiwa gati moja kwa Shilingi bilioni 6.6 wakati gharama halisi tag zile zikitengenezwa Mombasa ni Shilingi bilioni 1.6. Inaelekea sasa matengenezo ya meli na hizi tag kwenda Mombasa ndio chaka la watu kuvuta fedha jinsi wanavyotaka.”

Rais Samia ameenda mbali na kuelezea jinsi Mamlaka ya Bandari ilivyoingia katika mikataba ya kutengeneza mifumo mbalimbali, ambapo takribani Shilingi bilioni 12 zilitumika huku mikataba ikisitishwa na mifumo ikiwa haijakamilika na wala haitumiki. Inaonekana kumekuwa na uzembe wa kuweka mifumo inayoacha mianya ambayo inatumika katika upigaji.

“Karibuni hapa nina taarifa kwamba wafanyakazi wamechezea mifumo ile hasa wa sehemu za hesabu kiasi ambacho ukisoma mfumo unaonesha mizigo inayoshushwa imelipiwa na magetini kule wanasoma mizigo imelipiwa na mageti yanaruhusu mizigo kutoka ukweli ni kwamba mizigo haijalipiwa,” anabainisha Rais Samia akielezea jinsi udhaifu wa mifumo unavyotumika katika upigaji.

Rais Samia pia ameelezea jinsi alivyoamua kusimamisha mradi wa ujenzi wa matenki ya mafuta baada ya kuona ulikuwa umetengenezwa katika mazingira ya rushwa huku kukiwa hakuna mahitaji ya lazima, na Serikali ikiwa na matanki mengine kupitia ubia walionao na kampuni ya Puma.

Mikataba yote hii iliyotajwa ina sifa moja inayofanana: ni mikataba ambayo haijawekwa wazi, ilhali, ni mikataba inayohusika na kutoa huduma na bidhaa kwa watanzania.

Mikataba magumashi 

Katika hotuba yake pia Rais Samia anaelezea jinsi Kampuni ya Huduma za Meli ilivyoingia katika mkataba wa Shilingi bilioni 400 na kampuni ya Yutek Gemi İnşa. San. Ltd. Şti ya nchini Uturuki, huku kampuni hiyo ikionekana haina uwezo wowote.

Kwa namna ya kustaajabisha kampuni ya Yutek Gemi İnşa. San. Ltd. Şti iliweza kupata mikataba minne ya ujenzi wa meli. Kwanza, mkataba wa  ujenzi wa meli mpya ya kubeba mizigo bahari ya Hindi wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 55.2. Pili, ujenzi wa meli ya mizigo ziwa Victoria wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 39.5. Tatu mkataba wa kujenga meli ya mizigo na abiria ziwa Tanganyika wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 44.5 na mwisho ujenzi wa meli ya mizigo ziwa Tanganyika wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 42.5.

Unaweza kujiuliza kwa nini hakukua na maswali wakati wa tangazo. Maswali kama vile: imekuwaje kampuni isiyojulikana kupewa mkataba wa zaidi ya Shilingi bilioni 400? Jibu ni moja, mikataba ya manunuzi ya Serikali bado ni siri kati ya watoa huduma na watendaji wa Serikali. Umma haufahamu chochote kuhusiana na mikataba hiyo.

Pamoja na kuwa Rais Samia alishuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo ya ujenzi wa meli, Juni 15, 2021, Mkuu huyo wa nchi anaelezea waliyoyakuta baada ya kuunda timu ya wataalamu kufuatilia kampuni hiyo.

“Katika kumtafuta huyu mkandarasi imegundulika kwamba Yutek haina eneo lake la ujenzi wa meli badala yake imekuwa ikipata zabuni na wao ni madalali wanachukua zabuni wanatafta kampuni nyingine wanawapa kazi , wao ni madalali,” anaelezea Rais Samia, na kuongeza:

“Kampuni hiyo haina fedha, lakini pia iligundulika kwamba mbali na maelezo kuwa kampuni hii ina fedha zinazotosheleza ilibainika kwamba uwezo wake wa kifedha ni mdogo mno kwa sababu mpaka timu inaondoka Uturuki wameshindwa kutoa statement ya fedha.”

Embu fikiria kampuni isiyo na ofisi sahihi ya kazi, isiyo na fedha, inawezaje kushinda tenda ya kujenga meli nne, zaidi ya Shilingi bilioni 400?.

“Lakini jingine ni kwamba wasifu wa kampuni na uwezo wake katika ujenzi ni wa mashaka kwani haipo hata kwenye orodha ya wajenzi wa meli inayotolewa na umoja wa wajenzi wa meli nchini Uturuki,” anabainisha Rais Samia. “Lakini pia haikuwa na wafanyakazi wenye sifa za ujenzi wa meli na wala haina mitambo ya kujenga meli. Hadi sasa kampuni hiyo haijafanya lolote kwenye kazi hii ambayo tulisaini nao mwezi juni mwaka huu.”

Cha kustaajabisha katika yote ni kwamba bodi ya tenda inasema ilifanya ‘due diligence’ juu ya kampuni hii na kujiridhisha. Rais Samia tayari kaagiza kusitiswa kwa mchakato huo wa mkataba kupitia wakili wa serikali na Waziri lakini zaidi ameweza kumuondoa mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli.

Tukio hili la Kampuni ya Huduma za Meli na lile la Mamlaka ya Bandari linafanana sehemu moja: kote mikataba haikuwa wazi kwa umma na hata mwananchi wa kawaida akitaka kuiona hawezi kuiona.

Maendeleo bila kuendelea 

Ni takribani miaka mitatu sasa tangu Serikali izindue mfumo wa manunuzi ya kielectronic, TANEPS, mfumo ambao taasisi zote za umma wanatakiwa kuutumia. Ukifuatilia utagundua kuwa kampuni ya huduma za meli halijaweka chochote kwenye mfumo huu.

Lakini ukiachilia hilo pamoja na mfumo kuwa na sifa zote za kuleta uwazi, kwa kuwa na uwezo wa kuonyesha hatua zote za tenda kuanzia tangazo mpaka mkataba, mfumo huu bado mambo mengi hayaonekani, yanaonekana kwa watendaji wa Serikali na wazabuni.

Huwezi kuona mikataba ya manunuzi, nyaraka unazoweza kuziona ni matangazo ya zabuni na mpango wa manunuzi, ila hatua zingine za manunuzi zimefungwa na nje ya watendaji haiwezekani kuiona.

Ni nini kinafanya mkataba wa uzoaji taka kwenye mitaa yetu isichapishwe kwa uwazi, au mikataba ya ujenzi wa barabara, ni nini haswa kinachofanya mikataba hii ibakie sirini? Haya ni maendeleo bila kuendelea.

Sio rahisi kwa ukubwa wa nchi yetu kuondosha ufisadi katika hali hii. Mikataba kuwa wazi itaongeza ari na chachu kwa watendaji wa Serikali kuepuka vitendo vya ubadhirifu na pia kila mwananchi atageuka kuwa mlinzi mwenye taarifa juu ya namna kodi yake inavyotumika. Serikali iruhusu uchapishaji wa mikataba ya manunuzi.

Tony Alfred K ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tonyalfredk@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *