Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa, alikaribia kuwa mgombea urais wa kwanza kutoka chama cha upinzani kukishinda chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM). Nini ilikuwa siri ya mafanikio yake hata kama hakushinda? Ulikuwa ni uamuzi wake wa kukubali kufanya kazi na chama cha CHADEMA – chama ambacho kwa takribani muongo mmoja nyuma, kilijenga jina lake kwa kuibua ufisadi serikalini na ukimweka mwanasiasa huyo kama ‘Kuhani Mkuu’ wa ufisadi huo.
CHADEMA – kwa kutazama zaidi Realpolitik na kuweka mambo mengine pembeni, iliamua kufanya kazi na Lowassa ikifahamu kwamba itawaudhi baadhi ya wanachama na viongozi wake. Kwa kuchukua hatua hiyo, chama hicho kilimpoteza Dk Wilbrod Slaa, pengine mwanachama aliyeheshimiwa zaidi wa chama hicho wakati huo. Lakini ilikaribia kabisa kushinda kwenye uchaguzi.
Na kwa nini Lowassa alifanya watu wengi waende kupiga kura kumchagua? Ni kwa sababu alionyesha kutokuwa na kisasi dhidi ya wabaya wake wote – wa CCM na upinzani. Alikuwa aina ya mgombea ambaye hakuwa na kundi la watu waliokuwa na wasiwasi naye. Kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi, hata wanaCCM hawakuwa na wasiwasi endapo mgombea wa upinzani angeshinda uchaguzi.
Hiyo ni hadithi moja.
Kuna hadithi ya Raila Odinga kwenye uchaguzi wa mwaka 1997 na Raila Odinga wa mwaka 2002. Mwanzoni, alikuwa mgombea aliyeonekana kushika matamanio ya watu wake wa kabila la Wajaluo wa Kenya. Makabila mengine yakawa yanamwona kama Mjaluo. Alipohamia chama cha KANU – kilichomtesa kwa kumfunga jela kwa miaka nane na kuisumbua familia yake kwa ujumla, Raila akaanza kuonekana mtu tofauti. Ni yeye ndiye aliyewaambia Wakenya kwamba ‘Kibaki Tosha.’ Watu wakastaajabu, Raila ni wa kumwombea kura Mkikuyu? Leo, Raila ndiye pengine mwanasiasa pekee wa Kenya anayeweza kujisifu kuwa amevuka ukabila. Anakubalika karibu maeneo yote ya Kenya.
Barack Obama, kama angetaka, angebaki kuwa mgombea anayesimamia hasira za Waafrika. Nchini Marekani, watu weusi wananyanyaswa na wana hali mbaya kuliko wa rangi nyingine. Wana hasira na uchungu mwingi. Hakufuata mstari huo. Alifuata mstari ambao weusi wasio na msimamo mkali na watu wa rangi nyingi walijiona wako salama kwenye Urais wake. Akawania na kushinda uchaguzi. Ni mfano huohuo naweza kuutumia kwa Nelson Mandela na Afrika Kusini yake.
Unaweza kujenga hoja kwamba Marekani na Afrika Kusini bado zina matatizo yaleyale ya msingi yaliyokuwepo kabla ya ujio wa Obama na Mandela. Naamini kuna mambo katika uongozi yanazidi uwezo wa Rais au kiongozi aliye madarakani katika wakati husika. Kuna mambo yanaingia katika mchezo ambayo yanamzidi mtu mmoja.
Hapa sasa ndipo anapoingia Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa nini Samia ni fursa?
Kila nikimtazama Rais Samia, naona wazi fursa iliyo mbele yetu kama nchi. Nimekuwa mwanahabari hapa Tanzania kwa takribani miaka 17 na ninawafahamu kidogo viongozi wengi waliopo madarakani kwa sasa. Kila nikiwaweka kwenye mizania, naona kuna fursa nzuri ya kusogea mbele kidemokrasia wakati wake kuliko mibadala iliyopo.
Chukulia mfano wa Makamu wa Rais Dk Philip Mpango. Ingia Google na tazama video zake za zamani na utamfahamu ni mtu wa namna gani kisiasa. Mpango ni mchumi wa kiwango cha juu lakini tafsiri yake ya demokrasia na Uliberali haifanani kabisa na Samia. Mungu apishilie mbali, lakini kama kuna tatizo litatokea kwa Samia leo na ikabidi Mpango awe Rais wa Tanzania, labda itajulikana vizuri nilikuwa nasema nini wakati huu.
Naweza kutaja majina mengine mawili matatu lakini kwa sababu tayari Tanzania ina historia ya karibuni ya kuwa na Rais aliyekuwa Makamu Rais kabla, nikaona nitumie mfano ulio karibu na mawazo yenu.
Wanasema It takes two to Tango. Ili Samia acheze huu muziki vizuri, ni muhimu na wachezaji wengine nao wakaingia dancing floor kucheza. Pamoja na matatizo mengine yaliyopo nchini kwa sasa kwenye masuala ya demokrasia na haki za binadamu, kuna hatua ambazo Samia kapiga kusogea mbele na ingepaswa vinara wa upinzani kupiga hatua mbele zaidi ili kukutana naye sehemu.
Kesi na hukumu ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai ole Sabaya ni ishara mojawapo ya Samia kusogea. Kuachiwa kutoka gerezani na kwa watu walioonewa kufutiwa kesi ni ishara ya kusogea. Hatua ya kuruhusu watoto wa kike waliopata mimba ni ishara ya kusogea. Hatua ya Rais Samia kukubali kuhudhuria mkutano wa vyama vya siasa vya upinzani ni ishara mojawapo ya kusogea kwenye dancing floor.
Kinachohitajika ni hatua madhubuti za kisiasa kwenda kumshika mkono na kudensi naye. Kukaa mbali naye wakati tayari ameonyesha kusogea – hata kama hajanyoosha mkono kuonyesha kwamba anataka kudensi, ni jambo lisilotazama mbali. Binafsi, ukiniuliza, nitakwambia katika miezi hii michache madarakani ya Samia tumesogea kwa kiasi kikubwa kwenye utawala wa haki kuliko ilivyokuwa miaka minne nyuma.
Mbowe ni muhimu atoke gerezani
Mgogoro mkubwa wa kisiasa uliopo nchini kwa sasa ni suala la kushikiliwa gerezani kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe. Kama utaniuliza mimi, CHADEMA inatakiwa kufanya jitihada zote kuhakikisha Mbowe anaachiwa huru. Kesi yake, hata kama iko mahakamani kufuata mkondo wa sheria, ni kesi ya kisiasa pia. Kwa maoni yangu, inaweza kabisa kumalizwa kisiasa.
Mbowe ni mtu muhimu ndani ya CHADEMA. Bila yeye, CHADEMA isingevutia vijana kujiunga nacho mwanzoni mwa karne hii. Bila yeye, CHADEMA isingejipambanua kama chama chenye ubunifu na cha kinachoweza kufanya jambo gumu. Bila yeye, pengine CHADEMA isingeweza kupata rasilimali za kutosha kuweza kuendesha shughuli zake. Hakuna mwanasiasa mwingine ndani ya CHADEMA kwa sasa anayeweza kuzungumza mazungumzo nyeti na walio madarakani sasa kumzidi Freeman Mbowe.
Naamini pia kwamba siasa za sasa za Rais Samia ndiyo siasa hasa zinazomfaa Mbowe. Ili Mbowe atoke jela, ni lazima CHADEMA ifanye aina ya siasa ambazo haziwezi kufanywa kwa kukaa mbali na Rais Samia. Napata taabu kuiona CHADEMA inayokua wakati Mbowe akiwa jela.
Na jambo la Mbowe kuwa jela ni la binafsi kwangu. Nimewahi kuwa na rafiki kipenzi aliye jela na ninafahamu machungu ambayo familia, ndugu na jamaa wanapata kwa sababu ya mwenzao kuwa jela. Naamini pia kwamba kwa siasa za Tanzania, hakuna mwanasiasa aliyepanda chati kwa kukaa jela. Kila kitu kina mara ya kwanza lakini ningeogopa kumfanya Mbowe guinea pig wa kuona kama mwanasiasa wa Bongo anaweza kupanda chati kwa kukaa jela muda mrefu. Vipaji na uongozi wake unahitajika zaidi nje ya kuta za jela kuliko ndani.
Zitto, Mbowe na Upinzani
Kama ningekuwa Zitto Kabwe – Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, ningehudhuria mkutano wa Rais Samia na vyama vya siasa. Ningetumia mkutano huo kuzungumza naye mambo ambayo hatuwezi kuzungumza naye kwenye simu na tukamaliza. Ningetumia mkutano huo kumwomba atoe ahadi ya hadharani ambayo hawezi kuivunja mbele ya safari.
Kazi kubwa kuliko zote kwenye siasa ni kuzungumza. Unazungumza wakati wa furaha na unazungumza wakati wa huzuni. Unazungumza wakati wa vita na unazungumza wakati wa amani. Kinachobadilika ni maudhui, aina na namna ya kuzungumza lakini kuzungumza ndiyo mchezo wenyewe.
ACT-Wazalendo tayari kinashirikiana na CCM kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar. Wiki moja iliyopita, Zitto na viongozi wengine wa ACT-Wazalendo walikuwa kwenye mazungumzo na Rais Hussein Mwinyi kule Zanzibar. Dk Mwinyi na Samia wote ni wana CCM na itakuwa ni siasa za hovyo kama ACT-Wazalendo itachagua wanaCCM wa kuzungumza nao na wale wa kutozungumza nao.
Kama ilivyo CHADEMA, ACT-Wazalendo nayo ina ndoto za kuja kuongoza Tanzania siku moja. Na inafahamu kwamba CHADEMA si chama cha kwanza kuwa kikuu cha upinzani hapa Tanzania. TANU na ASP vilikuwa vyama vya upinzani huko nyuma. Kuna wakati NCCR-Mageuzi ndiyo kilikuwa chama kikuu cha upinzani, halafu ikaja TLP na kisha CUF. Zitto anafahamu kwamba kama atacheza karata zake za kisiasa vizuri, ACT-Wazalendo kinaweza kuja kuwa chama kikuu cha upinzani katika miaka ijayo.
Na vipi kama wakati huo ndiyo jahazi la CCM litakuwa limetota na linataka kuzama? Realpolitik inataka ACT-Wazalendo ijitazame yenyewe binafsi na kuona kama kuna upenyo wa chenyewe kuja kuwa kinara wa upinzani hapa Tanzania. Kukutana na Rais Samia kwao ni mojawapo ya njia ya kujenga taswira yao kama chama makini.
Uchambuzi wangu kuhusu siasa za upinzani nchini Tanzania ni kwamba kuna ombwe la kupata mwanasiasa ambaye anayakuna makundi yote yaliyopo nchini kama alivyokuwa Lowassa mwaka 2015. Tatizo kubwa lililopo ni kwamba kwa sasa Watanzania hawajamwona mwanasiasa huyo. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa na wapiga kura wachache na hilo lina tafsiri mbili kwangu – mosi watu hawakuwa wanamuunga mkono aliyekuwa mgombea wa CCM lakini pili hawakuona mbadala wake kwenye upinzani.
Na kuna tatizo kubwa la viongozi wa upinzani kuongozwa na mitandao ya kijamii. Wako viongozi wanashindwa kuchukua hatua ngumu za kiuongozi kwa kuhofia namna watakavyoonekana na wafuasi wao wa mitandaoni. Namna pekee ya kushinda hili ni kwa viongozi wa upinzani kuchukua nafasi yao kama viongozi na kuongoza wafuasi wao hawa wa mitandaoni.
Hili ni kundi kubwa la wafuasi lakini lenyewe linahitaji kuongozwa na si kuongoza vyama au itikadi zao. Kama viongozi wa upinzani wataendelea kuwa mateka wa wafuasi wao wa mitandaoni, safari yao kutaka kuifikisha Tanzania katika nchi ya ahadi itachukua muda mrefu.
Lakini kwa sasa, wakati huu, jambo la kwanza ni kukutana na Rais Samia katikati. Hofu yangu kubwa ni moja tu – kwamba anaweza kuamua kupiga hatua kurudi nyuma. Tutakuwa tumepoteza fursa kubwa ya walau kurudi katika mstari tulioanza kukaa miaka michache iliyopita.
Ezekiel Kamwaga ni mwandishi wa habari ambaye kwa sasa anasoma kuhusu siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha SOAS nchini Uingereza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni ekamwaga57@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.