Dar es Salaam. Mbunge wa Kuteuliwa na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge (Kilimo, Mifugo na Maji) Dk Bashiru Ally anafikiri kwamba kuna hadithi za kufurahisha na kuhuzunisha linapokuja suala la ushirika nchini Tanzania na mchango wake katika kuboresha maslahi na ustawi wa wakulima wadogo.
Dk Bashiru alieleza fikra zake hizo kwenye mada aliyoiwasilisha wakati wa Mkutano Mkuu wa 26 wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) uliofanyika mjini Morogoro kati ya Disemba 6 na Disemba 7 mwaka huu wa 2021.
Kwamba Tanzania ndani ya miaka 60 ya uhuru imefanikisha kuwa na vyuo vikuu vya masuala ya ushirika, kuwa na vyuo vikuu vya masuala ya kilimo na taaluma nyingi zinazoweza kusaidia katika uzalishaji, ni hadithi inayofurahisha kwa mujibu wa mwanazuoni huyo na Katibu Mkuu wa zamani wa chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM).
“[Lakini yanapokuja masuala ya] utegemezi wa mbegu, utegemezi wa mvua, utegemezi wa maarifa na mbinu za uzalishaji ni hadithi isiyofurahisha,” anasema Dk All. “Ukosefu wa soko lisilo la uhakika na linalomnufaisha mkulima ni hadithi isiyofurahisha. Hata masoko yakipatikana mauzo yanakuwa ni ya kuuza malighafi badala ya kuongeza thamani.”
Ifuatayo ni mada hiyo iliyopewa jina la Ushirika na Ustawi wa Wakulima Wadogo ambayo Katibu Mkuu Kiongozi huyo wa zamani aliiwasilisha mbele ya washiriki wa mkutano mkuu huo wa MVIWATA:
Niwapongeze kwa kuendeleza utamaduni wa kujenga mshikamano wa wazalishaji wadogo. Lakini niwatahadharishe, kwa sababu sitasema mambo mengi sana, kwamba fursa kama hizi, au vyombo kama hivi [Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania – MVIWATA] msivione kama vipo tu vina elea elea. Waingereza wanasema don’t take it for granted. Msibweteke. Mlikotoka ni mbali, mlipofika ni mbali na safari bado ni ndefu sana.
Wakati tunawapongeza waasisi na viongozi ambao wote nafurahi na najivuna kwamba nimeona uongozi wao. Mwenyekiti uliopo una kazi ya kudumisha mafanikio ambayo yamekwisha patikana.
Mimi sitasema mengi kwa sababu mengi yamekwisha semwa na mgeni rasmi kusema ukweli. Kwa hiyo, nimekuja hapa kuwasalimu na kukiri upya mbele yenu kwamba mimi ni rafiki wa kudumu wa MVIWATA. Msimamo wangu haujabadilika na hautabadilika, na sio msimamo wangu ni msimamo wa wote wanaoamini katika utu na usawa wa binadamu.
Kwa hiyo, mimi sina hatimiliki ya msimamo huu, na msimamo wa namna hii una gharama zake. Lazima uwe tayari kulipa gharama kwa sababu faida ya kusimamia haya tunayo yasimamia ni kubwa kuliko kusalimu amri. Naomba msisalimu amri kwa wanyonyaji, waporaji wa ardhi, wadhalilishaji hata kwa viongozi ambao wamepewa dhamana lakini hawazitumii kwa uwajibikaji. Msisalimu amri.
Nikiwa kwenye jukwaa la MVIWATA najisikia fahari sana kuliko majukwaa mengi ambayo nimekuwepo. Ndio jukwaa lenye usalama wa uhakika kuliko majukwaa mengine. Sina mashaka kama kuna mtu anaweza kunipiga gwala hapa niliposimama, majukwaa mengine ni mtihani.
Namshukuru Mungu sababu nimekalia majukwaa hayo yote ambayo ni mengi tu. Lakini moja ya majukwaa salama ni jukwaa la MVIWATA. Na kwa kweli hata usalama wa nchi, kwa maana ya usalama wa chakula, kwa maana ya uhuru wa nchi, haupo kama wakulima hawajasimama imara. Baada ya utangulizi huo naomba mniruhusu nikae kwa sababu nazungumza kwa tahadhari nisije ropoka.
Tumekuja hapa na Mwenyekiti wetu wa Kamati ya [Kudumu ya Bunge ya] Kilimo, Maji, Uvuvi na Mifugo, Mama [Christina] Ishengoma [Mbunge wa Viti Maalum – Chama cha Mapinduzi]. Kaalikwa kivyake, kwa nafasi yake na mimi nimealikwa kivyangu kwa nafasi yangu ya [u]rafiki wa MVIWATA lakini kule bungeni yeye ni mkuu wangu.
Nilipoteuliwa na kuapishwa nilikuta utaratibu ambao ni wa kikanuni kwamba lazima kila mbunge awe kwenye kamati na Mheshimiwa Spika [Job Ndugai] alinipa heshima ya kuchagua kamati ninayoitaka. Maana ana mamlaka yeye kikanuni, na kwa mfumo wa uongozi wa Bunge, kumpanga Mbunge kwenye kamati yoyote kulingana na vigezo anavyoona yeye ni muafaka. Kwangu mimi nilivyoomba Kamati hii ya Kilimo, Maji, Uvuvi na Mifugo, alinikubalia.
Kwa hiyo, hoja yangu ya pili, nikiwa bungeni na nikiwa katika Kamati hii ambayo nimeiomba mimi mwenyewe, nitasimamia misingi ya wakulima wadogo na taasisi zenye mtazamo huo, ikiwemo MVIWATA. Mama Ishengoma yupo hapa, pamoja na kwamba tumekuja kuwasikiliza lakini tunawahakikishia kabisa yanayozungumzwa yatafika bungeni.
Nafasi ya ushirika kwenye historia ya Tanzania
Mambo makubwa matatu ya kuzingatia unapojadili mada kama hii [ya Ushirika na Ustawi wa Wakulima Wadogo], la kwanza ni historia. Historia ya nchi yetu, ni historia ya kutawaliwa. Katika Azimio la Arusha, kuna tamko maarufu sana kwamba tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha, sasa tunataka mabadiliko ili tusinyonywe tena, tusidhulumiwe tena, tusinyanyaswe tena, tusipuuzwe tena. Kwa hiyo, historia hii mimi nadhani ndio msingi wa msimamo wa MVIWATA.
Kwa hiyo, jambo lolote mnalolifanya lazima mzingatie historia. Mama Ishengoma amesema hapa miaka 60 baada ya uhuru tunajadili kuhusu ustawi wa wakulima wadogo, tufanye nini kuwastawisha wakulima wadogo. Lakini niwahakikishie katika vitabu vya historia sahihi, harakati za ukombozi wa taifa hili na hata mataifa mengine nje ya Tanzania, kuna damu na jasho la wakulima wadogo.
Kwa hiyo, udogo tunaousema sio udogo wa mawazo. Kwa sababu kama kungekuwepo na udogo wa mawazo tusingepata uhuru. Udogo tunaousema unatokana na aina ya mifumo ya ukandamizaji tunayopambana nayo, na kwamba mifumo hiyo haiwezi ikabomolewa na tukajikomboa kwa mtu mmoja mmoja kwa sababu ya mbinu zake na maguvu yake.
Kwa hiyo, suala la historia kuhusu ushirika na mchango wa ushirika, kuhusu wakulima wadogo na mchango wao kwa kweli ni mapambano ya ukombozi wa nchi yetu kifikra, kimtazamo na kimsimamo.
Kama wakulima wasingekuwa na mshikamano na wavujajasho wengine, hasa wafanyakazi, pengine kazi ya kuikomboa Tanganyika, na hata kazi ya kuiunganisha Tanyanyika na Zanzibar kuwa Tanzania, ama ingechukua muda mrefu kukamilika, ama tungelipa gharama kubwa.
Uhai wa taifa hili, roho ya uchumi wa taifa hili, msingi wake na kiini chake ni wazalishaji wadogo ambao ni wakulima. Lakini si mkulima mmoja mmoja, ni wakulima katika mshikamano wao. Hapo ndipo inapokuja dhana ya ushirika. Kama ulivyo ujamaa, ushirika nao ni imani. Ubepari si imani, unyonyaji si imani. Ni mfumo wa kinyonyaji.
Ushirika ni chombo cha mshikamano wa wanaonyonywa dhidi ya wanyonyaji. Hiyo ndio historia ya ushirika. Kama unyonyaji usingekuwepo, dhulma isingekuwepo, kusingekuwa na haja ya kuwa na ushirika. Kila mmoja angefanya mambo yake akapata haki yake na akaishi. Kwa hiyo, historia ya taifa letu haiwezi ikatenganishwa na historia ya ushirika na mshikamano wa wazalishaji wadogo ikiwemo wakulima.
Historia hiyo ndio imezaa dira yetu. Kwa sababu naanza na historia ya kukutambulisha wewe nani na mazingira yako, mifumo yako ya maisha na kama historia ni ya kinyonyaji na ukandamizaji inapatikana dira sasa ya mapambano ambayo ndio dira ya ukombozi.
Taasisi zote zilizotambulishwa hapa zenye mtazamo huu na MVIWATA, dira yetu, ambayo pia ni imani yetu, ni dira ya ukombozi. Kwa hiyo, kazi ya ukombozi haijakamilika kwa sababu mifumo ya unyojaji na ukandamizaji haijashindwa wala haijabomolewa.
Jambo la tatu ni jihada sasa, kwa sababu historia na dira peke yake havitoshi. Lazima juhudi pia ziwepo. Sasa vyombo vya MVIWATA, ushirika na HakiArdhi [shirika lisilo la kiserikali linalopigania haki ya ardhi ] ndio vinaingia. Kwa sababu hivi ni vyombo vya kuwakusanya na kuhamasisha juhudi za kuendeleza mapambano ya ukombozi.
Kama hauwezi kuweka uwiano kuhusu ufahamu wa historia yako, ukakosa dira ya kukuongoza unakokwenda, hata ungekuwa na juhudi za kupambana na adui hutafanikiwa. Matokeo yake juhudi zikipishana na historia yako zikakosa mwelekeo kwa maana ya dira, mambo mawili yatatokea. Ni kupoteza nguvu bure, unajenga na kunaporomoka. Hali hii ikitokea mnakuwa na mkanganyiko na kulaumiana.
Kwa hiyo, kazi kubwa tulonayo ndugu mgeni rasmi ya kuimarisha vyombo hivi ni kuweka uwiano. Hasa kuwekeza katika kufahamu historia yetu, lakini pia kufuata dira sahihi ya tunakotaka kwenda. Sasa hizi juhudi na ahadi ulizotupa, kazi za Bunge, kazi za Serikali na vyombo vingine ni rahisi uwekezaji wajuhudi hizo kuwa na matokeo bora.
Hadithiza za kufurahisha, kuhuzunisha kuhusu ushirika
Nadhani katika eneo la kilimo bado hatujawa na uwiano huo. Ndio maana historia ya ushirika na ustawi wa wakulima ina pande mbili. Kuna hadithi ya kufurahisha na hadithi ya kuhuzunisha. Mimi nitaanza na hadithi ya kufurahisha ili tusikate tamaa, maana nikianza na hadithi ya kuhuzunisha tutakatishana tamaa na kwenye vita kukatishana tamaa ni dhambi na usaliti.
Hadithi ya kufurahisha ni kwamba MVIWATA ipo na Tanzania ipo na washirika wa MVIWATA wapo. Pili, juhudi za kujenga taifa moja la watu wanaozingatia usawa kwa kiwango fulani baada ya miaka 60 zimefanikiwa kwa sababu nchi bado haijasambaratika. Ni mataifa machache katika [bara la] Afrika ambapo mgeni rasmi anaweza akazungumza lugha inayoeleweka bila mkalimani, ndio sehemu ambapo hata mgeni anachukua muda mfupi sana hata kama anatoka Hispania kujua Kiswahili na kusikiliza ninayosema bila mkalimani.
Nchi yetu ndio nchi ambayo ujumbe unafika bila mkalimani na mtoa mada anaongea mpaka anamaliza bila mkalimani na mjadala ukianza muongoza mjadala anaongoza bila mkalimani na mnajadili na kutawanyika bila mkalimani kwa sababu ya lugha ya taifa.
Hata haya maarifa ambayo ninayojaribu kuyazungumza hapa sipati tabu sana kuyawasilisha kwenu na wakati mwingine mwenyekiti ungepata nafasi ya kukaa, mimi nina uzoefu nitakuwepo hapa siku mbili. Maswali na habari zinazotoka huku [wajumbe wa mkutano] hiko kiti kinachemka.
Kwa hiyo, tumejenga taifa ambalo, mfumo wa kuzalisha na kuwasilisha maarifa, mfumo wa kuwasiliana wakati wa kujadiliana ni mfumo unaotoa sura ya kitaifa. Si jambo dogo, ingawaje kuna baadhi ya wataalamu wetu bado wanakasumba ya kudhani kwamba maarifa lazima yawasilishwe kwa lugha ya kigeni na wengine wanapata shida sana kufanya kazi hiyo. Lakini tulipofikia wengi wanapata aibu kutowasiliana kwa Kiswahili hasa kwenye hafla kama hizi za watu wadogo wadogo. Hiyo nayo ni hadithi njema.
La tatu, yako mabadiliko makubwa kwa kiwango ambacho tulianza safari ya kupata uhuru sekta zote za msingi zinazoweza kusaidia uzalishaji hali yake ni bora zaidi kuliko miaka sitini iliyopita. Kwa mfano, kwenye kilimo na ushirika, tumefikia kama nchi kuwa na vyuo vikuu vya masuala ya ushirika, kuwa na vyuo vikuu vya masuala ya kilimo na taaluma nyingi zinazoweza kusaidia katika uzalishaji. Hapo sijazungumza sekta za miundombinu ya umeme, barabara, elimu, afya na kadhalika. Bado tuna nakisi lakini angalau baada ya miaka 60 kuna hadithi ya kufurahisha ya kusimulia.
Sasa mambo haya kama ushirika na vikundi kama hivi [vikundi vya wakulima wadogo] yakitumiwa vizuri, matatizo ambayo nitayataja na ambayo mgeni rasmi ameyataja kuna dalili ya kuyatatua.
Hadithi isiyofurahisha sasa, uchumi wetu bado ni duni na bado ni tegemezi. Ingawa matatizo hayo mawili yanaweza yakapunguzwa kwa kukuza uzalishaji kwenye kilimo. Hii sio hadithi ya kufurahisha kwa sababu nchi inayotegemea wakulima na wakulima wapo, nchi ya uchumi wa kilimo na wakulima wadogo, inapotokea baada ya miaka 60 bado uchumi wake ni duni na tegemeza basi hapo kuna mushkeli. Ni hadithi isiyofurahisha.
Yamegusiwa matatizo ya kilimo na mimi nitagusia machache kama utegemezi wa mbegu, utegemezi wa mvua, utegemezi wa maarifa na mbinu za uzalishaji ni hadithi isiyofurahisha. Ukosefu wa soko lisilo la uhakika na linalomnufaisha mkulima ni hadithi isiyofurahisha. Hata masoko yakipatikana mauzo yanakuwa ni ya kuuza malighafi badala ya kuongeza thamani.
Uchumi wa kilimo haujatuwezesha kupiga hatua ya uhakika na ya kuridhisha kwenye viwanda. Kwa hiyo, hakuna uhusiano kati ya kilimo na viwanda. Ndio maana pembejeo zote tunazozihitaji, ikiwemo mbolea, tunategemea viwanda vya nje. Hiyo ni hadithi isiyofurahisha.
Kwenye hadithi isiyofurahisha kuna hofu ya wazalishaji wadogo. Hofu ya kwanza kwenye sekta ya aridhi, amegusia mgeni rasmi. Kuzungumzia uhaba wa ardhi kwenye nchi kubwa kama Tanzania ni kuzungumzia tatizo ama watu wana hodhi ardhi bila kuiendeleza ama tuna tatizo la mipango ya matumizi yetu.
Hofu za wakulima wadogo
Kila unapoenda unaona ardhi ni tupu ukilinganisha na ardhi iliyoendelezwa ukiacha mijini. Lakini nenda uguse pale atatokea mwenye aridhi. Kwa hiyo, tumejaza ardhi pori katika nchi na hatujatathimini vya kutosha ili kuweza kupanga ardhi yetu na matumizi yake kwa wanaohitaji na walio tayari kuiendeleza.
Hofu kubwa hiyo sitaki kwenda zaidi kwa sababu ni mjadala wa kila mwaka. Na ukitaka kuchunguza hizo ardhi, yanayoitwa mashamba pori yale ya Serikali, au yale yaliyopimwa ambayo mgeni rasmi alisema yamekodisha, ardhi nyingi iliyolimbikizwa haijapimwa. Hii ni hofu kubwa na ni kazi kwetu kuifanyia kazi.
Hofu ya pili, ni mabadiliko ya tabia ya nchi. Kila mara linapotokea tatizo la mabadiliko ya tabia ya hali ya hewa nchi inayumba kabisa. Chanzo? Mada ipo tutaijadili lakini ni hofu kubwa. Mabadiliko ya tabia ya nchi yanaenda sambamba na usimamizi wa rasilimali zetu za maji. Tumeshindwa hata kuvuna maji hata ya mvua kwa kujenga mabwawa.
Hofu ya tatu ni uongozi na usimamizi duni wa taratibu zetu na taasisi zetu. Nitatoa mfano. Mgeni rasmi katika ofisi yako ya mkoa una sekritarieti lakini mtu anayekushauri kuhusu barabara, Bodi ya Mfuko wa Barabara ni mojawapo. Hii Bodi ya Mfuko wa Barabara ina mtandao wa watendaji katika eneo lake. Hivyo hivyo kwa anayekushauri kuhusu maji. Hivyo hivyo kwa anayekushauri afya, elimu na nishati. Lakini kwenye eneo la uzalishaji ni washauri hewa. Wapo washauri wa mishahara sio washauri wa kazi.
Sasa juhudi zisiporatibiwa kama nilivyozizungumzia. Tumejadili hapa mapendekezo, bajeti zimetengenezwa lakini ule mfumo wa uratibu haushuki chini mpaka kwenye eneo la uzalishaji. Ndio maana wewe [mkuu wa mkoa] ni rahisi kutoa taarifa ni barabara kilometa ngapi zimejengwa na zinazopangwa kujengwa na ambazo hazijajengwa, madarasa mangapi yamejengwa, mangapi yamekamilika na kadhalika. Lakini kwenye kilimo takwimu zilizopo ni za kubumba bumba. Hivyo hivyo kwenye viwanda. Katika ngazi ya mkoa na wilaya. Hivyo hivyo kwenye mifugo. Hivyo hivyo kwenye uvuvi.
Nchi gani ambayo ina uhakika na usalama wake kama eneo la uzalishaji mali uratibu wake na usimamizi wake ni wa kubabaisha? Hii sio hadithi nzuri. Kuna wakati kwenye kamati yetu, sasa sijui ntavunja kanuni labda nitapelekwa kwenye kamati ya maadili sijui, tumelijadili hili mara nyingi tukabaini Wizara ya Kilimo inaweza ikasaidia sana katika mipango mikakati na sera lakini kwenye utekelezaji TAMISEMI ndio yenye watu. Lakini pale TAMISEMI yupo Waziri ana manaibu waziri wawili, mmoja anamsaidia kwenye eneo la afya na mwingine anamsaidia kwenye eneo la elimu na Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Wakuu.
Kwenye eneo la uzalishaji, TAMISEMI haina uratibu wowote ama ngazi ya wizara, ama ngazi ya mkoa au wilaya ambao unaweza ukatekeleza majukumu yake na watu wakakaa kwenye nafasi, sio kupokea mshahara tu bali kufanya kazi. Bado tunajivuta vuta tu.
Kwa hiyo, tatizo kubwa ninaloliona mimi sio ufahamu mdogo wa historia yetu, tunao ufahamu wa kutosha kuliko nchi nyingi. Tunajua tulivyotawaliwa, tunajua utumwa, tunajua mapambano yetu, tunajua namna tulivyoanza ushirika, tunajua tulivyokwama. Historia hiyo tunayo na sitaki kuirudia.
Dira yetu haina mashaka sababu tunasema kilimo ndio uti wa mgongo na ardhi ni mali ya taifa. Yote kisera yako sawa, kwenye eneo la bidii na juhudi tunapoteana. Tusukumeni kurekebisha hilo.
Namaliza kwa hofu ile ile ya kuogopa kuropoka maana mimi nimepewa cheo cha ubalozi sikuhizi. Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni mawili tu. Kwanza, mambo haya ni magumu na utatuzi wake unahitaji tujadiliane mambo makubwa mawili: la kwanza tujadiliane ni kweli hii nchi itaendelezwa na wakulima wadogo wadogo na wavujajasho na tunaafikiana hivyo? Kama tunaafikiana hivyo tunaendaje kufikia malengo hayo?
Kipi kiwe mali ya soko, kipi kiwe mali ya umma
La pili la kujadiliana [ni], hivi kweli kila kitu ni bidhaa ya kupeleka sokoni? Au vipo vitu vyenye thamani kwa wote na hiyo thamani yake sio ya sokoni? Vipo vitu vya sokoni na nitataja baadhi yake hapa. Hivi kweli eneo la utafiti, sayansi na teknolojia ni cha wote ama ni cha wachache?
Tusipojadiliana hivyo isije tukafika mahali mtu akiwa na maarifa au jami ikawekeza akapata maarifa atavumbua mbegu, TARI [Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Kilimo] wakavumbua mbegu bora aiwekee kinga auze yeye au hii ni mali ya umma? Isipokuwa mali ya umma nani atamudu gharama za mbegu hiyo? Bila mbegu bora na za gharama nafuu kuna kilimo? Tunalo tatizo tunahitaji kulijadili kutenganisha mambo ambayo ni ya wote na mambo ya sokoni.
Hivi ardhi ikiwa na bei na inapanda bei kwa nguvu za soko kuna mtu atamudu ardhi hapa? Hata trekta kama unataka kuwabadilisha watu kutoka kwenye jembe la mkono kutumia teknolojia ya kisasa. Huo utaratibu uwe wa wote au kila mtu kivyake? Mijadala ni muhimu sana, mijadala ya kuuliza maswali ambayo wakati mwingine yana kera.
Zipo dalili kwamba tusipokuwa makini, ardhi inaelekea kuwa bidhaa kama ilivyo shati na kofia. Nimeambiwa hata mabadiliko ya tabia ya nchi kuna biashara inaweza ikafanyika ili kupambana na tatizo hilo.
Nimeambiwa hata mabadiliko ya tabia ya nchi wakulima wanaambiwa wanaweza wakalima mahindi yenye kusaidia mabadiliko ya tabia ya nchi na sio njaa ya tumboni. Iko mijadala hiyo. Je, sisi tupo upande gani katika msukumo mkubwa wa kubidhaisha kila kitu? Kuwa na jamii inayohusudu soko badala kuwa na jamii inayotumia soko katika maendeleo. Soko huria au soko kwa maendeleo?
Twende pamoja au mmoja mmoja?
Tunaweza tukafanya majaribio katika baadhi ya maeneo, lakini yako maeneo ndugu mgeni rasmi ambayo sote lazima tuwe na hati miliki kwa pamoja katika maeneo hayo. Kilimo chetu tunaweza kukinusuru au kukikuza tukikubaliana katika eneo hilo. Mbolea ikipanda ni tatizo la mkulima mmoja mmoja au ni tatizo la kitaifa? Tukikubaliana hivyo tunatafuta suluhu ya kitaifa.
Kutokujitegemea kwenye mbegu, ambako hakuna tofauti na utumwa kwa wenye maarifa ya kuzalisha mbegu, ni suala la mtu mmoja mmoja au ni suala la kitaifa? Kubadilisha uzalishaji wetu ili uwe na tija, kutoka kutumia zana duni kwenda kutumia zana za kisasa, ni suala la mtu mmoja mmoja au ni suala la kitaifa? Kusimamia ardhi kwa haki ili wote tuweze kunufaika na rasilimali ambayo imeumbwa na Mungu ni suala la mtu mmoja mmoja kwa nguvu zake au ni suala la kitaifa?
Kuwa na miundombinu ya umwagiliaji iliyotengenezwa kwa nguvu za pamoja kama ambavyo tulivyotengeneza barabara, shule na zahanati, tukawa na mabwawa yaliyotengenezwa kwa matumizi ya pamoja wakulima na wafugaji hilo ni suala la sekta binafsi au ni la wote? Kusimamia haki katika vipimo baada ya kuzalisha ili haki na bei ipatikane kwa vipimio sahihi ni jambo la kusimamiwa na mtu binafsi au ni jambo la kusimamiwa kwa pamoja? Hiyo ndio maana ya ushirika.
Ushirika ni chombo cha kuingoza jamii isipotee kuelekea kwenye kuhusudu soko, badala yake kutumia soko kunusuru wazalishaji. Ushirika utakuwa ni chombo cha kutusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Ushirika utatusaidia kukabiliana na unyonyaji katika masoko.
Ushirika utatusaidia kuongeza tija katika uzalishaji. Ushirika utatusaidia kuongeza mapato ya Serikali ambayo yatawezesha Serikali kuwekeza katika kujenga miundombinu ya kilimo. Ushirika utatusaidia katika kukusanya rasilimali fedha ili kuwakopesha wakulima wadogo wadogo kwa riba nafuu ili waweze kulipa na wapate ziada ya kuwawezesha kuendesha maisha yao. Ushirika ni suluhu ya matatizo mengi ya uchumi ikiwemo umasikini na ajira.
Tukienda mmoja mmoja wapo watakaofika na wapo wengi watakaobaki nyuma. Watakaobaki nyuma hawatakubali kuachwa kwa sababu hizo ni mbiu za kufa na kupona. Kwa hiyo, suala la kuwaacha wakulima wadogo waamue ni namna gani ya kupata mbegu bora mmoja mmoja, namna gani ya kupata ardhi nzuri mmoja mmoja, namna gani ya kupata mikopo mmoja mmoja, namna gani ya kuzuia ukame na kutunza mazingira mmoja mmoja hizo ni ndoto za mchana.
Yapo mambo ya kufanya mmoja mmoja na yapo mambo ya kufanya kwa pamoja. Eneo la uzalishaji kupitia wakulima na wazalishaji wengine wadogo wadogo ni suala la kuwaweka wazalishaji pamoja. Hiyo ndio kazi ya MVIWATA ambayo iko mbele yetu na lazima tuifanye.
Mwisho, lakini si kwa umuhimu, niwapongeze kwa kuanzisha radio. Nilipokuwa nakuja hapa wakati nazungumza nilimwambia Mkurugenzi wa MVIWATA hutakuwa na maana yoyote kama radio [MVIWATA FM] haitaanza kusikika.
Namshukuru Mungu wakati huo nilikuwa katika nafasi ya kutoa maagizo yatakayopokelewa kwa lugha ya ndio mkuu neno ambalo lilikuwa linanikera sana. Katika mambo ambayo nafurahi kuachana nayo ni hilo la kumweleza mwenzako halafu anasema nimekusikia mkuu. Nawapongezeni sana kwa kuwa na chombo hiko. Sasa kumbe mnaweza, sasa nawaachia jukumu jingine maana mkiachiwa kazi mnaweza.
Mambo matatu ya kufanyiwa kazi
Nawaachia mambo matatu makubwa. La kwanza, tafuteni kila namna ya kuhangaika kutafuta vyanzo vya mitaji kwa wakulima wadogo. Tunayo Benki ya Kilimo ya kitaifa ipo chini ya kamati yetu tunaendelea kuomba Serikali iongeze pesa, lakini zipo mbinu nyingi za kitaalamu tukihangaika kutengeneza vyanzo ambavyo mkulima anaweza kukopa, akanunua mbegu, akanunua trekta au jembe la kukokota, halafu akazalisha alafu akaweza kulipa.
Si lazima muanzishe mfuko wa MVIWATA lakini mnaweza mkatafuta mawazo. Maeneo mengine wakulima kwenye harakati zao nyingi wana mabenki yao. Hili hamjalifanya kama mlivyofanya vizuri kwenye suala la masoko na radio mmefanya vizuri. Kwenye eneo la mitaji usiokuwa msalaba kwa mkulima mdogo, usio mfilisi mkulima mdogo, unaomwezesha mkulima kununua mashine akakamua alizeti yake, huko bado tuko nyuma sana kitaifa lakini pia kwenye ushirika tupo nyuma.
Kulikuwa na wazo la kuwa na Benki ya Ushirika limekufa. Kuna orodha ya mabenki utitiri lakini hakuna benki ya ushirika. Huko nyuma kihistoria tumewahi kuwa na benki ya ushirika. Inawezekana mwenyekiti, mbona tumeweza vitu vingi. Kikwazo kikubwa hicho cha mtaji na mitaji ya hawa wazalishaji wadogo ni namna ya kutengeneza mfumo mzuri wa uhakika na wa kisasa unaotekelezeka watu wakaweza kupata mkopo. Iwe ni Benki ya Kilimo hiyo kiserikali ambayo tunaweza tukasukuma ambapo haitoshi na vyanzo vingine ambavyo msingi wake ni kuwahudumia wazalishaji wadogo
La pili, tafuteni mawazo ya kuongeza thamani ya mazao yote tunayoyazalisha. Yako maeneo tumeanza kuona mabadiliko. Kwenye mchele kuna mabadiliko kwa sababu viwanda vya kusindika sindika vipo kila mahala. Kwenye alizeti kuna mabadiliko, na nimeona kwenye maonesho yenu mmejitahidi kuongeza thamani, lakini bado ni kwa kiwango cha chini sana, tupange tuongeza uwezo wa kusindika mazao yetu.
Kule Kahama kwenye chama cha ushirika cha Kahama wamejiunga wakatafuta masoko, wakaongeza na thamani kidogo imesaidia kuchangamsha soko na bei. La tatu ni hili ambao mlifanya vizuri eneo la masoko bado ni tatizo.
Kwa hiyo, haya ninayoyasema kisera yako sawa kabisa, wizarani yapo sawa kabisa, ukienda kwa mkuu wa mkoa yapo sawa. Lakini ule utekelezaji unahitaji msukumo wenu [wakulima wadogo].