Mabishano makali yalitokea siku za hivi karibuni katika mtandao wa kijamii wa Twitter, hususan kati ya viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani vya ACT-Wazalendo na CHADEMA vilivyopishana misimamo kuhusu njia sahihi ya kupigania demokrasia na kumuokoa Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ambaye ameendelea kusota mahabusu akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi na uhujumu uchumi.
Kiini cha mabishano hayo ni mkutano uliokuwa umeitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji (Mstaafu) Francis Mutungi ambapo wadau mbalimbali, vikiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini, Jeshi la Polisi pamoja na wadau wengine walialikwa kwenda Dodoma kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini kutoka Desemba 16 mpaka Disema 17.
Angalau vyama viwili vya upinzani vya CHADEMA na NCCR-Mageuzi vilitangaza kususia mkutano huo huku vikitoa sababu mbalimbali, moja ikiwa ni ile kwamba CHADEMA, kwa mfano, haiwezi kushiriki mkutano huo huku Mwenyekiti wake Mbowe akiwa bado yuko rumande. ACT-Wazalendo, kwa upande wao, waliamua kushiriki, wakisema majadiliano ni mchakato muhimu wa kuchochea demokrasia na maridhiano katika nchi.
Kiini cha mnyukano
Hali hii ya baadhi ya vyama vya upinzani kususia mkutano huu na vingine kushiriki ilikuwa ni msukumo wa kwanza wa minyukano ambayo ingefuata baina ya viongozi na wafuasi wa vyama husika lakini hata na wachambuzi huru na wanaharakati wa haki za kisiasa na kijamii. Mnyukano huu, hata hivyo, ulichagizwa zaidi na salamu alizotoa Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Zitto Kabwe, ambaye pia ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Katika salamu zake hizo, Zitto alimueleza Rais Samia kwamba mmoja wa viongozi wa upinzani, Freeman Mbowe, hakuwepo katika hafla hiyo kwa kile Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) alichokiita “changamoto za kisheria” na kumuomba Mkuu huyo wa Nchi asaidie Mbowe kutoka “kwa kufuata taratibu zote za kisheria.” Katika majibu yake, Rais Samia alisema kwamba “heshima ya mtu inakuja kwa kuheshimu sheria,” akibainisha kwamba Mbowe anaweza akawa amevunja sheria. Hata hivyo, Samia alisema “kusameheana nako kupo.”
Viongozi, wanachama na wafuasi wengi wa CHADEMA hawakufurahishwa na kauli hii, na wengi katika ukosoaji wao walimtupia lawama Zitto Kabwe, wakimshutumu kumuombea msamaha Mbowe, kitu ambacho Zitto mwenyewe na viongozi, wanachama na wafuasi wengine wa ACT-Wazalendo walikikanusha vikali na kutengeneza mazingira ya myukano wa maneno uliodumu kwa takriban siku tatu mfululizo.
Matumizi ya lugha za matusi
Lakini katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, mnyukano huu wa maneno kati ya makada wa ACT-Wazalendo na CHADEMA uligubikwa na ukosefu mkubwa wa ustaarabu, huku nafasi ya ushawishi wa nguvu za hoja ikichukuliwa na kauli za kibaguzi, matusi, kashfa, na kudhalilishana.
Baadhi ya makada wa CHADEMA walitumia lugha chafu na zisizo za kiungwana dhidi ya wale waliokuwa wakiutetea uamuzi wa ACT-Wazalendo kushiriki mkutano huo, wengine wakienda mbali zaidi kuwaita watu hao “wajinga,” “wanaojipendekeza,” “mashoga” na kauli zingine zilizokosa utu na heshima. Kwa upande wao, baadhi ya makada wa ACT-Wazalendo walijibu mapigo kwa kuwaita wenzao “wasema ovyo” na “waliojawa na chuki.”
Demokrasia ni jukwaa au gulio la mawazo huru yanayotolewa na wadau tofauti yakishindanishwa ili kupata mawazo bora. Ubora wa mawazo unatambulika katika mahakama ya maoni ya umma, au the court of public opinion kama inavyojulikana kwa kimombo, kupitia chaguzi, kura za maoni, vyombo vya habari na kadhalika. Lakini, wote tunakubaliana kuwa ili mijadala ilete tija, lazima iwe huru na ya kistaarabu. Hili, kwa mtazamo wangu, lilikosekana kwenye mjadala wa hivi karibuni.
Hali hii ya ukosefu wa ustaarabu katika midahalo ya kisiasa ni dalili ya ukosefu wa ufahamu mpana juu ya demokrasia na uhuru wa kujieleza. Katiba ya Tanzania, Ibara ya 18, inatoa uhuru kwa kila mtu kuwa na maoni yoyote na kutoa mawazo yake. Ibara hii inatoa uhuru wa kutoa maoni lakini pia haiweki sharti maoni hayo yawe sahihi. Bahati mbaya, baadhi ya watu wanaamini usahihi wa mawazo yao kiasi kwamba wanadhani wengine hawawezi kuwa sahihi. Watu hao wanaojiona wapo sahihi muda wote wanadhani wana haki ya kuwanyamazisha wengine wenye maoni tofauti.
Ukiliangalia suala hili kimantiki, katika gulio la fikra, haiwezekani maoni yote yakawa sahihi. Lakini, uwepo wa maoni mengi, yenye mitazamo tofauti na yanayokinzana kunasaidia mchakato mzima wa kushindanisha hoja ili kupata mawazo bora zaidi.
Sababu za kihistoria
Jambo jingine linalochangia lugha chafu za matusi, zenye ukakasi na kudhalilishana, hususan kwa vyama hivi viwili vya CHADEMA na ACT-Wazalendo ni historia ambapo tangu Zitto afukuzwe CHADEMA kwa tuhuma za usaliti, amekuwa anatazamwa na chama chake hicho cha zamani kwa wasiwasi na kukosa imani naye.
Baadhi ya wana CHADEMA hawajaweza kumsamehe mwanachama mwenzao huyo wa zamani. Matokeo yake, kila misuguano inapotokea huamsha hisia za chuki za zamani. Ili kuvuka kikwazo hiki, lazima vyama hivi vikumbatie ule msemo usemao, yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Hali hii ya matumizi ya lugha chafu na zisizo za kistaarabu ina athari kubwa katika suala zima la umuhimu wa kutofautiana na kuvumiliana kwenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Kwanza, hali hii inashusha thamani ya mijadala muhimu kuhusu maendeleo ya nchi, hususan katika majukwaa ya mitandao ya kijamii, ambayo tunaitegemea katika ujenzi wa siasa za ushindani.
Sio siri kuwa katika zama hizi ambapo muamko wa ushiriki katika siasa uko chini dunia nzima, mitandao ya kijamiii ni muhimu sana. Mitandao ya kijamii ndio njia pekee madhubuti inayoweza kuwavuta vijana wapende kufuatilia siasa na waelewe uhusiano wake na ustawi wao binafsi na jamii kwa ujumla.
Mfano wa nyakati ambapo majukwaa ya mitandao ya kijamii ilileta tija ni kipindi Serikali ilipoanzisha tozo katika miamala ya fedha ya simu za mkononi ambapo watu wengi walipata uelewa na kuhamasika kupitia elimu, midahalo, utani na vibonzo. Nani pia hajui hamasa iliyojengeka kuhusu madai ya Katiba Mpya kupitia majukwaa haya? Tunaamini kuwa hali itazidi kuwa bora zaidi kadri watumiaji wa vifaa vya kisasa vya teknolojia za mawasiliano wanavyoongezeka.
Mafanikio haya yanaweza yasisambae kwa kasi inayotarajiwa, iwapo lugha chafu na matusi vitazidi kushamiri na kuifanya jamii ipoteze imani na wanasiasa na wanaharakati wa kidemokrasia. Hivyo basi, ili midahalo ya kisiasa izidi kustawi, lazima mitandao iwe salama kutokana na matusi na lugha chafu zisizo na staha, vinginevyo tusilaumu watu wakikimbia na kuacha sio tu kuchangia bali hata kusoma. Katika zama hizi ambapo vifaa vya teknolojia za mawasiliano vimeenea hadi kwa watoto, ni hatari zaidi mitandao kujaa matusi na lugha chafu.
Matusi na lugha chafu vina athari kubwa kwa demokrasia ya vyama vyenyewe. Mrejesho wa lugha za matusi dhidi ya waliofikiri kwa namna tofauti unamfanya hata mwanachama aogope kutoa maoni yaliyo kinyume na viongozi kwa hofu ya kuitwa msaliti, kutukanwa na kudhalilishwa utu wake.
Jukumu la vyama vya siasa
Niseme kwamba vyama vyenyewe vya siasa vina nafasi na jukumu kubwa katika kuhimiza matumizi mazuri ya majukwaa ya midahalo ya kisiasa sio tu mitandaoni bali hata katika mikutano ya ana kwa ana. Vyama vinaweza kuchukua hatua kadhaa za makusudi katika hili.
Kwanza, vyama vya siasa vinaweza kukemea tabia hii, kwa umoja wao, hadharani na bila kupepesa macho popote pale inapojitokeza. Wanasiasa wawafunze watu wao tabia ya uvumilivu wa kisiasa. Wakati mwingine si lazima kukubaliana. Ukiacha ukweli kwamba Mwenyezi Mungu amempa kila mtu upeo tofauti wa kufikiri, uzoefu wetu wa maisha ambao unachangia ujenzi wa mitazamo yetu pia ni tofauti, hivyo, si jambo la ajabu kutofautiana maoni ya kisiasa.
Viongozi wenyewe wa vyama vya siasa wanaweza pia kuonesha mfano kwa wafuasi wao kwa kufanya midahalo ya kuheshimiana, hata pale ambapo wanatofautiana sana kifikra na maono.
Hapa napenda kuwapongeza Zitto Kabwe na Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, ambao wamekosoana sana na kwa lugha yenye hisia kali katika suala hili la mkutano wa wadau wa vyama vya siasa lakini bila kutukanana. Hata walipopigana ‘spana’ kali, kama wanavyopenda kusema wenyewe, hawakuacha kuitana ‘brother.’
Mwisho katika suala la CHADEMA na ACT-Wazalendo, najua kuwa wengi tungependa kuona ushirikiano wa vyama hivi katika kupigania demokrasia lakini ujenzi wa siasa za kistaarabu katika midahalo na majadiliano ni muhimu zaidi na ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele.
Kama vyama haviwezi kushirikiana, visihasimiane walau!
Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.
2 responses
Kazi nzuri sana.
Kazi nzuri sana