The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tutathmini Utendaji Kazi wa Baraza la Mawaziri la Rais Samia

Uchambuzi huu unafanyika kwa kutoa alama maalumu kwa mawaziri wote. Alama A itamaanisha aliyefanya vizuri sana. B vizuri. C ikimaanisha kawaida. D ikiwa isiyoridhisha na F ikimaanisha mbaya.

subscribe to our newsletter!

Katika nchi zilizoendelea duniani, mojawapo ya utamaduni uliozoeleka ni ule wa kutumia mwisho wa mwaka kufanya tathmini ya utendaji wa Baraza la Mawaziri – kuanzia kwa Rais mwenyewe hadi kwa mawaziri wake aliowateua kushika nyadhifa zao. Kwa wenzetu, uchambuzi wa namna hii husubiriwa kwa hamu kwa sababu walau hutoa picha ya namna gani Serikali zao hufanya kazi.

Nimewahi kufanya uchambuzi wa namna hii katika gazeti la Raia Mwema miaka kadhaa nyuma, lakini mara hii nimeamua kufanya hivi kupitia The Chanzo kwa sababu natamani pia wasomaji wa njia ya mtandao nao wapate vitu ambavyo kwa muda mrefu vilikuwa vinapatikana kwenye magazeti pekee.

Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani Machi 2021 na hivyo Serikali yake bado haijatimiza mwaka mmoja madarakani. Hata hivyo, uchambuzi wa namna ninaotaka kuufanya hufanyika mwanzoni mwa mwaka na hivyo hautaweza kusubiri hadi Machi mwaka huu. Msingi wa hili ni kwamba kulikuwa na Baraza la Mawaziri kuanzia Januari hadi Machi wakati Rais Samia alipoingia madarakani na hivyo utaratibu utaendelea kama kawaida.

Uchambuzi huu utafanyika kwa kutoa alama maalumu kwa mawaziri wote. Alama A itamaanisha aliyefanya vizuri sana. B vizuri. C ikimaanisha kawaida. D ikiwa isiyoridhisha na F ikimaanisha mbaya.

Uchambuzi huu pia utafanyika kwa masharti mawili – utazingatia utendaji katika wizara walizopewa wakati wa Rais Samia na pia utazingatia pia wale waliotumikia nafasi zao kwa walau miezi sita ya kwanza ya Rais Samia. Kwa sababu hiyo, mawaziri wanne: Dk Ashatu Kijaji (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari); January Makamba (Nishati); Dk Stergomena Tax (Ulinzi) na Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Ujenzi na Uchukuzi), hawatahusika katika uchambuzi huu.

Rais Samia

Rais Samia alirithi madaraka ya uongozi wa Tanzania kukiwa na mitihani mikubwa mitano: kuipitisha nchi katika wakati wa mpito ikibaki salama; kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19; kuimarisha uchumi ulioathiriwa na ugonjwa wa UVIKO-19; kuirejesha Tanzania katika jumuiya ya kimataifa; na kurejesha utawala unaozingatia demokrasia ya vyama vingi.

Mtangulizi wa Samia, hayati John Magufuli, alitambulika kwa msimamo wake wa kukana athari hasi za UVIKO-19, kutojali masuala ya demokrasia na haki za binadamu na kuangalia zaidi ndani kuliko kujiimarisha kimataifa.

Tanzania sasa inatoa takwimu za UVIKO-19 kiasi cha Jumuiya ya Kimataifa kuanza kuunga mkono juhudi za kupambana na ugonjwa huo hapa nchini. Rais Samia ameanza kurejesha heshima ya Tanzania katika medani ya kimataifa, ameipitisha Tanzania salama katika wakati wa mpito na angalau uhuru wa kujieleza na kufanya shughuli za kisiasa umeanza kurejea nchini.

Kitendo cha kukamatwa na kuwekwa gerezani kwa Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe ndiyo doa pekee la Rais Samia katika utawala wake kwa kuzingatia changamoto alizozikuta. Ninampa alama A kwa sababu ya hatua nyingine za kidemokrasia, uhusiano wa kimataifa na ulinzi na usalama wa nchi.

Makamu wa Rais Mpango

Nafasi ya Makamu wa Rais nchini Tanzania ni nafasi ambayo kwa kawaida inamtaka mtu asiye na tamaa ya kumzidi bosi wake. Ni nafasi ya utulivu ambayo majukumu yake makubwa ni masuala ya Muungano na Mazingira.

Katika utawala wa Rais Samia, malalamiko kutoka Zanzibar kuhusu Muungano yamepungua. Tanzania imerejea rasmi katika mazungumzo ya mazingira duniani na ilishiriki ipasavyo katika Mkutano wa Dunia wa Mazingira uliofanyika Glasgow, Scotland mwaka 2021.

Ninampa Makamu wa Rais Dk Philip Mpango alama A.

Waziri Mkuu Majaliwa

Baada ya kuondolewa kwa TAMISEMI katika Ofisi ya Waziri Mkuu, majukumu na ukuu wa ofisi hii yamepungua kulinganisha na ilivyokuwa katika utawala wa awamu za tatu na nne (wakati wa Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete).

Bunge la sasa, kutokana na mazingira ya uchaguzi wa mwaka 2020, limepoteza msisimko na ladha iliyokuwepo kwenye mabunge ya awamu ya tatu na nne. Kwa baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, Bunge la sasa limepoteza mvuto kuliko hata lile la wakati wa utawala wa chama kimoja cha siasa.

Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana ingawa takwimu za kuongezeka kwa uwekezaji zimeanza kupanda tena. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anapaswa kutafuta eneo moja la kazi ambalo anaweza kutengeneza hiba (legacy) yake kama Waziri Mkuu.

Frederick Sumaye alisimamia ujenzi wa madawati kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Edward Lowassa akasimamia ujenzi wa shule za kata. Edward Sokoine atakumbukwa kwa kupambana na walanguzi na mafisadi na Rashid Kawawa kwa usimamizi wa Vijiji vya Ujamaa.

Kwa upande wake, Majaliwa yuko kila mahali lakini hana pa kushika. Ninampa alama C.

Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba

Wengi hawakutarajia wakati Rais Samia alipomtangaza Mwigulu kuwa Waziri wa Fedha. Kihistoria, nafasi ya Waziri wa Fedha imekuwa ikipewa mtu ambaye inaaminika kuwa ni mtu wa karibu/anayeaminika na Rais, mwenye kundi fulani la wafuasi ndani ya CCM au serikalini na mwenye maarifa ya uchumi. Ingawa kitaaluma Mwigulu ni mchumi, hakuonekana kuwa na sifa kubwa mbili za kwanza.

Katika wakati ambao amekuwa waziri, Mwigulu amefanikisha Tanzania kuanza kupata mikopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia. Amepandisha mapato ya Serikali na kuibua vyanzo vipya vya mapato – tozo; ambazo ingawa hazikupokewa vema na sehemu ya jamii ya Watanzania, lakini angalau waziri alikuja na mbinu ya kuongeza mapato ya Serikali.

Bado Serikali ina kazi kubwa ya kuongeza mapato zaidi na kutanua uchumi wake na hizo ndizo changamoto zijazo kwa Mwigulu. Ninampa alama A.

Waziri wa Mambo ya Nje Mulamula

Mwanadiplomasia mbobezi Liberata Mulamula aliteuliwa na Samia kuchukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi aliyehamishiwa katika Wizara ya Sheria na Katiba. Uteuzi wake uliashiria moja kwa moja lengo la Serikali ya awamu ya sita kuona masuala ya uhusiano wa kimataifa yanafanywa na watu wenye taaluma hiyo.

Mojawapo ya hiba za utawala wa Magufuli ilikuwa ni kuamini kwamba kazi za uhusiano wa kimataifa zinaweza kufanywa hata na watu wasio na taaluma hiyo. Uteuzi wa Mulamula ulifuatiwa pia na uteuzi wa mabalozi na wakurugenzi wa masuala ya kidiplomasia waliolelewa na kukulia na Wizara ya Mambo ya Nje.

Matokeo yake ni kwamba, taratibu, Tanzania imeanza kurejea katika duru za kimataifa na sasa mabalozi wetu katika nchi mbalimbali wameanza kuonyesha kwa vitendo nini hasa wanafanya.

Balozi Mulamula anapata alama B kwa sababu tu wizara yake, kama ilivyo ile ya ulinzi, huwa inachukuliwa kuwa ni ya Rais pia na hivyo mafanikio yake yanafanikishwa pia na Rais aliye madarakani.

Kama angeibuka na wazo la kipekee, kama la tozo kwenye wizara ya fedha, angeweza kupata alama A kama Mwigulu.

Waziri wa Kilimo Adolph Mkenda

Hii ni mara ya kwanza kwa Profesa Adolph Mkenda kuingia katika Baraza la Mawaziri baada ya muda mrefu wa kutumika kama Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na baadaye kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Ameonyesha mawazo mazuri katika masuala ya kukuza kilimo, akiwekeza nguvu zaidi katika uzalishaji wa ndani kiasi cha kuwa na msimamo kuhusu sukari uliowahi kukemewa hadharani na Rais Samia.

Hata hivyo, ni vizuri kuwa na Waziri wa Kilimo anayejua anachotaka na anayeamini katika uwezo wa wakulima wa taifa lake kukidhi mahitaji ya nchi. Ninampa alama B+.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mkumbo

Rais Magufuli alimteua Profesa Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji) katika baraza lake la kwanza la mawaziri lakini Samia alimhamishia katika wizara hii mpya katika mabadiliko ya kwanza ya Baraza la Mawaziri aliyoyafanya.

Katika wakati wake, Kitila amefanikiwa kukwamua mradi wa ujenzi wa eneo la biashara na lojistiki Kurasini ulioonekana kukwama kwa muda mrefu. Mradi huo unatarajiwa kuzinduliwa Februari mwaka huu na Rais Samia na unatajwa kama mradi mkubwa zaidi wa kwanza atakaozindua wakati wa urais wake.

Kitila pia alianza uwaziri katika wakati ambapo biashara na wafanyabiashara walikuwa na malalamiko mengi kuhusu masuala ya kubambikiwa kodi na kesi na sasa malalamiko ya namna hiyo yanaonekana kupungua.

Kama mradi wa Kurasini ukianza rasmi na malalamiko makubwa ya wafanyabiashara yakimalizika kabisa, anaweza kupata A katika miaka ijayo, lakini kwa sasa ninampa alama B+.

Waziri wa TAMISEMI Ummy Mwalimu

Ummy anaonekana kama mmoja wa wanasiasa nyota wa kike katika utawala wa Rais Samia. Eneo lake la kazi ni pana na lenye changamoto nyingi, kuanzia elimu, masoko, masuala ya halmashauri na miji na utawala wa wananchi kwa ujumla.

Kazi kubwa ya Waziri wa Tamisemi ni usimamizi na Ummy amekuwa akionekana katika maeneo mengi kusimamia matumizi ya umma.

Katika nchi masikini kama Tanzania yenye changamoto kubwa ya rasilimali, ni vigumu kwa waziri wa Tamisemi kupata alama A. Akitaka, Ummy anaweza kutafuta eneo moja au mawili ya kuyafanyia kazi ili kuongeza wajihi wake kisiasa.

Labda anatakiwa kuonekana mkali zaidi, kwa mantiki hiyo, ninampatia alama B-.

Waziri wa Afya Dorothy Gwajima 

Dk Gwajima alijijengea umaarufu serikalini akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ambako alisifika kwa usimamizi mzuri wa rasilimali za umma. Hata hivyo, wajihi wake kisiasa ulivurugika wakati wa utawala wa Rais Magufuli ambako alikuwa alama ya ukaidi wa Serikali kwenye kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19.

Katika utawala wa Samia, Gwajima amebadilika na amekuwa sehemu ya mafanikio mapya ya Serikali katika kupambana na UVIKO-19. Hata hivyo, sifa yake kama mtu aliyekana hadharani kuhusu athari hasi za ugonjwa huo hatari imebaki vichwani mwa watU na si mwanasiasa anayeaminika tena.

Katika Serikali yoyote, na katika mazingira ya sasa ya uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa au taharuki ya kiafya wakati wowote, ni hatari kuwa na waziri wa afya ambaye jamii yake haimwamini.

Nafikiri Dk Gwajima ni mtu mzuri na kusema kweli kama ningekuwa Rais Samia pengine ningependa kubaki naye kwenye Baraza la Mawaziri kwa sababu kila Rais anahitaji waziri mmoja anayejua yuko tayari kufa naye – ambavyo ndivyo Dk Gwajima alivyo.

Hata hivyo, katika muktadha wa uchambuzi huu, nashindwa kumwonea huruma, nampa alama D.

Waziri wa Madini Dotto Biteko

Kwa takribani miaka mitatu mfululizo, sekta ya madini imekuwa kinara wa kuingiza mapato ya fedha za kigeni kuliko sekta nyingine zote. Ongezeko hilo limekwenda sambamba na ongezeko la wastani wa mchango wa wachimbaji wadogo kwenye sekta hiyo.

Wakati Biteko akipewa nafasi hiyo na Magufuli, wachimbaji wadogo walikuwa katika mivutano ya mara kwa mara na kampuni kubwa za uchimbaji madini lakini sasa, kwa sababu ya ongezeko la masoko ya madini na kuachia fursa kwa wachimbaji wadogo, hali kwenye sekta imeanza kubadilika.

Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Samia alitia saini makubaliano ya uchimbaji madini wa kampuni kubwa katika maeneo matatu tofauti, uwekezaji wa kwanza mkubwa katika madini katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Kwa kasi hii, na kama bei za dhahabu na madini mengine zitaendelea kukua katika Soko la Dunia, huenda mchango wa sekta ya madini unaweza kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa kabla ya mwaka 2026 kama Mpango wa Maendeleo wa Taifa unavyoelekeza.

Nampa Biteko alama A.

Waziri wa Utawala Bora Mohamed Mchengerwa

Hili ni ingizo jipya katika Baraza la Mawaziri na Mchengerwa amekuwa mmoja wa mawaziri wanaoonekana sana katika vyombo vya habari wakitoa matamshi mbalimbali kuhusu masuala ya utumishi wa umma na utawala bora.

Hata hivyo, bado hajapata jambo la kipekee litakaloweza kumtofautisha na wenzake waliomtangulia katika ofisi yake. Kwa msingi huo, anapata alama C.

Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene

Kulinganisha na miaka minne iliyopita, walau sasa wizara hii imepunguza kasi ya kamatakamata ya wapinzani wa kisiasa wa Serikali, matukio ya watu kutekwa na kupotea yamepungua na nchi imeanza kuwa na ustaarabu – kuondoka matukio mengine ya hapa na pale.

Hata hivyo, hii ni wizara ambayo hadhi na mawaziri wake hulinganishwa na mwanasiasa mmoja anayeonekana kama aliitendea haki wizara hiyo – Augustine Mrema. Waziri wa Mambo ya Ndani anayependwa ni yule anayeonekana kupambana na majambazi, wauaji na anayetetea haki za raia wake.

Ninamfahamu Simbachawene kama mtu mwenye kujichanganya na watu lakini kwenye utendaji wake kama waziri, bado hajajionyesha hivyo kwa watu kama alivyokuwa Mrema miaka mingi nyuma yake.

Lakini walau, wakati Simbachawene akiwa waziri, watu wanaweza kunywa kahawa katika migawaha ya hadharani pasi na kuhofia usalama wao. Anapata alama B-.

Jenista Mhagama – Bunge, Sera, Ajira, Walemavu, Vijana

Mimi ni mpenzi wa mchezo wa mpira wa miguu na katika mchezo huo kumekuwa na historia ya wachezaji ambao huwa wanapangwa na makocha wao lakini washabiki huwa hawaelewi kwa sababu gani.

Kwa washabiki wa Manchester United, heshima hii ilikuwa ya Darren Fletcher. Uliza mtu yeyote mtaani ni lini mara ya mwisho walisikia kauli kutoka kwa Jenista akizungumzia matatizo ya ajira, vijana au mambo ya kisera kuondoa hotuba zake za bungeni na ni wazi wachache watakwambia.

Kuna kazi za nyuma ya pazia ambazo Jenista huzifanya bungeni au miongoni mwa wanasiasa wa chama tawala na wale wa upinzani ambazo wanaozijua ndiyo humpa madaraka yake mara kwa mara.

Miongoni mwa wananchi, Jenista ni mwanasiasa wa kawaida. Anachukua alama C.

Waziri wa Ardhi William Lukuvi

Kwa sasa, Lukuvi ndiye mbunge wa muda mrefu zaidi katika Bunge la Tanzania na ndiye waziri mwandamizi zaidi miongoni mwa mawaziri waliopo sasa katika baraza la Rais Samia.

Wakati wa utawala wa Rais Magufuli alikuwa miongoni mwa mawaziri waliokuwa wakionekana kuchapa kazi pasipo ‘kukanyaga’ miguu ya watu kama ilivyokuwa kwa vinara wengine wa utawala wa awamu ya tano.

Hata hivyo, kwenye utawala wa Rais Samia, ni kama vile Lukuvi amepunguza kasi na haonekani tena mara kwa mara akitatua na kusikiliza kero za wananchi kama ilivyokuwa huko nyuma.

Utendaji wake sasa ni wa kiwango cha kawaida. Ninampa alama C.

Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe

Wanaomfahamu Mwambe akiwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wanamfahamu kama mtu anayejua anachofanya na ambaye amedhamiria kweli kuifanya nchi yetu iwe mojawapo ya vivutio vya wawekezaji.

Inaonekana kuna tatizo katika siasa yake. Wakati Kitila alipokuwa akishika wadhifa huo kwenye utawala wa Magufuli, alikuwa akionekana huku na kule kuvutia wawekezaji na kutazama miradi.

Suala kubwa kwenye wizara hii ni kwamba waziri hana pa kushika kwa sababu kila anapokwenda ni eneo la wizara ya mwenzake. Kama wewe ni mtendaji kama Mwambe, kubaki na sera na maneno matupu siyo jambo zuri.

Ndiyo sababu pengine utendaji wake kama waziri umekuwa wa kawaida. Wizara ngumu. Anapata C.

Waziri wa Elimu Joyce Ndalichako

Profesa Joyce Ndalichako pengine si fisadi au mtu mbaya lakini utendaji wake kama waziri haujawahi kusifiwa tangu enzi za Magufuli.

Hana ushawishi wa kisiasa na ingawa anasimamia elimu na masuala ya teknolojia, yeye binafsi haijulikani kama hata ana akaunti ya mitandao ya kijamii ambako sehemu kubwa ya watu wake na shughuli za wizara yake zinaendelea.

Anapata D.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki

Mtangulizi wake, Luhaga Mpina, alijulikana kwa matukio ya kuchoma nyavu za wavuvi waliokuwa wakivua samaki kwa njia zisizokubalika kwa taratibu za sheria.

Ndaki, kwa upande wake, hajajiingiza katika matukio tata ya Mpina lakini pia hajafanya jambo lolote la kufanya watu waanze kuitazama wizara yake kipekee.

Ana utendaji wa kawaida. Anachukua C.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Shughuli Maalumu George Mkuchika 

Pengine Mkuchika ameathiriwa zaidi na matatizo ya kiafya yaliyomkumba wakati wa siku za awali za utawala wa Rais Samia. Hata hivyo, ofisi yake ilikuwa ikipewa watu ambao wanaaminika kuwa ni “watu wa Rais” au wanaowakilisha maslahi mapana ya nchi.

Watangulizi wa Mkuchika katika nafasi hiyo walikuwa ni wanasiasa mahiri kama Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wassira, Brigedia Moses Nnauye, Kingunge Ngombale Mwiru na Kanali Nsa Kaisi.

Tatizo kubwa la Mkuchika ni kwamba hana mvuto wa kisiasa, ushawishi au ukaribu na Rais ambao watangulizi wake katika nafasi hiyo walikuwa nao. Katika mazingira ya Rais Samia ya sasa ambapo anahitaji mtu mahiri kuimarisha mahusiano kati ya Serikali, CCM na vyama vya siasa vya upinzani, nafasi ya Mkuchika inahitaji mtu mwingine.

Mtu wa aina ya Balozi Khamis Sued Kagasheki, naweza kusema, na watu wengine wa aina yake, angeweza kumsaidia zaidi Samia kwenye nafasi hiyo. Ninampa Mkuchika alama D.

Waziri wa Muungano na Mazingira Selamani Jaffo

Katika utawala wa Rais Magufuli, Jaffo alikuwa akitajwa kama mmoja wa mawaziri vipenzi wa awamu ya tano akiwa ameshika wadhifa kwenye wizara ya Tamisemi. Kulinganisha na alikokuwa awali, sasa amehamishiwa katika wizara yenye majukumu machache lakini nyeti.

Kwenye wakati wake, Tanzania imerejea katika meza ya mazungumzo ya masuala ya mazingira na malalamiko kuhusu Muungano yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Labda kuwa na Rais kutoka Zanzibar kumekuwa na faida lakini wizara hii ni kama imepata msukuko mpya. Ninampa Jaffo alama B-.

Waziri wa Maji Juma Aweso

Mwanasiasa huyo kijana amepewa wizara inayotajwa kama changamoto namba moja ya Watanzania. Rais Magufuli alipata kusema kwamba kero ambayo amekuwa akiipata kila anakoenda kutoka kwa wananchi imekuwa ni ukosefu wa maji.

Mmoja wa mawaziri wanaozunguka sana mikoani kutatua changamoto za maji, Aweso ni mwepesi kukimbilia kuliko na shida au kero inayotajwatajwa na idadi ya Watanzania wanaopata maji inazidi kuongezeka kila uchao.

Tatizo kubwa la Aweso ni kwamba mzigo wa kero ya maji ni mzito na hadi pale watu watakapoanza kuacha kulalamika kuhusu upatikanaji wa maji, ndipo hasa haiba yake kisiasa itakapoanza kupanda.

Anajizolea alama B-.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa

Bashungwa anajitahidi kupambana katika wizara yake lakini tatizo kubwa analoonekana kuwa nalo ni haonekani kama ni mtu anayefiti kwenye wizara hiyo. Wakati naibu wake akiwa Abdallah Ulega, mapungufu ya Bashungwa yaliweza kufichwa kwa sababu msaidizi wake alikuwa mtu anayejulikana na wengi kwenye sekta hiyo na anayeifahamu.

Kulikuwa na utani wakati Bashungwa alipoteuliwa kwa mara ya kwanza na Rais Magufuli kama endapo amewahi kwenda uwanjani kutazama mpira, ngumi au riadha kabla hajateuliwa kushika wadhifa huo. Kuondolewa kwa Wizara ya Habari kwenye eneo lake kumepunguza zaidi nguvu ya wizara yake ya awali.

Innocent ana akili lakini huenda amewekwa mahali ambako moyo wake hauko. Hata kama kuna mafanikio katika ukuaji wa mchezo wa ngumi na udhamini katika soka, ni wachache watapeleka sifa kwa waziri.

Anapata alama C.

Waziri wa Katiba na Sheria Palamagamba Kabudi

Tatizo kubwa la mhadhiri huyu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni matamshi na tabia zake alizozionyesha wakati wa utawala wa Rais Magufuli. Siku zote, historia ya siasa ya Kabudi itahusishwa moja kwa moja na utawala wa Magufuli – iwe kwenye vita dhidi ya UVIKO-19, sheria za madini na mkanganyiko wa kauli zake kabla ya kuwa mwanasiasa na baada ya kuwa mwanasiasa.

Akiwa Waziri wa Sheria, baadhi ya watu waliokuwa wamekamatwa wakati wa utawala wa Magufuli wameachiwa na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) sasa imeanza kujijengea heshima iliyomong’onyoka wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Ni wakati huo pia, ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa makosa yaliyotokea wakati wa utawala wa Magufuli. Kwenye utawala wa Magufuli, haingekuwa rahisi kwa ofisi ya DPP iliyo chini ya Wizara ya Sheria, kufungua kesi dhidi ya mtu wa aina ya Sabaya.

Hata hivyo, kesi dhidi ya Mbowe imefunguliwa pia katika wakati ambapo Kabudi ni Waziri wa Sheria. Hili, kwa mtazamo wangu, pengine ndiyo doa kubwa zaidi katika utawala wa Samia – na linaanzia na kuishia katika wizara ya profesa huyu wa sheria. Jambo lingine katika utawala wa Samia ni kwamba Kabudi haonekani tena kuwa na makeke aliyokuwa nayo huko nyuma.

Pengine Rais Samia anahitaji kuachana na Kabudi kwenye timu yake ili kutengeneza mpaka baina ya utawala wake na ule wa mtangulizi wake. Ninampa Kabudi alama D.

Ezekiel Kamwaga ni mwandishi wa habari ambaye kwa sasa anasoma kuhusu siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha SOAS nchini Uingereza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni ekamwaga57@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi. 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

6 responses

  1. Kutokana na siri iliyo wazi kwamba Bwana Kamwaga ni mwana CCM nilitegemea pengine angewalamba tu viatu wakubwa kwa kuwapa maksi wasizostahili. I was wrong.
    Spot on haswa kwa kabudi, Lukuvi na Ndalichako. Sijakubaliana nawe kwa Waziri mmoja tu: Aweso kwa maoni yangu anaupiga mwingi mno. Alistahili wallahu A- kama siyo A.

  2. Mama amerithi baraza la Mawaziri . Hili siyo Baraza lake. Amerithi vipaumbele na mipango na mikakati ya JPM. Mama hana Vision yake yeye kama Rais na mambo yanamuendea kombo kwa sababu hata utashi wake. Kwa hiyo hizo credits ulizompa siyo fair. Labda tu kwa vile watanzania tumejenga tabia ya kujikomboa kwa Viongozi wetu ili mambo yakunyokee. Hapaswi kuwa na A. Ningempa B . Masuala ya kusimamai Haki za binadmu zero, Democrasi Zero, Uhuru wa vyombo vya kutenda Haki zero, Uhuru wa vyombo vya habri na wakutoa maoni zero,

  3. Uchambuzi mzuri na tathmini hii japo inaweza tafsiriwa kama maoni binafsi ya mwandishi lakini kwa kiasi fulani yanagusa kwa kiasi fulani hali halisi ya utendaji wa mawaziri katika nyakat zetu.
    Hongera mchambuzi

  4. Baada ya kusoma “uchambuzi” huu na kusikiliza hotuba ya SSH leo, nashawishika japo kwa kiasi kuwa “uchambuzi” huu is potentially a “paid content”. I will be watching this space.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts