Dar es Salaam. Wanajeshi watatu wa Kitanzania wanaosaidia juhudi za kulinda amani katika nchi ya Afrika Kati wameripotiwa kujeruhiwa baada ya gari iliyokuwa imewabeba kugonga kilipuzi ambacho hakikuwa kimegundulika awali.
Watanzania hao ni kati ya wanajeshi 14,000 waliopo nchini Afrika ya Kati kama sehemu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo unaoitwa MINUSCO.
MINUSCO upo nchini Afrika ya Kati tangu mwaka 2014 baada ya kuibuka kwa mapigano kati ya wanamgambo wa Kiislamu na Kikristo hali iliyopelekea amani kutoweka nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na MINUSCO mnamo Disemba 31, 2021, mmoja kati ya wanajeshi hao Watanzania alijeruhiwa sana kiasi ya kwamba alilazimika kusafirishwa kwenda mji mkuu Bangui kwa ajili ya matibabu zaidi.
Taarifa hiyo, hata hivyo, haikutaja majina ya Watanzania hao waliojeruhiwa kwenye shambulio hilo.
MINUSCO imesema kwenye taarifa yake kwamba tukio hilo lilitokea Disemba 30, 2021, majira ya saa tano kamili asubuhi saa za Afrika ya Kati pale msafara uliojumuisha Watanzania hao ulipoondoka mji wa Berbérati kuelekea kwenye vituo vya muda vya MINUSCO kwenye miji ya Gbambia na Amada-Gaza, inayopatikana kilomita 100 kaskazini-mashariki mwa Berbérati.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Kiongozi wa MINUSCO Mankeur Ndiaye amenukuliwa akilaani vikali shambulio hilo, huku akiwaombea majeruhi waweze kupona haraka.
“Licha ya mazingira magumu walinda amani wetu wanakabiliana nayo, yanayofanywa kuwa magumu zaidi na mabomu haya ya kutengeneza,” taarifa iliyotolewa na MINUSCO imemnukuu Ndiaye akisema. “MINUSCO imedhamiria kuendelea na jukumu lake hili la kudumisha amani na utulivu.”
One Response
asante kwa kushare habari hii muhimu