Dar es Salaam. Mnamo Disemba 23, 2021, Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma iliwaita kwa ajili ya usaili mamia ya vijana wa Kitanzania waliokuwa wameomba ajira mbalimbali za Serikali na mashirika yake. Usaili huo ulifanyika Dodoma, kati ya Januari 8 na 9, 2022.
Lakini kwa mujibu wa taarifa ilizozifikia The Chanzo, makumi ya vijana waliofika Dodoma kwa ajili ya usaili huo, walinyimwa fursa ya kushiriki kwenye zoezi hilo kwa visingizio ambayo wengi waliona havina msingi wowote. Visingizio hivi vingi vilihusu vyeti (vya kuzaliwa na kitaaluma) na vitambulisho (hususan kile cha NIDA).
Yafuatayo ni maelezo ya moja kati ya vijana hawa ambaye amekubali kuelezea uzoefu wake kuhusiana na kadhia hii kwa masharti ya kuhifadhiwa utambulisho wake. Kijana huyu, ambaye alihitimu mwaka 2014 kutoka moja ya vyuo vikuu vya Tanzania na shahada ya ukuzaji viumbe vya kwenye maji (BSc Aquaculture), alilazimika kusafiri kilomita 692 kutoka Kigoma anakoishi mpaka Dodoma kwa ajili ya usaili huo na bado hakuweza kushiriki kwenye zoezi hilo.
Ifuatayo ni simulizi yake:
Asubuhi ya Januari 9, 2022, niliamka alfajiri katika viunga vya jiji la Dodoma kutoka kwenye lodge niliyokuwa nimefikia maeneo ya Area A.
Asubuhi hii nilipaswa kuelekea eneo la ukumbi wa usaili wa mchujo kule Chuo Kikuu cha Dodoma kwenye ukumbi ujulikanao kama Auditorium ulio chini ya College of Informatics and Virtual Education (CIVE).
Ni usaili ulioratibiwa na Sekretarieti ya Ajira, taasisi ambayo ni mwajiri kwa niaba ya Serikali, taasisi na mashirika ya umma. Kuna kazi ya Serikali niliomba, na nimebahatika kuitwa kwenye usaili.
Kabla ya kwenda huko, nilihakikisha kwamba nina vitu vyote vinavyohitajika kwa ajili ya usaili huo, kama vile vyeti halisi vya kitaaluma na cha kuzaliwa pia kitambulisho, ambapo mimi nilibeba cha kazi.
Tangazo la kuitwa kwenye usaili lilisema kila msailiwa anapaswa kuwa na kitambulisho kimoja wapo kati ya hivi: Kitambulisho cha mkazi, kitambulisho cha mpiga kura, kitambulisho cha kazi, kitambulisho cha uraia au hati ya kusafiria.
Nazuiwa kuingia kwenye usaili
Lakini mbali na kukidhi matakwa ya tangazo hili, nilizuiwa kuingia kwenye chumba cha usaili kwa sababu eti sina kitambulisho halali cha NIDA. Mimi sikuwa na kitambulisho kweli, lakini nilikuwa na namba ambayo iliniwezesha kuona kitambulisho changu kwenye tovuti ya NIDA.
Lakini hata hivyo, tangazo la kuitwa kwenye usaili halikuweka sharti la kuwa na kitambulisho cha NIDA. Mimi nilikuwa na cha kazi ambacho wasaili walipaswa wakikubali kwa mujibu wa tangazo lao wenyewe.
Sikua peke yangu niliokumbwa na kadhia hii. Wenzangu wengi pia walizuiliwa kufanya usaili huo kwa visingizio mbalimbali, vingi vikihusisha kukosekana kwa cheti hiki au kile au kitambulisho cha utaifa.
Wengine waliopoteza nyaraka hizo, licha ya kuwa na loss report kutoka polisi, nao pia walizuiliwa. Tulijua ni masikhara tu mwanzo, kumbe wenzetu walikuwa wanamaanisha.
‘Jaza fomu, tutayamaliza’
Mtu aliyeonekana kama ni mkuu kwenye usimamizi wa zoezi hili hatimae alikuja kutuona watu tuliozuiwa kuingia kwenye usaili, ambao tulikuwa kama 30 hivi, na ambao kwa sasa tulikuwa tumewekwa pembeni.
Mazungumzo kati ya huyu mkuu na wenzangu yalikuwa mafupi tu, na ilipofika zamu yangu yalienda kama hivi:
Yeye: Una shida gani?
Mimi: Kitambulisho, nimeonyesha kitambulisho cha kazi ila nimeambiwa nikae pembeni tukusubiri.
Yeye: Embu tukione.
Mimi: [Natoa kitambulisho cha kazi na kumwonesha].
Bosi: Aha, taasisi yako ndogo, hata siijui, jaza fomu pale.
Mimi: Kwenye tangazo mliandika kitambulisho cha kazi kinaruhusiwa, mlimaanisha wafanyakazi wa taasisi zipi, za Serikali tu au hata na za binafsi?
Yeye: Wewe jaza fomu bwana tutayamaliza.
Nikafanya kama nilivyoelekezwa. Lakini sikubahatika kuingia kwenye usaili, baada ya mkuu huyo aliyenihoji kuniambia mimi na wenzangu wenye tatizo kama langu kwamba tulipaswa kukabidhi vielelezo vyetu vikiwa vipo kwenye seti, na kwamba ikiwa kielelezo kimoja tu kimekosekana kwenye seti hiyo basi hatukidhi vigezo vya kusailiwa.
Sikumuelewa anamaanisha nini na hakukuwa na fursa ya kuomba ufafanuzi!
Niliumia sana
Mkuu yule akaondoka na kuacha maagizo kwa polisi waliokuwepo pale kwamba tuondoshwe kwenye eneo lile. Binafsi niliumia sana kwani kama kitambulisho cha kazi ninacho na kimetajwa kwenye tangazo la kuitwa kwenye usaili.
Kwa nini nimekatazwa kuingia kwenye chumba cha usaili? Kitu kilichonisumbua zaidi ni kwamba hakuna mfumo wa kukata rufaa kwenye michakato kama hii pale unapohisi umeonewa.
Hata hivyo, nilijaribu kuwasilisha malalamiko yangu kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKURURU) kupitia namba yao ya bure ya 113, lakini licha ya kujaribu kuipiga zaidi ya mara 20 sikufanikiwa kupata mtu wa kuongea naye kutoka kwenye mamlaka hiyo.
Roho iliniuma, nikaishia kunung’unika na kulaumu mfumo. Hawa watu wenye mamlaka kwa nini ni wakatili hivi? Mbona wana maamuzi ya kikatili hivi? Kwa nini wanandika wasiyoyatekeleza? Kitambulisho cha taasisi ndogo kinakuaje?
Je, mwajiri ambaye amesajiliwa na mamlaka za usajili husika kitambulisho chake kinakuaje hakitambiliwi na watu wa taasisi zingine na zingine zinakikubali na kukupatia huduma?
Nikawaza labda ni njia tu ya kupunguza watu kwenye zoezi hilo ili lizidi kuwa rahisi kwa waendeshaji wake. Nikawaza pia wanaweza kuwa tayari wana watu watu wao na kwamba zoezi zima linafanywa kama geresha tu, kuonesha umma kwamba kuna usaili umefanyika, kuonesha kwamba ajira za Serikali hupitia mchakato fulani.
Ni jana tu Januari 13, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alitaja upendeleo kwenye utoaji wa ajira kama moja ya mambo asiyoyapenda na ambayo yanafanyika kwenye Serikali yake.
Sekretarieti ya ajira ibadilike
Sekretarieti ya ajira wanapaswa kujitafakari upya. Unaita kwenye usaili wa mchujo watu zaidi ya 100, nafasi tatu na lazima mtu asafiri kutoka anakotoka kwenda mpaka Dodoma kwenye usaili wa kuandika unaotumia dakika 40 tu. Kutokana na maendeleo ya kiteknojolojia yanayoendelea kutokea duniani, jambo hili linapaswa likome.
Ni muhimu kuwatumia vijana wetu waliosomea mambo ya TEHAMA kubuni mfumo utakaotatua kero hii. Mfumo huu utamuepusha mtu anayetafuta ajira kuingia gharama za ziada na asizozimudu wakati wa mchakato wa utafutaji ajira.
Viongozi wetu pia waache kukariri mambo na kung’ang’ania ukale, kwamba kitambulisho ili kiwe kitambulisho lazima uweze kukishika, na kwamba kile kilichopo mtandaoni hakina sifa ya kuitwa kitambulisho. Mwelekeo wa dunia kwa sasa ni kufanya kila kitu kiwe mtandaoni, ikiwemo fedha ambapo sasa ili uweze kufanya matumizi siyo lazima uwe na fedha taslimu.
Kitu kingine ambacho nakiona ni cha kutilia mkazo ni hii dhana kwamba taasisi ili ikidhi vigezo vya kuwa taasisi ni lazima iwe ni taasisi ya Serikali; au kwamba kwa sababu wewe taasisi huifahamu basi moja kwa moja kwamba taasisi hiyo haipo kwenye uso wa dunia.
Katika nyakati ambazo shughuli nyingi zilizokuwa zinafanywa na Serikali zinakabidhiwa kwa taasisi na mashirika binafsi, kuendeleza mtazamo huo ni kubaki kwenye ukale ambao kwa maoni yangu hauna tija yoyote kwa taifa.
Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala hii, wasiliana na mhriri wetu kupitia editor@thechanzo.com.